ADABU ZA DHIFA (TARATIBU ZA KUMPOKEA MGENI NA KUMKARIBISHA MGENI)

Muislamu Mkamilifu wa Imani anaamini uwajibu wa kumkirimu mgeni wake na kumpa heshima na taadhima anayostahiki kwa mujibu wa sheria.

Haya yote ni natija ya kuifanyia kazi kauli ya Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – :

 “Yeyote mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho, basi na amkirimu mgeni wake” Bukhariy na Muslim.

Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – anazidi kutuonyesha nafasi ya mgeni kwa kutuambia :

“Yeyote mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho, basi amkirimu mgeni zawadi yake.” (Maswahaba) wakauliza : Ni ipi hiyo zawadi yake (mgeni) ? (Mtume) akajibu :

 “Ni mchana na usiku wake, na ugeni ni siku tatu na (siku) zinazozidi hizo ni sadaka” Bukhariy na Muslim.

Tutabainikiwa kutokana na hadithi hizi mbili kwamba kitendo cha mtu kumpokea na kumkirimu mgeni wake, ni alama miongoni mwa alama za imani.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa ukimuona mtu anamshughulikia na kumkirimu mgeni wake, basi mshuhudie kwamba mtu huyo yuna Imani.

Pia tunafahamishwa kwamba ugeni unaotambulika kisheria, muda wake ni siku tatu, muda/kipindi hiki ndicho muislamu amelazimishwa na sheria kumkirimu mgeni.

Ama ule muda unaozidi siku tatu, akimfanyia ikramu mgeni wake, basi hiyo itatokana na wema wake na hiyo ni sadaka na akiba aitangulizayo mbele ya Mola wake.

“NA KHERI MTAKAZOZITANGULIZA KWA AJILI YA NAFSI ZENU, MTAZIKUTA KWA ALLAH. HAKIKA ALLAH ANAYAONA (yote) MNAYOYAFANYA” [2:110]

Ni kwa sababu hizi na nyinginezo, ndio imemlazimu muislamu kuzifuata adabu na taratibu zifuatazo katika suala zima la dhifa na upokezi wa mgeni :

 

  1. TARATIBU ZA WITO WA KUTEMBELEWA

1.      Awaalike kuja kumtembelea watu wema, wachamungu kwa ajili ya kutabaruku nao na wala asikaribishe watu waovu, mafasiki. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – :

“Usisuhubiane ila na muumini na wala asile chakula chako ila mchamungu” Ahmad, Abuu Dawoud, Tirmidhiy, Ibn Hibbaan na Al-Haakim.

2.      Asiwakhusishe na chakula chake matajiri peke yao bila ya mafakiri, yaani asiwaalike matajiri watupu akawaacha mafakiri na masikini.

Hili tunalipata katika kauli hii ya Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – :

“Shari ya chakula ni chakula cha walima(karamu ya harusi) wanachoalikwa matajiri bila ya mafakiri” Bukhariy na Muslim.

3.      Asikusudie kwa mwaliko wake kujifakharisha na kujionyesha mbele za watu bali akusudie kuifuata suna ya Bwana Mtume na mitume waliokuwa kabla yake kama Nabii Ibrahimu –rehema na amani ziwashukie wote-.

Nabii Ibrahimu kutokana na ukarimu wake mkubwa, alikuwa akiitwa (Abu Dhwiyfan) baba wa dhifa. Vile vile anuwie kuwafurahisha nduguze waislamu. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anasema :

“Amali ipendezayo zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu baada ya zile za faradhi ni kumfurahisha muislamu” Twabraaniy.

4.      Asimualike mtu ambaye ana yakini kuwa itamuwiya uzito kuhudhuria na atakerwa na baadhi ya jamaa watakaohudhuria.

Haya yote ni kuepuka kumuudhi na kumkera muislamu, jambo ambalo limeharimishwa.

 

B. ADABU/TARATIBU ZA KUITIKA MWALIKO :

1.      Mtu anapoalikwa na nduguye muislamu, inampasa ahudhurie bila kuchelewa ila kama ana udhuru.

Na ni vema kama udhuru umejulikana mapema, amfahamishe na kumtumia salamu mwenye shughuli mapema. Muongozo huu tunaupata katika hadithi zifuatazo : Amesema Mtume wa Allah –Rehema na Amani zimshukie – :

“Atakayealikwa basi na aitike mwaliko” Muslim. Na amesema tena :

“Lau ningealikwa maguu/makongoro ya mbuzi ningeliitikia (mualiko huo) na lau ningelipewa mkono (wa mbuzi) ningeliupokea”.

2.      Asibague katika kuitikia mwaliko baina ya fakiri na tajiri, kwa sababu kutokuitika fakiri/masikini ni kumvunja moyo na kuonyesha jeuri na kibri juu yake kwamba ana nini cha kukualika mtu kama wewe.

Miongoni mwa visa vilivyopokelewa ni kile kisa cha mjukuu wa Mtume. Siku moja Al-Hassan ibn Ally –Allah awawie radhi wote wawili – alilipitia kundi la masikini wakiwa wametandika vipande vya mkate chini ardhini wakila.

Walipomuona mjukuu wa Mtume, wakamkaribisha wakamwambia : Karibu ule pamoja nasi chakula cha mchana, ewe mtoto wa binti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie -. Akawajibu :

“Naam, hakika Mwenyezi Mungu hawapendi watu wenye kibri.” Akashuka katika nyumbu wake aliyekuwa amempanda na kula pamoja nao.

3.      Asibague baina ya mwaliko wa mbali na ule wa karibu. Akialikwa karibu huenda, akialikwa mbali haendi.

Mtu akiletewa mialiko miwili, basi auitikie ule mualiko wa kwanza kumfikia na atoe udhuru kwa ule mwaliko wa pili hata kama ulikuwa unatoka kwa mtu mtukufu.

 

4.      Asiache kuitikia mwaliko eti kwa sababu amefunga swaumu ya suna bali ahudhurie.

Ikiwa mwenye shughuli hatofurahi mpaka ale, basi na ale kwa sababu kumfurahisha muislamu ni miongoni mwa mambo ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

Kama hakula basi na awaombee Mwenyezi Mungu.

Haya yote tunayapata katika kauli za Bwana Mtume zifuatazo : Amesema Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie –

“Atakapoalikwa mmoja wenu na auitikie (mwaliko huo) akiwa amefunga na awaombee Mungu na akiwa hakufunga na ale” Muslim.

Na akasema tena : “Nduguyo amejikalifisha kwa ajili yako na wewe unasema Mimi nimefunga ?”

5.      Anuiliye kwa kuitikia kwake mwaliko wa nduguye kumuenzi na kumtukuza nduguye huyo ili apate thawabu. Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – amesema :

 “Hakika si vinginevyo, matendo yote yamefungamana na nia na kila mtu atalipwa kwa mujibu wa nia yake …”.

Kwani kwa nia njema tendo la Mubaah kama hili la kuitika mwaliko hugeuka na kuwa TWAA ambayo Muislamu hulipwa thawabu juu yake.

 

C. ADABU/TARATIBU ZA KUHUDHURIA MWALIKO :

1.      Asichelewe kufika kiasi cha kuwatia wasiwasi wenyeji wake bali afike kwa muda unaotakiwa. Kadhalika asiende mapema mno, akawashtukiza kabla hawajajiandaa, kwani hili litawakera na kuwaudhi wenyeji wake.

 

2.      Akishahudhuria asiende kukaa mbele mpaka akaribishwe. Mwenye shughuli akimuashiria kukaa mahala fulani, basi na akae hapo, asikae mahala pengine.

 

3.      Mwenye shughuli asiwaweke watu muda mrefu kiasi cha kuwachosha bali afanye haraka kuwaandalia chakula, kwa sababu kufanya hivyo ni katika jumla ya kumkirimu mgeni alikosema Mtume –Rehema na Amani zimshukie.

 

4.      Mwenye shughuli asiondoshe chakula kabla ya wageni wake hawajamaliza kula.

 

5.      Ampe mgeni wake chakula cha kutosha kwa sababu kumpa chakula kichache kisichomtosha ni kuvunja murua, na kumpa chakula kingi kuliko uwezo wake, huko ni kujionyesha. Yote haya mawili hayapendezi katika sheria.

 

6.      Mgeni akishukia mahala asikae zaidi ya siku tatu ila kama mwenyeji wake atamshikilia akae zaidi basi na akae. Anapotaka kuondoka amtake idhini mwenyeji wake.

 

7.      Mgeni anapoondoka ni juu ya mwenyeji wake kumsindikiza, kwani huko pia ni katika jumla ya kumkirimu mgeni.

 

8.      Mgeni aondoke bila ya kuwa na kinyongo na wenyeji wake hata kama aliona upungufu fulani kwa upande wao. Kwa sababu hii ndio tabia njema ambayo humuwezesha mtu kufikia daraja ya mfungaji mchana akeshaye usiku.

Hizi kwa mukhtasari ndizo adabu na taratibu zinazohusiana na zoezi zima la dhifa na kumkaribisha mgeni katika uislamu kama alivyotuelekeza na kutufundisha bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie -.

 

ADABU ZA DHIFA (TARATIBU ZA KUMPOKEA MGENI NA KUMKARIBISHA MGENI)

Muislamu Mkamilifu wa Imani anaamini uwajibu wa kumkirimu mgeni wake na kumpa heshima na taadhima anayostahiki kwa mujibu wa sheria.

Haya yote ni natija ya kuifanyia kazi kauli ya Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – :

 “Yeyote mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho, basi na amkirimu mgeni wake” Bukhariy na Muslim.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *