MAANA;
Wasia ni neno lenye asili ya lugha ya Kiarabu ni neno ambalo limetumika ndani ya Qur-ani Tukufu, hadithi za mtume na baki ya maandishi mengine ya kiarabu.
Neno hili kama lilivyotumika ndani ya Qur-ani na Sunah lina maana ya maneno yenye maadili maonyo yanayolenga :-
Kunasihi/kuamrisha juu ya ama kutenda au kutokutenda jambo fulani.
Kuadabisha na kutoa muongozo juu ya suala zima la maisha.
Kuelekeza, kukosoa na kurekebisha tabia .
CHIMBUKO:
Asili na chimbuko la darsa yetu hii ya wasia ni kauli yake Allah Mola Mwenyezi ambayo ni wasia wake kwa walimwengu wote:
“…NA KWA YAKINI TULIWAUSIA (amri) WALIOPEWA KITABU KABLA YENU, NA NYINYI (pia) KWAMBA MUMCHE ALLAH (wasia)…” (4:131)
Na inaeleweka wazi kwa kila mmoja wetu kwamba kumcha Allah (Taqwa) ni kujiepusha na makatazo ya Allah na kuyatekeleza maamrisho yake.
LENGO/MADHUMUNI:
Darsa hizi za wasia zinalenga kumjenga musislamu kiutu na kitabia ili:-
Maisha yake yote yatoe taswira ya Uislamu, yaani awe ni Uislamu unaotembea.
Awe ni kigezo cha utu na tabia njema katika jamii anayoishi nayo.
Afikie daraja ya Ucha–Mungu (Taq-wa) kwa kutenda anayoamrishwa katika wasia na kuacha anayokatazwa.
Mpenzi msomaji wetu, darsa hizi za wasia ambazo ni sehemu ya somo la Akhlaaq zitakujia katika mfululizo utakaokuwa chini ya anuani munasibu.
Ni matarajio yetu makubwa kwamba wasia huu maridhawa utakunufaisha katika maisha yako binafsi, ya kijamii, ya ulimwengu huu na ule ujao.
Kwa fadhila zake Allah ambaye ndiye aliyetuelekeza katika sula zima la wasia. Sasa kwa msaada wake Allah tuingie katika darsa zetu hali ya kuwa tunakusudia kujiusia sisi nafsi zetu na wewe msomaji wetu.