KANUNI:
Kila linalopingana na suna yeyote miongoni mwa suna za swala tulizokwisha zibainisha katika darasa zilizotangulia. Hilo linaingia ndani ya uzio wa yaliyo karaha kutendwa ndani ya swala.
Na makruhu (lilio karaha): Ni kila lile ambalo mswaliji akiacha kulitenda ndani ya swala hulipwa thawabu na wala haadhibiwi kwa kulitenda.
Kwa mfano kuacha takbira za maguroguro, yaani kuhama kutoka katika nguzo moja hadi nyingine, ni makruhu. Kwa sababu kuzileta hizo takbira ni suna. Na pia kuacha kuleta dua ya ufunguzi wa swala ni makruhu, kwa sababu ni suna kuileta.
Isipokuwa kuna baadhi ya mambo maalumu ambayo ni suna kujiepusha nayo na ni karaha kwa mswaliji kuyatenda. Yafuatayo ni baadhi ya mambo hayo:
KUGEUKA KWA SHINGO NDANI YA SWALA:
Ni jambo la makruhu mswaliji kugeuka kwa kuizungusha shingo yake ndani ya swala ila kama kuna dharura implekeayo kufanya hivyo.
Imepokelewa kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Allah mtukufu haachi kuwa ni mwenye kumuelekea mja wake ndani ya swala yake maadamu hajageuka. Akigeuka naye (Allah) hukengeuka naye (mja wake)”. Abuu Daawoud & wengineo
Na Bwana Mtume amekwisha bainisha kwamba kugeukageuka ndani ya swala hakika si vinginevyo ila:
“Ni uporaji anaoufanya shetani katika swala ya mja” Bukhaariy
Hii ni kwa sababu kugeuka ndani ya swala kunapingana na unyenyekevu unaotakiwa ndani ya swala.
Ama kukiwa na dharura inayomlazimisha kugeuka kama vile kumuangalia adui anayemnyemelea mathalan, katika hali hii si karaha kugeuka.
Hii ni iwapo ugeukaji huo utahusisha shingo tu bila ya kifua.
Ama iwapo mswaliji atageuka kwa kutumia kifua akawa amekengeuka na Qiblah, hapo swala yake itabatilika kwa kuacha kwake nguzo ya swala ambayo ni kuelekea Qiblah.
Ama kutupa jicho tu bila ya kugeuka si vibaya, ijapokuwa si vizuri kufanya hivyo bila ya kuwa na dharura.
Imekuja katika hadithi ya Aliy Ibn Sheibaan-Allah amuwiye radhi-amesema: Tulifika kwa Mtume wa Allah-rehema na Amani zimshukie-tukaswali pamoja naye. Akamuona kwa jicho pembe mtu mmoja hanyooshi mgongo wake katika rukuu na sijida, akasema:
“Hana swala hasiyeunyoosha uti wa mgongo wake”.-Yaani hatulizani katika rukuu yake. Ibn Hibbaan
KUANGALIA JUU:
Si suna kwa mswaliji kuswali huku anaangalia juu, kwani kufanya hivyo ni karaha. Imepokelewa kutoka kwa Anas-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Wana nini watu wanaonyanyua macho yao juu ndani ya swala zao?”
Kisha akasema: “Wakome kufanya hivyo au macho yao yatapokonywa”. Bukhaariy
KUFUNGA NYWELE AU KUPANYA NGUO:
Ni karaha kwa mswaliji kuswali huku amefunga nywele au kupanya nguo. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Nimeamrishwa kusujudu kwa kutumia viungo saba na wala nisikunje nguo wala nywele”.
Bukhaariy
KUSWALI NA ILHALI CHAKULA KIKIWA TAYARI KIMETENGWA:
Ni karaha kwa mswaliji kuswali na ilhali chakula kiko mbele yake tayari kwa kuliwa na nafsi yake ikawa inakitamani.
Ukaraha huu unatokana na kule kushughulishwa nafsi, jambo ambalo huondosha unyenyekevu ndani ya swala.
Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah amuwiye radhi-amesema: Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
“Itakapowekwa Ashaa (chakula cha usiku) ya mmoja wenu na swala ikakimiwa, basi na anzeni na Ashaa hiyo na wala hasifanye haraka mpaka amalize”.
Bukhaariy & Muslim
KUSWALI KATIKA HALI YA KUBANWA NA HAJA NDOGO AU KUBWA:
Mswaliji hatakiwi kuswali na huku amebanwa na haja ndogo au kubwa, kwa sababu katika hali kama hii haitamkinika kuipa swala haki yake.
Yaani unyenyekevu na kuhudhuria ndani ya swala kutakosekana. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Hakuna swala mbele ya chakula wala mtu anaposukumwa na vichafu viwili”. –Yaani haja ndogo na kubwa. Muslim
KUSWALI HUKU UNASINZIA:
Ni karaha kuswali katika hali ya kusinzia sana, kwa sababu ni muhali katika hali hii mtu kudhibiti anachokisema na kukifanya ndani ya swala yake.
Imepokelewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Ataposinzia mmoja wenu na ilhali anaswali, basi na alale mpaka usingizi umuishe. Kwani mmoja wenu akiswali huku anasinzia, huenda akawa analeta istighfaari na kumbe anajitukana mwenyewe (anajilaani)”. Bukhaariy & Muslim
KUSWALI KATIKA SEHEMU ZIFUATAZO:
Ni karaha kwa mswaliji kuswali hamamuni (mahala pa kukoga pa jumuia), njiani/barabarani, sokoni, makaburini, kanisani, majaani na mahala ipumzikiapo mifugo.
Ukaraha huu unatokana na dhana ya kuwepo najisi katika baadhi ya sehemu hizo na kushughulika moyo katika sehemu nyingine.
Imepokelewa kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Ardhi yote ni msikiti (ni mahala pa kuswalia) ila makaburini na hamamuni”.
“Msiswali katika mapumzikio ya ngamia”. Ibn Hibbaan