Ilipita miaka mitatu il-hali Mtume wa Mwenyezi Mungu akiulingania Uislamu kwa siri. Maswahaba wa Mtume – Allah awawie -Allah amuwie radhi wote – pia hawakubakia nyuma bali walikuwa bega kwa bega na Bwana Mtume wakiwalingania watu Uislamu.
Wakawa wanautikia wito huu wa kuingia huu wa kuingia katika Uislamu watu ambao Mwenyezi Mungu alikwisha waandikia uongofu miongoni mwa wanaume na wanawake wa Makkah.
Kwa hiyo idadi ya waislamu ikawa inazidi kidogo kidogo siku hata siku, hii ni kwa sababu watu waliogopa kusilimu kwa kuchelea shari na nguvu ya makurayshi. Ikawa wanaosilimu, husilimu kwa tahadhari kubwa, kwa kuchelea wasijulikane.
Ili kuepuka kugongana na kukwaruzana na jamaa zake Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie- alitafuta mahala pa faragha, palipo mbali na watu ili pawe ndio kito chake cha kukutana na maswahaba wake.
Mahala hapa pateule hapakuwa pengine ila ni nyumba ya Bwana Arqam bin Abil-Arqam, iliyoko jirani na Jabali Swafaa.
Bwana Arqam alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa makurayshi waliosilimu mwanzo kabisa. Historia ya Uislamu haiandikiki bila ya kuitaja nyumba hii.
Ndani ya nyumba hii ndimo Mtume alikuwa akikutana na maswahaba wake akiwawaidhi, akiwaswalisha, akiwasomea wahyi/ufunuo wa Qur-ani uliomshukia na kuwafundisha jinsi ya kuishi na mafundisho hayo ya Qur-ani.
Kwa hivyo nyumba hii ikawa ndio msikiti wao wa kwanza wakifanya ibada zao humo, ikawa ndio chuo cha mafunzo na malezi na ikawa ndio klabu yao ya ushauri – nasaha na upangaji na upangaji wa mikakati na mipango ya baadaye.
Pamoja na upinzani mkubwa wa makurayshi Bwana Mtume akaendelea kulingania kwa siri mpaka ilipomshukia kauli yake Mwenyezi Mwenyezi Mungu Mtukufu :
“BASI YATANGAZE ULIYOAMRISHWA (wala usijali upinzani wao) NA UJITENGE MBALI NA (vitendo vya) HAO WASHIRIKINA” [15:94].
Baada ya amri na tangazo hili, hapa sasa ndipo Bwana Mtume akabadilisha mtindo wa ulinganiaji.
Akaanza kuulingania Uislamu kwa dhahiri bila ya khofu wala uficho. Akapanda juu ya jabali Swafaa na akaanza kuwaita watu kwa sauti ya juu :
“Enyi jamaa zangu!” Akawaita jamaa/watu wake kwa namna na mtindo uliokuwa umezoeleka miongoni mwao walipokuwa na jambo muhimu.
\Zikamuitikia na kumjia koo zote kumi na mbili za makurayshi, walipokusanyika ndipo akawaeleza alilowaitia, akaanza kwa kusema :
“Mnaonaje, lau nitakwambieni kwamba nyuma ya jabali hili (Swafaa) kuna jeshi linakuja kukushambulieni, Je mtanisadiki ?” Wote wakajibu kwa sauti moja :
Ndio, wewe kwetu hutuhumiwi kwa baya lolote, na kamwe hujapata kutuongopea. (Mtume) akawaambia :
“Basi (ikiwa ni kweli hayo muyasemayo) mimi ni muonyaji kwenu nyinyi mbele ya adhabu kali ! Enyi wana wa Abdul Mutwalib! Enyi wana wa Abdi-Manaaf! Enyi wana wa Taym! Enyi wana wa Makhzuum! Enyi wana wa Asad! … Hakika Mwenyezi Mungu ameniamrisha kuwaonya jamaa zangu wa karibu na mimi similiki manufaa yenu ya duniani na wala similiki fungu lenu la akhera ila mtakaposema : Hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila ALLAH pekee. Enyi kusanyiko la Makurayshi, ziokoeni nafsi zenu kutokana na adhabu ya moto, kwani mimi sitakufaeni chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Hakika mfano wangu nanyi ni mfano wa mtu aliyemuona adui, akakimbia haraka kuwaambia jamaa zake wamuwahi adui, akawa apiga ukelele : Eeh! Eeh! Mmevamiwa, mmevamiwa!
Kabla Mtume hajamaliza kusema, Abuu Lahab {Ami yake} akamkata kauli na kumwambia : “Umeangamia ewe mwana kuangamia! …. Hivi hili ndilo ulilotukusanyia?”
Abu Lahab ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kumjibu, kumuudhi na kumkadhibisha Bwana Mtume na kumfukuzia watu.
Hapo ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akaishusha kauli yake :
“PANA KUANGAMIA MIKONO MIWILI YA ABU LAHAB! NAYE AMEKWISHAANGAMIA. HAYATAMFAA MALI YAKE WALA ALIVYOCHUMA. (Atakapokufa) ATAUINGIA MOTO WENYE MWAKO (mkubwa kabisa). NA MKEWE, MCHUKUZI WA KUNI (za fitna). (Kama kwamba) SHINGONI MWAKE IKO KAMBA ILIYOSOKOTWA (anayochukulia kuni za fitna hizo)” [111:1-5]
Mkewe Abu Lahab, Ummu Jamiyl alikuwa akimchukia sana Bwana Mtume na alikuwa akifanya zoezi la kumfitinisha Mtume na jamaa zake kwa kueneza maneno ya uzushi na uongo mpaka Mwenyezi Mungu akamsifia kwa sifa mbaya kabisa, akamuita MCHUKUZI WA KUNI. Hii ni sifa ya ufitina na uchochezi.
Kwa ujumla mama huyu mbaya na mumewe walikuwa ni maadui wakubwa wa Bwana Mtume.
Ukelele wa Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – katika jabali Swafaa haukupotea bure bali ulileta taathira fulani katika jamii ya Makurayshi mjini Makkah.
Tangu siku ile khabari za da’wah zikaenea mji mzima wa Makkah, zikawa ndizo khabari zilizoyatawala mabaraza na vilabu vya Makkah. Watu wakawa wanaulizana kwa shauku ya kuaka kujua : Ni dini gani hii anayolingania Muhammad ?
“BASI WAKO MIONGONI MWAO AMBAO ALLAH AMEWAONGOA, NA WAKO MIONGONI MWAO AMBAO UPOTOFU UMETHUBUTU JUU YAO” [16:36]. Wale ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu alikwishawaandikia kuongoka wakawa wakimuendea Mtume kwa uficho kumtaka awape ufafanuzi wa maelezo ya kina kuhusiana na dini mpya anayoilingania.
Naye Nabii Muhammad akawa anawakinaisha kimaelezo, walipotosheka wakatangaza kusilimu.
Ama wale ambao walioandikiwa uovu tangu azali, hawa waliipa mgongo da’wah ya Mtume, wakashindwa kuiona haki kuwa ni haki na kuifuata.
Hawa waligawika makundi mawili; kundi moja lilikuwa na msimamo wa kumkataa Bwana Mtume na dini yake bila ya kumfanyia uadui.
Kundi jingine lilimpinga vikali na kumpiga vita kwa hali na mali na kupanga mikakati ya kuwazuia watu wasimfuate Mtume.
Wengi miongoni mwa watu wa kundi hili la pili walikuwa ni viongozi na matajiri, hawa waliiona dini hii mpya ni hatari kwa maslahi na nyadhifa zao katika jamii.
Muhammad akikubalika na jamii na kushika hatamu za uongozi, atakuwa na sauti na hili litapelekea kuanguka kwa nyadhifa na maslahi yao.
Miongoni mwa maadui wakubwa katika kundi hili, walikuwa ni Abu Jahl bin Hisham, Abu Lahab bin Abdul-Mutwalib na Uqbah bin Abi Mua’yt.
Hawa wawili Abu Jah na Uqbah walikuwa ni jirani zake Mtume, wakimuudhi upeo wa kumuudhi. Katika hili Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anasema katika riwaya iliyopokelewa na Bi Aysha – Allah amwie radhi –
“Nilikuwa ninaishi na majirani wawili wabaya; baina ya Abi Lahab na Uqbah bin Abi Muayt, walikuwa wakichukua utumbo wa mbuzi na kuja kuutupia mlangoni kwangu mpaka takataka zao wakizitupia mlangoni kwangu!” Naye Bwana Mtume akiziondosha taka zile na kusema :
“Enyi wana wa Abdi Manaf, ni ujirani gani huu ?”.
Watu wanyonge yaani watumwa, wajakazi, masikini na mafakiri wa Makkah wakawa wanamfuata na kumsikiliza Mtume kila alipokuwa akiulingania Uislamu.
Hawa walikuwa wamechoshwa na mfumo wa uonevu na ukandamizaji wa dini ya Makurayshi. Kwa hivyo walikuwa na matumaini kwamba Uislamu ndio mfumo wa maisha utakaowakomboa kutoka katika udhalimu, uonevu na unyanyasaji.
Uislamu ndio utakaowapa matumaini ya maisha bora, haki na usawa na kuwatoa katika tabaka la chini ambako walionekana kuwa ni sawa na wanyama au duni kuliko wanyama.
Na kweli Uislamu uliwawekea misingi madhubuti ya maisha na ukawafungulia mlango wa matumaini ya amani, salama na utulivu.
Bwana Mtume alikuwa akiwaambia kwamba gharama na thamani pekee wanayotakiwa kuitoa kama kiingilio na tiketi ya mfumo huu mpya uliosheheni haki, uadilifu na usawa ni kwa wao kuijaza mioyo yao imani ya Allah, Mungu Mwenyezi asiye na mshirika na maisha yao yote yapambwe na amali/matendo mema.
Mwenyezi Mungu akawaongoza masikini hawa, wakawa wanaingia katika dini yake makundi kwa makundi.
Naye Bwana Mtume akiwapokea kwa wema na ukarimu mkubwa na akiwafanya sawa na wale waumini ambao walikuwa ni viongozi na watu watukufu.
Hakumbagua baina ya tajiri na masikini, mnyonge na mwenye nguvu wala baina ya Mwungwana na Mtumwa. Bwana Mtume akajiweka baina yao daraja ya ndugu mwenye huruma na mzazi rahimu
“…ANAWAAMRISHA MEMA NA ANAWAKATAZA MABAYA NA KUWAHALALISHIA VIZURI NA KUWAHARIMISHIA VIBAYA NA KUWAONDOLEA MIZIGO YAO NA MINYORORO ILIYOKUWA JUU YAO (yaani sheria ngumu za zamani na mila za kikafiri).” [7:157].
Mtume aliwaonyesha mfano mwema wa tabia nao wakimfuata na kumuiga na wakizifuata nyayo zake katika matendo na kauli. Wakimtii twaa ya kweli na upendo – tunamwomba Mola wetu Mtukufu awaridhie maswahaba wa Mtume wake wote- Amin.