Bila ya shaka kila mmoja wetu amepata kuliona jengo refu, imara na madhubuti, likampendeza na kumvutia kiasi cha kujikuta anasimama kulishangaa.
Ni dhahiri kuwa jengo hili zuri ni natija ya msingi imara, nguzo madhubuti, kuta zilizoundwa na mkusanyiko wa matofali, vyuma vya pua na baki ya vifaa vingine vya ujenzi.
Mkamatano na mshikamano wa matofali umezaa kuta imara, mkusanyiko wa kuta hizi ukazaa jengo zuri lililosimama juu ya msingi madhubuti usiotetereka ukiungwa mkono na nguzo thabiti.
Ni kutokana na mchanganyiko na muungano wa vitu vyote hivi ndio likapatikana jengo imara na madhubuti likushangazalo.
Huu ndio mfano wa uma wa Kiislamu kama jengo moja, madhubuti na imara. Kama unavyoelezwa na kauli ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Muumini kwa muumini mwenzie ni kama (mfano wa) jengo likamanatalo baadhi moja na nyingine.” Bukhaary, Muslim & Tirmidhiy.
Matofali hapa ya kulijenga na kulisimamisha jengo hili juu ya msngi imara ni umoja, mshikamano na mapenzi chini ya udugu wa Kislamu.
Sasa ni lazima vipatikane mchanga, saruji na maji ya kutengenezea matofali ya umoja mapenzi na mshikamano utakaowafikisha katika kuitekeleza amri ya Mola wao:
“NA SHIKAMANENI KWA KAMBA (dini) YA ALLAH NYOTE NA WALA MSIACHANE (msitengane/msifarikiane)…..” (3:103)
Sasa basi ili kuwafikisha waislamu kuwa uma mmoja kama anavyowataka Mola wao:
“KWA YAKINI HUU UMMA WENU NI UMMA MMOJA, NA MIMI NI MOLA WENU (mmoja) KWA HIVYO NIABUDUNI.” (21:92)
Na kuwafikisha kujihisi mwili mmoja kama alivyosema Mtume wao-Rehema na Amani zimshukie:
“Mfano wa waumini katika kupendana kwao, kuhurumiana kwao na kuoneana kwao sikitiko ni mithili ya mwili mmoja. Kinapoumwa kiungo kimoja katika (mwili) huo, baki ya mwili hushirikiana nacho katika homa na kukesha .” Bukhaariy & Muslim
Ndio uislamu ukaweka haki za kila muislamu juu ya nduguye muislamu.
Haki ambazo kama zitafuatwa na kila muislamu kama itakiwavyo, bila ya shaka zitakuwa na msaada mkubwa katika kuleta umoja, mapenzi na mshikamano baina ya waislamu.
Haki hizi pia zina dhima ya kulinda na kuhifadhi umoja na mshikamano wa uma wa Kiislamu.
Haki za muislamu kwa muislamu mweziwe ni nyingi mno, miongoni mwa hizo ni kama zinavyoelezwa na kauli ya Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie:
“Haki za muislamu kwa muislamu ni sita:
Ukikutana nae mtolee salamu, na
Akikuita (akikualika) muitike,
Akikutaka nasaha/ushauri mnasihi
Akipiga chafya na akamuhimidi Allah, mshemue (mwambie “Yarhamukal-laah”),
Akiumwa mkague (mjulie hali) na
Akifa lifuate jeneza lake (kamzike)”.
Katika hadhithi hii Bwana Mtume anatubainishia haki kadhaa baina ya waislamu kama ifuatavyo:
SALAMU:
Muislamu anapompitia nduguye muislamu, anapomzuru au anapotaka idhini ya kuingia nyumbani au kazini kwake ni haki ya ndugu yake huyo kumtolea tamko la amani.
Tamko litakalomuhisisha amani na kuituliza nafsi yake, kwa kumtolea salamu kwa tamko la:
ASSALAMU ALAYKUM WARAHMATULLAAH. Hayo ndio maamkizi ya waislam leo duniani na kesho kule akhera:
“…MAAMKIANO YAO HUMO YATAKUWA SALLAMUN ALAYKUM (za kila upande, yaani Amani tu juu yenu na furaha na salama).” (14:23)
Maamkizi haya ya kiislamu ni suna kokotezwa (muakadah) kama ilivyothibiti kutoka kwa Bwana Mtume.
Na maamkizi haya ni katika jumla ya sababu za kuleta mshikamano, mtungamano na mapenzi baina ya waislamu kama umma. Hili linashuhudiwa na kauli yake Mtume wa Allah- Rehema na Amani zimshukie:
“Wallah, hamtangia peponi mpaka muwe waumini na hamtakuwa waumini mpaka mpendane. Basi hivi nikuambieni jambo mtakapolitenda mtapendana, enezeni salamu baina yenu.” Muslim
Bwana Mtume ambaye anasifiwa na Mola wake:
“NA BILA SHAKA UNA TABIA NJEMA KABISA.” (68:4)
Alikuwa akimuandiliza kwa salamu kila anayekutana nae, yaani anapokutana na mtu yeye ndiye huanza kumtolea salamu mtu huyo.
Kadhalika hakuwapuuza watoto wadogo, bali ili kuwajengea mapenzi alikuwa akiwatolea salamu anapowapitia. Huyu ndiye Mtume ambaye Allah anatuambia:
“BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA (ruwaza nzuri) KWA MTUME WA ALLAH (lakini mfano huo ni) KWA MWENYE KUMUOGOPA ALLAH NA SIKU YA MWISHO NA KUMTAJA ALLAH SANA.” (33:21)
Ilivyo suna katika salamu ni mdogo kuanza kumtolea salamu mkubwa wake na wachache wawatolee salamu walio wengi.
Aliyepanda kipando (mnyama/gari n.k) amsalimu mwenda kwa miguu. Lakini iwapo mtu mwenye kuwajibika kutoa salamu hakuifuata suna hii ya Mtume, isiwe ni sababu ya kutokuamkiana.
Huyu aliyekuwa na haki ya kuanza kusaliminwa, atoe salamu isipotee.
Kwa hivyo itakaposadifu kuwa mdogo hakumtolea salamu mkubwa, basi yeye amtolee salamu huyo mdogo ili ahodhi ujira na fadhila ambazo agezipata lau angeanza yeye kutoa salamu. Amesema swahaba wa Mtume Ammaar Ibn Yaasir–Allah awawiye radhi:
“Mambo matatu mtu akiyakusanya hukamilika imani yake:-
Uadilifu kwa nafsi yako, na
Na kuutolea salamu ulimwengu, na
Kutoa wakati wa dhiki”. Bukhaariy
Muradi wa kuutolea salamu ulimwengu ni kumsalimia na kumuamkia kila unayekutana nae. Ikiwa kuanza kutoa salamu ni suna, basi bila ya shaka kuijibu salamu ni fardhi toshelezi (kifayah).
Yaani mmoja wa wanakundi waliosalimiwa akiitikia atakuwa amewatoshea wenzake kutokana na kuitikia kwake huko. Uwajibu huu wa kuitikia salamu ni amri ya Allah katika kitabu chake kitukufu:
“NA MANPOAMKIWA KWA MAAMKIO YO YOTE YALE, BASI ITIKIENI KWA YALIYO BORA KULIKO HAYO, AU REJESHENI YAYO HAYO HAKIKA ALLAH ANAFANYA HISABU YA KILA KITU.” (4:86)
KUITIKA WITO:
Humtokea mwanadamu neema za Allah zikamfurahisha mithili ya kuoa au kuozesha, kuruzukiwa mtoto, kuponywa maradhi, kufaulu mtihani, kupata cheo na kadhalika.
Ili kumshukuru Allah Mola mneemeshaji huamua kufanya karamu halali na kuwaalika ndugu na majirani zake kuja kushirikiana nae katika furaha yake hiyo.
Ndio Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie–akatuambia:
“Akikuita (akikualika) muitike,” kwani kuitika wito wa ndugu yako muislamu ni “Suna kokotezwa”.
Usuna huu unatokana na yale yanayopatikana katika kuitika wito, ikiwa ni pamoja na kuimarisha udugu wa Kiislamu na kujenga mapenzi na mshikamano.
Ni kweli kuwa mtu anapokualika katika jambo lake, huwa amekuthamini upeo, sasa kama hukumuitika huwa umemvunja moyo na kumfanya ajiulize kwa nini.
Na pengine akahisi kudharauliwa na hivyo kumfanya ajenge chuki badala ya mapenzi. Kwa hivyo basi ni suna kuitika wito wa nduguyo muislamu kama hauna udhuru mkuu.
Na hata kama umeudhurika basi ni vema ukamfahamisha kabla pamoja na kumuomba akuwiye radhi. Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie anatuambia:
“Akialikwa mmoja wenu chakula, basi na aitike (mualiko huo), akiwa hakufunga na ale na akiwa amefunga basi na awaombee Mungu (waliomualika)”. Ahmad, Muslim, Abuu Daawoud, Tirmidhiy & Ibn Maajah.
TANBIHI: Si suna kuhudhuria karamu ambayo:-
Wamealikwa matajiri au watu mashuhuri pekee na kubaguliwa masikini na wanyonge Mtume wa Allah– Rehema na Amani zimshukie anatuasa:
“Shari ya chakula (ni) chakula cha karamu, wanaalikwa matajiri na kuachwa mafakiri…” Bukhaariy, Muslim, Abuu Daawoud, & Nasaai.
Inawachanganya pamoja wanamume na wanawake na wanamume ambao si maharimu.
Ndani yake kuna jambo la haramu kama ulevi na kucheza muziki au karamu kufanywa mahala pa shari kama baa.
NASAHA:
Mwanadamu kimaumbile ni kiumbe anayekumbana na magumu yake.
Kadhalika kimaumbile mwanadamu ni kiumbe tegemezi anayeishi katika kundi na asiyeweza kujitegemea mwenyewe katika uamuzi khususan wa magumu ya maisha.
Sasa mwanadamu anaposibiwa na jambo gumu likamuhemeza asijue la kufanya na kuhitajia ushauri nasaha kutoka kwako. Hapo ndipo Mtume wako– Rehema na Amani zimshukie–anakwambia: “Akikutaka nasaha/ushauri, mnasihi.”
Yaani atapokujia nduguyo muislamu kukutaka ushauri katika lililomsibu au analotaka kulifanya, basi ni wajibu wako kumpa ushauri/nasaha njema.
Na utambue kwamba hilo alilojia ni haki yake aliopewa na Uislamu, na wewe kumpa nasaha na ushauri unaolenga kujenga au kutatua ni sehmu ya dini kwani Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie– ametuambia:
“Dini ni nasaha kwa ajili ya Allah, kitabu chake, Mtume wake, viongozi wa waislamu na watu wote.”
Muslim, Ahmad, Nasaai & Abuu Daawoud.
Hata kama hakukujia kukutaka ushauri na ukaona kuwa atafikwa na madhara au janga fulani kutokana na mwenendo fulani alionao.
Basi ni wajibu wako umkusudie na umnasihi kwa mapenzi ya udugu wa Kiislamu, lakini ni vema ukatambua kuwa wajibu wako ni kutoa nasaha tu na sio kumlazimisha kufuata nasaha.
Kadhalika ni kheri ikiwa utatambua kwamba nasaha/ushauri ni amana, kwani anayekuja kukutaka ushauri huwa ameakuamini na kukuthamini.
Kwa hivyo basi ni wajibu wako nawe kujithaminisha kwake na kuonyesha kuwa unastahiki heshima aliyokupa kwa kumpa ushauri mzuri.
Kama hukufanya hivyo, yaani kwa makusudi mazima ukaamua kumpa ushauri nasaha utakaomtosa, utakuwa umemkhini (umemfanyia khiyana). Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie anatuambia:
“…Atayempa nduguye ushauri kwa jambo ambalo anajua uongofu uko katika jingine, kwa yakini amemkhini” Abuu Daawoud & Al-Haakim
Na Allah Mola Mwenyezi anatuambia:
“…HAKIKA ALLAH HAWAPENDI WAFANYAO KHIYANA.”
CHAFYA:
Kupiga chafya kunaonekana kuwa ni tendo la kawaida tu, kwa hivyo wengi wetu huwa hatuizingatii chafya.
Bwana Mtume tabibu aliyefundishwa na Allah ana mtazamo tofauti na wetu kuelekea chafya. Yeye anaiona chafya kuwa ni miongoni mwa neema za Allah kwa mwanadamu ambazo ni wajibu wake kumshukuru kwazo Mola wake.
Mtazamo huu wa Mtume wa Allah unatokana na ukweli kwamba mtu anapopiga chafya, huwa anautoa ukungu uliotanda katika ubongo wake.
Ukungu huu hautoki ila kwa njia hiyo ya kupiga chafya na kama haukutoka huweza kumsababishia mwanadamu madhara makubwa.
Kwa kulizingatia hili ndio chafya inapata hadhi ya kuwa neema inayohitajisha shukurani na himda kwa Allah aliyetuwekea utaratibu huu wa kupiga chafya.
Kwa hivyo ni haki ya nduguyo muislamu anapopiga chafya na akamuhimidi Allah, yaani akasema (Al-hamdulillaah), umshemue.
Kumshemua mtu aliyepiga chafya ni kumuombea dua kwa kumwambia:
(Yar-hamukal-laah)-yaani Allah akurehemu. Hivi ndivyo alivyotufundisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
“Atapopiga chafya mmoja wenu na aseme: (Al-hamdulillaah) na nduguye (amsikiaye akisema hivyo) amwambie: (Yar-hamukal-laah). Atakapomwambia (Yar-hamukal-laah) nae (huyo mpiga chafya) amwambie: (Yahdiykumul-laahu wayuswlih baalakum)”. Bukhaariy
Mpiga chafya kama hakusema (Al-hamdulillaah) mara tu anapopiga chafya, huwa amejidhulumu mwenyewe haki ya kushemuliwa.
Utamshemua mpiga chafya mara ya kwanza, ya pili na ya tatu kwa kumwambia: (Yar-hamukallaah).
Akipiga tena chafya mara ya nne utamwambia: (‘Aafakallaah) yaani Allah akuafu, kwa sababu sasa hiyo itakuwa sio chafya ya kusafisha na kuuondoa ukungu bali ni ya ugonjwa.
Kwa hivyo unamuombea afya, huu ndio Uislamu ambao kila muumini anapaswa kuufuata. Lakini kwa masikitiko makubwa tumeyatupilia mbali mafundisho haya na kuuiga utamaduni wa kimagharibi.
Leo sia ajabu bali ni sehemu ya maendeleo muislamu anapopiga chafya kusema (I am sorry) badala ya kusema (Al-hamdulillaah) kama alivyoelekezwa na Mtume wake.
KUJULIWA HALI (KUKAGULIWA) MGONJWA:
Mwanadamu anapopatwa na maradhi, humuondoka hali yake ya kawaida na mahala pake kuchukuliwa na maumivu, machungu, udhaifu na unyonge.
Maradhi yakimzidia hutambaliwa na khofu ya mauti na kukata tamaa ya kuishi.
Katika hali na mazingira haya magumu, mwanadamu humuhitajia sana mtu wa kumjali, kumuangalia, kumsaidia na kumliwaza.
Mtu wa kumtembelea (kumkagua) na kumuombea Mungu katika katika kipindi hiki ambacho humkumbuka sana Allah Mola Muumba wake.
Huyu humfungulia mlango wa matumaini ya kupona kwa kushirikiana nae katika machungu yake.
Ni kwa kuyazingatia yote haya ndio Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akatuagiza: “Akiumwa mkague”.
Kwa hivyo basi kumzuru mgonjwa ni haki yake aliyopewa na Uislamu. Na tendo hili hujenga baina ya waislamu huruma, mapenzi na mshikamano.
Kadhalika humpa nafuu mgonjwa na kumkumbusha huyu aliyekuja kumuona thamani ya siha (afya njema) akapata kumshukuru Allah kwa neema ya siha.
Ilivyo suna kwa mwenye kumkagua/kumtembelea mgonjwa akifika amuulize hali, anajisikiaje, ampe matumaini ya kupona na amuombee Mungu. Aseme kama alivyotufundisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
“ALLAAHUMMA RABBAN-NAASI, ADH-HIBIL-BA’ASA, WASHFI ANTAS-SHAAFIY, LAA SHIFAA ILLAA SHIFAAUKA, SHIFAA LAA YUGHAADIRU SAQAMAN”. Bukhaariy & Muslim
MAANA: “Ewe Mola wa watu wote! Ondosha ubaya na uponye kwani wewe ndiye mponyaji. Hakuna ponyo (liwezalo kuponya)ila ponyo lako, ponyo lisiloacha ugonjwa wo wote (bila ya kuuponya)”.
Hii ndio dua anayoombewa mgonjwa na zipo nyingine kadhaa kama zilivyopokewa kutoka kwa Mtume wa Allah.
Kadhalika kunampasa mwenye kumuangalia mgonjwa kumkumbusha mgonjwa kutubia kwa njia ya hekima bila ya kumtisha na kumfanya ahisi kufa kufa.
Kwa mfano anaweza kumwambia: Kwa yakini katika maradhi yako haya unachuma kheri nyingi, kwa sababu maradhi ni sababu inayomtakasa mja na Allah akamfutia dhambi zake.
Kwa hivyo bila ya shaka kwa kufungika kwako huku kutokana na maradhi ni fursa adhimu. Fursa itakayokupatia ujira na thawabu nyingi mbele ya Allah kwa kukithirisha kwako wakati huu kuleta dhikri, istighfaari na dua.
Vile vile kunamlazimu mwenye kwenda kumuangalia mgonjwa, kuchunga wakati wa kwenda huko ili aende wakati muafaka.
Asiende mapema asubuhi kwani inamkinika mgonjwa akawa kapata usingizi wakati huo, baada ya kukesha kwa maumivu na machungu wakati wa usiku.
Kadhalika isiwe usiku sana wakati ambao mgonjwa kachoka na anataka kupumzika, lakini anashindwa kukuambia ondoka ninataka kupumzika.
Vile vile asikae muda mrefu sana kwa mgonjwa au kumpa khabari za huzuni na kutisha. Pia yatakikana kuchunga, kuheshimu na kufuata amri na maelekezo ya daktari, kama daktari amekataza kuzungumza na mgonjwa, basi usimsumbue kwa kumzungumzisha.
Au amekataza kutoingia watu wengi kwa mgonjwa kwa wakati mmoja, basi na waingie wale tu wanaoruhusiwa.
Ni kheri pia ikiwa kila unapokwenda kumuona mgonjwa ukamchukulia zawadi ya kile akipendacho, chakula au matunda yatakayomuongezea nguvu.
Na sio vitu kama sigara na pombe vitakavyochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa maradhi yake. Mpe msaada wa pesa kiasi cha uwezo wako ili zimsaidie katika kugharamia matibabu na kuendesha mambo ya nyumbani kwake.
Kwa ujumla kumtembelea mgonjwa na kumsaidia ni jambo lenye fadhila kubwa. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Kwa hakika Allah atasema siku ya kiyama: Ewe mwanadamu, niliumwa hukuja kuniona. (Mwanadamu) aseme: Ewe Bwana Mlezi wangu, vipi ningekuja kukuona na ilhali wewe ndio Mola wa walimwengu wote? (Allah) atamwambia: Je, hukujua kwamba mja wangu fulani anaumwa? Je, hukujua kama ungelienda kumuona ungenikuta mimi kwake?…”. Muslim
KUMZIKA:
Kila kilicho hai hakina njia ya kukwepea mauti:
“KWA YAKINI WEWE UTAKUFA NA WAO PIA WATAKUFA”. [39:30]
Mtu anapokufa, huwa ni pigo na msiba mkubwa kwa familia husika, kwani huwa limekauka na kuanguka tawi katika mti wa familia.
Na familia huwa imepungukiwa na tofali miongoni mwa matofali yanayoijenga familia hiyo. Mafungamano na mahusiano baina ya muislamu na nduguye muislamu, hayakatiki kwa kufa mmoja wao.
Bali kamba ya mahusiano haya huendelea kuungwa na maagano ya mwisho. Haya kwa mujibu wa sheria ni pamoja na kumkosha, kumkafini (kumvika sanda), kumswalia na kulisindikiza jeneza lake mpaka makaburini.
Ambako mwili wake utatiwa kaburini mwake na kuzikwa kama alivyosema Allah:
“KATIKA HII (ardhi/udongo) TUMEKUUMBENI, NA HUMO TUTAKURUDISHENI, NA KUTOKA HUMO TUTAKUTOENI MARA NYINGINE (muwe hai tena)”. [20:55]
Yote haya ndio yanayoifasiri kivitendo kauli ya Bwana Mtume-Rehema zimshukie-aliposema: “Na akifa lifuate jeneza lake”.
Mambo haya yana mchango mkubwa kabisa katika kuiliwaza familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha msiba. Miongoni mwa maneno ya ta’azia ambayo muislamu anatakiwa kuwaambia wafiwa ni pamoja na:
“FALILLAAHI MAA A’ATWAA WALILLAAHI MAA AKHADHA, WA KULLU SHAYN ‘INDAU BIAJALIN MUSAMMAA”.
MAANA: “Ni chake Allah alichokitoa na ni chake Allah alichokitwaa na kila kitu kina muda maalumu mbele yake”. Bukhaariy & Muslim.
Katika kuyatenda yote haya kuna fadhila na ujira mkubwa, hivi ndivyo anavyosema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
“Atakayehudhuria jeneza mpaka likaswaliwa, basi yuna yeye ‘Qiyraatw’, na atakayelihudhuria mpaka likazikwa yuna ‘Qiyraatw’ mbili. (Mtume) akaulizwa ni nini hizo Qiyraatw mbili? Akasema: Ni mithili ya majabali mawili makubwa”. Bukhaariy & Muslim.
Hizi ni sehemu tu ya haki za muislamu kwa nduguye muislamu kama zilivyoelezwa na Mtume wa Uislamu katika hadithi yake.
Kwa hakika haki za muislamu kwa muislamu mwenziwe ni nyingi mno kathiri, lakini yamkinika kuzikusanya zote na kauli ya Mtume:
“Muislamu ni ndugu ya muislamu:-
Hamdhulumu wala hamsalimishi (kwa maadui).
Na atakayekuwa katika haja ya nduguye (akamsaidia), Allah atakuwa katika haja yake yeye.
Na atakayemuondoshea shida muislamu, Allah atamuondoshea shida miongoni mwa shida za siku ya kiyama.
Na atakayemsitiri muislamu, Allah atamsitiri siku ya kiyama”. Bukhaariy & Muslim
Ikiwa kila mmoja wetu atazichunga na kumtekelezea nduguye muislamu haki zake ambazo chimbuko lake ni udugu wa imani.
Basi hapana shaka kwamba huruma, mapenzi, umoja na mshikamano vitatawala baina ya waislamu.
TANBIHI:
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amewakataza wanawake kulisindikiza jeneza mazikoni. Imekuja katika hadithi iliyopokelewa na Ummu ‘Atwiyyah:
“Tumekatazwa kuyafuata majeneza (mazikoni)…” Muslim
Si katika mila ya Uislamu kile kinachojulikana leo kama “last respect” ambacho huhusisha kukashifiwa kwa maiti na watu wakawa wanapita mbele yake mmoja baada ya mwingine kwa imani ya kutoa heshima ya mwisho.
Huu si Uislamu yaani si sehemu ya mafundisho aliyotuachia nabii Muhammad-Rehema na Amani zimshukie.