VITA VYA UHUD-MAKURAYSHI WAANZA KUJIANDAA KWA AJILI YA VITA

Fikra waliyokuwa wakiifanyia kazi makurayshi tangu kumalizika kwa vita vya Badri.  Ilikuwa ni kukusanya nguvu zake zote, kwa lengo la kuelekeza pigo la kuvunjavunja  litakalommalizia mbali Bwana Mtume na maswahaba wake.

Kwa pigo hili takatifu watakuwa wameifagilia mbali na kuitokemeza kabisa dini yake hii mpya inayotishia utukufu na maslahi yao.

Wakaanza kufanya maandalizi motomoto kwa ajili ya kuitimiza fikra yao hii. Wakaaza kuchanga pesa, kukusanya zana za vita na kuyapelekea wajumbe wake makabila ya waarabu yaliyo pembezoni mwao kuomba ushirikiano wao ili kuufanikisha mkakati wao huu.

Miongoni mwa wajumbe (mabalozi) hawa alikuwa Abuu Azah; mshairi aliyetendewa wema na Mtume kwa kumuacha huru bila ya fidia katika vita vya Badri.

Nae kwa kuonyesha shukrani zake kutokana na ukarimu aliotendewa akachukua ahadi ya kutokumsaidia ye yote dhidi ya Mtume wala kuwa miongoni mwa adui zake. 

Akavunja ahadi aliyoiweka mwenyewe akaenda pamoja na wajumbe wengine sehemu za Kinaanah na Tihaamah, kuwahamisha watu wa sehemu hizo kujiunga nao katika vita hii dhidi ya Mtume.

Katika kipindi cha takribani mwaka mzima Makurayshi waliendelea kukusanya mali, washirika na kutayarisha chakula kitakachokidhi mahitaji ya jeshi.

Mpaka vikafikia kiwango  walichokikusudia katika tathmini yao, wakaridhika na maandalizi hayo na kuona kuwa yamekamilika na kutimia.

Na kwamba yanaweza kuwafikisha katika lengo lao na kuwahakikishia ushindi. Karibu na kumalizika kwa mwaka wakatoka na jeshi linalotoa mvumo wa sauti ya kutisha kutokana na wingi wa idadi yake. 

Walitoka pamoja na washirika wao wa Tihaamah na Kinaanah, pamoja na ndugu zao wa yamini; Wahabeshi wa Banil-Mustwaliq na Banil-Huun Ibn Khuzaymah.

Wakaelekea Madinah wakiwa na hamasa iendeshwayo na ukali wa ghadhabu ya kutoa pigo la kuvunjavunja na kuhilikisha. 

Wanawake wa Kikurayshi nao hawakubakia nyuma, walikuwa bega kwa bega na waume, baba na kaka zao wakiwahamasisha na kuwatia mori na ari.

Kongozi wa wanawake hawa alikuwa ni Hindu Bint Utbah; mkewe Abuu Sufyaan Ibn Harb.  

Miongoni mwa waliotika wito wa makurayshi dhidi ya Bwana Mtume na kujiunga na jeshi lao, alikuwa ni Abuu Aamir Al-Ausiy.

Huyu ni mtu wa kabila la Ausi (Ausi na Khazraji ni makabila makuu ya waarabu wa Madinah), alikuwa mpinzani wa Mtume na akiukanusha utume wake.

Huko nyuma alijitia utawa akidai kumgonjea Mtume atakayeletwa katika zama hizo.  Akiwatajia watu sifa za Mtume huyo na akiwaambia:

Hakika zimekurudia zama za kuja kwake. Bwana Mtume–Rehema na  Amani zimshukie–alipohamia Madinah na sifa zake kuwadhihirikia maanswaari kama walivyoambiwa wakamfuata na kumuamini.

Abuu Aamir kuona hivyo, akamfanyia husuda Mtume na kuukanusha utume wake. Alikuwa ni kiongozi wa Ausi kama alivyokuwa Abdullah Ibn Ubayyi kwa Khazraj; wawili hawa wote walimfanyia hasadi Mtume.

Lakini Abdullah Ibn Ubayyi aliingia katika Uislamu kinafiki na huyu alijitenga kabisa na Uislamu na kuendelea kuwa kafiri. Akatoka na kundi lake la watu khamsini miongoni mwa vijana wa kiausi, akakaa Makah akiwaunga mkono makurayshi na kuwahimiza kupigana na Mtume. Makurayshi walipoazimia kutoka kwenda Uhud,

Abuu Aamir aliwaahidi Makurayshi kuwashawishi jamaa zake Ausi kumtupa mkono Bwana Mtume.  Watoke katika safu ya waislamu wajiunge na safu ya mushrikina yatakapokutana vitani makundi mawili hayo. 

Alitegemea kuyafikia haya kutokana na nafasi/cheo alichokuwa nacho huko nyuma kwa kabila lake.  Akiamini kabisa kwa cheo chake hicho ataweza kuigawa safu ya waislamu.

 

MAKURAYSHI ALFU TATU WAELEKEA UHUD.

Mwanzoni mwa mwezi wa Shawwaal (Mfunguo mosi) wa mwaka wa pili wa Hijrah, lilitoka Makah kuelekea Uhud jeshi lenye kila alama ya maangamizi. Jeshi hili lenye imani ya ushindi kwa asilimia mia moja liliongozwa na Sufyaan Ibn Harb. 

Bendera ya jeshi ikibebwa na Twalhah Ibn Abuu Twalhah, kuliani mwa jeshi alikuweko kamanda Khaalid Ibn Al-Waleed na kushotoni Ikrimah Ibn Abuu Jahli.  Huku askari wa miguu wakiongozwa na Swafwaan Ibn Umayyah.

Hili ndilo jeshi la askari alfu tatu, jeshi lenye maandalizi makubwa na kamili, miongoni mwao wakiwemo wapanda farasi mahiri mia mbili, mia saba wenye vifuniko vya chuma kama kinga ya mwili (armoured) dhidi ya shambulizi za panga, mikuki, mishale na kadhalika. 

Wengi wa askari wakiwa wamepanda wanyama, wakifuatiwa na kundi kubwa la watumwa wa kuwasaidia na kuchunga mizigo yao.

Miongoni mwa watumwa hawa alikuwemo mmoja Muhabeshi aitwaye “Wahshiy”, huyu alikuwa na umahiri mkubwa wa kihabeshi wa kurusha mikuki. Bwana wake Jubayr Ibn Mutw-im akamshakizia kumuua Sayyidna Hamzah Ibn Abdul–Mutwalib; ami yake Mtume, na akamwambia: “Ukimuua Hamzah utakuwa huru”.

Kadhalika Hindu Bint Utbah alimuahidi kwa kumuua Hamzah kumpa mali mengi. Haya yalikuwa ni kutaka kulipa kisasi kutokana na Sayyidna Hamzah kuwauwa katika vita vya Badri, Twuaimah Ibn Adiy; ami yake Jubayr na Utbah Ibn Rabeei; baba yake Hindu.

 

MIKAKATI YA MAKURAYSHI.

Mwenendo na mpangilio wa vita wa Makurayshi ulidhihirisha kuwa walipanga mikakati maalum ili kujihakikishia ushindi mkubwa katika vita hivi. Mkakati wao ulikuwa ni kuwashambulia waislamu ndani ya Madinah kwa mtindo wa kushtukiza, kabla hawajajiandaa na hivyo kukosa nafasi ya kutoa upinzani. 

Mkakati huu ukishindwa kutokana na kuvuja kwa khabari ya kutoka kwao ikawafikia waislamu wakajiandaa.  Basi utumike mkakati wa kuzigawa safu zao katika medani ya vita. Huu ukishindwa, basi utumike mkakati wa kumuua Mtume wa Allah, kisha wauawe maswahaba wakubwa (viongozi) katika muhajirina (wa Makah wenzao).

Mauaji ya watu hawa yatawaacha waislamu wakiwa wamesambaratika hawana kiongozi wa kuongoza mapambano.  Jambo hili litawapa ushindi usio na gharama kubwa. Mikakati hii ndio iliyowapelekea makurayshi kutoka kwa siri ili wasiwashtue waislamu.

Wakaenda kwa uficho mpaka wakapiga kambi katika bonde la Uhud lililo kiasi cha umbali wa maili tano kutoka Madinah.

Lau si kuwa Sayyidina Abbas Ibn Abdul-Mutwalib kumuandikia barua Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie- kumjuza juu ya kutoka kwa Makurayshi. 

Jeshi hili lingeingia mjini Madinah wakati wenyeji wake wakiwa katika mghafala. Kwa mujibu wapokezi wa Sira ni kwamba Sayyidina Abbas alimuandikia barua  Mtume wa Allah kumfahamisha khabari ya makurayshi na maandalizi yao yote; watu,  zana na namna walivyopania.

Akamtuma kupeleka barua hii mtu mmoja kutoka katika ukoo wa Baniy Ghifaar. Tarishi huyu akaunga mwendo mchana na usiku mpaka akafika Madinah baada ya siku tatu. Alipofika Madinah akang’amua kuwa mtume hayupo hapo, yupo Qubaa nje kidogo ya Madinah mjini. 

Akamfuata huko na kumkabidhi barua, Bwana Mtume akaipokea na kumpa Ubayyi Ibn Ka’ab kumsomea. 

Baada ya kumsomea, Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie–akamtaka asiitangaze khabari hiyo.

Halafu Mtume akamuendea Sa’ad Ibn Rabeei akamjuza khabari ya barua. Sa’ad akamwambia Mtume: “Wallah mimi ninatarajia kuna kheri katika jambo hili”.

Mayahudi na wanafiki wakaivumisha khabari ya barua, ikatangaa kwa watu jambo ambalo makuryshi walilichelea kutokea.

Al-Waaqidiy amepokea kutoka kwa Abdullah Ibn Amrou Ibn Abiy Hakiymah Al-Aslamiy–amesema:

“Abuu Sufyaan alipopambazukiwa akasema: Ninaapa kwa Allh kwamba wamempelekea Muhammad khabari za kwenda kwetu na wamemtahadharisha na kumjuvya idadi yetu. 

aKwa hiyo, wao sasa wanalazimikiana na ngome zao, sidhani kama tutakabiliana nao ana kwa ana. Swafwaan akamwambia:

Wakitotoka kupambana nasi katika mbuga hii jangwani, tutaviendea viunga vya mitende vya Ausi na Khazraji na na kuifyekelea mbali yote.

Hivyo tutawaacha wakiwa hawana mali na hawataweza kuuzuia ufakiri abadan.  Na iwapo watatutokea basi idadi yetu ni kubwa mno kuliko yao na tuna silaha nyingi kuliko wao. Isitoshe sisi tuna farasi wao hawana, tena sisi tunapigana kwa ajili ya kisasi na wao hawana kisasi nasi”.

 

VITA VYA UHUD-MAKURAYSHI WAANZA KUJIANDAA KWA AJILI YA VITA

Fikra waliyokuwa wakiifanyia kazi makurayshi tangu kumalizika kwa vita vya Badri.  Ilikuwa ni kukusanya nguvu zake zote, kwa lengo la kuelekeza pigo la kuvunjavunja  litakalommalizia mbali Bwana Mtume na maswahaba wake.

Kwa pigo hili takatifu watakuwa wameifagilia mbali na kuitokemeza kabisa dini yake hii mpya inayotishia utukufu na maslahi yao.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *