ZISHUKURU NEEMA ZA ALLAH

Ndugu yetu katika imani-Allah azithibitishe imani zetu-kwa mara nyingine tena tunamshukuru Allah kwa kutukutanisha tena katika ukumbi wetu huu wa wasia maridhawa.

Leo kwa mapenzi ya imani ninakuusia kuzishukuru neema za Allah alizotuneemesha bure. Yatupasa kufahamu kuwa kushukuru neema ni katika jumla ya makamu matukufu na daraja za juu.

Hivi ndivyo Allah Mola Mtukufu anavyotuambia kuhusiana na suala zima la shukrani ya neema, haya na tuzingatie pamoja:

“KULENI KATIKA VILE ALIVYOKUPENI ALLAH, VILIVYO HALALI NA VIZURI. NA SHUKURUNI NEEMA ZA ALLAH, IKIWA KWELI MNAMUABUDU YEYE”. [16:114]

Mpenzi ndugu yangu-Allah atuhidi-ikiwa tutaitafakari aya hii, basi tutambua kwamba:-

i.                    Vyote tulivyo navyo ambavyo pengine hutusahaulisha tukaacha kumuabudu Mola wetu tumepewa na Allah. Kwa hivyo vyote ni mali na milki yake ambayo:

  “…HIYO NI FADHILA YA ALLAH, HUMPA AMTAKAYE. NA ALLAH NI MWENYE FADHILA KUU (kabisa juu ya viumbe vyake)”. [57:21]

ii.                  Katika jumla ya alivyotupa Allah, viko ambavyo hivyo ni halali na vizuri na viko vile ambavyo ni haramu na vibaya.

    Tunatakiwa tule vile vilivyo halali na vizuri na tumshukuru Allah kwa neema zake hizo. Na tuache kuvikurubia vile vya haramu ambavyo tukiwafikiwa kuchunguza tutatoka na natija kuwa ni vibaya vyenye madhara na si vingine.

i.                    Kumshukuru Allah Mruzukuji kwa neema zake ni kielelezo tosha kuwa tunamuabudu na ni sehemu ya ibada isiyo na shaka.

Haya baada ya tafakuri hii ya pamoja na tuendelee kuiangalia shukrani ya neema za Allah ndani ya Qur-ani Tukufu, tusome kwa mazingatio:

“…KULENI KATIKA RIZIKI YA MOLA WENU NA MUMUSHUKURU…” [34:15]  Qur-ani inazidi kutupa khabari za shukrani, haya tusome na tuwaidhike:

“….(Tukawaambia) FANYENI (amali nzuri), ENYI WATU WA DAUDI KWA KUSHUKURU (neema mlizopewa). NA NI WACHACHE WANAOSHUKURU KATIKA WAJA WANGU”. [34:13]

Ndugu yangu mpenzi-Allah atuwafikishe kupendana kwa ajili yake-aya inatufahamisha pamoja na mambo mengine kwamba:-

ii.                  Kuishukuru neema ya Allah ni kutenda amali njema ambazo faida na manufaa yake huturejea sisi wenyewe bila ya kumzidishia Mruzukuji cho chote.

iii.                Kumbe wanaomshukuru Mola wao kwa neema alizowapa ni wachache, basi tujitahidi kuwa miongoni mwa wachache hao kwa fadhila zake Allah.

Tuelewe na tuyakinishe kuwa tunapomshukuru Mola wetu kwa neema zake alizotupa kwa kutenda amali njema zimridhishazo.

Shukrani zetu hizi haziruki patupu bali tuna jazaa maridhawa kwa Mola wetu. Hivyo ndivyo Qur-ani Tukufu; kitabu kisicho na shaka inavyotuambia, haya tusome na kusadiki:

“…NA ALLAH ATAWALIPA WANAOMSHUKURU”. [3:144]

Ni kheri kwetu ikiwa tutambua kwamba asili ya shukrani ni mja kujua kuwa neema zote alizonazo za dhahiri na zile za batini zinatoka kwa Allah.

