MTUME WA ALLAH AFICHA DHAMIRA YAKE

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasonga mbele na maswahaba wake mpaka akafika katika bonde la Badri.

Hapo akapiga kambi kando ya bonde lililo karibu na Madinah.

Bwana Mtume alikuwa katika hadhari kuu, akalifanya suala na makusudio yake kuwa ni siri kubwa.

Alifanya hivyo ili khabari isije kuvuja na kuwafikia wanafiki na majasusi wa Makurayshi.

 Alifanya hivi ili kuficha mikakati na muelekeo wake, hiyo ikiwa ni mojawapo ya mbinu za vita.

 Akaamrisha zikatwe kengele walizofungiwa ngamia shingoni na akawa kila anapopiga kambi mahala hupeleleza khabari za Makurayshi. Akiuliza khabari zao kwa uficho na hadhari kuu.

Ibn Is-haaq na wanazuoni wengine wa Sira-Allah awarehemu- wamepokea kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipiga kambi karibu kabisa na Badri.

 Akampanda mnyama yeye na mmoja wa maswahaba wake, wakaenda mpaka kwa mzee mmoja muarabu. Mtume akamuuliza khabari zilizomfikia za Makurayshi, Muhammad na maswahaba wake. Yule mzee akamjibu:

“Ukitupa khabari utapata khabari”. Mtume akamwambia: “Ni nipe nikupe?”.

Akajibu: Naam, yule mzee akaanza kusema: :Hakika imenifikilia khabari kwamba Muhammad na maswahaba wake wametoka siku kadha kadha.

Ikiwa mtu aliyenieleza amesema kweli, basi hapana shaka wao leo watakuwa wamefika mahala kadha kadha.

Ikasadifu kuwa ndio mahala khasa alipopiga kambi Mtume na maswahaba wake. Na khabari zilizonifikia ni kwamba Makurayshi nao wametoka siku kadha kadha.

Ikiwa huyo aliyenipasha khabari amesema kweli, basi wao leo watakuwa wamefika mahala kadha. Ikasadifu kuwa ndio mahala khasa walipo Makurayshi wakati ule.

Yule mzee alipomaliza kueleza khabari zake, akamuuliza Mtume: “Nyinyi ni watu wa wapi?” Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamjibu:

 Sisi ni watu wa sehemu zile zenye maji”, huku akiashiria kwa mkono wake upande wa Iraq, kisha wakaondoka. Yule mzee akabaki akijisemea: “Hawa si watu wa pande zile zenye maji, kweli ni watu wa pande za maji za Iraq, hata!” Mtume akarejea kuungana na maswahaba wake pale walipopiga kambi.

Jua lilipokuchwa na kiza kikaanza kuingia akawatuma Aliy Ibn Abiy Twaalib, Zubeir Ibn Al-Awwaam, Sa’ad Ibn Abiy Waqaasw na kundi la maswahaba wake kwenda katika eneo lenye maji la Badri.

Waende wakapeleleze khabari za Makurayshi, walipofika hapo wakawakuta watekamaji wa Makurayshi wakichota maji.

Wakawakamata vijana wawili miongoni mwao, wakawaleta mpaka kwa Mtume nae akiwa anaswali.

Ikawa wao wanawauliza vijana wale: Nyinyi ni watumishi wa nani?

Wakitaraji kwamba vijana wale ni miongoni mwa watekaji maji wa msafara wa Makurayshi. Wale vijana wakajibu:

Sisi ni wateka maji wa Makurayshi (waliotoka Makkah), wametutuma kuja kuwatekea maji. Maswahaba wakadhania kuwa vijana wale wanaongopa, wakaanza kuwapiga huku wakiwauliza nao wakisema:

Sisi ni wateka maji wa Makurayshi (sio wa msafara). Walipozidiwa na kipigo wakasema: Sisi ni wateka maji wa Abuu Sufyaan, wakaacha kuwapiga. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipomaliza kuswali akawaambia:

“Walipokuambieni ukweli mliwapiga na walipokuongopeeni mkawaachia! Wallah, wamesema kweli wao ni wateka maji wa Makurayshi”.

Kisha Mtume akawauliza khabari za Makurayshi, wakamjibu:

Wao wallah wako nyuma ya hili fungu la mchanga unaloliona kando ya bonde hili lililo mbali na Madinah. Mtume akaendelea kuwauliza: “Wako watu wangapi?” Wakamjibu: wengi tu, akawauliza tena akawaambia: “Nataka idadi yao ni wangapi?” Wakamjibu hatujui.

 Akawauliza: “Wanachinja ngamia wangapi kila siku?” Wakasema: siku moja huchinja ngamia tisa na siku nyingine kumi. Hapo ndipo Mtume aliposema:

“Watu hawa ni kati ya mia tisa na alfu”. Kisha akawauliza tena: “Nani miongoni mwa watu watukufu wa Makurayshi yumo humo?” Wakaanza kumtajia majina ya watukufu wao wote. Mtume akawaeleza maswahaba wake, akawaambia:

“Haya hii sasa ndio Makkah imekutupieni vipande vya maini yake (wanawe watukufu)”. Waislamu wakatambua kutokana na kauli hiyo ya Bwana Mtume kwamba sasa ni vita tu, hakuna njia ya kuviepuka.

Wakajua kuwa hawana budi kupambana na adui mwenye nguvu zaidi na maandalizi ya kutosha kuliko wao.

Hebu tuipe nafasi Qur-ani Tukufu nafasi itueleze hali ilivyokuwa katika uwanja wa vita:

“…SIKU YALIPOKUTANA MAJESHI MAWILI (siku ya vita vya Badri-jeshi la waislamu na jeshi la makafiri). NA ALLAH NDIYE MWENYE UWEZA JUU YA KILA KITU. (Kumbukeni) MLIPOKUWA KANDO YA BONDE LILILO KARIBU (na Madinah) NAO (makafiri) WALIKUWA KANDO YA BONDE LILILO MBALI, NA ULE MSAFARA (wa Makurayshi uliokuwa na mali yao) ULIPOKUWA CHINI YENU (upande mwingine kabisa) NA KAMA MNGELIPEANA MIADI MNGALIKHITILAFIANA. LAKINI (mmekutana hivi hivi na jeshi lao la vita) ILI ALLAH ALIPITISHE JAMBO LILILOKUWA LAZIMA LITENDEKE; KUSUDI YULE AANGAMIAYE (akakhitari ukafiri) AANGAMIE KWA DALILI ZILIZO DHAHIRI (alizokataa kuzifuata) NA ANAYEHUIKA (yaani anyeufuata Uislamu) AHUIKE KWA DALILI DHAHIRI. NA HAKIKA ALLAH NI MWENYE KUSIKIA MWENYE KUJUA”. [8:41-42]

 

SHETANI APATA UPENYO KATIKA NYOYO ZA BAADHI YA WAISLAMU.

Hapa sasa ndipo shetani-mlaaniwa-alipopata upenyo akaziingia baadhi ya nyoyo za watu dhaifu wa imani.

Akaanza kuwasawirishia udogo (uchache wa idadi yao) na silaha duni walizonazo pamoja na maandalizi dhaifu.

Akawasawirishia Makurayshi walivyotoka na nia ya vita, wakiwa wengi na zana nyingi na bora za vita.

Wakawaweka mbele ya jeshi wakati wa kutoka watukufu wao kama dalili na ishara ya kuwakinaisha waumini kwamba wao wamejiandaa kwa vita virefu.

Shetani akazidi kuwasawirishia, akawanong’oneza mioyoni mwao, haya mnafikiri natija itakuwa nini yatakapokutana majeshi mawili haya?!

Jeshi hili lenu limetoka bila ya maandalizi na jeshi la wenzenu lina maandalizi ya kutosha kabisa. Hapana shaka natija na matokeo ya kukutana kwa majeshi mawili haya yako wazi kwamba nyinyi mtashindwa tu na si vinginevyo.

Hivi ndivyo shetani alivyopenya na kuingia katika nyoyo za waislamu waliokuwa madhaifu wa imani.

Sehemu waliyopiga kambi waislamu ilikuwa mbali na maji, hapo walipokuwa na yalipo maji kulikuwa na tambarare ya mchanga ambayo miguu huzama ndani yake mtu atembeapo.

Waislamu wakaishiwa na akiba ya maji waliyokuwa nayo, wakapatwa na kiu kikali kabisa kiasi cha kushindwa kustahamili tena.

Walikuwa katika hali ngumu sana, hawana maji ya kunywa wala ya kujitwaharishia ili wapate kuswali na wakati huo bado kulikuwa hakuna rukhsa ya kutayamamu.

Hali hii ngumu ikampa shetani upenyo mwingine, akaanza kuwatia wasiwasi waislamu na akatia chuki mioyoni mwao.

Na akawatishia kufa kwa kiu kabla hawajafyekwa na Makurayshi na  wengine kuchukuliwa mateka na kufanywa watumwa na adui.

Ni vema tukakumbuka kwamba maji jangwani ni asili ya uhai mbali ya kuwa yanaweza kutumika kama silaha ya ushindi dhidi ya adui.

Jeshi linalokosa maji jangwani hupoteza nguvu zake kabla ya kupoteza uhai wake. Nyoyo zinazoingia mapambanoni katika hali na mazingira kama haya huingiwa na kiwewe na kizaizai kikubwa.

MSAADA WA MBINGUNI.

Katika hali ya mkanganyiko na kukata tamaa, ndipo ulipokuja msaada kutoka mbinguni. Allah Mola Muweza akateremsha mvua, waislamu wakanywa na kujitwaharisha, wakajaza maji vyombo vyao na kuwanywesha wanyama wao.

Mchanga ukashikamana, miguu yao ikathibiti katika ardhi baada ya kuwa ilikuwa inazama na wakaweza kutembea na kwenda bila ya taabu kama mwanzo.

Waislamu wakastarehe na kupumzika kutokana na hali ya shida iliyowasibu, ukawapata usingizi wakalala. Hawakuzinduka kutoka usingizini mwao ila na hali yao ikawa imebadilika, khofu yao ikawa ni amani na wasiwasi wao ukageuka kuwa utulivu.

Uoga wao ukabadilika na kuwa ujasiri na uthabiti, tahamaki wakawa ni watu wengine kabisa sivyo kama walivyokuwa punde tu. Allah Karimu anaizungumzia hali hii ndani ya Qur-ani Tukufu, hebu na tumtegee sikio:

“(Kumbukeni) ALIPOKULETEENI USINGIZI ULIOKUWA (alama ya) SALAMA ITOKAYO KWAKE, NA AKAKUTEREMSHIENI MAJI MAWINGUNI ILI KUKUTWAHARISHENI KWAYO NA KUKUONDOLEENI UCHAFU WA SHETANI NA KUZIPA NGUVU NYOYO ZENU NA KUITHUBUTISHA MIGUU YENU CHINI (isiwe inazamazama mchangani)”. [8:11]

 

MTUME WA ALLAH AFICHA DHAMIRA YAKE

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasonga mbele na maswahaba wake mpaka akafika katika bonde la Badri.

Hapo akapiga kambi kando ya bonde lililo karibu na Madinah.

Bwana Mtume alikuwa katika hadhari kuu, akalifanya suala na makusudio yake kuwa ni siri kubwa.

Alifanya hivyo ili khabari isije kuvuja na kuwafikia wanafiki na majasusi wa Makurayshi.

 Alifanya hivi ili kuficha mikakati na muelekeo wake, hiyo ikiwa ni mojawapo ya mbinu za vita.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *