MASURUFU (GHARAMA ZA KUJIKIMU/MAHITAJI)

Masurufu ni tafsiri ya moja kwa moja ya neno la Kiarabu “NAFAQAH” ambalo limetwaliwa kutoka katika neno “AL-INFAAQ” ambalo kimsingi linamaanisha “UTOAJI/KUTOA” na “KUTUMIA/UTUMIZI”. Na neno hilo halitumiwi ila katika wigo wa kheri/wema.

Na neno hili NAFAQAH/MASURUFU katika Istilahi ya Fiq-hi ni: Kila anacho kihitajia mwanaadamu kwa njia ya lazima/dharura; yaani chakula, maji, mavazi na makazi.

 

 

    ii.            Aina za masurufu:

         Kuna aina tano za masurufu/mahitaji, kama zifuatavyo:

(a)    Masurufu ya mtu binafsi (yeye mwenyewe).

(b)   Masurufu ya matawi (watoto) kwa mashina (wazazi).

(c)    Masurufu ya mashina (wazazi) kwa matawi (watoto).

(d)   Masurufu ya mke kwa mume.

(e)    Masurufu mengineyo.

Hebu sasa tuanze kuichambua kila moja ya aina tano hizi za masurufu kwa utaratibu:

(a)   Masurufu ya mtu binafsi:

         Hakika cha chini kabisa kinacho muwajibikia mtu katika masurufu, ni kuanza na mahitaji yake yeye mwenyewe akiliweza hilo. Na masurufu ya mtu binafsi, ndio hutangulizwa kabla ya masurufu mengineyo.

Na aina hii ya masurufu, inakusanya/inachanganya kila anacho kihitajia mtu katika makazi, mavazi, chakula, maji, matibabu na mengineyo katika mahitaji ya lazima.

Na masurufu binafsi haya yanapasa kutoka katika mali yake mwenyewe maadam anamiliki kiasi cha mali ambayo inaweza kumpatia mahitaji/matumizi yake.

Dalili/ushahidi wa haya, imepokewa kutoka kwa Jaabir-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtu mmoja wa kabila la Baniy Udhrah alimuacha huru mtumwa wake kwa muangiko wa mauti yake. Habari hizo zikamfikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akauliza: “Je, unayo mali nyingine mbali na mtumwa huyu?”, akajibu: Sina. Ndipo Mtume akasema: “Nani atakaye mnunua kwangu (mtumwa) huyu?” Akanunuliwa na Abdullah Al-Adawiy-Allah amuwiye radhi-kwa dirham mia nane. Mtume akazileta dirham hizo, akampa kisha akasema: “Anza na nafsi yako uitolee sadaka, kikizidi chochote basi hicho ni cha wanao. Na kikizidi chochote katika (fungu la) wanao, basi hicho ni cha ndugu (jamaa zako). Na kikizidi kitu katika (fungu la) ndugu zako, basi ni hivi na hivi”. Bukhaariy [6367] & Muslim [997]-Allah awarehemu.

 

(b)   Masurufu ya matawi (watoto) kwa/juu ya mashina (wazazi):

         Matumizi ya mtoto yanamuwajibikia mzazi. Baba ndiye ametwikwa jukumu la kuwakimu kimaisha watoto wake wote; wa kiume na wa kike. Wakiwa hawana baba, jukumu linahamia kwa babu yao mzaa baba, naye akitokuwepo basi jukumu hilo litachukuliwa na ndugu wa karibu wa babu/baba yao.

Na dalili/ushahidi wa hili ndani ya kitabu cha Allah, ni kauli yake Atukukiaye: “…NA WAKIKUNYONYESHEENI, BASI WAPENI UJIRA WAO…” [65:06]

Basi kitendo hiki cha kumuwajibishia mume ujira wa kunyonyeshewa watoto wake, kinapelekea kuwajibisha moja kwa moja chakula/matumizi yao. Na Allah-utakati wa mawi ni wake-amesema: “NA WAZAZI WANAWAKE WAWANYONYESHE WATOTO WAO MIAKA MIWILI KAAMILI KWA ANAYE TAKA KUTIMIZA KUNYONYESHA. NA JUU YA BABA YAKE CHAKULA CHA KINA MAMA, NA NGUO ZAO KWA MUJIBU WA ADA…” [02:233]

Kwa kuwa kumnasibisha mtoto kwa baba yake kwa “Laamu ya Ikhtiswaaswi” nayo ni ile (LAUU), kunapelekea kumtwika majukumu mdau wa ukhusiswaji huo, ambaye ni baba, gharama za matunzo na matumizi ya mtoto wake. Na kadhalika uwajibishaji wa chakula cha mama mnyonyeshaji mtoto na nguo zake, kunafahamisha uwajibishaji wa chakula na nguo za mtoto ni katika mlango wa aula (ubora).

Ama dalili/ushahidi wa hili katika Sunna: Imepokewa kutoka kwa Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-ya kwamba Hind Bint Utbah alisema: Ewe Mtume wa Allah! Hakika Abu Sufyaan ni mtu mnyimi, hanipi kinacho nitosha mimi na wanawe ila kile ninacho kitwaa bila ya yeye kujua. (Mtume) akasema: “Twaa (katika mali ya mumeo) kiasi kinacho kutosha wewe na wanao kwa mujibu wa ada”. Bukhaariy [5049] & Muslim [1714]-Allah awarehemu.

Hivi ndivyo ilivyo, na wajukuu wanaambatishwa na watoto kwa sababu ya kuchanganya nasaba na haja kwa kila mmoja; watoto na wanawake.

 

Sharti za kuwajibisha masurufu ya matawi (watoto) kwa mashina (wazazi):

         Kunashurutizwa ili kuwajibisha masurufu ya matawi kwa mashina, kupatikana sharti zifuatazo:

                                          1.          Shina (mzazi) awe na uwezo wa ziada ya chakula chake mwenyewe na chakula cha mke wake cha mchana na usiku (siku moja).

Angalia basi, ikiwa kile anacho kimiliki hakitoshi katika kipindi hiki, ila kinamtosha yeye binafsi au yeye na mke wake tu, hapo hakalifishwi kutoa masurufu kwa matawi. Na ushahidi wa hili, ni ile kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo sema: “Anza na nafsi yako”. Muslim [997]-Allah amrehemu.

 

                                          2.          Tawi (mtoto) liwe ni fakiri na kunashurutizwa pamoja na ufakiri wake huo, kupatikane mojawapo ya wasifu ufuatao:

(a)    Ufakiri na utoto, au

(b)   Ufakiri na ulemavu, au

(c)    Ufakiri na uwendawazimu.

    Kwa muktadha wa maelezo haya basi, mtoto mdogo aliye fakiri, baba yake ndiye anaye kalifishwa kutoa masurufu yake. Kama baba hayupo, basi jukumu hilo litabebwa na babu yake. Na vile vile fakiri aliye mlemavu na ulemavu ulio kusudiwa hapa ni kutokuwa na uwezo wa kufanya kazi. Na hali kadhalika fakiri aliye mwendawazimu. Na muradi/mapendeleo ya ufakiri ni kule kushindwa/kutokuwa na uwezo wa kuchuma mali (ujasiriamali).

Angalia, lau mtoto atakuwa mzima (ana fya njema) na baleghe, anao uwezo wa kuchuma, masurufu yake si wajibu kwa baba yake. Ikiwa mathalan kujishughulisha na elimu (kusoma) ndiko kuliko mzuia kutafuta chumo, pataangaliwa:

F     Ikiwa elimu hiyo aitafutayo imefungamana na wajibu wake binafsi, kama vile masuala ya akida/imani na ibada. Huko kutahesabiwa kuwa ni kushindwa kutafuta chumo na hapo masurufu yake yatakuwa ni wajibu kwa baba yake.

F     Ama ikiwa hiyo elimu anayo shughulika nayo, ni katika elimu toshelezeana zinazo hitajiwa na jamii, kama vile elimu ya tiba, ufundi/teknlojia na nyinginezo. Kwa kujishughulisha na elimu hizo, mtoto huyu hatoki katika wigo wa kuwa kwake ni muweza wa kuchuma. Na baba wakati huo atakuwa na khiari; baina ya kumuwezesha katika kupata elimu hiyo anayo itafuta na kumpa masurufu. Na baina ya kumkatia masurufu na kitendo hicho kitamlazimisha kwenda kuchuma ili kukidhi mahitaji yake.

 

 

Kiwango/kiasi cha masurufu:

         Masurufu haya hayana kadiri yanayo kadiriwa/pimiwa kwayo ila ni utoshelezi na huo utoshelezi huwa ni kwa mujibu wa ada ya mahala husika, ndani ya uwezo wa mtoa masurufu. Allah Ataadhamiaye anasema: “MWENYE WASAA ATOE KADIRI YA WASAA WAKE, NA MWENYE DHIKI ATOE KATIKA ALICHO MPA. ALLAH HAMKALIFISHI MTU ILA KWA KADIRI YA ALICHO MPA. ALLAH ATAJAALIA BAADA YA DHIKI FARAJA”. [65:07]

 

Je, masurufu haya huwa ni deni juu ya shina (mzazi) unapo pita wakati wake?

         Masurufu ya matawi (watoto) unapo pita muda wake, hayawi ni deni juu ya mtoaji (shina), kwa sababu masurufu hayo ni msaada unao toka kwa shina (mzazi) kwenda kwa tawi lake (mwanawe). Kwa hivyo basi, masurufu hayo sio umiliki wa haki maalumu, lakini hayo ni umakinisho wake kwa sababu ya msukumo wa mafungamano ya udugu. Hii ndio asili na ndio hukumu pale ambapo mahusiano baina ya watoto na baba yao ni ya kawaida. Ama kukitokea mzozo baina yao, hapo kadhi ataingilia kati kuutatua. Na ndipo kadhi atamuwajibishia baba kutoa masurufu maalumu au atawapa watoto idhini ya kukopa kiwango maalumu cha mali kwa dhima ya baba yao. Hapo sasa hakika masurufu haya ndio yanakuwa deni juu ya dhima ya mzazi, utakapo pita wakati wake na wala hayapomoki kwa kupita muda. Kwa sababu yalikwisha geuka kupitia ile hukumu ya kadhi kuwa ni umiliki baada ya kuwa ni msaada mtupu na umakinisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *