SWALA YA MWENYE KHOFU

MAANA:

Katika darsa hii tutakapoitaja khofu tutakuwa tukimaanisha na kuikusudia khofu iliyo kinyume cha amani.

Hali au mazingira yo yote ambayo hayamuhakikishii mja amani, utulivu na usalama, hali na mazingira hayo ndiyo tunayoyaita khofu.

Ni ndani ya mazingira hayo ya khofu ndimo muislamu anapata kibali na rukhsa ya kuswali swala ya khofu.

 

NINI SWALA YA KHOFU:

Makusudio ya swala ya khofu ni ile swala ambayo inayotekelezwa na kuswaliwa katika hali na mzingira ya vita; mazingira yasiyo na amani wala usalama.

Ndani ya swala hii mna rukhsa na wepesi usiopatikana katika swala nyingine zinazoswaliwa katika mazingira ya kawaida (amani).

 

HALI YA SWALA ZA KHOFU:

Swala ya khofu ina hali kuu mbili kwa kutegemeana na hali ilivyo katika uwanja wa vita.

 

HALI YA TAHADHARI:

Hii ni hali ambayo jeshi huwa katika utayarifu wa vita likitazamia kulipuka kwa vita wakati wo wote.

Kwa hivyo huwa katika hali ya ulinzi ili kuweza kukabiliana na shambulizi lo lote la ghafla.

Katika hali hii swala huswaliwa kwa utaratibu maalumu kinyume na ule utaratibu wa kawaida ili kuwawezesha waislamu kuswali kwa jamaa nyuma ya imamu mkuu (kiongozi) au amiri jeshi mkuu (kamanda) au naibu wao anayeendesha shughuli zote za jeshi.

 

DALILI/USHAHIDI:

Utekelezaji wa swala katika mazingira na utaratibu huu maalumu uliokhitalifiana na ada (kawaida) ni agizo la Allah lililomo katika kauli yake alipomwambia Mtume wake:

“NA UNAPOKUWA PAMOJA NAO (waislamu katika vita) UKAWASWALISHA; BASI KUNDI MOJA MIONGONI MWAO WASIMAME PAMOJA NAWE (wanaswali) NA WASHIKE SILAHA ZAO. NA WATAKAPOMALIZA SIJIDA ZAO BASI NA WAENDE NYUMA YENU (kwa kulinda); NA LIJE KUNDI JINGINE AMABALO HALIJASWALI, LISWALI PAMOJA NAWE, NAO WASHIKE HADHARI YAO NA SILAHA ZAO (humu ndani ya swala; maana) WALE WALIOKUFURU WANATAKA MGHAFILIKE NA SILAHA ZENU NA VITU VYENU ILI WAKUVAMIENI MVAMIO WA MARA MOJA. WALA SI VIBAYA KWENU IKIWA MNAONA UDHIA KWA SABABU YA MVUA AU UGONJWA, KUONDOA SILAHA ZENU. NA MSHIKE HADHARI YENU, HAKIKA ALLAH AMEWAANDALIA MAKAFIRI ADHABU ITAKAYOWADHALILISHA”. [4:102]

Sura hii ya swala ya khofu iliyotajwa ndani ya aya hii ina namna mbili katika utekelezaji wake kama alivyozibainisha Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwa kauli na amali (vitendo).

Namna mbili hizi zinakhitilafiana kwa kigezo cha mahala alipo adui kutokea pale walipo waislamu; adui yuko upande wa Qiblah au upande mwingine.

 

NAMNA YA KWANZA:

Namna hii ya swala ya khofu hutumika wakati ambapo adui yuko upande wa Qiblah na vita bado havijauma.

Katika hali hii, jeshi la waislamu linapotaka kuswali swala ya jamaa moja bila ya kuigawa katika jamaa nyingine ndogo ndogo ili kupata fadhila za jamaa moja kubwa.

Imamu atawapanga maamuma wake safu mbili, nne au zaidi kulingana na idadi ya watu na ukubwa wa eneo la swala.

Atawaswalisha, imamu akienda sijida isujudu pamoja nae ile safu ya mbele inayomuandamia pekee, hivi ni iwapo maamuma wako safu mbili tu.

Ama wakiwa ni safu nne, basi zisujudu pamoja na imamu zile safu mbili za mwanzo tu. Utaratibu ni huu huu hata kwa jamaa yenye zaidi ya safu nne.

Safu moja au mbili zilizobaki zitawalinda wenzao waliosujudu pamoja na imamu dhidi ya harakati zo zote za shambulizi la ghafla kutoka kwa adui.

Imamu atakaposimama kutoka katika sijida ya pili ya rakaa ya kwanza pamoja na ile safu ya kwanza au ya pili.

Hapa sasa ndipo zitaenda sijida zile safu nyingine zilizobakia na kisha kuinuka kuja kujiunga na imamu katika kile kisimamo cha rakaa ya pili.

Imamu atakapoenda katika sijida ya rakaa hii ya pili, litasujudu pamoja nae lile kundi lililokuwa likilinda mwanzo (katika rakaa ya kwanza).

Na nafasi yao ya ulinzi itachukuliwa na ile safu au safu za mwanzo zilizosujudu pamoja na imamu katika rakaa ya kwanza.

Kisha makundi yote haya yatakutana katika tashahudi na kutoa salamu pamoja nyuma ya imamu wao.

Hivi ndivyo Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alivyowaswalisha maswahaba wake katika mojawapo ya vita vya haki dhidi ya batili.

Kwa kitendo hiki cha Mtume, namna hii ya swala ya khofu ikawa ni suna katika kila hali na mazingira yanayoshabihiana na mazingira yale.

Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbaas-Allah awawiye radhi-amesema:

“Alisimama Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na watu (maswahaba) wakasimama pamoja nae. Akakabiri (akaleta takbiratul-Ihraam) nao wakakabiri. Baadhi ya watu miongoni mwao wakarukuu, kisha wakasujudu pamoja nae (Mtume). Kisha (Mtume) akainuka kwa ajili ya rakaa ya pili, basi wakasimama wale waliosujudu na kuwalinda wenzao. Likaja lile kundi jingine, likarukuu na kusujudu pamoja nae, wote wakiwa ndani ya swala lakini wakilindana”. Bukhaariy

 

NAMNA YA PILI:

Namna hii huchukua nafasi wakati ambapo adui huwa ametapanyika, hayuko upande wa Qiblah na vita bado havijaanza.

Namna ya swala za khofu zilizosuniwa katika hali na mazingira kama haya ni kama zifuatavyo:-

Jeshi lijigawe makundi mawili; kundi moja lisimame mkabala wa adui na kulilinda kundi jingine ambalo wakati huo litakuwa likiswali jamaa pamoja na imamu.

Imamu aliswalishe kundi hili la pili rakaa moja. Atakapoinuka kuswali rakaa ya pili, kundi hili litamfariki (litaacha kumfuata) imamu na kutimiza rakaa ya pili kila mtu peke yake. Kisha baada ya kutoa salamu liende kushika zamu ya ulinzi.

Sasa lije lile kundi la kwanza lililokuwa likilinda limfuate imamu katika hii rakaa yake ya pili.

Kunampasa imamu kuirefusha sana rakaa yake hii ya pili ili kuliwezesha kundi hili kuja kuungana nae baada ya lile jingine kwenda kushika zamu.

Imamu ataswali nalo rakaa ya pili ambayo kwa upande wao itakuwa ndio rakaa ya kwanza. Imamu atakapokaa tashahudi, litainuka na kutimiza rakaa ya pili na kuja kuungana nae hapo katika tashahudi atakapokuwa anawangojea na atatoa salamu pamoja nao.

Hivi ndivyo Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alivyoswali na maswahaba wake katika vita vya ‘Dhaatir-riqaa’.

Imepokelewa kutoka kwa Swaalih Ibn Khawwaat kutoka kwa waliomshuhudia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiswali katika vita vya Dhaatir-riqaa swala ya khofu:

“Kwamba kundi moja lilipiga safu pamoja nae (Mtume) na kundi jingine likawa mkabala wa adui. (Mtume) akaswali na lile kundi lililokuwa pamoja nae rakaa moja, kisha Mtume akathibiti hali ya kusimama nao wakatimiza (swala) peke yao. Kisha wakaondoka wakapiga safu mkabala (welekeya) wa adui. Likaja lile kundi jingine akaswali nalo ile rakaa nyingine iliyobakia ya swala yake, kisha akathibiti hali ya kukaa, wakatimiza wenyewe (rakaa yao ya pili), kisha akatoa nao salamu”. Bukhaariy, Muslim & wengineo.

Kuitekeleza swala kwa namna mbili hizi na ilhali waislamu wakiwa mapambanoni na adui ni sura inayotoa picha ya kuihifadhi na kuichunga swala ya jamaa na usalama wa waislamu.

Na ya kwamba muislamu hana udhuru wala uchochoo wa kuiacha swala hata katika mazingira ya vita seuze katika mazingira ya amani.

 

HALI YA MAPAMBANO

Hii ndio hali ya pili ya swala ya khofu.

Katika hali hii ya kuuma kwa vita, hakuna namna maalumu ya swala iliyopokelewa, bali kila mtu anatakiwa kuswali kwa namna inavyomkinikia.

Ataswali huku akipigana akienda kwa miguu au akiwa amepanda mnyama.

Kadhalika anaweza kuswali akiwa anatembea bila ya kupigana au akiwa amesimama.

Katika hali hii anaruhusiwa kuswali kwa kuelekea upande inakotokea khatari, ni mamoja imesibu kuwa ndio upande wa Qiblah au la.

Na atayafanya matendo ya rukuu na sijida kwa kuotezea yaani kwa kukitukutisha kichwa chake hali ya kushiria hiyo rukuu na sijida.

 

Yatakikana kuotezea kwa sijida kuwe ni zaidi kuliko kuotezea kwa rukuu ili kufarikisha au kutofautisha baina ya viwili hivyo; sijida na rukuu. Ikiwamkinikia kufuatana na kuswali jamaa pamoja itakuwa ni bora hata kama watakhitalifiana kimuelekeo, huyu kaelekea huku na yule kaelekea kule au maamuma akamtangulia imamu wake.

Kuhusiana na haya tunasoma:

“ANGALIENI SANA SWALA (zote kuziswali, khasa jamaa) NA (khasa) ILE SWALA YA KATI NA KATI. NA SIMAMENI KWA UNYENYEKEVU KATIKA KUMUABUDU ALLAH. NA KAMA MKIWA NA KHOFU (kuswali kidasturi; mmo katika kupigana, basi swalini) NA HALI YA KUWA MNAKWENDA KWA MIGUU AU MMEPANDA (wanyama). NA MTAKAPOKUWA KATIKA AMANI, BASI MKUMBUKENI ALLAH (swalini) KAMA ALIVYOKUFUNZENI YALE MLIYOKUWA HAMUYAJUI”. [2:238-239]

Imamu Bukhaariy amepokea riwaya kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-katika kuitaja kwake swala ya khofu.

Baada ya kuzitaja aina mbili zilizotangulia (kuelezwa katika darsa iliyopita) akasema:

Na khofu ikiwa bado ni kubwa kushinda hivyo, waliswali hali ya kuwa wanakwenda kwa miguu au hali ya kupanda (wanyama), wakiwa wameelekea Qiblah au wakiwa hawakuelekea. Imamu Maalik akasema: Amesema Naafii:

Simuoni Abdullah Ibn Umar kuwa kayataja hayo (aliyoyataja) ila ni kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Katika hali hii ya mapambano husamehewa harakati na matendo anayoyafanya mwenye kuswali kwa kulazimishwa na hali hiyo ya vita, matendo na harakati ambazo hazisameheki katika hali ya amani.

Maneno na ukelele, hivi havisameheki kwa sababu hakuna dharura inayohitajisha kufanya hivyo. Katika hali hii mtu akipatwa na najisi isiyosameheka kama vile damu na mfano wake, swala yake itakuwa ni sahihi lakini kutamuwajibikia kuikidhi baadae akiwa katika hali ya amani.

Ni vema ukatambua kwamba aina hii ya swala tuliyoitaja imeruhusiwa kuswaliwa kwa kaifia hii katika kila vita vya kisheria.

Na katika mazingira ambayo mtu anakuwa na khofu kubwa, kama wakati anamkimbia adui au mnyama mkali.

Kilichozingatiwa katika kuwekwa sheria ya kuswali kwa namna hii iliyokhalifiana na ada/dasturi ya swala ni kuchunga kuitekeleza swala katika wakati wake uliowekwa na sheria. Hii yote ikiwa ni kuamrika na kauli yake Allah isemayo:

 “…KWA HAKIKA SWALA KWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA NYAKATI MAKHSUSI”. [4:103]

 

FALSAFA/HEKIMA YA KUSHARIIWA (KUWEKWA SHERIA) SWALA YA KHOFU.

Falsafa/hekima pekee ya kushariiwa swala ya khofu ni kumfanyia mja wepesi ili aweze kuitekeleza nguzo hii kuu ya dini katika hali na mazingira yo yote yale.

Ili kuonyesha kuwa Uislamu ni dini inayokwenda sambasamba na maumbile ya mwanadamu:

 “BASI UELEKEZE USO WAKO KATIKA DINI ILIYO SAWA SAWA-NDILO UMBILE ALLAH ALILOWAUMBIA WATU (yaani dini hii ya Kiislamu inawafikiana barabara na umbo la binadamu) HAKUNA MABADILIKO KATIKA MAUMBILE YA VIUMBE VYA ALLAH. HIYO NDIO DINI ILIYO HAKI, LAKINI WATU WENGI HAWAJUI”. [30:30]

Kadhalika swala hii ya khofu ni kielelezo cha wazi kinachoonyehsa wepesi wa dini hii ya Kiislamu kama alivyosema Allah:

“…ALLAH ANAKUTAKIENI YALIYO MEPESI WALA HAKUTAKIENI YALIYO MAZITO….” [2:185]

“…WALA HAKUWEKA JUU YENU MAMBO MAZITO KATIKA DINI (nayo dini hii) NI MILA YA BABA YENU IBRAHIMU…” [22:78]

Pia kwa kuzingatia kuwa swala ni mawasiliano na kiungo baina ya mja na Mola wake ikawekwa swala hii ya khofu ili mja asikatikiwe na mawasiliano na Mola wake katika kipindi hiki kigumu ambacho anayahitajia zaidi mawasiliano hayo.

Kupitia mawasiliano hayo amuombe Mola wake nusra na ushindi dhidi ya maadui wake aliojisabilia maisha yake katika kupambana nao.

Ndani ya mawasiliano hayo atamtaja Bwana Mlezi wake, utajo ambao utampa utulivu wa moyo na makini ya akili, vitu ambavyo ni nyenzo muhimu sana katika uwanja wa mapambano.

Ni utulivu na umakini huu ndivyo vitakavyomuwezesha kupanga mikakati na mbinu zitakazomsaidia na kumuhakikishia ushindi. Tusome na tuamini:

“…SIKILIZENI! KWA KUMKUMBUKA (kumtaja/kumdhukuru) ALLAH NYOYO HUTULIA”. [13:28]

Isitoshe kumdhukuru Allah katika hali ngumu hii ya vita ni sababu kuu ya ushindi na nusra, tusome na tuamini tukitaka:

“ENYI MLIOAMINI! MKUTANAPO NA JESHI (la makafiri) KAZANENI BARABARA (wala msikimbie) NA MUMKUMBUKE ALLAH KWA WINGI ILI MPATE KUFAULU”. [8:45]

 

HITIMISHO:

SWALA HAIPOMOKI KWA HALI YO YOTE ILE IWAYO.

Inabainika kutokana na maelezo yote haya yanayoitaja swala ya khofu kwamba swala haipomoki kwa hali yo yote ile iwayo maadam mtu ana akili timamu.

Si mwendawazimu na ni mkubwa si mtoto mdogo.

Hivi ndivyo kusema kuwa mja hana udhuru wo wote utakaompa kibali cha kuacha kuswali, hilo lingelikuwepo basi angelikipata kibali hicho katika hali ya vita.

Kilichoruhusiwa si kuacha kuswali bali ni wepesi wa kuswali kwa mujibu wa mazingira na hali aliyomo mtu.

Msafiri kwa mfano ameruhusiwa kujumuisha swala mbili iwe ni mjumuisho wa kutanguliza au ule wa kuakhirisha na kukusuru yaani kuziswali swala za rakaa nne, rakaa mbili mbili badala ya nne.

Hakuambiwa asiswali eti kwa kuwa tu yumo safarini bali Uislamu kwa kuutambua uzito na taabu ya safari ukampa wepesi wa namna fulani katika kuitekeleza nguzo hii ya swala.

 

SWALA YA MWENYE KHOFU

Katika darsa hii tutakapoitaja khofu tutakuwa tukimaanisha na kuikusudia khofu iliyo kinyume cha amani. Hali au mazingira yo yote ambayo hayamuhakikishii mja amani, utulivu na usalama, hali na mazingira hayo ndiyo tunayoyaita khofu. Ni ndani ya mazingira hayo ya khofu ndimo muislamu anapata kibali na rukhsa ya kuswali swala ya khofu.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *