Leo ulimwenguni kote kutokana na kile kinachojulikana kama wimbi la kwenda na wakati, uhuru na haki ya mtu kufanya/kuishi atakavyo; si jambo la kushangaza wala kustaajabisha kuwaona vijana wa kiume wakiwa wamejipamba kwa kuvaa mikufu, pete na hata hereni za dhahabu.
Hili leo si geni tena bali ni jambo la kawaida na fakhari hata katika miji ya mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi, ambako asilimia kubwa ya wakazi wake ni wafuasi wa dini ya Kiislamu kwa miongo ya miaka.
Uvaaji huu wa dhahabu kwa vijana wa kiume umeingizwa pande zetu hizi za Afrika ya Mashariki na vijana waliotoka huku kwenda nchi za Ulaya kutafuta ajira hasa ya ubaharia.
Hawa waliporejea wakiwa wameuiga utamaduni huo wa kigeni na kuwaathiri vijana wengine, limbukeni wenye kuiga kila kiingiacho mjini.
Utamaduni huu wa vijana wa kiume kujipamba kwa kuvaa dhahabu unakwenda kinyume na utamaduni wa mila ya Kiislamu.
Mwenyezi Mungu amemuumba mwanamume na Mwanamke na kumpa kila mmoja maumbile na tabia zinazotofautiana na mwenzake.
Ikiwa hili linaashiria kitu, basi si kingine bali ni kutofautiana pia katika nafasi na majukumu ya kila mmoja wao. Nadharia inaonyesha kuwa tabia na maumbile ya mwanaume ni ukakamavu na ugumu, wakati ambapo tabia na maumbile ya kike ni ulaini na ulegevu.
Uislamu unamtaka mwanaume alelekee katika mazingira yaliyo mbali na udhaifu,unyonge na anasa zinazoweza kunlegeza ili aweze kuwa imara na mwenye nguvu katika kupambana na harakati za maisha ya kila siku, ambapo sehemu kubwa ya jukumu hilo amebebeshwa yeye na sheria .
Sasa kwa kuzingatia kuwa madini ya dhahabu na hariri ni vitu vya anasa ambavyo humfanya mvaaji aonekane amependeza machoni mwake yeye mwenyewe kwanza na machoni mwa wengine na natija yake ni kuvaana na maumbile ya kupendeza ambayo ni ulaini na ulegevu.
Pengine kwa njia moja au nyingine hii ndio inaweza kuwa hekima/falsafa ya kuharamishwa dhahabu na hariri kwa wanaume kwa kuwa inakubaliana na tabia na maumbile yao.
Hebu tujaribu kuwa wakweli, tuwatie katika mizani ya haki na uadilifu wanaume wenye kuvaa dhahabu na wasiovaa dhahabu, tutagundua nini?
Bila ya shaka mtakubaliana na mimi kuwa ipo tofauti ya dhahiri baina yao, wavaao dhahabu watakuwa wameathirika na tabia na maumbile ya kike.
Taathira hii utaiona katika mwendo wao, uzungumzaji wao, uvaaji wao na wakati mwingine huiga hasa tabia za kike kama vile kusuka nywele na kutumia vipodozi.
Ni kweli usiopingika kwamba kujua hekima/falsafa ya kuharamishwa dhahabu na hariri kwa wanaume, hii ni elimu isiyo na manufaa na ni ujinga usiodhuru.
Usiulize hekima kwa kuwa kumeshurutishwa katika kuulizia hekima ya amri au makatazo, awe huyo muamrishaji/mkatazaji analingana sawa na kufanana na huyo muamrishaji/mkatazwaji na hapa ni suala la Mungu Muumba Muamrishaji na mwanadamu kiumbe muamrishwa.
Kwa mantiki hii mwanadamu hana budi kuikubali na kuipokea amri kwa kuwa Mola wake ameamrisha/amekataza,kisha baada ya kutekeleza aliloamrishwa ndipo anaweza kutafuata kujua hekima/falsafa ya amri ile.
Lakini kule kujua hekima/falsafa iliyomo katika amri au katazoisiwe ni sharti ambalo kwanza ni lazima litimizwe kabla ya kuamrika au kukatazika. Muislamu wa kweli anaambiwa na Mola wake:
“HAIWI KWA MWANAUME ALIYEAMINI WALA KWA MWANAMKE ALIYEAMINI, ALLAH NA MTUME WAKE WANAPOKATA SHAURI,WAWE NA HIARI KATIKA SHAURI LAO. NA MWENYE KAMUASI ALLAH NA MTUME WAKE, HAKIKA AMEPOTEA UPOTOFU ULIO WAZI (kabisa) [33:36]
Kuharamishwa uvaaji wa dhahabu kwa wanaume kumethibiti katika hadithi nyingi sahihi zilizopokelewa kutika kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu –Rehema na Amani zimshukie.
- Amepokea (riwaya) Imamu Bukhaariy, Muislam na Ahmad kwamba Mtume wa Allah “Amekataza (kuvaa) pete ya dhahabu”.
- Imepokelewa kutoka kawa Ibn Abbaas-Allah awawiye radhi-kwamba Mtume wa Allah aliiona pete ya dhahabu kidoleni mwa mtu, akamvua na kuitupa (huku) akisema
“ Mmoja wenu analikusudia kaa la moto na kulivaa mkononi?” Mtu yule akaambiwa baada ya kwenda zake mtume “ Itwae pete yako unufaike nayo. Akawajibu Wallah hapana, kamwe sitaichukua ikiwa aliyeitupa ni Mtume wa Allah –Rehema na Amani zimshukie.” Muislam
- Na katika jumla ya riwaya zilizopokelewa kwamba Mtume wa Allah –Rehema na Amani zimshukie amesema : “ Ye yote mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho basi asivae hariri wala dhahabu.” Al-musnad {Musnadul–Imam Ahmad}