Na kwamba hakupewa kwa kuwa anastahiki bali ni kutokana na fadhila na ihsani ya Allah tu. Mja akiukiri ukweli huu usiokufurika (usiopingika) utamuongozea katika kuzishukuru neema hizo za Mola wake.

Pia tutambue kuwa ni sehemu ya shukrani kufurahikia kuwepo kwa neema za Allah juu ya waja wake.

Furaha hii iwe ni kwa kuzingatia kuwa neema hizo ni wasila (njia na msaada) katika kutenda amali za twaa na kupatia ukuruba wa Allah.

Shukrani haikomelei hapo katika kuzifurahikia neema, bali pia kukithirisha kumuhimidi Allah na kumsifia kwa neema hizo ni katika namna ya shukrani.

Hali kadhalika haipungui kuwa ni shukrani kumtii Allah kupitia msaada wa neema zake na kuzitumia neema hizo kwa namna airidhiayo na kuipenda.

Kufanya hivi ndio upeo na ukomo wa shukrani. Ni katika kuonyesha shukrani zetu juu ya neema za Allah kutokuwa na kibri kwa sababu tu ya neema tulizoneemeshwa nazo.

Na ambazo kwa hakika hatuzimiliki na ndio maana tukifa tunaziacha hapa hapa kama tulivyozikuta wakati wa kuzawa kwetu.

Kutokujifakharisha na kujivuna kwa waja wa Allah kwa sababu ya neema za Allah na kutokuzifanyia fisadi neema hizo, hivi ndivyo Qur-ani Tukufu inavyotunasihi:

“NA UTAFUTE KWA YALE ALIYOKUPA ALLAH MAKAZI MAZURI YA AKHERA, WALA USISAHAU SEHEMU YAKO YA DUNIA NA UFANYE WEMA KAMA ALIVYOKUFANYIA. WALA USITAFUTE KUFANYA UFISADI KATIKA NCHI, BILA SHAKA ALLAH HAWAPENDI MAFISADI”. [28:77]

Haiachi kuwa ni sehemu ya shukrani kutokuruka mipaka ya Allah na kuzidi katika jeuri na kuwafanyia uadui waja wake Allah Mtoaji bure neema hizo zikupazo jeuri.

Ndugu yangu katika Allah-Allah ayazidishe mapenzi yetu-elewa kuwa ye yote mwenye kuacha kumtii Allah, mwenye kuwa na kibri, mwenye kujifakharisha na kujivuna.

Mwenye kufanya fisadi na jeuri, mwenye kuchupa mipaka na kuwafanyia uadui waja wa Allah. Akayafanya yote haya kwa sababu tu ya neema alizoruzukiwa na Allah, huyu bila ya shaka yo yote atakuwa amezikufuru (amezikanusha) neema za Allah na wala hazishukuru kwa anavyopaswa.

Tuelewe bayana kuwa kitendo cha kuzikufuru neema za Allah ni sababu tosha ya kupokonywa neema hizo, na ziada ya hayo ni kuzibadili  kuwa nakama (adhabu na mateso). Hebu na tuitafakari pamoja kauli hii ya Allah Mola Mtukufu:

“HAYO (ya kuwafika balaa hizi) NI KWA SABABU ALLAH HABADILISHI KABISA NEEMA ALIZOWANEEMESHA WATU, HATA WABADILISHE WAO YALIYOMO NYOYONI MWAO (wende nyendo mbaya ndipo Allah awaondoshee neema yao)…” [8:53]

Na kitendo cha kuzishukuru neema za Allah hakimaanishi ila kumzidishia mwenye kushukuru ziada ya neema. Hii ndio ahadi ya Allah anayowatangazia waja wake, haya na tuipokee kwa mikono miwili:

“NA (kumbukeni) ALIPOTANGAZA MOLA WENU (kuwa) KAMA MKISHUKURU NITAKUZIDISHIENI NA KAMA MKIKUFURU (jueni) ADHABU YANGU NI KALI SANA”. [14:7]

Mpenzi ndugu katika imani, yatakikana tufahamu kwamba ni sehemu ya shukrani kuiona kubwa neema hata kama ni ndogo na duni machoni mwako au kwa mtazamo wako.

Wewe usiangalie udogo au uduni wa neema bali uangalie ukubwa na utukufu wa Mneemeshaji wa neema hiyo unayoidogesha na kuidunisha.

Kisha utambue kuwa Allah ana neema adida kwa waja wake zisizodhibitika.

Mja kama kiumbe dhaifu hawezi kuzidhibiti zote akazesha seuze kuzishukuru imuwajibikiavyo. Allah anatuambia ndani ya Qur-ani yake aliyotushushia ili iwe muongozo kwetu, haya na tumsikilize:

“NA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH HAMTAWEZA KUZIHISABU…” [16:18]

Yampasa mwanadamu asimuangalie mtu aliyemzidi kineema kwa jicho la kupata kama yeye au kumzidi.

Hii ni kwa sababu hili linaweza kumpelekea kuitweza na kuidharau neema hiyo ya Allah aliyomneemesha kwa kuilinganisha na ile aliyopewa mwenziwe aliyemzidi.

Dharau na twezo hili litamfanya asiishukuru neema hiyo aliyopewa yeye na ikawa ni sababu ya kupokonywa neema hiyo anayoidharau.

Natija ikawa hakupata kingi mithili ya alichopewa mwenziwe kwa hekima azijuazo Mpaji Mneemeshaji. Na kuondokewa na kile kidogo alichopewa kwa sababu ya kutokumshukuru Mola wake kwa kidogo hicho alichompa bila ya kujaza fomu ya maombi.

Tuelewe na tukiri kuwa Allah amewafadhilisha katika neema zake baadhi ya waja wake kuliko wengine kwa sababu, hekima na siri anazozijua yeye mwenyewe:

“TAZAMA JINSI TULIVYOWAFADHILISHA (hapa duniani) BAADHI YAO (viumbe) KULIKO WENGINE; NA BILA SHAKA AKHERA NI YENYE VYEO VIKUBWA ZAIDI NA VYENYE KUFADHILIANA ZAIDI (pia)” [17:21]

Na hakuna yo yote katika viumbe wake mwenye haki ya kuhoji ugawaji wake wa neema na fadhila zake kwa waja wake.

Kwa hali hii basi, linalomuelea mja ni kuridhia mgao wa Mola wake na kisha kumshukuru kwa fungu alilomgawia miongoni mwa neema zake. Na amuombe ziada ya fadhila na neema zake huku akiamini kuwa:

“…HAZINA ZA MBINGU NA ARDHI NI MALI ZA ALLAH…” [63:7]

Na aamini kuwa Allah hutenda alitakalo na ni Muweza juu ya kila kitu. Haya na tuukhitimishe wasia wetu huu kwa kumuomba Allah kama alivyoombwa na Mtume Sulayman-Amani imshukie:

EE MOLA WANGU! NIPE NGUVU NISHUKURU NEEMA YAKO ULIYONINEEMESHA MIMI NA WAZAZI WANGU, NA NIPATE KUFANYA VITENDO VIZURI UVIPENDAVYO, NA UNIINGIZE KWA REHEMA YAKO KATIKA WAJA WAKO WEMA”. [27:19]

 

ZISHUKURU NEEMA ZA ALLAH

Ndugu yetu katika imani-Allah azithibitishe imani zetu-kwa mara nyingine tena tunamshukuru Allah kwa kutukutanisha tena katika ukumbi wetu huu wa wasia maridhawa.

Leo kwa mapenzi ya imani ninakuusia kuzishukuru neema za Allah alizotuneemesha bure. Yatupasa kufahamu kuwa kushukuru neema ni katika jumla ya makamu matukufu na daraja za juu.

Hivi ndivyo Allah Mola Mtukufu anavyotuambia kuhusiana na suala zima la shukrani ya neema, haya na tuzingatie pamoja:

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *