Msemo “Rushwa ni adui wa haki”, kelele zinapopigwa ulimwenguni kote na wanasiasa, viongozi na serikali na wale wa dini dhidi ya rushwa.
Haya yote ni ishara na dalili wazi juu na namna jamii inavyoathirika na kukerwa na mdudu mbaya huyu, rushwa.
Rushwa ni mdudu mwenye athari mbaya sana kwa jamii, mdudu anayeua bila huruma haki za kimsingi na za kijamii.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuasa:
“WALA MSILIANE MALI ZENU KWA BATILI NA KUZIPELEKA KWA MAHAKIMU ILI MPATE KULA SEHEMU YA MALI YA WATU KWA DHAMBI NA HALI MNAJUA” [2:188].
Amesema swahaba wa Mtume-Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi-katika kuitafasiri aya hii: Katazo hili linamuhusu mtu mwenye kumiliki mali bila ya uhalali wowote, kisha akamuendea hakimu kutaka kupata uhalali wa kumiliki na ilhali anajua fika kuwa haki si yake.
Huyo aelewe kuwa anapata dhambi na anachokila ni haramu.
Aya inafahamisha kuwa hukumu ya huyu hakimu kumuhalalishia dhalimu na kumpa haki asiyoistahiki haibadilishi chochote hakika na ukweli.
Hakika itabakia pale pale mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa mali ile si haki yake na ukweli ni kuwa mali itabakia kuwa ni haramu inayompatia dhambi za uovu wake huo.
Kwa mantiki hii, hakimu muhalalishaji wa haramu hali anajua na dhalimu muhalalishiwa haramu hali nafsi yake inakiri kuwa haramu wawili hawa watashirikiana katika dhambi za uovu huu.
Mwenyezi Mungu anatukataza na kutuonya katika aya hii kula au kuchukua mali ya mtu kwa njia ya batili yaani kwa njia isiyo ya halali.
Kula mali ya mtu katika njia ya batili ni pamoja na kupokonya, kupora,kudhulumu,kupokea rushwa na kadhalika. Kwa nini Mwenyezi Mungu amesema:
” WALA MSILIANE MALI ZENU“, akatumia neno KULA badala ya KUCHUKUA.
Neno KULA limetumika kwa kuwa ndio makusudi na lengo kuu la kuchukua/kupata mali. Mporaji anapopora ili ale, dhalimu anadhulumu apate kula, mpokea rushwa anapokea pia kwa ajili ya Tumbo.
Hili ndilo lengo la kwanza, kisha ndio hufuatia mengine kama vile kuvaa,kujenga,kununua gari,shamba na kadhalika.
Ndio maana watu husikika wakisema (Fulani anakula mali za watu) wakiimanisha: Anachukua mali za watu bila ya uhalali,kwa njia batili.
Mwenyezi Mungu amewaumba wanadamu na akawapangia na kuwawekea sheria zitakazoyatawala maisha yao katika ulimwengu huu wa muda,ili waishi kwa amani,salama na utulivu.
Mwenye nguvu asimdhulumu mnyonge wala mkubwa asimuonee mdogo. Basi mfanyakazi anayepokea rushwa kwa ajili ya kutoa huduma,huyu anaivunja misingi ya amani katika jamii, anavuruga nidhamu/utaratibu wa sheria.
Huyu mbali ya kuwa ana hatia mbele ya mahakama adilifu ya Mwenyezi Mungu pia anaikosea jamii nzima kwa kuwa anapokea ujira kwa kuivunja amani.
Mtoaji wa rushwa pia haiepuki hatia kwa kuwa kutoa anatoa ujira kufisidi/kuharibu uadilifu. Mali anayoipokea mlaji rushwa ni moto na ataadhibiwa kwa uchukuaji wa mali hiyo adhabu kali kabisa, kwa sababu ya kuvunja kwake sheria ambayo misingi yake mikuu ni uadilifu na amani.
Hebu uone ubaya na athari ya rushwa kwa jamii kupitia mifano hali ifuatayo:
Serikali/Shirika la umma limetangaza nafasi za kazi.
Wananchi wenye sifa zinazotakiwa wakajitokeza kujaza nafasi hizo. Mtu aliyekabidhiwa na umma dhamana ya kuhoji watu hawa na hatimaye kuwaajiri wanaostahiki.
Huyu anayapiga teke maadili na muongozo wa kazi yake,badala ya kuwachagua watu kwa sifa husika, yeye anawachagua watu kwa vigezo vya udugu, na kwa kupewa rushwa.
Natija ya uchaguzi huu ni kuwapa ajira watu wasiostahili, jambo ambalo litasababisha utendaji mbovu usio na ufanisi, utendaji utakaopelekea kufilisika na hatimaye kufa kwa shirika ambalo ni mali ya umma.
Uharibifu wa mtu mmoja huyu mwenye maradhi hatari ya rushwa unasababisha kuathirika kwa jamii nzima ni kwa sababu hii ndiyo Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie –akaikemea vikali rushwa aliposema “Mtoaji na mpokeaaji rushwa (wataingia ) motoni”. At-twabraaniy.
Utamuona leo daktari anayetupilia mbali maadili ya kazi yake, anavua utu wake na kuuvaa unyama.
Anamuacha mgonjwa kufa mbele ya macho yake eti tu kwa sababu hakupewa chai (rushwa).
Huu ndio ukweli na sote tunishuhudia hali hii kila leo. Mdudu rushwa ameiondosha kabisa huruma ndani ya moyo wa daktari kiasi cha kuwa maisha ya binadamu mwenziwe hayana thamani kama hakupewa rushwa.
Ni kutokana na athari hii mbaya ya rushwa ndio Bwana Mtume –Allah amshushie Rehema na Amani –akasema “Allah amemlaani mtoaji na mpokeaji rushwa na mkaa kati yao”. Ahmad
Hebu tuangalie hakimu anayepewa dhamana ya kusimamia haki. Huyu kwa sababu ya kitu kidogo alichopewa (rushwa) anampa haki mtu asiyestahiki na kumnyima mwenye haki au anamfunga mtu kwa dhuluma kwa sababu tu kuna mtu anataka kumkomoa au anamuachia huru mtuhumiwa aliyetiwa hatiani na sheria kwa ajili ya kupewa rushwa.
Hizi ni baadhi tu za athari nyingi za rushwa kwa jamii. Rushwa ikienea katika jamii husika, tabia za watu zitaharibika,utu na heshima vitatoweka na badala yake unyama,chuki na uadui ndivyo vitaitawala jamii hiyo kama tulivyoona katika mifano yetu hai.
Mla rushwa ni mtu mbaya na hatari sana katika jamii. Huyu hana utu, hana haya wala huruma na ndio maana Bwana Mtume hakumuonea haya kumshushia laana za Mwenyezi Mungu.
Ewe ndugu yangu uliyelemazwa na maradhi ya rushwa hebu jiulize na kisha ujihurumie. Jee, unaweza kuibeba laana ya Mola wako?
Kulaaniwa na Mwenyezi Mungu maana yake ni kutengwa na Rehema za Mola duniani na akhera , Je, utasalimika ikiwa hukupata rehema za Mola wako?
Kutokupata rehema kunaamaanisha kupata ghadhabu je ndugu yangu unao ubavu wa kuhimili ghadhabu za Mola wako.
Ikemee nafsi yako, acha kuanzia leo tabia mbaya ya kupenda na kupokea rushwa kwa huduma ambayo unawajibika kuitoa huku ukiitafakari kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:-
“ANAYEFANYA MEMA ANAJIFANYIA (mwenyewe) NAFSI YAKE,NA MWENYE KUTENDA UBAYA NI JUU (ya nafsi)YAKE (vilevile) NA MOLA WAKO SI DHALIMU (hata kidogo) KWA WAJA (wake). [41:46]
Chagua sasa,kuendelea kula rushwa kwa khasara na maangamivu ya nafsi yako mwenyewe au kuacha kula rushwa kwa faida na maslahi ya nafsi yako. Kumbuka
“Rushwa ni adui wa haki” na mla rushwa ni “Adui wa Mungu, Mtume na watu wote”.