SHAMBULIZI LA SAWIYQ

MAKURAYSHI WAFANYA JARIBIO LA KUREJESHA HESHIMA YAO ILIYOPOTEA KWA KUSHINDWA KWAO KATIKA VITA VYA BADRI. 

Ulipoingia mwezi wa Dhul-Hijjah (Mfunguo wa tatu) yaani baada ya kupita takriban miezi miwili na nusu tangu kumalizika kwa vita vya Badri. Alitoka Abuu Sufyaan na askari wapanda wanyama mia mbili wa kikurayshi, kuwafuata mayahudi wa Banin–nadhwiyr.

Wakamgongea Huyay Ibn Akhtwab kumuulizia khabari za Mtume na maswahaba wake, naye akakataa kuwafungulia. 

Wakaondoka wakaenda kumgongea Sallam Ibn Miksham, huyu akawafungulia, akawakaribisha na kuwakirimu.  Kisha akawapa khabari zote anazozifahamu juu ya Mtume.

Wakabakia pale mpaka usiku wa maladaku (karibu na alfajiri), ndipo Abuu Sufyaan akatoka na jeshi lake mpaka mahala panapoitwa “Uraydhw,” hii ni sehemu iliyo umbali wa maili tatu kutoka Madinah.  Hapo akafanya uharibifu na ukatili mkubwa, akamuua mmoja katika Answaar na mtumishi wake, akachoma nyumba kadhaa na chakula cha mifugo. 

Kwa kitendo chake hiki haramu akaona tayari ameshatekeleza yamini (kiapo) yake, huyoo akakimbia kurudi Makah Turejee nyuma kidogo tuone asili ya yamini hii ya Abuu Sufyaan iliyompelelekea kufanya unyama huu. 

Ikumbukwe kuwa miongoni mwa waliouawa katika vita vya Badri walikuwemo Utbah Ibn Rabeii ambaye ni baba mzazi wa Hindu (mkewe Abuu Sufyaan), ami na kaka ya Hindu pia waliuawa.

Kwa msiba huu mkubwa uliompata Bi. Hindu akaapa kulipa kisasi kwa Mtume na maswahaba wake kutokana na watu wake hawa waliouawa. 

Ili kuonyesha hisia zake za uchungu akakihama kitanda cha mumewe Abuu Sufyaan na akajiharamishia manukato mpaka alipe kisasa cha watu wake hawa. 

Nae Abuu Sufyaan katika kumuunga mkono mkewe katika machungu yake hayo, akaapa maji kutokugusa kichwa chake (hataoga) mpaka awalipie kisasi makurayshi na kurejesha heshima yao baina ya waarabu.  Ni kiapo hiki (yamini) ndicho kilichomsukuma Abuu Sufyaan kufanya yote aliyoyafanya “Uraydhw.”

Haya sasa na tuendelee, khabari za shambulizi hili zikamfikia Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie. 

Akawaita maswahaba wake, akatoka na watu mia mbili katika Muhajirina na Answaar kuwafuatia maadui hawa. 

Huku Abuu Sufyaan na watu wake wakijitahidi kwenda mbio kadri wawezavyo ili wasikutwe njiani kabla ya kuingia Makkah. 

Ili wawe wepesi katika kukimbia kwao wakawa wanatupa njiani baadhi ya mizigo iliyobebwa na wanyama wao. 

Wakatupa vyombo vilivyobeba chakula chao kikuu kilichojulikana kama “Sawiyq”; hii ni aina ya chakula kinachotengenezwa kwa unga wa ngano/shayiri mithili ya chapati. 

Waislamu wakapita wakikiokota chakula hicho bila ya kukutana nao, kwani tayari walikuwa wameshaingia katika himaya yao. 

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie–akarejea Madinah baada ya siku tano tangu alipotoka kufuatia uchokozi huu wa Makurayshi. 

Na alikuwa amemtawalisha Abuu Lubaabah Bishri Ibn Al-Mundhir kushika nafasi yake kwa kipindi chote alichokuwa nje ya Madinah. 

Katika shambulizi hili waislamu walijikusanyia  Sawiyq nyingi na ndio ikawa sababu ya kuitwa shambulizi hili kwa jina hili la “Shambulizi la Sawiyq”.

Machoni mwa Makurayshi kukimbia huku kwa Abuu Sufyaan ilikuwa ni sawa na kushindwa na kuwapa ushujaa waislamu. 

Ili kufuta mawazo na fikra hizi wakaanza matayarisho kabambe kwa vita vikubwa.  Vita vitakavyowarudishia heshima na tisho lao miongoni mwa makabila ya Waarabu. 

Haikuwa heshima/utukufu pekee ndio uliowapelekea kutaka kuingia vitani tena.  Bali ilikuwepo dharura nyingine, dharura ya usalama wa misafara yao ya biashara kwenda Shamu na kurudi Makah. 

Kwani sasa njia iliyozoeleka haina amani kutokana na waislamu kuivizia kwa lengo la kuiteka.  Ikawa hapana budi kupanga mikakati itakayowahakikishia usalama wa misafara yao hiyo.

 

MAKURAYSHI WAUPITISHA MSAFARA WAO WA KIBIASHARA KATIKA NJIA IELEKEAYO IRAQ.

Siku moja Swafwaan Ibn Umayyah alisimama na kuwaambia Makurayshi wenzake:

“Hakika Muhammad na watu wake wametuharibia biashara yetu, hatujui tuwafanyeje nao bado wameweka vizuizi katika njia yote ya pwani. Na wenyeji wa pwani wamefunga nao ahadi na isitoshe wengi wao wameshawafuata, hatujui tuishi wapi sasa? Tukiendelea kubakia katika miji yetu tutakula rasilimali yote mpaka kisisalie kitu.  Na bila ya shaka maisha yetu hapa Makah yanategemea kwa kiasi kikubwa biashara ya Shaam katika majira ya kusi na ile ya Habashah (Abyssinia) majira ya Kaskazi.” 

Al-Aswad Ibn Mutwalib akainuka na kumwambia:

“Cha kufanya sasa ni kuiachilia mbali njia hii ya pwani na tuitumie njia ya Iraq, kwani hiyo ni ardhi ya uwanda wa juu haipiti njia hii ye yote miongoni mwa watu wa Muhammad.”

Akamfahamisha juu ya mtu mmoja wa kabila (ukoo) la Baniy Bakri Ibn Waail aitwaye Furaat Ibn Hayaan ili amuongoze katika njia hiyo. 

Swafwaan akajiandaa tayari kwa msafara wa kupitia njia hii mpya iliyopendekezwa na Al-Aswad, akakusanya  fedha (madini) na bidhaa mbalimbali zenye thamani ya Dir-ham alfu moja (hizi ni pesa nyingi sana kwa wakati huo).

Msafara ukaanza safari huku ukiamini kwamba khabari ya kutoka kwao haitavuja na kuwafikia mahasimu wao; waislamu lakini kumbe bila ya kujua mmojawapo wa majasusi wa Kiislamu tayari alikuwa ameshainusa khabari hiyo. 

Na bila kuchelewa akautimiza wajibu wake akaifikisha kwa Bwana Mtume nae bila ya kufanya ajizi akaanza kuifanyia kazi khabari ile. 

Akamtuma Zayd Ibn Haarithah kukiongoza kikundi cha wapandaji mia moja miongoni mwa Muhajirina na Answaar. 

Wakaenda mpaka wakautokezea kwa ghafla msafara ule katika eneo liitwalo “Al-Qaradah”.  Hili ni eneo lenye maji la Najid, wanamsafara ule wakatimua mbio kutokana na khofu ya kushitukizwa walikokuwa hawakukutarajia kabisa. 

Wakakimbia wakiuacha msafara na mali zake zote na kutoa fursa kwa waislamu kuichukua ngawira baridi isiyo na vita/mapambano. 

Hii ndio ngawira nono ya kwanza waliyoipata waislamu bila ya kuitolea nguvu.  Bwana Mtume akaipiga mafungu matano na kuigawa baina ya maswahaba wake.

Jaribio hili la waislamu lililofanikiwa likawa ni miongoni mwa sababu zenye nguvu zilizowafanya Makurayshi kufanya juhudi za makusudi kutaka kuwaonyesha waislamu nafasi yao. 

Suala sasa likawa si tu suala la kulinda hadhi na kurejesha heshima yao, bali suala la ama kufa au kupona.  Ama Makurayshi waendelee kuwa dhalili na dhaifu mbele ya Muhammad na watu wake na kukubali hili bila shaka ni kuchagua kuangamia. 

Au wajiandae kutoa pigo la kusambaratisha litakalo wahifadhia maisha yao na kuwarejeshea kitisho chao (awe) baina ya makabila ya Waarabu.  Kwa hivyo Makurayshi wakaanza kukusanya nguvu zao tayari kabisa kuwavamia waislamu Madinah kwa lengo la kuwasagasaga kabisa na kukata mzizi wa fitna. 

Katika kipindi hiki cha mpito kuelekea vita vikali vinavyopikwa na makurayshi yalitokea mapambano ya hapa na pale baina ya waislamu na baadhi ya makabila yaliyokuwa yakiishi jirani na Madinah. 

Mapambano yaliyoishia kuwapa ushindi na ngawira waislamu ambao sasa walianza kuonekana kama wababe wa vita wanaochukua nafasi ya Makurayshi katika medani hii ya vita.

Kila mara Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–alipopata khabari ya kujikusanya kikundi cha watu hawa dhidi yake. 

Alikitokea ghafla na maswahaba wake kabla hakijajiandaa na kukifagilia mbali na kuwaacha wakikimbilia majabalini.

Mapambano haya ni pamoja na shambulizi la “Ghatw-faan,” sehemu za Najid katika mwezi wa Rabiul-Awwal (Mfunguo sita) mwaka wa tatu wa Hijrah. 

Na shambulizi la Baniy Sulaym katika sehemu ya “Bahraan”, lililofanywa katika mwezi wa Jumaadal-Uula (mfunguo nane) wa mwaka huo huo.

Baadhi ya wanahistoria wanaieleza sababu ya machafuko haya yaliyofanywa na makabila haya kuwa ni kutokana na ushirika wao na makurayshi.

Wengine wanasema yalikuwa ni ya kulinda na kutetea maslahi yao, kwa sababu kwa kiwango kikubwa maisha yao yalitegemea kodi ya njia iliyotolewa na misafara ya kibiashara ya makurayshi inayopita kwao wakati wa kwenda na kurudi. 

Waislamu walipowakatia makurayshi njia yao hii, makabila haya yakajichelea dhiki na taabu.

 

SHAMBULIZI LA SAWIYQ

MAKURAYSHI WAFANYA JARIBIO LA KUREJESHA HESHIMA YAO ILIYOPOTEA KWA KUSHINDWA KWAO KATIKA VITA VYA BADRI. 

Ulipoingia mwezi wa Dhul-Hijjah (Mfunguo wa tatu) yaani baada ya kupita takriban miezi miwili na nusu tangu kumalizika kwa vita vya Badri. Alitoka Abuu Sufyaan na askari wapanda wanyama mia mbili wa kikurayshi, kuwafuata mayahudi wa Banin–nadhwiyr.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *