KUJIZUIA NA HARAMU NA MAMBO MACHAFU

Chimbuko na chemchem ya somo letu hili linalobeba anuani ya kujizuia na haramu/mambo machafu ni kauli yake MwenyeziMungu aliposema :


“NA WAJIZUILIYE NA MACHAFU WALE WASIOPATA CHA KUOLEA MPAKA AWATAJIRISHE KATIKA FADHILA ZAKE …..” [24:33]

Kujizuia na haramu/mambo machafu ni nguvu na uwezo uliomo ndani ya nafsi ya binadamu wa kuyadhibiti na kuyashinda matashi na matamanio ya nafsi yake yasimpondoe na njia ya MwenyeziMungu, ambayo ghalibu/mara nyingi ndio kazi ya nafsi kama tunavyosoma :


“NAMI SIJITAKASI NAFSI YANGU; KWA HAKIKA (kila) NAFSI NI YENYE KUAMRISHA SANA MAOVU, ISIPOKUWA ILE AMBAYO MOLA AMEIREHEMU….” [12:53]

Kuizuia nafsi na mambo yaliyoharamishwa ambayo mengine hujidhihirisha katika sura ya mvuto na ladha kiasi cha kuichukua mateka nafsi ya mwanadamu, ni miongoni mwa mambo na sifa tukufu anazotakiwa kupambika nazo mwanadamu ili apate kuushinda ule unyama alioumbiwa na kuwa mtu mkamilifu wa utu na ubinadamu.

Mwanadamu akiweza kufika hapo kwa kuyashinda matashi na matamanio ya nafsi yake basi atakuwa amejihakikishia kufaulu leo ulimwenguni na kesho akhera. Haya yamethibitishwa na maneno matukufu ya MwenyeziMungu :


“NA KWA NAFSI NA ALIYEITENGENEZA. KISHA AKAIFAHAMISHA UOVU WAKE NA WEMA WAKE. BILA SHAKA AMEFAULU ALIYEITAKASA (nafsi yake). NA BILA SHAKA AMEJIHASIRI ALIYEUZA (nafsi yake) [91:7-10]

Kutokana na aya hizi tunatambua kuwa kumbe nafsi ya mwanadamu tayari imekwishapewa uwezo na ujuzi wa kujua jema na baya na kisha ikaachiwa uhuru wa kuchagua kufuata jema au baya/ovu ili ikalipwe kesho akhera kwa mujibu wa uchaguzi ilioufanya hapa duniani. Qur-ani inatuambia :


“HAKIKA SISI TUMEMUONGOZA (tumembainishia) NJIA (zote mbili: kuwa hii ndiyo ya kheri na hii ndiyo ya shari) BASI (mwenyewe tena) ATAKUWA MWENYE SHUKRANI AU AWE MWENYE KUKUFURU (kukanusha)” [76:3]

Uwezo wa kujizuia na haramu/ mambo machafu huzaa tabia njema na nzuri, uwezo huu humfanya mwanadamu awe na subira kwa maana ya subira ya kweli.

Aweze kusubiri kuyashinda maovu na kuendelea kusubiri katika kutenda mema ambayo mara nyingi nafsi huyaona kuwa ni magumu na mazito.

Humpa mwanadamu kukinai na kutosheka na kile alichokadiriwa na kupewa na Mola wake, jambo ambalo ni utajiri mkubwa kama alivyosema Bwana Mtume –Rehma na amani zimshukie –
“Utajiri si (mtu) kuwa na mali nyingi lakini utajiri ni utajiri wa nafsi (ya mtu kutosheka)” Ahmad, Muslim, na Tirmidhi.

Kujizuiya na haramu humfinyanga mwanadamu kuwa mkarimu na mpaji.

Kwa ujumla tunaweza kusema nguvu na uwezo huu wa kuidhibiti nafsi isifuate matashi na matamanio yake ni KHAZINA ya asokuwa na mali na ni taji la asokuwa na utukufu.

Hebu na tujiulize basi ni nini sababu ya utukufu huu au mwanadamu afanye nini hata aweze kuifikia daraja hii tukufu ambapo ataweza kuwa juu ya nafsi yake akaweza kuitawala na sio nafsi kumkalia mbele na kumburuzia ? Mwanadamu hawezi kukifikia kilele hiki ila kwa kuachana na :

i. Tamaa mbaya. Bwana Mtume –Rehma na amani zimshukie – anatuasa :

“Jilindeni kwa Allah kutokana na tamaa yenye kupelekea katika chuki/ghadhabu na (kutokana) na tamaa iongozayo kwenye kisichotumainiwa na (kutokana) na kutamani pasipo na matumaini”. Ahmad,Al-twabraaniy na Al-haakim.

ii. Pupa katika kuchuma mali :

Hili ndio mama wa maovu yote, kwa sababu mwanadamu anapokuwa lengo lake ni kujikusanyia na hatimaye kujilimbikizia mali kwa kuichelea umasikini, basi sera zake huwa ni kupata tu bila kuzingatia anapata kwa njia gani, ya halali au ya haramu.

Katika hali hii mwanadamu huyu yuko tayari kukabiliana na kikwazo chochote kinachoweza kumzuia asifikie lengo lake; hata ikibidi kuitoa roho ya mwanadamu mwenziwe ndipo apate, basi yuko tayari kufanya hivyo kwa gharama yeyote ile. Mtume wa MwenyeziMungu – Rehma na amani zimshukie – anatuhadharisha :

“Hakika kila umati una fitna yake na fitna ya umati wangu ni mali” Al-tirmidhi, Ibn Hibbaan, na Al-Haakim.

iii. Kuridhia na kichache unachokipata. Amesema Bwana Mtume – Rehma na amani zimshukie –

 Bila ya shaka amefaulu aliyejinyenyekesha kwa Mola wake na akaruzukiwa chenye kumtosha na MwenyeziMungu akamkinaisha na alichompa” Ahmad, Muslim, Al-tirmidhi, na Ibn Maajah.

Mwanadamu hawezi kuifikia daraja ya kujizuia na haramu/mambo machafu kwa ukamilifu, mpaka pale atakapoweza kuukemea na kuuzuia ulimi wake, macho, masikio, tumbo na baki ya viiungo vyake vingine vya mwili.

Asiunyooshe mkono wake katika kutoa au kupokea rushwa, asiutumie mkono wake kumdhuru mtu bila ya haki, asiutumie ulimi wake kutukana, kufitinisha, kusengenya, kusema uongo, kutoa ushahidi wa uongo na kama hayo.

Ayazuiliye masikio yake kusikiliza maneno machafu ya kipuuzi na kila kilichoharimishwa kukisikiliza.

Macho yake yasiwaangalie wanawake/wanaume wasio halali yake, asivikodolee macho ya tamaa vilivyomo mikononi mwa watu, asiwatizame watu kwa jicho la dharau.

 Asiliruhusu tumbo lake kula riba, mali ya yatima na chochote kile kilichoharimishwa. Asiitumie tupu (uchi) yake mahala pasipo halali yake.

Ili mradi anatakiwa akizuie kila kiungo chake na kila lililoharamishwa na kukatazwa huku akiitafakari kauli ya Mola wake :


“HAKIKA MASIKIO NA MACHO NA MOYO; HIVYO VYOTE VITAULIZWA” [17:36]

Mtume wa MwenyeziMungu – Rehma na amani zimshukie – anatuambia

“Ukiwa nayo mambo matatu basi hakikudhuru kilichokufutu/kilichokupita katika dunia; ukweli wa mazungumzo, kuhifadhi amana na kujizuia na tamaa”

 

KUJIZUIA NA HARAMU NA MAMBO MACHAFU

Chimbuko na chemchem ya somo letu hili linalobeba anuani ya kujizuia na haramu/mambo machafu ni kauli yake MwenyeziMungu aliposema :


“NA WAJIZUILIYE NA MACHAFU WALE WASIOPATA CHA KUOLEA MPAKA AWATAJIRISHE KATIKA FADHILA ZAKE …..” [24:33]

Kujizuia na haramu/mambo machafu ni nguvu na uwezo uliomo ndani ya nafsi ya binadamu wa kuyadhibiti na kuyashinda matashi na matamanio ya nafsi yake yasimpondoe na njia ya MwenyeziMungu, ambayo ghalibu/mara nyingi ndio kazi ya nafsi kama tunavyosoma

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *