ADABU/TARATIBU ZA MAAMKIZI NA KUTAKA IDHINI (KUBISHA HODI)

Msingi wa somo hili lililobeba anuani hii ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo :

“NA MNAPOAMKIWA KWA MAAMKIO YEYOTE YALE, BASI ITIKIENI KWA YALIYO BORA KULIKO HAYO, AU REJESHENI YAYO HAYO. HAKIKA ALLAH ANAFANYA HISABU YA KILA KITU” [4:86]

Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia mtakapotolewa salamu kwa kuambiwa ASSALAAM ALEYKUM, basi nyie jibuni/itikieni kwa kusema

WA-ALAYKUMUS SALAAMU WARAHMATULLAH na mkitolewa salamu kwa kuambiwa ASSALAAMU ALEYKUM WARAHMATULLAH, basi nyinyi itikieni kwa kusema

WA-ALAYKUMUS SALAAM WARAHMATULLAH WABARAKATUH.

Au itikieni salamu kama mlivyosalimiwa bila ya kuongeza ziada yeyote. Kwa mfano mtu akikusalimia ASSALAAMU ALEYKUM, nawe uitikie WA-ALAYKUMUS SALAAM na kama hivi.

Haya ndio maamkizi rasmi ya kiislamu kama alivyotufundisha Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie -.

Kwa hiyo waislamu wanatakiwa wasalimiane kwa salamu hii, kwa sababu chimbuko la salamu hii ni jina tukufu la Mwenyezi Mungu ASSALAAMU è MWENYE SALAMA/MTOAJI WA SALAMA.

 Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – anatuthibitishia ukweli huu, aliposema :

“Hakika ASSALAAMU ni jina miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu lililowekwa ardhini, basi enezeni salamu baina yenu” Bukhariy kutoka kwa Anas.

Maamkizi na salamu hii ya kiislamu yanabeba nembo ya AMANI na UTULIVU kutokana na asili ya neno lenyewe.

Kama vile muislamu anamwambia mwenziwe : Usikhofu Amani ya Allah i pamoja nawe.

Salamu hupelekea watu kuzoeana na kupendana na pia ni dalili na ishara ya adabu njema. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anatuambia :

“…Je, nikufundisheni/nikufahamisheni jambo mtakapolitenda mtapendana ?, Enezeni salamu baina yenu” Muslim, Abu Daawoud, Tirmidhiy na Ibn Majah kutoka kwa Abu Hurayrah. Enezeni salamu maana yake mtoleeni salamu mumjuaye na msiyemjua.

Maamkizi/Salamu hii ndiyo salamu ya watu peponi, Tunasoma :

“…NA MAAMKIANO YAO HUMO NI (kusema) SALAAMUN (ALEYKUM) …” [10:10]

TANBIHI :

Isieleweke kuwa ni HARAMU waislamu kuamkiana kwa maamkizi mengine yasiokuwa haya, bali maamkizi haya ndiyo yapewe umuhimu na nafasi ya kwanza.

Kisha ndipo wanaweza kuendelea na salamu kama vile : Shikamoo !, Habari Gani ? Subalkheri ! Good morning na kadhalika.

Muislamu anatakiwa kufuata adabu/taratibu zifuatazo katika salamu/maamkizi

  1. Mdogo aanze kumtolea salamu mkubwa, wachache waanze kuwatolea salamu walio wengi, aliyesimama amtolee salamu aliyekaa, aliyepanda kipando amtolee salamu aendaye kwa miguu. Muongozo huu tunaupata kupitia hadithi zifuatazo :
    1. Amesema Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – “Mdogo amsalimie mkubwa, na mpita njia (amsalimie) aliyekaa, na wachache (wawasalimie) walio wengi” Bukhariy kutoka kwa Abu Hurayrah.
    2. “Aliyepanda amsalimie aendaye kwa miguu, na aendaye (amsalimie) aliyekaa, na wachache (wawasalimie) walio wengi” Bukhariy.
  2. Ni karaha kumtolea salamu mtu aliyeshughulishwa na jambo, mpaka amalize, kama vile msomaji, muadhini, mlaji, anayeswali, na aliyeko msalani.
  3. Ukikutana na kundi la watu, usimkhusishe mtu mmoja na salamu yako kwa kumwambia ASSALAAMU ALYEKUM Said (Mathalan). Bali wote watolee salamu hata kama huwajui. Imepokelewa na Abdallah ibn Umar –Allah awawie Radhi – kwamba mtu mmoja alimwuliza Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – Uislamu upi ndio bora ? (Mtume) akajibu “Lisha chakula, na umtolee salamu umjuaye na usiyemjua” Bukhariy na Muslim.
  4. Toa salamu kwa sauti yenye kusikika kwa upole na bashasha. Sio unatoa salamu kwa sauti ya ukali huku ukiwa umenuna au umekunja uso.
  5. Unapoingia nyumbani mwako, mtolee salamu mkeo na watu wote wa nyumbani. Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – alimwambia Anas ibn Maalik : “Unapoingia nyumbani kwako, watolee salamu, itakithiri kheri ya nyumba yako” Tirmidhiy. Tunauthibitisha muongozo huu kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu : “NA MNAPOINGIA KATIKA MAJUMBA TOLEANENI SALAMU; (maamkio haya) NI ZAWADI ITOKAYO KWA ALLAH, YENYE BARAKA NA MEMA …”[24:61]
  6. Jitahidi siku zote kuwa wewe ndio wa kwanza kuwatolea watu salamu. Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – amesema : “Hakika bora zaidi ya watu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule awaanzaye watu kwa salamu” Abuu Dawoud na Tirmidhiy.

Hizi ni baadhi tu ya taratibu za salamu.

 

KUTAKA IDHINI YA KUINGIA (KUBISHA HODI)

Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia :

“ENYI MLIOAMINI ! MSIINGIE NYUMBA AMBAZO SI NYUMBA ZENU MPAKA MUOMBE RUHUSA (mpige hodi) NA MUWATOLEE SALAMU WALIOMO HUMO ….” [24:27]

 

Na akasema tena : “NA WATOTO MIONGONI MWENU, WATAKAPOBALEGHE BASI NA WAPIGE HODI KAMA WALIVYOPIGA HODI WALE WA KABLA YENU …” [24:59]

Katika aya hizi Mwenyezi Mungu Mtukufu anatufundisha adabu na taratibu za kuingia katika nyumba za watu, anatutaka :

  1. Tubishe hodi kabla ya kuingia. Na hodi hubishwa mara tatu, kama hapana majibu katika mara tatu hizo, basi shika njia uondoke. Huu ndio muongozo tuupatao katika kauli ya Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – : “Kubisha hodi ni mara tatu, ukipewa idhini (ingia) na kama hukujibiwa rudi/nenda zako” Bukhariy na Muslim.
  2. Tuwatolee salamu watu wa nyumba tuikusudiayo. Imepokelewa kutoka kwa Kildah ibn Al-Hanbal –Allah amuwie radhi – amesema : Nilikwenda kwa Mtume –Rehema na Amani zimshukie – nikaingia na sikumtolea salamu, akasema “Rudi (toka nje, uingie tena) useme : Assalaam Aleykum, je niingie?” Abu Dawoud na Tirmidhiy.
  3. Ukisha bisha hodi, kaa pembeni ya mlango, kuliani ama kushotoni. Usikae mkabala na mlango, kiasi cha kufunguliwa mlango tu, ukaweza kuona ndani moja kwa moja. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anatuambia  “Hakika si vinginevyo kubisha hodi kumewekwa kwa ajili ya jicho” Bukhaariy na Muslim.
  4. Unapobisha hodi ukaulizwa wewe ni nani, sema mimi ni fulani, taja jina lako na wala usiseme “mimi”. Haya ndio maelekezo tunayopata katika hadithi zifuatazo :

Imepokelewa kutoka kwa Ummu Haniy –Allah amuwie Radhi – amesema :

Nilimwendea Mtume –Rehema na Amani zimshukie – naye akiwa anakoga na Fatmah akiwa anamsitiri, (Mtume) akauliza “Nani huyo?”(baada ya Ummu Haniy kumtolea salamu). Nikajibu : Ni mimi Ummu Haniy. Bukhaariy na Muslim.

Imepokelewa na Jaabir –Allah amuwie Radhi – amesema : Nilimuendea Mtume –Rehema na Amani zimshukie – nikagonga mlango, (Mtume) akauliza : “Nani huyo ?” nikajibu : mimi (Mtume) akasema “Mimi, mimi” Kana kwamba Mtume aliichukia jawabu hiyo (isiyotaja jina) Bukhaariy na Muslim.

Hizi ni baadhi tu ya adabu na taratibu za kubisha hodi kama zilivyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie.

 

ADABU/TARATIBU ZA MAAMKIZI NA KUTAKA IDHINI (KUBISHA HODI)

Msingi wa somo hili lililobeba anuani hii ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo :

“NA MNAPOAMKIWA KWA MAAMKIO YEYOTE YALE, BASI ITIKIENI KWA YALIYO BORA KULIKO HAYO, AU REJESHENI YAYO HAYO. HAKIKA ALLAH ANAFANYA HISABU YA KILA KITU” [4:86]

Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia mtakapotolewa salamu kwa kuambiwa ASSALAAM ALEYKUM, basi nyie jibuni/itikieni kwa kusema

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *