SWALA YA IJUMAA

I/. UBORA WA SIKU YA IJUMAA:

Siku ya Ijumaa ni siku bora na tukufu miongoni mwa siku za dunia, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ameitaja siku ya Ijumaa kama hivi:

“Bora ya siku uliyochomozewa na jua ni siku ya Ijumaa, ndani yake ameumbwa Adamu-Amani imshukie-na ndani yake ametiwa peponi. Na ni ndani yake (siku hiyo) alitolewa humo (peponi) na wala hakitasimama kiyama ila ndani ya siku ya Ijumaa”. Muslim-Allah amrehemu.

Kwa hivyo basi, kunamuwajibikia muislamu kuitukuza, kuienzi na kuiheshimu siku ya Ijumaa kwa kukithirisha kutenda amali njema na kujiepusha na madhambi.

Katika hadithi nyingine Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema:

“Bwana wa siku mbele ya Allah ni siku ya Ijumaa (ni bora) kuliko siku ya kuchinja (Eidil-adh-ha) na siku ya Fitri”. Shaafiy & Ahmad-Allah awarehemu.

Zimepokelewa hadithi nyingi kutoka kwa Bwana Mtume zikitaja fadhila na ubora wa siku hii ya Ijumaa. Hii ni siku ambayo umo ndani yake wakati (muda fulani) ambao mja hamuombi Mola wake ndani yake cho chote cha kheri ila humpa.

Ni kwa ajili ya fadhila hizi tulizozitaja na nyinginezo, Allah akaichagua siku hii kuwa ni Idi (sikukuu) ya kila juma (wiki) ya waislamu.

Akawaamrisha waja wake kuipa umuhimu wa pekee siku hii, wajipambe kama walivyoelekezwa na kufundishwa na Mtume wao.

Waache shughuli zao na waharakie kuiendea ibada ya swala ya Ijumaa. Wakutanike pamoja ndani ya siku hii ili iwe ni nembo, alama na kielelezo cha umoja wao na dalili na ishara ya nguvu yao.

Siku hii ni zawadi kwa umati Muhammad kwani ni sababu ya kufutiwa dhambi zao na ni kirudufisho cha ujira na thawabu.

Lakini kwa masikitiko makubwa, uzoefu unaonyesha kuwa waislamu wamekuwa ni watu wa kuzembea na kupuuza kila kitu.

Hata kufikia kiasi cha kudharau matukufu ya dini yao yaliyotukuzwa na Mola Muumba wao, huu ni msiba mkuu na haya ni maangamivu.

Leo siku ya Ijumaa machoni na mioyoni mwa waislamu wengi si cho chote na wala si lo lote ila ni siku tu kama zilivyo baki ya siku nyingine za juma.

Hili halihitaji ushahidi kwani linashuhudiwa bayana na kila mmoja wetu. Waislamu tumeipuuza siku yetu tukufu ya Ijumaa, siku iliyokuwa na nafasi,cheo, daraja na iliyopewa umuhimu wa pekee na mababu zetu (wahenga).

Wazee wetu hao wema waliutambua umuhimu, utukufu na ubora wa siku ya Ijumaa, hivyo wakawa wakiingojea kwa hamu na shauku kuu.

Waliingojea kama mtu mwenye kiu ayangojeavyo maji baridi au mithili ya mgonjwa aingojeavyo siku ya kupona na kupoa kwake.

Wakawa wanakoga, wananadhifisha nguo zao, wakajitia manukato na wakienda mapema msikitini kuhudhuria swala ya Ijumaa.

Wakienda msikitini ilhali wamefunikwa na staha, heshima, utulivu na unyenyekevu. Nyoyo zao zikiwa zimesheheni khofu ya Allah Bwana Mlezi wao na ndimi zao zikiwa majimaji kwa utajo (dhikri) wa Mola wao.

Macho yao yakiwa yamesitiriwa na maharamisho ya Allah, hata wakiingia msikitini kila mmoja wao akiwania kuchukua nafasi iliyo karibu na khatibu; nafasi ya mbele.

Walifanya hivi kutokana na kupupia kwao kuhodhi fadhila za safu ya kwanza na kustafidi na khutba.

Khatibu anapopanda juu ya mimbari na kuanza kukhutubu, huwa makini, nyoyo zao zikizingatia, usikivu (masikio) wao huwa wazi.

Khatibu hamalizi khutba yake ila huwaliza wote; janibu ya twaa na janibu ya maasi. Janibu ya maasi hulia kutokana na kuichelea adhabu na ghadhabu ya Allah.

Wakati ile janibu ya twaa ikilia kutokana na tamaa ya fadhila na thawabu za Allah.

Enyi ndugu waislamu, tuchungeni adabu za siku hii tukufu, tujinadhifisheni, tujipambeni na tujitieni manukato kwa ajili ya siku hii adhimu.

Tutokeni majumbani mwetu kwa unyenyekevu kuelekea kwenye nyumba za Allah. Twendeni mapema na tukiingia msikitini kila mmoja wetu akae kwa adabu, heshima, staha na utulivu.

Tutahadharini na kufanya kitendo au kusema kauli itakayomuudhi Allah, Mtume wake na waja wake mithili ya kukata/kukengeuka shingo za watu.

Tueleweni kwamba kuwaudhi waislamu ni jambo linalopomosha ujira na kubatilisha thawabu adhimu za Ijumaa.

Atakayeingia msikitini miongoni mwetu na ilhali khatibu anakhutubu, basi na asikae chini ila baada ya kuswali rakaa mbili khafifu (nyepesi).

Tunapomaliza kuitekeleza fardhi hii ya swala ya Ijumaa, tusiwe na haraka ya kutoka msikitini.

Tukae tuswali suna, tulete dua na tumuombe Mola wetu maghfira, radhi na uongofu. Mola wetu Mtukufu tunamuomba airejeshe haiba na utukufu wa siku ya Ijumaa katika nafsi, nyoyo, roho na miili yetu-Aamiyn.

 

II/. KUSHARIIWA (KUWEKWA SHERIA) SWALA YA IJUMAA:

 

Swala ya Ijumaa imeshariiwa nayo ni miongoni mwa fadhila alizoukhusu nazo Allah umati huu. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba yeye alimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema:

“Sisi  ndio wa mwisho (kuletwa duniani), wa mwanzo (kuingia peponi) siku ya kiyama isipokuwa wao walipewa kitabu (sheria) kabla yetu. Kisha hii (Ijumaa) ni siku yao ambayo walifaradhiwa wakakhitalifiana katika siku hiyo. Allah akatuongoza sisi, basi watu wanatufuata katika siku hii; Mayahudi kesho (Jumamosi) na Manaswara kesho kutwa (Jumapili)”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Swala ya Ijumaa ilifaradhishwa katika kipindi cha utume cha Makah, punde kidogo kabla ya Hijrah.

Lakini haikumkinika kuswaliwa kutokana na udhaifu waliokuwa nao waislamu wakati huo na kupelekea kushindwa kukusanyika pamoja kwa ajili ya swala hii. Mtu wa mwanzo aliyewakusanya watu na kuwaswalisha swala hii ya Ijumaa Madinah kabla ya Hijrah ya Bwana Mtume, alikuwa ni As’ad Ibn Zaraarah-Allah amuwiye radhi. Hivi ndivyo ilivyopokelewa katika riwaya ya Ka’ab Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi-kama alivyopokea Imamu Abuu Daawoud na wengineo.

 

III/. HUKUMU YA SWALA YA IJUMAA NA DALILI YA UFARADHIFU WAKE:

Wanazuoni wamekongamana kwamba swala ya Ijumaa ni  FARDHI AYN (faradhi binafsi), HURU ambayo si badali ya swala ya Adhuhuri.

Ila tu pale inapofutu, basi kunamuwajibikia muislamu kuswali Adhuhuri rakaa nne. Ufaradhifu na uwajibu wa swala ya Ijumaa kwa muislamu unatokana na kauli hii ya Allah:

“ENYI MLIOAMINI! KUKIADHINIWA KWA AJILI YA SWALA SIKU YA IJUMAA, NENDENI UPESI KUMTAJA ALLAH  NA ACHENI BIASHARA. KUFANYA HIVI NI BORA KWENU, IKIWA MNAJUA (hivi basi fanyeni)”. [62:9]

Muradi wa “KUMTAJA ALLAH” hapa katika aya hii kama walivyoeleza wanazuoni ni SWALA YA IJUMAA na KHUTBA yake.

Hii ni kwa sababu ndani ya swala na khutbah hutajwa jina la Allah. Na mapendeleo ya ibara “ACHENI BIASHARA” ni zile shughuli zota anazozifanya mwanadamu katika kujipatia riziki yake ya kila siku. Iwe ni biashara, kilimo, ajira, uvuvi  na nyinginezo.

Kwa upande wa hadithi, zipo hadithi nyingi zilizopokewa katika kutaja uwajibu wa swala hii ya Ijumaa. Miongoni mwa hadithi hizo ni hizi zifuatazo:-

v     Twaariq Ibn Shihaab-Allah amuwiye radhi-amepokea kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Ijumaa ni haki ya wajibu juu ya kila muislamu…” Abuu Daawoud-Allah amuwiye radhi.

v   Imepokelwa kutoka kwa Abuu Hurayrah na Ibn Umar-Allah awawiye radhi-kwamba wao walimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema juu ya mimbari yake:

“Wakome wakome watu kuacha kwao (swala za) Ijumaa au Allah azipige mihuri nyoyo zao kisha watakuwa miongoni mwa walioghafilika”. Muslim & wengineo-Allah awarehemu.

 

SWALA YA IJUMAA

I/. UBORA WA SIKU YA IJUMAA:

Siku ya Ijumaa ni siku bora na tukufu miongoni mwa siku za dunia, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ameitaja siku ya Ijumaa kama hivi:

“Bora ya siku uliyochomozewa na jua ni siku ya Ijumaa, ndani yake ameumbwa Adamu-Amani imshukie-na ndani yake ametiwa peponi. Na ni ndani yake (siku hiyo) alitolewa humo (peponi) na wala hakitasimama kiyama ila ndani ya siku ya Ijumaa”. Muslim-Allah amrehemu.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *