Muislamu hukuona kulala kwa jicho la kuwa ni miongoni mwa neema ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaneemesha waja wake kwa maslahi na manufaa yao ya kimwili, kiakili na kiroho. Tusome na tutafakari :
“NA KWA REHEMA ZAKE AMEKUFANYIENI USIKU NA MCHANA ILI MPUMUE NA MTAFUTE FADHILA ZAKE (hapo mchana) NA ILI MPATE KUSHUKURU” [28:73]
.Na tusome tena : “NA TUKAUFANYA USINGIZI WENU KAMA KUFA (ili mpate kupumzika)” [78:9].
Hii ni kwa sababu kupumzika mtu usiku baada ya harakati za kuchosha za maisha za mchana kutwa, huusaidia mwili wa binadamu kuendelea kukua na kuwa mchangamfu, wenye nguvu ili mwanadamu aweze kutekeleza majukumu yake aliyopewa na Mola wake.
Sasa ili mwanadamu aweze kuishukuru neema hii ya kupata muda wa kupumzika (kulala) hana budi kuzichunga na kuzifuata adabu na taratibu zifuatazo katika kulala kwake :
1. Asichelewe kulala baada ya swalatil-Ishaa ila kwa dharura muhimu, kama vile kudurusi elimu (kusoma), au kuzungumza na mgeni.
Muongozo huu unapatikana katika hadithi iliyopokelewa na Abu Barzah kwamba Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa akichukia kulala kabla ya Swalatil Ishaa na kuzungumza baada yake. Bukhaariy na Muslim. Muislamu anatakiwa alale mapema ili aweze kuamka usiku kuswali.
2. Ajitahidi kulala akiwa na udhu. Hili ni kwa kuitekeleza kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipomwambia Baraai bin Azib – Allah amuwie Radhi –
“Unapotaka kulala, tawadha udhu wako wa swala” Bukhariy na Muslim.
3. Anapopanda kitandani aanzie kulalia upande wake wa kulia na alalie mto.
Hapana ubaya wowote ikiwa baada ya kushikwa na usingizi atageukia upande wa kushoto. Maelekezo na mafundisho haya tunayapata katika kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipomwambia Baraai bin Aazib
“Unapotaka kulala, tawadha udhu wako wa swala, kisha lalia upande wako wa kulia”. Na pia katika neno lake :
“Unapokiendea kitanda chako il-hali ukiwa twahara basi litegemezee mto taya/shavu lako lako la kulia”
4. Asilalie tumbo lake (asilale kifudifudi) mchana au usiku. Haya ni kwa mujibu wa riwaya iliyopokelewa iliyopokelewa kwa Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – kwamba amesema : “Huo ni ulalaji wa watu wa motoni” Na amesema tena : “Huo ni ulalaji asioupenda Mwenyezi Mungu Mtukufu”\
5. Alete dua na dhikri zilizopokelewa kutoka kwa Bwana Mtume. Miongoni mwa dhikri hizo ni hizi zifuatazo :
a. Aseme
SUBHANALLAH WALHAMDU LILLAH WALLAHU AKBAR *33,
Kisha aseme LAA ILAHA ILLA LLAH WAHDAHU LA SHARIKA LAHU LAHUL MULK WALAHUL-HAMD WAHUWA ALAA KULLI SHAY-IN QADIR.
Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipomwambia Aliy na Bintiye Fatmah – Allah awawie radhi – walipomtaka Bwana Mtume awapatie mtumishi wa kuwasaidia shughuli za nyumbani :
“Je nisikufundisheni lililo bora kuliko hili mliloliomba ? Mnapotaka kulala semeni SUBHANALLAH mara 33, AL-HAMDULILLAH mara 33 na ALLAHU AKBAR mara 34, haya ni bora zaidi kuliko mtumishi.” Muslim
b. Asome Suratil Fatiha (Al-Hamdu) na mwanzo wa Suratil Baqarah mpaka kwenye neno MUFLIHUUN, na ayatil Kursiy na aya za mwisho wa sura. Haya ni kwa mujibu wa riwaya zilizopokelewa katika kulipondokesha jambo hili.
c. Dua yake ya mwisho kabisa kabla ya kulala iwe ni dua hii iliyopokelewa kutoka kwa Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
{kiarabu}
6. Akiamka asubuhi alete dhikri zifuatazo :
a. Aseme atakapoamka kabla hajainuka kitandani :
ALHAMDU LILLAHI-LLADHIY AHYAANAA BAA’DA MAA AMAATANAA WA ILAYHIN NUSHUUR.
b. Ainue macho yake juu na asome : INNA FII KHALQIS-SAMAAWATI WAL-ARDHI -> aya kumi za mwisho za suratil Aali Imraan.
Azisome aya hizo atakapoamka kwa ajili ya tahajjud (swala ya usiku) kwa kuifuata kauli ya Ibn Abbaas –Allah awaridhie –
“Nilipolala kwa ndugu wa mama yangu Maymuna, mkewe Mtume – Rehema na Amani zimshukie – Mtume alilala mpaka nusu ya usiku au kabla yake kidogo au baada yake kidogo. Halafu aliamka na akawa anaupangusa usingizi usoni mwake kwa mkono wake, kisha akazisoma zile aya kumi za mwisho wa Suratil Aali Imran halafu akaenda akatawadha vema na akaswali” Bukhaariy.
c. Aseme mara nne : ALLAHUMMA INNIY ASBAHTU BIHAMDIKA USH-HIDUKA WA USH-HIDU HAMALATA ARSHIKA, WAMALAAIKATAKA, WAJAMII KHALQIKA ANNAKA ANTAL-LAHU LAA ILAHA ILLA ANTA WA ANNA MUHAMMADAN ABDUKA WARASULUKA” Dua hii ni zao la kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
“Atakayesema maneno hayo mara moja, Allah ataiwacha huru roho ya (mwili) wake na (adhabu ya) moto, na atakayesema mara tatu, Allah ataiwacha huru robo tatu yake na moto na akiyasema mara nne, Allah atamuacha huru yeye mzima na moto” Abu Dawoud.
d. Aseme anapouweka mguu wake kwenye kizingiti cha mlango hali akitoka nje :
BISMILLAH TAWAKKALTU ALAL-LAH LAA HAWLA WALAA QUWWATA ILLA BILLAH. Amesema Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
“Mja atakapoyasema maneno haya, huambiwa umeongozwa na umetoshezwa” Tirmidhiy.
e. Akivuka kizingiti cha mlango aseme :
ALLAHUMMA INNI AUDHUBIKA AN ADHWILLA AU UDHWALLA, AU AZILLA AU UZALLA, AU ADHLIMA AU UDHLAMA, AU AJ-HALA AU YUJHALA ALAYYA”
Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Ummu Salamah : Hakupatapo kutoka nyumbani kwangu Mtume – Rehema na Amani zimshukie – katu ila aliyainua macho yake mbinguni/juu na kusema
“ALLAHUMMA INNIY AUDHUBIKA AN ADHWILLA AU UDHWALLA …” Abu Dawoud.