Msafara alioutokea Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-katika shambulio (Ghaz-wah) la Ushayrah, ulikuwa ndio msafara mkubwa na wenye mali nyingi sana kuliko misafara yote iliyotangulia.
Khabari zikamfikia Bwana Mtume kwamba tayari msafara huo umeshaondoka Shamu na huko njiani kurudi Makkah.
Mtume akautokea na kuwaambia maswahaba wake:
“Huo msafara wa makurayshi (unakuja) na ndani yake mna mali zenu (mlizoziacha Makkah), haya utokeeni huenda Allah akaufanya ngawira kwenu”.
Mtume aliupania sana msafara huu usimponyoke wakati wa kurudi kwake Makkah, kama ilivyojitokeza wakati wa kwenda na huko nyuma kwa misafara mingine kama hiyo.
Mtume akaukusanyia msafara huo kila aliye mwepesi; asiye na udhuru. Na akamuamrisha kila aliyekuwa na kipando (mnyama) atoke pamoja naye.
Watu wakaharakisha kutoka bila ya kuwa na maandalizi yo yote ya vita kwa kudhania ni suala la msafara tu.
Na kwa kudhania kuwa Mtume wa Allah hatolazimika kupigana vita kama ilivyokuwa ikitokea mara kwa mara huko nyuma.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alitoka kuuzengea msafara huu siku ya Jumamosi, mwezi kumi na mbili Ramadhani/02 A.H. (Januari 624).
Alitoka na idadi ya Muhajirina na Answari ipatayo mia tatu na kumi na kitu.
Kabla ya kutoka alikuwa tayari amekwisha watuma Twalhah Ibn Abdillah na Sa’ad Ibn Zayd kupeleleza khabari za msafara ule.
Lakini ikasadifu Mtume kutoka na maswahaba wake kabla ya kurejea kwa wapelelezi wake na kumletea taarifa ya upelelezi wao.
Mtume alifanya hivyo kutokana na pupa aliyokuwa nayo ili msafara usimponyoke na kama tahadhari isije ikawa wapelelezi wake wamefikwa na la kufikwa.
BWANA MTUME ALIKAGUA JESHI LAKE NA KUWAREJESHA MADINAH WALE WOTE WALIOTHIBITIKA KUWA BADO NI WADOGO (SIO WATU WAZIMA).
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akashika njia, akaenda zake mpaka akafika sehemu iitwayo “Buyuut-Suq-yaa”.
Hili ni eneo lenye maji matamu (yasiyo na chumvi), umbali wa maili moja kutoka mji wa Madinah.
Bwana Mtume akapiga kambi hapo siku ya Jumapili, kisha ndipo lilipoanza zoezi la kulikagua jeshi lake. Akampa amri ya kurejea Madinah kila aliyemuona kuwa ni mdogo na hawezi kubeba silaha pindipo vita vitauma.
Wakawa miongoni mwa waliopewa amri ya kurudi ni mabwana Abdullah Ibn Umar, Raafii Ibn Khadiyji, Al-Baraai Ibn Aazib, Usaid Ibn Hudhwayr, Zayd Ibn Al-Arqam na Zayd Ibn Thabit.
Mtume pia alimkagua Umeir Ibn Abiy Waqaaswi na kumuona kuwa bado ni mtoto asiyeruhusiwa kushiriki vitani. Umeir akalia sana baada ya kutakiwa arejee, Mtume kuona hivyo ikabidi amruhusu kujiunga na jeshi na kusonga mbele.
Al-Waaqidiy amepokea kutoka kwa Sa’ad Ibn Abiy Waqaaswi-kwamba yeye mwenyewe amesema:
Nilimuona ndugu yangu Umeir Ibn Abiy Waqaaswi kabla hatujakaguliwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akijifichaficha. Nikamuuliza : Una nini ewe ndugu yangu? Akanijibu:
Mimi ninachelea Bwana Mtume asije kuniona mdogo na kuniamuru kurudi na ilhali mimi ninapenda kutoka, huenda Allah akaniruzuku shahada (kufa shahidi). Akasema: (Sa’ad): Akakaguliwa na Bwana Mtume akamuona kuwa bado ni mdogo, akamwambia: “Rudi”.
Umeir akalia ndipo Bwana Mtume akamruhusu. Akasema (Al-Waaqidiy): Sa’ad akawa akisema: Nilikuwa nikimbebea kamba (upachikio) za upanga wake. Akauawa shahidi (kama alivyotamani) katika vita vya Badri akiwa na umri wa miaka kumi na sita tu.
WALIKUWA WAKIPOKEZANA VIPANDO KUTOKANA NA UCHACHE WA VIPANDO UKILINGANISHA NA IDADI YA WATU.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie- akaanua kambi hapo “Buyuut-Suq-yaa”, akaondoka kusonga mbele kwa lengo la kutimiza azma yake. Akiwa na askari wapiganaji (combatants) wapatao mia tatu na tano (305).
Katika hao walikuwemo Muhajirina wapatao sabini hivi na kiasi cha Answaari mia mbili na arobaini hivi.
Hawakuwa na farasi ila wawili tu na ngamia kama sabini tu. Kutokana na uchache wa vipando walivyokuwa navyo ikawalazimu kupanda kwa zamu; hawa wanapanda na wale wanatembea.
Baada ya umbali fulani wale waliokuwa wamepanda wanashuka na kuwapa fursa ya kupanda wenzao waliokuwa wakitembea. Idadi ya watu iliwalazimisha kila watu wanne wapokezane kupanda ngamia mmoja. Mmoja anapanda watatu waliobakia wanakwenda kwa miguu.
Bwana Mtume naye hakuiepa hali hii, naye ilimkumba. Akawa anapokezana kupanda na Aliy Ibn Abiy Twaalib na Marthad Ibn Abiy Marthad.
Hamzah Ibn Abdul Mutwalib (Ami yake Mtume) yeye alipokezana na Zayd Ibn Haarithah, Abuu Kabshah na Anasah; hawa walikuwa ni mahuru wa Bwana Mtume.
Ama Abuu Bakri, Umar na Abdurahmaan Ibn Auf, wao pia walishirikiana ngamia mmoja. Hivi ndivyo ilivyokuwa hali ya kikosi hiki, kila watu wanne au watatu walipokezana kupanda na kutembea.
Bwana Mtume pamoja na kuwa kwake kiongozi aliyestahiki heshima zote, lakini hakukubali wala kuona raha ila ashirikiane na askari (maswahaba) wake katika raha na shida.
Apande na kutembea inapofika zamu yake kama ilivyokuwa kwa watu wengine wote. Ilipomalizika zamu yake ya kupanda alishuka, hapo wenzake humwambia: Endelea kupanda ewe Mtume wa Allah. Nae akiwajibu kwa kusema:
“Nyinyi hamna nguvu ya kutembea kunishinda mimi na mimi si mkwasi wa ujira kuliko nyinyi”.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-hakuwa amefunga bendera ya vita alipotoka Madinah. Lakini tangu alipotoka “Buyuut-Suq-yaa” alipokuwa amepiga kambi, aliwaweka watu wake katika hali ya utayarifu wa vita ikiwa vitatokea.
Mtume alifanya hivyo kutokana na uwezekano kuwa adui anaweza kuwashtukiza ghafla nao wakiwa hawajajiandaa.
Nao kila walivyosonga mbele ndivyo walivyozidi kujitoma katika ardhi inayomilikiwa na mushrikina.
Ni kutokana na haya yote ndiyo Bwana Mtume akaanza kuwapanga watu wake kwa namna ambayo watasalimika na shambulio la ghafla.
Akamuweka mbele ya jeshi Qays Ibn Abiy Swa’aswa’ah na nyuma akamuweka Zubeir Ibn Al-awwaam.
Akaamuru kila mtu ashike silaha yake tayari kwa lo lote litakalotokea. Akafunga bendera tatu za vita; bendera nyeupe iliyobebwa na Musw’ab Ibn Umeir na bendera nyingine mbili nyeusi.
Moja alikuwa nayo Aliy Ibn Abiy Twaalib na nyingine alikuwa nayo mtu mmoja katika Maanswari.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliwatanguliza mbele yake majasusi wake wawili ili wampelelezee na kumletea khabari za adui.
Hawa hawakuwa wengine ila ni mabwana Basbas Ibn Amri na Adiy Ibn Abiy Zaghbaa. Katika kuitekeleza amri ya Mtume, mabwana hawa walikwenda mpaka eneo la maji la Badri.
Hapo waliwakuta vijakazi wawili wakichota maji, wakafahamu kutokana na mazungumzo yaliyokuwa yakijiri baina yao kwamba wao (vijakazi) wanaungojelea ule msafara wa Makurayshi.
Na kwamba msafara huo utafika mahala hapo kesho yake. Haraka na bila kuchelewa wakarudi kwa Mtume na kumpasha khabari ile.