Ibada ya swala ina nafasi na daraja kubwa sana katika Uislamu, kwa sababu nyingi tu , baadhi ya sababu zinazoifanya swala iwe na nafasi ya umuhimu wa pekee ni kama zifuatavyo:-
1. Swala ndio muhimu na nguzo kubwa ya dini kama tunavyofahamishwa na kauli ya Bwana Mtume Rehema na Amani zimshuke. “Swala ndio nguzo ya dini, swala ndio ufunguo wa kheri zote” Twabaraany na Al-Haakim.
2. Swala ndio ibada ya kwanza kabisa aliyoiwajibisha Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake katika ule usiku Mtukufu usiku wa nafasi ya Bwana Mtume ya Israa na Miraji.
Na ndio ibada pekee aliyopewa Mtume Mbinguni bila ya wasita (Ukati) wa Malaika Jibrilu kwani ibada nyingine zote alipewa hapa hapa duniani kupitia kwa Malaika Jibrilu-Allah amshushie amani.
3. Swala ndio ibada ya mwanzo kabisa atakayohisabiwa na kukaguliwa mja siku ya kiyama kabla ya ibada nyinginezo.
4. Swala ndio ilikuwa wasia wa mwisho wa Bwana Mtume kwa uamti wake wakati anafariki dunia hii baada ya kuikamilisha kazi aliyopewa na Mola wake.
5. Swala ndio ibada pekee iliyotajwa zaidi ya mara sabini (70) ndani ya Qur-ani, miongoni mwa sehemu ilizotajwa swala ndani ya Qur-ani Tukufu ni hizi hapa:-
“SOMA ULIYOLETEWA WAHYI (uliyofunuliwa) KATIKA KITABU (hiki ulicholetewa) NA USIMAMISHE SWALA BILA SHAKA SWALA (ikisaliwa vilivyo) HUMZUILIYA (huyo mwenye kuswali na) MAMBO MACHAFU NA MAOVU……….” (29:45)
Tusome tena
“ANGALIENI SANA SWALA (zote kuziswali, khasa jamaa) NA (khasa) ILE SWALA YA KATI NA KATI. NA SIMAMENI KWA UNYENYEKEVU KATIKA KUMUABUDU ALLAH” (2: 238).
Hivi ni chache tu miongoni mwa aya nyingi zilizoitaja ibada hi ya swala .
6. Swala ndio ibada bora kuliko ibada zote kama tunavyofahamishwa na hadithi ifuatayo:
Mtu mmoja alikuja kumuuliza Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
juu ya amali iliyo bora kbisa kuliko zote, (Mtume) akamjibu “Swala “ akauliza tena Halafu ipi (amali gani inayofuata?) (Mtume) akajibu ,
“Halafu Swala” Akauliza tena, Halafu ipi? Akamjibu “Swala” mara tatu Ibri Hibbaan.
Kauli ya jumla tunaweza kusema na si kusema tu bali kusema kwa kinywa kipana kabisa kwamba nafasi/umuhimu wa swala katika Uislamu ni kama umuhimu wa kichwa katika kiwiliwili.
Kama kisivyokuwa na uhai kiwiliwili kilichojitenga/kutenganishwa na kichwa chake ndivyo asivyokuwa na uhai Uislamu wa mtu asiyeswali bali inawezekana asiwe na Uislamu kabisa kwa nini ?
hivyo ndivyo tunayoelewa kutokana na kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshuke “Hakika baina ya mja na shiriki ni ukafiri ni kuacha swala” Muslim.