SABABU ZA KUTAYAMAMU

Muislamu hatayamamu kwa sababu tu amejisikia kufanya hivyo, akaacha kutawadha.

Bali uislamu umeweka hali na mazingira maalumu, ambamo humo ndimo mtu anaruhusiwa kuitumia na kuitekeleza sheria hii ya tayamamu.

Hali na mazingira haya ndio yanayojulikana kisheria kama sababu za kutayamamu.

Sababu zinazomuhalalishia muislamu kutayamamu ni nne kama ifuatavyo;

1.      Kukosa maji. Mtu anaweza kuyakosa maji kinadharia au kisheria.

Kuyakosa maji kinadharia ni kama vile mtu kuwa safarini na akayakosa maji au akawa na maji yasiyomtosheleza kutawadhia.

Ama kuyakosa maji kisheria ni mtu kuwa na maji lakini akawa anayahitajia kwa kunywa yeye mwenyewe au hayawani mwingine ambaye ni muhtaramu.

Ni mamoja anataka kuyanywa sasa hivi au baadaye. Kutayamamu kwa sababu ya kukosa maji ni ruhusa itokanayo na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu

 “…………… NA HAMKUPATA MAJI, BASI KUSUDIENI (TAYAMAMUNI) UDONGO (MCHANGA) ULIO SAFI (TWAHARA) ………..” (5:6)

Katika sunnah, kukosa au kutokupata maji ni sababu inayomuhalalishia mtu kutayamamu kutokana na hadithi hii; Imepokelewa kutoka kwa Imraan Ibn Huswain amesema;

Tulikuwa safarini pamoja na Mtume – Rehema na Amani zimshukie – akawaswalisha watu (maswahaba), tahamaki kuna mtu mmoja amejitenga na watu wale (hakuswali pamoja nao).

 Mtume akamwambia

“Ni jambo gani lililokuzuia usiswali pamoja nasi ? Akajibu mtu yule; Ewe mtume wa Mwenyezi Mungu, limenipata janaba na (hapa) hapana maji (ya kukoga). Mtu akamwambia; Tumia mchanga, kwani huo unakutosheleza.” Bukhaariy na Muslim.

2.      Maji kupatikana mbali. Mtu atakapokuwa mahala ambapo hakuna maji karibu.

Kutokea hapo alipo mpaka kuyafikia maji ni umbali wa kilometa mbili na nusu (2.5km) na kuendelea/na zaidi.

Katika mazingira haya mtu anaruhusiwa kutayamamu na wala haimuwajibikii kuhangaika kuyatafuta maji kwa sababu ya taabu, shida inayoweza kumpata katika utafutaji huo.

3.      Kushindwa kuyatumia maji. Kushindwa kunaweza kuwa kinadharia au kisheria.

Kushindwa kutumia maji kinadharia ni kama vile maji yanapatikana karibu na mahala alipo, lakini baina ya mahala alipo na yalipo maji kuna adui kama vile majambazi wanaopora na kunyang’anya mali na pengine kuua au kuna mnyama hatari kama vile simba au chui.

Katika hali na mazingira kama haya, muislamu anapewa ruhusa ya kutayamamu ili asiitie hatarini nafsi yake, kwa sababu tu ya kutafuta maji ya kutawadhia. Tusome;

“… WALA MSIJITIE KWA MIKONO YENU KATIKA MAANGAMIZO …” (2:195) Ama kushindwa kuyatumia maji kisheria kunapatikana katika sura hizi;

a.      Kuchelea kuzuka kwa maradhi kwa sababu ya kutumia maji.

b.      Kuzidi kwa maradhi ikiwa mtu atatumia maji.

c.       Maradhi kuchelewa kupona iwapo atatumia maji. Ni mamoja ikiwa mtu atayajua haya kutokana na uzoefu alionao au kwa kuambiwa na daktari bingwa.

Katika hali zote hizi mtu anaruhusiwa kutayamamu na wala haimuwajibikii kutawadha.

Haya ndio mafundisho na eleweko linalopatikana katika hadithi hii ya Bwana Mtume; Imepokelewa kutoka kwa Jaabir -Allah amuwiye radhi – amesema;

Tulisafiri, mtu mmoja miongoni mwetu alipatwa na jiwe likampasua kichwa chake. Kisha (majeruhi huyu) akajiotelea (usiku). Akawauliza wenzake;

Je, mnanipatia ruhusa ya kutayamamu (kutokana na jeraha nililo nalo ?) Wakamwambia hatukupatii ruhusa ilhali unaweza kutumia maji.

Mtu yule akaoga (ili apate uhalali wa kuswali) akafa (kutokana na kudhuriwa na maji).

 Tuliporudi safari na kufika kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie – akaelezwa habari ile (ilivyokuwa). (Mtume) akasema

 “Wamemuua, Allah awauwe na wao!! Kwa nini wasiulize kama hawajui, hakika dawa ya ujinga ni kuuliza. Hakika si vinginevyo ilikuwa inamtoshea kutayamamu na kufunga kitambaa kwenye jeraha lake, kisha akapakaza juu yake (maji) na akaosha sehemu nyingine ya mwili wake.” Abuu Daawoud.

4.      Baridi kali.

Hii ndio sababu ya nne inayomuhalalishia mtu kutayamamu badala ya kutawadha.

Iwapo mtu atakuwa na yakini kuwa atadhurika kutokana na kutumia maji katika mazingiria ya baridi kali sana na ikawa hana njia yoyote ya kumuwezesha kuchemsha maji, ataruhusika kisheria kutayamamu.

Hii ni kwa sababu swahaba wa Mtume Amri Ibn Al-aaswi- Allah amuwiye radhi- alitayamamu kutokana na janaba lililompatia, akaacha kuoga kwa kuchelewa kuangamia (kufa) kutokana na baridi.

Bwana mtume – Rehema na Amani zimshukie-akalikiri hili na wala asilipinge, kwa hivyo likawa ni miongoni mwa mambo/sababu zinazomuhalalishia mtu kutayamamu.

Riwaya hii imepokewa na Abuu Daawoud na kusahihishwa na Ibn Hibaan na Al-Haakim.

 TANBIHI:

Ni vema ikakumbukwa kwamba katika hali hii ya kutayamamu kwa sababu ya baridi itamuwajibikia mtu huyo kuzikidhi na kuzirudia kuziswali swala zote alizoziswali kwa tayamamu iliyotokana na sababu hiyo.

Hili lifanyike mara tu atakapoweza kuyatumia maji.

Muislamu atakapotokewa na mojawapo ya mambo manne hayo tuliyoyataja, ndio anapata ruhusa na kibali cha kutayamamu badala ya uoga au kutawadha kwa mujibu wa sheria.

 

SABABU ZA KUTAYAMAMU

Muislamu hatayamamu kwa sababu tu amejisikia kufanya hivyo, akaacha kutawadha.

Bali uislamu umeweka hali na mazingira maalumu, ambamo humo ndimo mtu anaruhusiwa kuitumia na kuitekeleza sheria hii ya tayamamu.

Hali na mazingira haya ndio yanayojulikana kisheria kama sababu za kutayamamu.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *