Ewe ndugu yangu mpenzi katika imani-Allah akurehemu-ninakuusia bila ya kuisahau nafsi yangu kwamba usipende mali na cheo.
Fahamu na uelewe kwamba kupenda cheo na mali ni miongoni mwa majanga makubwa ikiwa havikutimiziwa haki yake.
Kwani cheo na mali ni amana na dhima iliyo mabegani mwako. Kutokana na uzito wa amana hii na ukubwa wa majukumu yake, ndio kukawa kupenda mno mali na cheo ni jambo lililokaripiwa na kukemewa sana. Allah Mola Mwenyezi anatuambia:
“HIYO NYUMBA YA AKHERA TUTAWAFANYIA WALE WASIOTAKA KUJITUKUZA (cheo) KATIKA ARDHI WALA (kufanya) UFISADI, NA MWISHO (mwema) UTAWATHUBUTIKIA WACHA-MUNGU”. [28:23] Mola wetu akazidi kutuambia: “ENYI MLIOAMINI! YASIKUSAHAULISHENI MALI YENU WALA WATOTO WENU KUMKUMBUKA ALLAH. NA WAFANYAO HAYO, HAO NDIO WENYE KUKHASIRIKA”. [63:9]
Akatuambia tena:
“BILA SHAKA MALI ZENU NA WATOTO WENU NI JARIBIO (kwenu, mtihani kutazama mtakhalifu amri za Allah kwa ajili yao au mtafuata amri zake). NA KWA ALLAH KUNA UJIRA MKUBWA KABISA”. [64:15]
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anatuasa juu ya suala zima la kupenda mno mali na cheo, anasema:
“Hawakuwa mbwa mwitu wawili wenye njaa walioachiwa katika kundi (zizi) la mbuzi na kondoo. Ni wenye kufanya fisadi (uharibifu) mkubwa zaidi katika kundi hilo kuliko fisadi ya kupenda mali na utukufu (ukubwa/cheo) katika dini ya mtu muislamu”.
Maana ya kauli hii ya Mtume wa Allah ni kwamba mapenzi ya mali na cheo.
Yanaifisidi na kuiharibu dini ya mwenye vitu hivyo zaidi kuliko fisadi inayoweza kufanywa na mbwa mwitu wenye njaa kali katika kundi la wanambuzi na kondoo.
Kwa hivyo, elewa na ufahamu ewe ndugu yangu ya kwamba mtu atakayepupia mno kupenda cheo na kutafuta utukufu na ukubwa katika nyoyo za watu.
Huyu kwa mwenendo na tabia yake hii huwa amejitia mwenyewe majangani.
Hawezi kuyaepa maafa ya jeuri/kibri kitokanacho na mali, ria (kujiona na kujigamba), kujipamba na sifa asizokuwa nazo na kuacha kuinyenyekea haki na wenye haki. Na mithili ya haya miongoni mwa mabalaa mengineyo.
Jua ewe ndugu yangu kwamba muislamu kama mwanadamu mwingine ye yote hakatazwi kuwa na mali au cheo au kujijenga kimaisha, dhana hii si sehemu ya mafundisho sahihi ya Uislamu.
Sasa basi, ikiwa hivi ndivyo ni kwa nini basi mali na cheo vikashtumiwa na kusemwa sana katika Uislamu?
Ikiwa hili ndilo swali linaloweza kuzigubika fikra na mawazo yako, basi ninakuambia na kukuomba unitegee sikio la usikivu.
Ninasema kinachoshtumiwa na kukaripiwa ni kuipenda mali au cheo kupindukia, kiasi cha kumfanya mtu kuvitafuta kwa gharama na njia yo yote ile.
Iwe ni kwa kumtoa mwanadamu mwenziwe kafara, kudhulumu au kunyang’anya, yote haya mtu yu tayari kuyafanya muradi tu apate cheo au mali.
Cheo na mali hii vikamuweka mbali na Allah jambo ambalo ndilo lengo mama la kuumbwa kwake na kuletwa katika ulimwengu huu. Hawa ndio watu wanaoambiwa na Allah:
“KUMEKUGHAFILISHENI KUTAFUTA WINGI (wa mali, jaha {cheo} na watoto na kujifakharisha kwa hayo). HATA MUMEINGIA MAKABURINI (mumekufa kabla ya kufanya kheri yo yote). SIVYO HIVYO! KARIBUNI HIVI MTAJUA (kuwa sivyo hivyo). KISHA (nasema) SIVYO HIVYO! KARIBUNI HIVI MTAJUA (kuwa sivyo hivyo). SIVYO HIVYO! LAU KAMA MNAJUA UJUZI WA YAKINI (kuwa sivyo hivyo msingefanya hivyo). HAKIKA MTAUONA MOTO. KISHA (nasema) MTAUONA KWA YAKINI (moto). KISHA KWA HAKIKA MTAULIZWA SIKU HIYO JUU YA NEEMA (mlizopewa mlizitumiaje”. [102:1-8]
Ni ukweli usiopingika kwamba wengi miongoni mwa wenye mali na vyeo wako mbali kabisa na Allah Mola Muumba wao, hawana khabari nae hata kidogo.
Na kwa wanadamu wenziwao wamejawa na viburi, dharau na udhalilishaji ila wale ambao Allah amewafunika na rehema zake.
Hii ndio mali na hicho ndicho cheo kinachosemwa vibaya na kukaripiwa na Uislamu, fahamu na elewa hivi.
Ama mtu atakayetafuta cheo au mali kwa nia njema tu, akaitaka mali ili imsaidie kuipata akhera kutokana na kuitumia kwake katika mambo ya kheri na wema.
Kwa ajili ya kuilinda dini na nafsi yake dhidi ya uadui wa madhalimu na kwa ajili ya kuwasaidia watu.
Na mali hiyo ikamfanya asimsahau Mola wake, bali ikazidi kumsogeza karibu nae kwa kumuabudu na kumshukuru kwa neema alizomneemesha.
Mali kama hii si vibaya wala dhambi mtu kuimiliki huku akitambua kuwa mali hiyo ni mtihani kwake na hesabu yake kesho mbele ya Mola wake ni nzito na ngumu:
“MALI NA WATOTO NI PAMBO LA MAISHA YA DUNIA. NA VITENDO VIZURI VIBAKIAVYO NDIVYO BORA MBELE YA MOLA WAKO KWA MALIPO NA TUMAINI BORA (kuliko hayo mali na watoto”. [18:46]
Huku akijikumbusha na mtihani wa mali uliompata Qaarun na mwisho wake ulivyokuwa kama inavyosimulia Qur-ani Tukufu na tuitegee sikio la kuwaidhika:
“HAKIKA QAARUN ALIKUWA KATIKA WATU WA MUSA, LAKINI ALIWAFANYIA DHULMA. NA TULIMPA KHAZINA AMBAZO FUNGUO ZAKE ZINAWATOPEZA WATU WENYE NGUVU (kuzichukua). WALIMWAMBIA WATU WAKE: USIJIONE (usijigambe) HAKIKA ALLAH HAWAPENDI WANAOJIONA. NA UTAFUTE KWA YALE ALIYOKUPA ALLAH MAKAZI MAZURI YA AKHERA, WALA USISAHAU SEHEMU YAKO YA DUNIA, NA UFANYE WEMA KAMA ALLAH ALIVYOKUFANYIA, WALA USITAFUTE KUFANYA UFISADI KATIKA NCHI, BILA SHAKA ALLAH HAWAPENDI MAFISADI. AKASEMA: HAKIKA NIMEPEWA HAYA KWA SABABU YA ILIMU NILIYONAYO. JE, HAKUJUA KWAMBA ALLAH AMEWAANGAMIZA KABLA YAKE WATU WALIOKUWA WENYE NGUVU ZAIDI KULIKO YEYE NA WENYE MKUSANYO MWINGI ZAIDI (wa mali kuliko wake yeye)? NA WABAYA HAWATAULIZWA MAKOSA YAO (Allah mwenyewe anayajua yote). BASI AKAWATOKEA WATU WAKE KATIKA PAMBO LAKE. WAKASEMA WALE WANAOTAKA MAISHA YA DUNIA: LAITI TUNGELIPATA KAMA ALIYOPEWA QAARUN, HAKIKA YEYE NI MWENYE BAHATI KUBWA. NA WAKASEMA WALE WALIOPEWA ILIMU: OLE WENU! MALIPO YA ALLAH NI MAZURI KWA YULE ANAYEAMINI NA KUFANYA VITENDO VIZURI (kuliko aliyonayo huyu Qaarun) WALA HAWATAPEWA HAYO ISIPOKUWA WAFANYAO SUBIRA. BASI TUKAMDIDIMIZA YEYE (Qaarun) NA NYUMBA YAKE ARDHINI, WALA HAPAKUWA NA KUNDI LO LOTE LA KUMSAIDIA KINYUME NA ALLAH, WALA HAKUWA MIONGONI MWA WALE WALIOWEZA KUJISAIDIA. NA WAKAWA WANASEMA WALE WALIOTAMANI CHEO CHAKE JANA: E-E-E- (kweli) ALLAH HUMZIDISHIA RIZIKI AMTAKAYE MIONGONI MWA WAJA WAKE (na hali ya kuwa mbaya, hampendi). NA HUDHIKISHA (riziki ya anayemtaka), ASINGETUFANYIA HISANI ALLAH BILA SHAKA ANGETUDIDIMIZA (kama alivyomdidimiza kwani sisi tuliitamani hali yake) O! KWELI HAWAFUZU MAKAFIRI”. [28:76-82]