MTUME AWEKEWA VIKWAZO

Makurayshi walipoona na kutambua kuwa njia, mbinu na hila zote walizozitumia ili kupambana, kuzuia na hatimaye kuliua kabisa wimbi la harakati za dawah ya Bwana Mtume zimegonga ukuta, hazikuzaa matunda yoyote bali ndio zilizidi kulichochea wimbi hilo.

Wakaona uislamu unazidi kudhihiri na kuenea kwa kasi kubwa isiyoweza kuzuilika. Wakaona wanazidi kuwapoteza watu muhimu na mihimili kwa upande wao na watu hao hao kuwa ni sababu ya uislamu kuzidi kupata nguvu na himaya.

Walipoona kukua kwa nguvu ya waislamu, waislamu ambao walikuwa wakiziswali swala zao kwa uficho mkubwa sasa wanathubutu na kujasiri kuswali hadharani mbele ya macho yao katika haram (eneo takatifu) ya Al–kaaba.

Wakaweza kusoma Qur-ani mbele ya kadamnasi ya makurayashi, jambo ambalo halikupata kufanywa huko nyuma.

Hapa sasa ndipo makurayshi walipohemewa wasijue la kufanya hasa walipokuwa hawawezi kukabiliana na Bwana Mtume kwa hoja.

Baada ya kutafakari na kuumiza vichwa kwa muda mrefu wakaibuka na kile walichoamini kuwa ndio silaha kali itakayoua na kuangamiza kabisa harakati za Nabii Muhammad.

Silaha hii haikuwa nyingine bali ni ile silaha ya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na kijamii, silaha ambayo imekuwa ndio mtindo wa mabeberu na madhalimu wa leo.

Mwanasira mkubwa Is-haaq – Allah amerehemu – anatusimulia hali ilivyokuwa, anasema;

“Makurayshi walipoona kwamba maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – wamefikia katika nchi ambayo wamepata amani na kwamba (mfalme) Najaash amewazuia (amekataa kuwatoa) wale waliokimbilia kwake. Na (waliopoona) kwamba Umar amesilimu, yeye na Hamzah Ibn Abdil–Mutwalib wamekuwa pamoja na Mtume wa mwenyezi Mungu na maswahaba wake na Uislamu ukaanza kuenea katika makabila (mbali mbali ya Waarabu). Walikutana na kula njama za pamoja katika kuweka azimio la pamoja dhidi ya Baniy Haashim na Baniy Mutwalib (koo za Mtume). Wakaweka azimio la kutokuwaolea wala kuwaoza, kutokuwauzia chochote wala kununua kutoka kwao. Wakakongamana kwa hilo na kuandika azimio la mkataba, kisha wakalibandika azimio hilo ndani ya al-Kaaba ili kuzitia nguvu nafsi zao. Makurayshi walipofikia uamuzi huo, Baniy Hashim na baniy Mutwalib wakaungana pamoja na Mzee Abu Twaalib wakaingia katika ngome / boma lake. Alitoka katika baniy Haashim Abu Lahab – Abdul–Uzzah Ibn abdul-Mutwalib akaungana na Makurayshi dhidi ya jamaa zake.”

Kwa mujibu wa wanazuoni wa sira na taarikh (Historia) tukio hili la vikwazo lilikuwa katika mwaka wa saba wa Utume.

Hivyo ndivyo Baniy Haashim na Baniy Mutwalib walivyozuiliwa katika boma la Abu Twaalib pamoja na wanawake na watoto wao, wakiwa hawana mawasiliano yoyote na yeyote.

Hawapati chakula, maji wala kitu chochote. Makurayshi wakazidisha ukatili wao mpaka ikafikia mfanyabiashara yeyote anayekuja mjini makkah kuleta bidhaa za mazao ya chakula wao (makurayshi) humuwahi akiwa bado nje ya mji wakainunua bidhaa yote aliyokuwa nayo kwa maradufu ya thamani.

Walifanya hivyo ili kuhakikisha kuwa hakuna chakula kinachowafikia Waislamu mpaka wasalimu amri na waache harakati zao. Abu Lahab na Abu Jahli ndio waliokuwa viongozi wa kusimamia harakati hizi za vikwazo dhidi ya Waislamu.

Abu Lahab, yeye alikuwa akiwachochea wafanya biashara wawapandishie bei ya bidhaa Waislamu ili washindwe kununua.

Nao wafanya biashara, kwa upande wao walikuwa wakuitikia wito huu wa Abu Lahab wakiwapandishia bei waislamu mara dufu ya mara dufu.

Muislamu akifikishwa hapo, hushindwa kununua chochote na kuamua kurudi kambini mikono mitupu na kuwaona watoto wakilizana kwa njaa.

Ama Abu Jahli, yeye daima alikuwa macho kuhakikisha kuwa vikwazo vinatekelezwa ipasavyo na hakuna mtu yeyote anayekwenda kinyume na maazimio ya vikwazo dhidi ya Waislamu.

Abu Jahli alifanya hivyo ili kuhakikisha kuwa vikwazo vinafikia lengo lake ambalo lilikuwa ni kuwalazimisha Baniy Haashim na Baniy Mutwalib waache kumkingia kifua Bwana Mtume na na wamsalimishe mikononi mwa makurayshi wamuue.

Au Bwana Mtume aache na kuzitupilia mbali harakati zake za Daawah na kwa hali hiyo watakuwa wameukatilia mbali mzizi wa fitna “Uislamu” kama walivyoliona hilo kwa maono na mtazamo wao.

Vikwazo hivi vikaendelea kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu ilhali Baniy Haashim na Baniy Mutwalib (Waumini na wasio waumini) wote kwa pamoja wakiwa kambini katika boma la Mzee Abu Twaalib.

Hali ikawawia ngumu mpaka wakalazimika kula majani na mizizi ili kujinusuru maisha yao kutokana na janga hili la njaa ambalo lilisababishwa na vikwazo vya makurayshi dhidi yao. Habari na vilio vilivyotokana na vikwazo hivi zikawafikia watu na Waarabu waliokuwa wakija Makkah katika musimu wa Hijjah.

Watu hawa wakawa wakiulizana juu ya Daawah hii iliyowapelekea Makurayshi kutokuwa na huruma hata chembe na kuwawekea ndugu zao wenyewe vikwazo hivi vibaya ambavyo havijapata kutokea katika historia ya Waarabu.

Baada ya kujiuliza huku, Waarabu wakatambua kuwa ni lazima Daawah hii itakuwa ni kitu hatari sana, kwa hivyo wakataka kujua hakika na ukweli wake.

Wakaanza kuwatuma vijana wao kwenda kule kambini kupeleleza habari za Daawah hii ya Nabii Muhammad na madhumuni/malengo yake.

Hii ikawa ndio sababu ya kuenea kwa habari za Uislamu baina ya Waarabu. Mambo yakawa kinyume na matarajio ya Makurayshi, kwani lile walilotaka kulificha na kulizuia lisienee sasa ndilo linafichuka na kuenea kwa kasi.

Tena sasa Mtume hapati taabu ya kulingania Uislamu bali watu wenyewe sasa ndio wanazitafuta habari za Uislamu.

Habari za Uislamu zikafika mjini na vitongojini (Vijijini). Hapa sasa, Makurayshi wakatambua kwamba vikwazo vyao vimepita bure, havikutimiza lengo lake.

Wakahisi kuwa Waarabu hawakupendezwa wala kufurahishwa na kitendo chao hiki kibaya na wakachelea kupoteza heshima na utukufu wao baina ya Waarabu kutokana na ukatili wao huu.

 Hapa sasa, Makurayshi wakaanza kugawanyika na kutofautiana katika swala zima la vikwazo.

 Baadhi yao wakajiwa na hisia za utu na kuona ubaya wa kitendo walichokifanya dhidi ya ndugu zao wenyewe.

Wakaanza kulidiriki swala hili kwa njia za uficho, wakaanza kutoa misaada ya chakula kwa ndugu zao hawa waliowekewa vikwazo na kuishi kambini.

Miongoni mwa watu hawa waliwathiriwa na hisia hizi za utu, alikuwa ni Bwana Hishaam Ibn Amri.

Huyu alikuwa akimchukua ngamia wake na kumbebesha shehena ya chakula, kisha hutoka nae usiku katika hali ya uficho na kwenda nae mpaka katika kambi ya wahanga/waathirika wa vikwazo vile.

Akifika huko, humfungua na kushusha shehena yote ya chakula kwa wahanga bila ya kuchukua chochote kutoka kwao kama malipo.

Bwana yuyu aliendelea na zoezi lake hili mpaka pale Makurayshi walipongamua na kumtolea maneno ya ukali kiasi cha kutaka kumuua.

 Abu Sufyaan Ibn Harb akawambia nduguze Makurayshi

“Mwacheni! Mtu anawaunga nduguze. Ama mimi ninaapa kwa jina la Allah, lau sisi sote tungelifanya kama afanyavyo yeye ingelikuwa ni jambo bora kabisa”

Miongoni mwa waliokuwa wakipeleka chakula alikuwemo pia Bwana Hakimu Ibn Hizaam.

Siku moja akiwa katika harakati zake za kupeleka chakula kama alivyojipangia akiwa na mtumishi wake amebeba ngano, akakutana njiani na mtu muovu Abu Jahli.

Bwana Hakiim alikusudia kumpelekea chakula kile shangazi yake Bi Khadijah mkewe Bwana Mtume ambaye alikuwa ni miongoni mwa wahanga wa vikwazo kule kambini.

Abu Jahli akamwambia hakim

“Unawapelekea chakula Baniy Haashim? Wallah huendi wewe wala chakula chako mpaka nikufedheheshe mjini Makkah!”

 Wakiwa katika mzozo huo, akawatokea Abul-bakhtary Ibn Hishaam, akamuuliza Ab Jahli:

 “ Una nini wewe na yeye ? chakula chake, anampelekea shangazi yake, hivi unamzuia asimpelekee? Muachie aende zake”

Abu Jahli akagoma katakata, mpaka wakaanza kutukanana. Abul-bakhtariry akachukua mfupa wa ngamia akampiga nao Abu Jahli na kumtoa ngeu, hapa ndipo Bw. Hakim akapata penyo akashika njia na kwenda zake

 

MTUME AWEKEWA VIKWAZO

Makurayshi walipoona na kutambua kuwa njia, mbinu na hila zote walizozitumia ili kupambana, kuzuia na hatimaye kuliua kabisa wimbi la harakati za dawah ya Bwana Mtume zimegonga ukuta, hazikuzaa matunda yoyote bali ndio zilizidi kulichochea wimbi hilo.

Wakaona uislamu unazidi kudhihiri na kuenea kwa kasi kubwa isiyoweza kuzuilika. Wakaona wanazidi kuwapoteza watu muhimu na mihimili kwa upande wao na watu hao hao kuwa ni sababu ya uislamu kuzidi kupata nguvu na himaya.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *