HAKI ZA WATOTO

Ni vema ikaeleweka kwamba tunapozungumza kuhusu watoto, tunazikusudia jinsia zote mbili. Yaani watoto wa kiume sambamba na wale wa kike.

Katika Uislamu hakuna chembe ya ubaguzi, watoto wote wana haki sawa kwa wazazi wao kwa mujibu wa sheria.

Watoto wamepewa haki nyingi na Uislamu, kubwa kuliko zote ni haki ya malezi. Wazazi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata malezi bora.

Malezi ambayo yatawaandaa kimwili na kiroho. Wapate elimu itakayowapa ufahamu wa kutosha juu ya ulimwengu wao, wakaweza kuyafurahia maisha ulimwenguni humu.

Sambamba na malezi haya yatakayo wahakikishia maisha bora, watoto wana haki ya kupata malezi ya kiroho. Ili kuwafanya waendelee kuwa binadamu wenye ubinadamu na utu.

Ipandwe mbegu njema ya imani na tabia njema ndani ya nafsi zao. Kuhusiana na hili tunasoma:

“ENYI MLIOAMINI! JIOKOENI NAFSI ZENU NA WATU WENU, NA MOTO AMBAO KUNI ZAKE NI WATU NA MAWE…” [66:6]

Ni dhahiri kuwa wazazi hawatoweza kuwaokoa watu wao wa nyumbani (familia) na adhabu ya moto kama wanavyotakiwa na Mola wao, ikiwa hawatowalea watoto wao kwa mujibu wa imani yao. Nae Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-analielezea jukumu hili la wazazi kupitia kauli yake hii:

“Nyote nyie ni wachunga na nyote mnawajibika (wenye kuulizwa) kwa wachungwa (mliopewa kuwachunga) wenu. Mwanamume ni mchunga kwa watu wake wa nyumbani na ataulizwa juu ya wachungwa wake (aliwachungaje)”. Bukhaariy & Muslim

Kutokana na kauli ile ya Allah na kauli hii ya Bwana Mtume, utaona kuwa watoto ni amana iliyomo shingoni mwa wazazi.

Na kwamba siku ya Kiyama wataulizwa kuhusiana na amana hii waliyopewa. Ni kwa kuwapa watoto malezi ya kiroho (kidini) ndio wazazi wanaweza kujitoa katika dhima ya uchunga huu na hivyo kuwa na la kujibu mbele ya Mola wao.

Ni kwa malezi haya ndio watoto watatengenea na kuongoka na hapo ndipo watakapokuwa ni burudani/pozo la macho (nyoyo) ya wazazi, leo duniani na kesho akhera. Allah Mola Mwenyezi anatuambia ndani ya Qur-ani:

“NA WALE WALIOAMINI NA WAKAFUATWA NA VIZAZI VYAO NA WATOTO WAO KATIKA IMANI. TUTAWAKUTANISHA NA HAO JAMAA ZAO, WALA HATUTAWAPUNJA KITU KATIKA (thawabu za) VITENDO VYAO; KILA MTU ATALIPWA KWA KILA ALICHOKICHUMA”. [52:21]

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Anapokufa mja hukatika amali zake ila mambo matatu:

Sadaka yenye kuendelea, au

Elimu yenye kunufaisha baada yake, au

Mtoto mwema atakayemuombea Mungu”.

Muslim.

Haya ndio matunda ya kumlea mtoto malezi mema ya kiroho (kidini), malezi ambayo yatamfanya awe mtoto mwenye manufaa kwa wazazi wake hata baada ya mauti.

Leo ulimwengu unataabika na kupiga kelele kuwa watoto wa siku hizi hawana adabu na maadili yameporomoka.

Janga hili halitusibu kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na wazazi wengi kughafilika na jukumu lao la malezi na khasa malezi haya ya kiroho.

Wazazi hawajali na wala hawaulizi watoto wao wamekwenda wapi, wamerudi nyumbani saa ngapi. Wala hawajishughulishi kujua wanasuhubiana na nani kama marafiki na wenza.

Wazazi hawachukui taabu ya kuwaelekeza watoto wao lipi lifaalo kutendwa na kwa nini.

Na lipi lisilofaa kutendwa na kwa nini, bali huuachia ulimwengu kuwafanyia kazi hiyo.

Kwa kuupa ulimwengu jukumu si lake, ndio leo tumefika hapa tulipo.

Hali imekuwa mbaya kiasi ambacho mtoto anafikia hatua ya kumpiga mzazi wake. Hebu tujifunze kwa kumuiga mzazi/mlezi mwema kama tunavyoelezwa na Qur-ani:

“…KILA MARA ZAKARIA ALIPOINGIA CHUMBANI (kwake) ALIKUTA VYAKULA PAMOJA NAYE (huyo Maryamu). AKASEMA: EWE MARYAMU! UNAPATA WAPI HIVI? AKASEMA: HIVI VINATOKA KWA ALLAH NA ALLAH HUMRUZUKU AMTAKAYE BILA KUWAZA (mwenyewe)”. [3:37]

Huyu ndiye mlezi alijuaye vema jukumu na dhima yake ya ulezi. Leo wewe mzazi unafahamu fika kwamba binti yako hana kipato wala chumo lo lote, bado anakutegema wewe katika mahitaji yake yote.

Binti huyu anakuja nyumbani na nguo nzuri, viatu vya gharama, vitu vya dhahabu na simu ya mkononi. Wewe kimya unakodolea macho, humketishi chini ukamuuliza anakovipata.

 Unangojea mpaka siku moja atakapokuja na mtumbo ndio umfukuze nyumbani na kumkana kuwa sio mwanao! Kumbuka hajipigaye mwenyewe huwa halii. Jambo la kustaajabisha ni kuwa utawaona wazazi hawa wanaowanyima watoto wao haki yao ya msingi ya malezi, wanapupia kwa pupa zote suala la mali.

Wanatumia sehemu kubwa ya muda wao katika kuwekeza mali na kukesha katika kupanga mikakati ya kuiendeleza.

Ni ukweli usiopingika kwamba, ghalibu mali hii inayowapeleka mbio pengine huja kuifaidi watu wengine kabisa.

Wasio na uchungu nayo, washindwe hata kumtaja kwa wema na kumuombea Mungu. Ama watoto ambao ndio tumaini na tegemeo lake duniani na akhera, hawajali na wala hana muda wa kuhakikisha kuwa wanapata malezi ya kidini.

Mzazi ni vema ukakumbuka kwamba, kama ambavyo ni jukumu lako kuulea mwili wa mwanao kwa kumpa chakula, maji na nguo.

Ni vivyo hivyo imekuwajibikia kuulea moyo na roho ya mwanao kwa kumpa elimu kama chakula. Kumpandikizia imani ya kweli kama maji na kuivisha roho yake kwa vazi la taq-wa (ucha-Mungu):

“ENYI MLIOAMINI! HAKIKA TUMEKUTEREMSHIENI NGUO ZIFICHAZO TUPU ZENU NA NGUO ZA PAMBO, NA NGUO ZA UTAWA (yaani kucha Mungu) NDIZO BORA…” [7:26]

Na miongoni mwa haki za watoto zilizo katika dhima ya wazazi wao ni kuwapa huduma zote muhimu wanazozihitajia kwa ajili ya ustawi wao wa baadae.

Ni wajibu wako kama mzazi uliyejibebesha dhima ya ulezi, kuhakikisha kuwa mwanao anapata elimu itakayomsaidia kimwili na kiroho leo duniani na kesho akhera.

Anapata chakula bora cha kujenga, kutia nguvu na kuulinda mwili dhidi ya maradhi.

Chakula kitakacho dhamini afya njema ya kiwiliwili, akili na haiba. Anapata maji safi na salama ya kunywa, anapata nguo za heshima na sitara zinazoendana na majira aliyomo.

Anapata mahala pazuri na salama pa kulala, mahala ambapo patamuhakikishia mapumziko mazuri. Yatakayoupumzisha mwili na akili yake na hivyo kumfanya aamke kesho akiwa na nguvu na akili mpya.

Hii ni sehemu ya wajibu wako kwa mwanao, na kuutekeleza wajibu wako huu ni namna moja ya kuishukuru neema uliyoneemeshwa na Mola wako.

Neema ya watoto na neema ya mali. Ni sehemu ya wendawazimu kwa mtu aliyekunjuliwa riziki na Mola wake, kisha akafanya ubakhili katika kuwahudumia wanawe.

Elewa watoto wamepewa haki na sheria kuchukua sehemu ya mali yako kwa ajili ya kukidhi haja na mahitaji yao ya msingi.

Lakini bila ya kufanya israfu wala ubadhirifu. Hivi ndivyo alivyofutu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika kadhia (suala) ya Hind Bint Utbah, kama ilivyokuja katika riwaya ya Bukhaariy na Muslim.

Katika jumla ya haki za watoto ni kupata mapenzi sawa ya wazazi.

Mzazi asionyeshe kumpenda sana mtoto mmoja kuliko wengine, khasa anapokuwa ni baba mwenye zaidi ya mke mmoja.

Au ikawa anawapenda zaidi watoto wa kiume kuliko wale wa kike. Mapenzi haya yakamuongozea kumpa mtoto kipenzi zawadi na kuwanyima wale wengine.

Elewa ewe mzazi, hayo si mapenzi bali ni kuwagawa wanao na kuwajengea chuki baina yao. Kufanya hivi ni dhuluma na Allah hawapendi watu madhalimu.

Hutokea wazazi wengine wakampenda zaidi mtoto wao fulani na kumpa kila akitakacho. Pengine hata kumuandikia wasia kuwa wakifa apewe kitu fulani na kuwanyima wale wengine.

 Hufanya hivi eti kwa sababu mtoto fulani huyu ndiye anayewatii, kuwasikiliza, kuwahudumia na baki ya wema mwingine.

Wema wake mtoto fulani huyu hauwi mbele ya macho ya sheria ndio sababu inayompa haki zaidi kwenu wazazi kuliko nduguze.

Haya ni masuala mawili tofauti; suala la wajibu na suala la haki. Mtoto kuwatendea wema wazazi wake ni wajibu wake na ujira wake uko mbele ya Allah.

Na sio kupewa vitu vya wazazi na kuwanyima wale wengine. Imepokelewa kutoka kwa Nu’umaan Ibn Bashiyr-Allah awawiye radhi-kwamba baba yake (mzee) Bashiyr Ibn Sa’ad alimpa yeye (Nu’umaan) hiba ya kijana mtumishi. (Baba) akamueleza Mtume-Rehema na Amani zimshukie-khabari ile, Mtume akamuuliza:

“Je, umewapa watoto wako wote kama hivyo?” Akajibu: Hapana, (Mtume) akasema : “(Kama hukuwapa wote), basi irejeshe hiba yako”.

Na katika riwaya nyingine Mtume alisema (kumwambia Bashiyr): “Mcheni Allah na fanyeni uadilifu baina ya watoto wenu”.

Na katika tamko lingine alisema: “ Mshuhudize juu ya jambo hili mwingine, kwani mimi sishuhudii dhulma”. Bukhaariy & Muslim

Bwana Mtume anauita upendeleo kwa baadhi ya watoto kuwa ni DHULMA na dhulma ni HARAMU.

Lakini lau mzazi atampa mmoja wa wanawe kitu anachokihitaji na mwingine hakihitajii.

 Mathalan mtoto mmoja anahitaji vifaa nya shule, au tiba au kuoa, si UPENDELEO kumkidhia haja yake hiyo kwa sababu yule mwingine hahitajii kitu hicho wakati huo.

Mzazi atakapoutekeleza vema wajibu wake kwa wanawe kwa kuwapa malezi yale ya kimwili na kiroho.

Utekelezaji huu wa wajibu utawajengea watoto hisia na mazingira ya kuwatendea wema wazazi wao na kuchunga haki zao.

Kinyume chake, yaani mzazi atakapoacha kuutekeleza vema wajibu wake huo, itakuwa ni sababu itakayowapa watoto uhalali wa kuwatupa wazazi na kutowashughulikia watakapokuwa wakubwa.

 

HAKI ZA WATOTO

Ni vema ikaeleweka kwamba tunapozungumza kuhusu watoto, tunazikusudia jinsia zote mbili. Yaani watoto wa kiume sambamba na wale wa kike.

Katika Uislamu hakuna chembe ya ubaguzi, watoto wote wana haki sawa kwa wazazi wao kwa mujibu wa sheria.

Watoto wamepewa haki nyingi na Uislamu, kubwa kuliko zote ni haki ya malezi. Wazazi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata malezi bora.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *