Jueni na eleweni enyi ndugu zanguni Waislamu kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia mafanikio ya duniani ni ya muda mfupi, yenye kwisha na kuondoka, na mafanikio ya akhera ndiyo yenye kusalia/kubakia milele.
Haya mafanikio ya kudumu, hayapatikani ila kwa kupitia barabara ngumu ya “TAQ-WA” kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii na kumfuata Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie-.
Katika jumla ya nguzo kuu za Taqwa ni kuufunga huu mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao Allah ameujaalia kuwa ni REHMA kwa viumbe.
Nao kama mjuavyo ndio mwezi ambao imeteremshwa ndani yake Qur-ani Tukufu ikiwa ni muongozo kwa watu wote.
Muongozo uliosheheni hoja wazi za uongofu na upambanuzi baina ya haki na batili. Ramadhani pia ni mwezi ambao hufunguliwa ndani yake milango ya pepo na kufungwa milango ya moto.
Ni kwa kuuzingatia umuhimu na nafasi ya mwezi wa Ramadhani, ndipo Bwana Mtume akaitoa Khutba yake tukufu, khutba ya kihistoria, khutba kongwe katika kuupokea na kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Imepokelewa na Salmaan Alfaarisy – Allah amuwie Radhi – amesema : Alitukhutubia Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – katika siku ya mwisho ya mwezi wa Shaabani, akasema :
“Enyi watu, umekufikieni mwezi mtukufu wenye baraka. Ndani ya mwezi huu umo usiku wa LAYLATIL QADRI usiku ambao ni bora kuliko miezi alfu moja. Mwenyezi Mungu amejaalia funga ya mwezi huu kuwa ni FARADHI na kisimamo (cha ibada) cha usiku wake kuwa ni SUNA. Atakayejikurubisha (kwa Mola wake) ndani ya mwezi huu kwa (kutenda) jambo lolote la kheri, (malipo, jazaa yake) itakuwa ni kama mtu aliyetekeleza fardhi katika miezi mingine. Na atakayetekeleza fardhi katika mwezi huu, atakuwa ni kama mtu aliyetekeleza fardhi sabini katika miezi mingine. Na mwezi huu ni mwezi wa SUBIRA, nao ni mwezi ambao mwanzo wake ni REHEMA na katikati yake ni MAGHFIRA/MSAMAHA WA ALLAH na mwisho wake ni KUACHWA HURU NA ADHABU YA MOTO. Yeyote atakayemfuturisha mfungaji ndani ya mwezi huu, (ujira wa futari hiyo) utakuwa ni maghfira ya madhambi yake (mfuturishaji) na kuachwa huru na adhabu ya moto na atapata ujira kama aupatao mfungaji bila ya kupungua chochote katika ujira/thawabu zake (mfungaji)”. Tukasema :
Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sio sote tunaweza kupata (kitu) cha kumfuturisha huyo mfungaji. (Mtume) akawajibu :
“Mwenyezi Mungu humpa thawabu hizi yule atakayemfuturisha mfungaji ndani ya mwezi huu kwa onjo/funda ya maziwa au (kokwa ya) tende au funda ya maji. Na atakayemshibisha ndani ya mwezi huu mfungaji, itakuwa ujira (wa shibe hiyo) ni maghufira ya madhambi yake (mshibishaji) na Mola wake atamnywesha katika hodhi (birika) langu funda moja ambayo hatopata kiu baada yake kabisa. Na atakuwa na ujira kama aupatao mfungaji bila ya kupungua chochote katika ujira wake (mfungaji). Na atakayempunguzia kazi mtumishi/mfanyakazi wake ndani ya mwezi huu, Mwenyezi Mungu atamghufiria madhambi yake na kumuacha huru na adhabu ya moto. Basi kithirisheni sana ndani ya mwezi huu mambo manne. Mtamridhisha Mola wenu kwa kutenda mambo mawili kati ya manne hayo; na mambo mawili hamjikwasii (hamna budi) nayo. Ama hayo mambo mawili mtakayoridhisha nayo Mola wenu ni shahada (kushuhudia kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila ALLAH) na mumtake maghfira. Na ama yale mambo mawili msiyojikwasia nayo ni mumuombe Mola wenu pepo na mjilinde/mjikinge kwake na (adhabu) ya moto”. Ibn Khuzaymah katika sahihi yake.
MAELEZO :
Ikiwa tunafuatana pamoja, tunaweza tukaigawa hadithi hii tukufu ambayo ni khutba kongwe iliyo hai hadi leo na itaendelea kuwa hai mpaka mwisho wa dunia.
Khutba hii iliyotolewa na Khatibu mahiri, Bwana Mtume katika kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, inagawanyika katika sehemu kuu tatu au tuseme ina vipengele vikuu vitatu.
Ukiizingatia hadithi utakuta mwanzo wa khutba yake, Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anawafahamisha maswahaba na umma mzima juu ya utukufu, ubora, cheo na nafasi ya mwezi wa Ramadhani. Kuna hekima/falsafa gani ndani ya maelezo haya ?
Mtume anauelezea mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa namna gani ili muislamu aujue, kwani waswahili husema asiyekujua hakuthamini.
Akishaujua atauthamini na kuupa hadhi yake unayostahili. Kuuthamini na kuupa heshima mwezi wa Ramdhani ni kuzidisha sana TWAA kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya namna mbali mbali za ibada na mambo mengine ya kheri.
Sehemu ya pili ya hadithi, Bwana Mtume anataja fadhila/faida na ubora wa mwezi wa mtukufu wa Ramadhani na kuwa ibada yeyote inayofanywa ndani ya mwezi huu hailingani kithawabu/kiujira na ile ibada inayofanywa katika miezi mingine.
Kwa hiyo basi, Ramadhani ni ndio musimu wako wa ibada. Kadhalika Bwana Mtume anatuelezea malipo na thawabu adhimu anazozipata mja mwenye kumfuturisha nduguye muislamu katika mwezi huu wa Ramadhani.
Hapa Bwana Mtume anaashiria moyo wa ukarimu na upendo utakiwao waislamu wajipambe na kuwa nao.
Kwani waislamu wakipendana watakuwa ni wamoja na mshikamano, na wakishikamana watautawala ulimwengu na hapatakuwa na nguvu ya kuwashinda, si magharibi wala mashariki.
Kisha ndipo Bwana Mtume akaikhitimisha khutuba yake kwa kutoa wito muhimu kwa waislamu.
Akawataka wakithithirishe sana kumpwekesha Mola wao kwa kuleta kalima ya shahada na wamtake sana maghfira.
Hali kadhalika akawataka waislamu wakithirishe mno kumuomba Mola wao pepo na wamuombe awakinge na moto wa jahanamu.
Ili kuutekeleza wito huu ndipo wanazuoni wetu wema -Allah awarehemu- wakatuwekea uradi uletwao msikitini ndani ya mwezi wa Ramadhani. Chimbuko la uradi huu ni ile sehemu ya mwisho ya hadithi. Uradi wenyewe ni huu :
ASH-HADU AN LAA ILAHA ILLA-LLAHU NASTAGHFIRULLAH, NAS-ALUKAL-JANNATA WANA’UDHU BIKA MINAN-NAAR ALLAHUMMA INNAKA AFUWWUN, TUHIBBUL-AFWA FA’FU ‘ANNAA YAA KARIIM
Tunashuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah, Tunakuomba maghfira (msamaha wa madhambi) Ewe Allah, Tunakuomba pepo na tunajikinga kwako na moto, Ewe Allah, wewe mimi ni msamehevu na unapenda msamaha, basi tusamehe Ewe KARIMU.
Haya shime ndugu zanguni waislamu, tukithirishe kuuleta uradi huu ndani ya mwezi wa mavuno; mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeuitikia wito wa Bwana Mtume kwa maslahi na faida yetu wenyewe.
TUNDA LA RAMADHANI :
Karibu ndugu yangu muislamu katika bustani ya Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie – uchume utakavyo na kula kiasi chako matunda matamu, mazuri yasiyokwisha hamu; matunda ya Ramadhani.
Ili ufaidike na kunufaika na matunda haya unatakiwa uingie ndani ya bustani hii tukufu kwa unyenyekevu, utulivu, adabu, heshima na usikivu.
TUNDA LA KWANZA – DUA YA KUFUTURU
Amepokea Ibn Majah kutokana na hadithi ya Abdillah Ibn Amri (amesema Mtume) :
YUNA MFUNGAJI WAKATI WA KUFUTURU KWAKE DUA ISIYOREJESHWA (yenye kujibiwa bila ya kipingamizi)”. Ni kwa sababu hiyo ndiyo Mtume alikuwa akisema (wakati wa kufuturu) :
[ALLAHUMMA INNIY LAKA SWUMTU WA’ALAA RIZQIKA AFTWARTU FAGH-FIRLIY MAA QADDAMTU WA MAA AKHARTU DHAHABAD-DHWAMAU WABTALLIT-‘URUQU WATHABATAL AJRU IN-SHAALLAHU TAALA]
Maana yake :
“Ewe Mola wa haki ni kwa ajili yako tu nimefunga na nimefuturu kwa riziki yako. Basi (nakuomba) unisamehe dhambi zangu zilizotangulia na zijazo. Kiu kimeondoka na mishipa imelowana na ujira umethibiti pindipo atakapo Mwenyezi Mungu Mtukufu”
Haya shime ndugu zanguni waislamu, tumuige Mtume wetu katika hili na mengineyo ili tutengenekewe duniani na akhera. Usikubali kuipoteza fursa hii adimu ya kukubaliwa duao, omba na Mola Karimu atakupa.
TUNDA LA PILI : FADHILA ZA KUHARAKIA KUFUTURU:
Imepokelewa hadithi kutoka kwa Abuu Hurayrah – Allah amuwie Radhi – amesema, Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie-
“AMESEMA MWENYEZI MUNGU : HAKIKA WAJA WANGU WAPENDEZAO SANA KWANGU NI WALE WAHARIKIAO KUFUTURU” Ahmad na Tirmidhi.
MAELEZO :
Ni vema mtu akafanya haraka kufuturu, maadam ana uhakika wa kutua/kuzama kwa jua.
Ikiwa hana uhakika, basi ni vema akasubiri adhana ili asije akafuturu kabla ya muda. Haya zingatia upendwe na Mola wako