Ni suna thabiti kutoka kwa Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie–kusujudu sijida ya msomo. Suna hii inawahusu wote wawili; msomaji wa Qur-ani na msikilizaji, iwe ni ndani ya swala au nje ya swala.
I/. SABABU YA KUSUJUDU SIJIDA YA MSOMO:
Suna ya sijida ya msomo inapatikana kwa moja ya mambo mawili haya:-
1. Kusoma aya ya Qur-ani ambayo ndani yake kuna paliposuniwa kusujudu, au
2. Kuisikia aya hiyo ikisomwa na mtu mwingine.
II/. DALILI/USHAHIDI WA SIJIDA YA MSOMO:
Kama tulivyokwishaeleza kwamba sijida ya msomo ni suna iliyothibiti kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na ushahidi ni hadithi zifuatazo:-
Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar–Allah awawiye radhi– amesema:
“Alikuwa Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie –akitusomea sura ambayo ndani yake kuna sijida. Basi (hapo) husujudu nasi husujudu (pamoja nae) kiasi hata mmoja wetu hapati mahala pa kuliweka paji lake la uso (kutokana na wingi wa watu)”.
Na katika riwaya iliyopokelewa na Abuu Daawoud:
“Mtume– Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akitusomea Qur-ani. Anapoipitia (aya ya) sijida hukabiri na kusujudu, nasi tukasujudu pamoja nae”.
III/. FADHILA ZA SIJIDA YA MSOMO:
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie–amesema:
“Mwanadamu ataposoma aya ya sijida na akasujudu, shetani hujitenga na kulia akisema: Ee ole wangu, mwanadamu ameamrishwa kusujudu akasujudu, basi yamuelea kupata pepo ya Allah.Nami nimeamrishwa kusujudu nikakhalifu amri ya (Mola wangu ), basi nitaingia motoni”. Muslimu.
IV/. HUKUMU YA SIJIDA YA MSOMO:
Sijida ya msomo hukumu yake ni suna ambapo mtu akisujudu hupata thawabu na akiacha kusujudu hapati dhambi. Lakini tu atakuwa amejidhulumu mwenyewe fursa ya kujaza na kuithakilisha mizani yake ya kheri. Dalili ya haya ni hadithi zifuatazo:-
Imepokelewa na Sayyidna Umar–Allah amuwiye radhi–amesema Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie:
“Enyi watu hakika sisi (tunaposoma Qur-ani) tunazipitia aya za sijida. Atakayesujudu (mahala hapo) hakika atakuwa amesibu (amepatia ) na asiyesujudu, basi hapana dhambi juu yake”. Bukhaariy
Na imekuja katika riwaya ya Ibn Umar–Allah awawiye radhi:
“Hakika hakutufaradhishia kusujudu ila tutakapo”.
V/. SHARTI ZA SIJIDA YA MSOMO:
Sharti zilizoshurutizwa katika sijida ya msomo ni nafsi ya sharti zilizoshurutiziwa swala. Sharti hizo ni pamoja na
twahara ya hadathi ndogo na kubwa.
Kuelekea Qiblah wakati wa kusujudu, na
Kusitiri tupu.
Na baki ya sharti nyingine zilizotajwa katika kusihi kwa swala.
VI/. NAMNA YA KUSUJUDU SIJIDA YA MSOMO.
Ni kusujudu msomaji na msikilizaji wa Qur-ani anapoifia aya ya sijida.
Kusujudu sijida moja iliyo baina ya takbira mbili, takbira ya kuliweka paji la uso juu ya ardhi na takbira ya kuliinua kutoka hapo.
Kisha hutoa salamu na wala hasomi Tashahudi.
Imependelewa kwa mtu mwenye kusujudu sijida ya msomo amuombe Allah kwa dua njema, hii ni kwa sababu katika sijida ndipo mahala mja huwa karibu zaidi na Mola wake. Kwa mantiki hii na kujibiwa dua akiomba pia huwa karibu zaidi mahala hapo kuliko mahala pengine.
VII/. MAHALA ZILIMO SIJIDA ZA MSOMO:
Jumla ya sijida za msomo ndani ya Qur-ani Tukufu ni kumi na tano kama ifuatavyo:-
SURA AYA
Al-a’araaf (7) :206
Ar–ra’ad (13):15
An-nahl (16) :49
Bani Israil (17):107
Maryam (19) :58
Al–Hajj (22):18
Al–Hajj (22):77
Al–Furqaan (25) :60
An–naml (27):25
As-sajdah (32):15
Swaad (38):24
Fuswilat (41):37 (Ha-Miym–sajdah)
An–najm (53):62
Al-inshqaaq (84):02
Al-alaq (96):19