MURUA

Murua ni sifa njema ambayo muislamu wa kweli anapaswa kujipamba nayo ili kuweza kuitoa sura ya Uislamu wake nje watu/ulimwengu uweze kuuona Uislamu wake.

Kwa hivyo Murua ni mwonzi/kioo kinachotoa nje taswira ya Uislamu wa mtu.

Hii ni sifa ambayo humpelekea na kumsukuma mtu kushikamana na tabia zote njema na kujipamba na sifa na ada nzuri.

Tabia hii huchangiwa kwa kiasi kikubwa na hima kubwa anayokuwa nayo mtu katika kuyapupia mambo mema ya kheri na kuchunga heshima na hadhi yake. Vigezo viwili hivi:

  1. Kupupia kufanya kheri
  2. Kuchunga hadhi.

Ndivyo vyanzo vikuu vya tabia hii njema ya murua.

Mtu akiwa na ari kubwa katika kutenda mambo mema na akawa na hadhari kuu katika kuchunga heshima yake isivunjwe, basi ni dhahiri kuwa ari na hadhari hiyo vitamfanya ahodhi tabia njema na kujipamba na sifa nzuri na kujiepusha na kila ambalo kwa namna moja au nyingine litapelekea kuvunjika heshima yake machoni mwa watu.

Natija ya hali hii ni mtu kuwa mkarimu, na ukarimu ni miongoni mwa sifa tukufu za Mwenyezi Mungu Mtukufu ambazo muislamu anatakiwa ajipambe nazo.

Amesema Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie

“Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mkarimu apendaye ukarimu, na hupenda tabia tukufu na huchukia tabia duni (mbaya)” Abu Nuim, Twabaraaniy, Al-Haakim na Al-baihaqiy. Kadhalika hali hii itamzalishia mwenye kuwa nayo tabia ya kutokuwaudhi na kuwakera wenzake au kuwasababishia madhara jambo ambalo uislamu unalikemea vikali kabisa. Bwana mtume – Rehema na Amani zimshukie anatuasa katika hili –

 “Atakayedhuru au kusababisha madhara, Allah atamshushia madhara (na yeye) na atakayefanya uzito naye atafanyiwa uzito na Allah.” Ahmad, Abuu Daawoud, Tirmidhy, Nasani na Ibn Maajah.

Tunaweza kuigawa tabia hii ya murua katika mapote/makundi mawili makuu, kama ifuatavyo:

1: Murua ambao uzaao tabia tukufu na sifa njema katika nafsi ya mwanadamu.

Aina hii ya murua humsukuma mja kushikamana na dini kwa maana yake halisi, kujipamba na tabia/sifa njema kama vile kusema ukweli, kutekeleza ahadi, kusaidia masikini na mayatima, ukarimu na kadhalika.

Pia humlazimisha kujiepusha na mambo ya haramu kama vile kusema uwongo, kutoa ushahidi wa uwongo, kula mali ya yatima, kula riba na mengi mengineyo.

2: Murua hutoao/huletao athari kwa watu wengine.

Aina hii ya murua humpelekea mtu kutoa ushauri, nasaha kwa wenziwe kwa nia njema ya kujenga na kutengeneza kwa sababu anaiamini kauli ya Mtume wake;

 “Atakayemshauri nduguye (mwanadamu mwenziwe) jambo ili-hali anatambua kuwa uongofu uko katika jambo jinigine, hakika amemkhini” Abuu Daawoud na Al-haakim, atakuwa na huruma kwa viumbe wenzake, atatekeleza amana kwa kuifanyia kazi kauli ya mola wake;

“HAKIKA ALLAH ANAKUAMRISHENI KUZIRUDISHA AMANA KWA WENYEWE (wanaozistahiki) …” (4:58)

Atauzuilia mkono, ulimi na viungo vyake vyote na kila la haramu na ataweza kutunza siri. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anatuambia kuhusiana na suala zima la murua;

“Atakayeamiliana (Atakayechanganyika na wenziwe kimaisha) na watu, akawa hawadhulumu, akazungumza nao akawa hawaongopei na akawaahidi akawa havunji ahadi basi huyo ndiye mtu ambaye umekamilika murua wake na kudhihiri uadilifu wake na imewajibika kumfanya ndugu.”

Katika hadithi hii tukufu, Bwana Mtume anatubainishia sifa za mtu mwenye murua, sifa hizo ndizo zitkazotusaidia kumjua ni nani ana murua na nani si mtu wa murua. Sifa hizo kwa mujibu wa hadithi ni pamoja na:-

  1. Kutokuwa dhalimu. Mtu aliye mkamilifu wa murua hayuko tayari kudhulumu wala kudhulumiwa, hili linatokana na kuikiri, kuikubali na kuimini kwake kauli ya mola wake isemayo;

“………………. MSIDHULUMU WALA MSIDULUMIWE.” (2:279) Muislamu hakubali kudhulimiwa kwa sababu anaamini kufanya hivyo ni katika jumla ya kuutekeleza uislamu wake kuvitendo. Tusome kwa tafakari, mazingatio na mwisho tutende kwa mujibu wa tafakari na mazingatio yetu;

NA WALE WANAOLIPIZA KISASI BAADA YA KUDHULUMIWA, HAO HAKUNA NJIA YA KULAUMIWA. BASI LAWAMA IKO JUU YA WALE WANAODHULUMU WATU NA WAKAWAFANYIA JEURI KATIKA ARDHI PASIPO HAKI; HAO NDIO WATAKAOPATA ADHABU IUMIZAYO.” (42: 41 – 42)

Amesema Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – katika hadithil– qudsiy:

“Amesema Mwenyezu Mungu Mtukufu; enyi waja wangu, hakika mimi nimeiaharamisha dhulma juu ya nafsi yangu, na nimeifanya baina yenu kuwa ni haramu, basi msidhulumiane ………….” Muslim.

Hii ni mojawapo mongoni mwa sifa za mtu aliye na mrurua kamili kwa mujibu wa hadithi.

  1. Sifa ya pili ya tu mkamilifu wa murua ni kutokusema uwongo.

Muislamu uliyekamilika murua wake hathubutu na wala hajasisri kabisa kusema uwongo, kwa sababu anaamini kuwa kusema/kuzua uwongo ni sifa ya makafiri wasioziamini aya za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kuhusiana na hili tunasoma

“MWANAOZUA UWONGO NI WALE WASIOZIAMINI AYA ZA ALLAH NA HAO NDIO WAONGO” (16:105)

kadhalika muislamu mkamilifu wa murua hasemi uwongo kwa kuwa anayekubali, anayaamini na kuyafuata mafundisho ya Mtukufu Mtume wake – Rehema na Amani zimshukie – aliposema;

“……….. jiepusheni na uwongo, kwani uongo huongozea/hupelekea katika uovu na uovu hupelekea motoni, na mtu haendelei kusema na kuupupia uwongo mpaka ataandikwa mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa ni muongo.” Ahmad, Bukhaariy, Muslim, Abuu Daawoud na Tirmidhiy.

  1. Kutokuvunja ahadi. Hii ndio sifa ya tatu ya mtu mkamilifu wa murua. Muislamu aliyeiva na kukomaa kimurua havunji ahadi aliyoitoa yeye mwenyewe kwa khiyari yake, kwa sababu anatambua kutekeleza ahadi ni amri ya mola muumba wake, Tusome:

 “…………..NA TIMIZENI AHADI KWA HAKIKA AHADI ITAULIZWA (SIKU YA KIYAMA) (17:34) “NA TIMIZENI AHADI MNAZOZITOA KWA JINA LA ALLAH MNAPOAHIDI; WALA MSIVUNJE HIZO AHADI BAADA YA KUZITHUBUTISHA ……………” (16:91)

Muislamu anaizingatia na kuitia matendoni kauli ya Mtume wake – Rehema na Amani zimshukie:

“Hana Imani asiyekuwa na amana na wala hana dini asiyekuwa na ahadi” Ahmad, Abu Yaalaa, Ibn Hibbaan na Al-baihaqiy.

 

MURUA

Murua ni sifa njema ambayo muislamu wa kweli anapaswa kujipamba nayo ili kuweza kuitoa sura ya Uislamu wake nje watu/ulimwengu uweze kuuona Uislamu wake.

Kwa hivyo Murua ni mwonzi/kioo kinachotoa nje taswira ya Uislamu wa mtu.

Hii ni sifa ambayo humpelekea na kumsukuma mtu kushikamana na tabia zote njema na kujipamba na sifa na ada nzuri.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *