Nasabu yake Bwana Mtume – Allah amrehemu na kumshushia amani – kwa upande wa mama yake:-
Yeye ni Muhammad Bin Aaminah Bint Wahab Bin Abdi Manaf Bin Zuhrah Bin Hakiym. Huyu Mzee Hakiym ndiye Kilaab ambaye ni babu wa tano wa Mtume kwa upande wa baba yake.
Tumekwishaeleza huko nyuma kwamba huyu Mzee Qusway ambaye ni babu wa nne katika
mlolongo wa babu zake Mtume ndiye aliyeweka mpango wa mji wa Makkah na akawaunganisha pamoja Waarabu kwa kuondosha ukabila.
Baada ya kifo cha Mzee Qusway, hatamu za uongozi wa mji wa Makkah zilishikwa na babu wa pili wa Mtume Mzee Haashim. Huyu alikuwa tajiri na ndiye aliyeasisi mfumo wa biashara za Kusi na kaskazi kama ulivyoelezwa na Qur-ani:-
“ILI KUWAFANYA MAKURESHI WAENDELEE. WAENDELEE NA SAFARI ZAO ZA WAKATI WA KUSI (kwenda yaman) NA WAKATI WA KASKAZI (kwenda Shamu, ndio maana tukajaalia jeshi la ndovu kushindwa) (102:1-2)
Pia Mzee huyu ndiye aliyesimamia usambazaji wa maji na chakula kwa wageni wote wanaokuja kufanya ibada katika Al-kaaba na hili linaashiria ukarimu walikuwa nao Waarabu.
Naye ndiye mtu wa mwanzo aliyeanzisha uokaji na usambaji wa mikate katika mji wa Makkah na hili linaonyesha ni jinsi gani alivyowajibika kwa jamii iliyompa dhamana ya uongozi.
Mwenyezi Mungu aliitakasa nasabu ya Mtume kutokana na uchafu wa kijahilia.
Mababa zake wote walikuwa ni watu watukufu na viongozi kama ambavyo mamama zake pia walikuwa ni wanawake waungwana,watakasifu wasio na uchafu wowote.
Lifuatalo ni jedwali na kielelezo kinachoonyesha nasabu ya Mtume kuanzia kwa babu wake wa nne Mzee Qusway. Jedwali hili litatusaidia kuelewa koo za Maqureshi huko mbele.