UFUMBUZI WA MTUME KATIKA MZOZO WA UWEKAJI WA “HAJAR ASWAD”

Watu wa Makkah walipoona kwamba jengo la nyumba ya Mwenyezi Mungu “Al-Kaaba” limeanza kuonyesha nyufa na kubomoka, viongozi wao waliona kuna umuhimu wa kuibomoa nyumba hiyo na kuijenga upya.

Hivyo basi likapitishwa azimio la ujenzi wa “Al-Kaaba” katika kikao chao na ndipo mikakati ya ujenzi ilipoanza.

Kila kabila likapewa jukumu lake katika kazi ile tukufu ya ujenzi wa nyumba tukufu ya Mtukufu Mwenyezi Mungu.

Bwana Mtume nae hakubakia nyuma bali alishirikiana bega kwa bega na jamaa zake katika kazi ile tukufu ya ujenzi akibeba mawe mabegani pamoja nao.

Jengo lilipomalizika na kufikia hatua ya kuliweka “Hajar Aswad” {Jiwe Jeusi} mahala pake hapo ndipo ulipoanza mzozo wa nani apewe heshima na nafasi ya kuliweka jiwe lile tukufu mahala pake huku kila kabila likigombea nafasi hiyo na kujiona lina haki zaidi kuliko kabila jingine.

Mzozo huu ulikuwa mkubwa sana kiasi cha kuhatarisha hali ya amani na utulivu waliyokuwa nayo kwa kukurubia kulipuka vita baina yao.

Viongozi wao wenye busara waliona ni vema wakaketi chini kuutafutia ufumbuzi mzozo ule mbaya.

Ni vema ikumbukwe kwamba kikao kile kilifanyika ndani ya “Al-Kaaba”, baada ya kipindi kirefu cha kuchangia fikra na mawazo ndipo wakakubaliana kwa kauli moja kuwa wamfanye kuwa ni hakimu mtu yeyote atakayekuwa wa mwanzo kuingia mle kupitia “Baniy Shaybah”, mlango huu leo unajulikana kama “Babus-Salaam”.

Hivyo wote wakayakazia na kuyakodolea macho yao upande wa mlango ule, kwa hekima anazozijua mwenyewe Mwenyezi Mungu akajaalia wa mwanzo kuingia baada ya muafaka ule awe ni Bwana Mtume – Rehma na Amani zimshukie -. Alipoingia tu wote wakamfurahikia na kumpokea kwa shangwe huku wakisema

“Huyu ni mtu mwaminifu na sote tunamkubali na kumridhia”. Wakamuhadithia tatizo lao nae aliwasikiliza kwa makini kabisa.

Walipomaliza akaikunjua shuka yake ya kujitanda na kuitandika chini, kisha akalichukua “Hajar Aswad” na kuliweka katikati ya shuka ile, hapo ndipo alipomtaka kila kongozi wa kabila kuliwakilisha kabila lake kwa kunyanyua ncha ya shuka ile.

Wakalibeba “Hajar Aswad” wote kwa pamoja mpaka mahala linapotakiwa liwekwe. Hapo sasa ndipo Bwana Mtume akalichukua kwa mkono wake mtukufu na kuliweka mahala pake.

Kwa hekima yake hiyo, mzozo ule ukaisha na makurayshi wakashangazwa sana na upeo wa kufikiri na uelekevu wa akili ya Bwana Mtume, kijana mwenye umri usiopindukia miaka thalathini na tano akaweza kufanya walichoshindwa kukifanya watu wazima na akawa ameinusuru jamii yake na janga la balaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe lililokuwa linawojongolea kutokana na mzozo wa uwekaji “Hajar Aswad”.

 

UFUMBUZI WA MTUME KATIKA MZOZO WA UWEKAJI WA “HAJAR ASWAD”

Watu wa Makkah walipoona kwamba jengo la nyumba ya Mwenyezi Mungu “Al-Kaaba” limeanza kuonyesha nyufa na kubomoka, viongozi wao waliona kuna umuhimu wa kuibomoa nyumba hiyo na kuijenga upya.

Hivyo basi likapitishwa azimio la ujenzi wa “Al-Kaaba” katika kikao chao na ndipo mikakati ya ujenzi ilipoanza.

Kila kabila likapewa jukumu lake katika kazi ile tukufu ya ujenzi wa nyumba tukufu ya Mtukufu Mwenyezi Mungu.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *