ADABU ZA BARAZA

Muislamu maisha yake yote ni ya unyenyekevu, na yenye kufuata mfumo wa Uislamu.

Mfumo ambao unazigusa nyanja zake zote za maisha yake ya kila siku.

Katika mfumo huu kamili wa maisha, muislamu anafundishwa hata jinsi ya kukaa, ake vipi katika baraza na akeje na wenzake barazani.

Hivyo basi, zifuatazo ni taratibu/adabu anazopaswa muislamu kuzifuata katika ukaaji wake barazani:-

1.      Mtu anapotaka kukaa katika baraza, anatakiwa kwanza awatolee salamu wanabaraza aliowakuta pale, ndipo tena aketi pale ilipokomea baraza.

Hapaswi kumuinua mtu mahala alipokaa ili akae yeye na wala asikae baina ya watu wawili aliowakuta ila baada ya kupata idhini yao.

Maelekezo na muongozo huu tunaupata kutokana na hadithi zifuatazo za Nabii Muhammad Rehema na Amani zimshukie ;

Asimuinue, Asimuinue mmoja wenu mtu mahali alipokaa ikisha akakaa yeye, Lakini fanyianei wasaa au peaneni nafasi” Bukhaariy na Muslim.

Na ikiwa Ibn Umar – Allah amuwiye radhi anapopishwa na mtu mahala pake alipokaa, hakai mahala hapo. Na Jaabir Ibn Samrah -Allah amuwiye radhi – amesema;

” Tulikuwa tunamuendea Mtume – Rehema na Amani zimshukie – mmoja wetu hukaa pale ilipokomea baraza” Abuu Daawoud na Tirmidhiy.

Na amesema Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie ” Si halali kwa mtu kuwatenganisha watu wawili ( kwa kukaa kati yao) ilaa kwa idhini yao “Abuu Daawoud na Tirmidhiy.

2.      Mtu atakapoinuka mahala alipoketi kwa haja fulani, basi atakaporudi yeye ndiye mwenye haki ya kuketi mahala hapo.

Kwahiyo kama mtu aliketi baada ya kuinuka kwake, inampasa ampishe mwenyewe na asiendelee kung’ang’ania kukaa.

Mwongozo huu ni natija ya kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – aliposema

” Atakapoinuka mmoja wenu mahala alipokaa kisha akarejea basi yeye ndiye mwenye haki zaidi na mahala hapo”. Muslim.

3.      Asikae katikati ya baraza,. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Hudhayfah – Allah amuwie radhi – kwamba Mtume wa Aallah Rehema na Amani zimshukie

” amemlaani mtu anayekaa katikati ya baraza” Abuu Daawoud.

4.      Muislamu anapoketi katika baraza, anapaswa kuzichunga na kuzifuata adabu zifutazo:

  1. Akae kwa utulivu na unyenyekevu . asikae kwa kishindo na mbwembwe ili watu wajue fulani kaingia.
  2. Asipote / asipache vidole vyake.
  3. Asichezeechezee ndevu zake au pete yake.
  4. Asichokonowe meno yake au kutia kidole puani mwake.
  5. Asitemeteme mate hovyo, au kujikohoza kohoza na kupiga chafya kwa sauti ya juu.
  6. Ikiwa hapana budi kuzungumza basi azungumze maneno ya sawa sawa.
  7. Ajiepushe na kufanya mzaha na wala asimkate mtu maneno wakati anapozungumza bali amsikilize mpaka amalize.

 

5.      Muislamu atakapojilazimisha kuzifuata adabu na taratibu hizi kwa sababu ya mojawapo kati ya mambo mawili haya:

a.      Kutokuwaudhi na kuwakera wenziwe kwa tabia au vitendo vyake kwa kuzingatia kuwa ni haramu kumuudhi muislamu. ” Na muislamu (wa kweli ) ni yule ambaye waislamu ( wemzake) wamesalimika na (shari) ya ulimi na mkono wake”

b.      Apate mapenzi ya ndugu zake na kupata kuzoeana nao, kwani sheria imemlazimisha kujipendekeza kwa nduguze waislamu na imemuhimiza kuzoeana nao.

 

6.      Muislamu anapokaa katika njia wanayopita watu (barabarani – mbele ya nyumba yake) basi ni lazima ahakikishe anazifuata adabu zifuatazo.

a.       Ayainamishe macho yake, asimkodolee macho mwanamke apitaye au aliyesimama mbele ya nyumba yake.

b.      Asiwaudhi na kuwakera wapitanjia kwa kuwatukana au kuwatamkia maneno yatakayowaudhi au kuwaaibisha. Asimpige mpita njia bila ya haki, asipore mali ya mtu na wala asizuie njia.

c.       Aitikie salaam ya kila atakayemsalimu miongoni mwa wapita njia, kwa sababu kuitikia salamu ni wajibu kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. ” NA MNAPOAMKIWA KWA MAAMKIO YO YOTE YALE, BASI ITIKIENI KWA YALIYO BORA KULIKO HAYO AU REJESHENI HAYO HAYO…” [ 4:86 ]

Adabu na taratibu zote hizi ni kwa ajili ya kuitekeleza kivitendo kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie. ” Tahadharini/ jiepusheni na kukaa majiani maswahaba na kusema: Hatuna budi kukaa, kwani hizo ndizo baraza zetu za kuzungumzia. ( Mtume ) akawaambia: Ikiwa hamtaki ila kuendelea kukaa, basi ipeni njia haki yake. Wakauliza ; Ni ipi hiyo haki ya njia ? Mtume akawajibu ni kuinamisha macho, kuondoa kero (lenye kuudhi), kuitikia salaam, kuamrisha mema na kukataza mabaya”

Katika baadhi ya riwaya / mapokezi kuna ziada isemayo ( na kumuongoza aliyepotea) Bukhaary na Muslim

MAELEZO:

Kuamrisha mema njiani kulikotajwa katika hadithi ni kama vile mtu amebarizi (amekaa barazani ) na wenziwe, halafu ikatolewa adhana.

Baada ya adhana hakuna yeyote kati ya wanabaraza aliyeinuka kwenda kusali, hapo ndipo itamuwajibikia kuwaamrisha kuitikia adhana, kwa kwenda msikitini kuswali.

Mfano mwingine, mtu amekaa barazani kwake, mara tahamaki akapita mtu mwenye njaa au aliye uchi (hana nguo ) basi ni wajibu amsaidie chakula au nguo akiwa na uwezo.

Kama yeye hana uwezo, basi awaamrishe wanziwe kumpa mtu yule chakula au nguo, kwani kumpa chakula au kumvisha asiye na nguo ni miongoni mwa mambo mema ambayo imetupasa kuamrisha.

Kukataza maovu njiani ni kama vile kumuona mtu akimuonea mwenziwe na kumpiga bure pasi na sababu au anampora mali yake. Hapa ndipo inampasa mkaa njiani aukemee uovu ule na kumsaidia anayedhulumiwa ikiwa anaweza na kama hawezi peke yake basi atafute msaada wa watu ili wamnusuru mdhulumiwa, na Allah ndiye ajuaye zaidi.

Kadhalika katika jumla ya adabu za baraza ni kumtaka maghfira Mwenyezi Mungu Mtukufu wakati ainukapo barazani.

Kwani huenda akawa ameteleza wakati wa baraza kwa kusema au kutenda lililokatazwa, basi hiyo Istighfaari itakuwa ndio kituo cha kosa hilo.

Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie alikuwa anapotaka kuinuka barazani husema {kiarabu};

( SUB-HAANAKA ALLAAHUMMA WABIHAMDIKA ASH-HADU AN LAA ILAAHA ILLA ANTA ASTAGHFIRUKA WA ATUUBU ILAYKA) na alipoulizwa sababu ya kusema hivyo alijibu; “ni kafara ya (kosa / dhambi ) inayopatikana barazani” Tirmidhiy

ADABU ZA BARAZA

Muislamu maisha yake yote ni ya unyenyekevu, na yenye kufuata mfumo wa Uislamu.

Mfumo ambao unazigusa nyanja zake zote za maisha yake ya kila siku.

Katika mfumo huu kamili wa maisha, muislamu anafundishwa hata jinsi ya kukaa, ake vipi katika baraza na akeje na wenzake barazani.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *