Swala imemuwajibikia kila Muislamu aliyebaleghe (mkubwa) mwenye akili timamu. Zitakapopatikana na kutimia kwa mtu sifa tatu hizi:-
1. Uislamu.
2. Kufikia baleghe (ukubwa) na
3. Akili timamu.
Hapo atakuwa amekalifishwa na kuwajibishiwa na sheria kuitekeleza ibada hii ya swala, na si kuitekeleza tu basi, bali kuitekeleza kwa namna aliyoifundisha kwa maneno na matendo Bwana Mtume.
Hebu tuangalie kwa ufafanuzi kidogo sifa tatu hizi ambazo ndizo zinamvika mja taji la kuwajibikiwa na swala. Tuanze na
i. UISLAMU. Hii ndio sifa ya kwanza au tuseme ndio sifa mama.
Kwa kigezo hiki swala haiwi wajibu kwa kafiri, hii ni kwa sababu kutangulia shahada ambayo ndio tiketi ya kusafiri na gari Uislamu ni sharti ya amri ya swala.
Yaani ili mtu awe na sifa ya swala ni lazima kwanza atamke shahada ambayo itamvisha Uislamu, hapo ndipo atawajibikiwa na swala.
Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipokuwa akimpa maelekezo swahaba wake Muaadh – Allah amuwiye radhi,
“Walinganie washuhudie kwamba hapana Mola pasaye kuabudiwa kwahaki ila Allah pekee na kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Allah, ikiwa wao watakutii katika hilo, basi waambie kwamba Allah amewafaradhishia swala tano kila siku, mchana na usiku” Bukhaariy.
(ii) KUFIKILIA BALEGHE (kwa mkubwa), Hii ndiyo sifa ya pili inayomfanya mtu awe na haki na wajibu wa kushiriki katika ibada ya swala. Sifa hii haimaanishi zaidi ya kuwa swala si wajibu/faradhi kwa mtoto mdogo.
Mtoto mdogo kwa mtazamo wa sheria ni yule ambaye hajafikilia baleghe/ hajawa mkubwa. Baleghe kisheria hupatikana kwa mojawapo ya mambo matatu hayo:-
a) Mvulana au msichana kufikia umri wa miaka kumi na tano (15) ya mwezi muandamo.
b) Kujiotelea usingizini na kutokwa na manii katika umri wa miaka tisa na kuendelea. Hii ni kwa wote, mvulana na msichana.
c) Msichana kuanza kupata hedhi kwa kutimiza miaka tisa (9) na kuendelea.
Kijana wa kiume na wa kike akitokewa na mojawapo ya mambo matatu haya, kisheria atakuwa amefikia umri wa majukumu .
Ambapo hapo atatakiwa kutenda yote aliyoyaamrisha Allah na kuyaacha yote aliyoyakataza, na hapa ndipo dhana ya dhambi na thawabu huchukua nafasi.
Sifa hii ya pili tunaipata kupitia kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie,
“ Kalamu imeondoshwa kwa aina tatu za watu : kwa mtu aliyelala mpaka atakapoamka, kwa mtoto mapaka atakapobaleghe na kwa mwendawazimu mpaka atakaporudiwa na akili” Abuu Daawaid na Al-Haakim.
Naam, pamoja na kwamba swala haikufaradhishwa na kuwajibishwa kwa mtoto mdogo, lakini ni sunah na imependekezwa na sheria kwa baba, mama au mlezi wa mtoto aanze kumuamrisha mwanae kuswali atakapofikia umri wa miaka saba.
Amchape akiacha kuswali wakati akiwa na umri wa miaka kumi. Hizi zote ni hatua za kumjengea mtoto hisia na mazoea ya ibada hii ya swala atakapokuwa mkubwa.
Kimaumbile ni rahisi kwa mtoto kukua na kuishi na lile alilolizoea tangu utotoni na ni vigumu mno kwake kulitekeleza ukubwani lile ambalo hakulizoea tangu alipokuwa mtoto.
Uzoefu umeuthibitisha na kuukiri ukweli huu, na hii ndio hekima na falsafa ya neno lake Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie,
“Waamrisheni watoto wenu kuswali watakapofikia umei wa miaka saba, na wapigeni kwa kuiacha (swala) wakifikia miaka kumi na watengeni katika malazi” Tuimidhiy.
Yaani watoto wa kiume na wale wa kike wasilale pamoja baada ya kufikia umri wa miaka kumi.
(iii) AKILI TIMAMU: Ili mtu awajibikiwe na swala ni lazima awe na sifa hii ya akili timamu.
Kwa mantiki hii swala si wajibu/faradhi kwa mwendawazimu kwa sababu hana nguvu ya kujua alitendalo. Hivyo ndivyo tunavyofahamishwa na kauli ya Bwana Mtume tuliyoitaja katika nukta/kipengele cha pili…
”……na kwa mwendawazimu mpaka atakaporudiwa na akili.”