JIEPUSHE NA GHURURI ZA DUNIA

Ewe ndugu mpenzi katika imani-Allah akurehemu. Ninamuomba Allah atuwafikishe kufahamu kuwa miongoni mwa mambo yenye kuhilikisha ni “ghururi”.

Pengine utataka kuniuliza ghururi ni nini? Ikiwa hivyo ndivyo, basi ninakusihi uniazime sikio la usikivu. Ninasema, ghururi: ni kitendo cha mtu kuichanganya nafsi yake kwa kuionyesha mambo/vitu kinyume na uhalisia wake.

Kwa mantiki hii, tunaweza kusema kuwa ghururi ni madanganyo ya nafsi yanayotokana na uoni dhaifu (ujuzi duni) katika dhana nzima ya dini.

Pia kutokana na maarifa lemavu juu ya uhalisia wa dini ambao husababishwa na kujikingikiwa (kutokujua) athari ya amali mbaya na vitimbi vya adui shetani.

Ghururi huchangiwa kwa kiasi kikubwa na matamanio ya nafsi yanayomtawala na kumpeleka hovyo mwanadamu. Allah Mola Mtukufu anatutahadharisha waja wake na ghururi, anatuambia:

“ENYI WATU! BILA SHAKA AHADI YA ALLAH NI HAKI. BASI YASIKUGHURINI (yasikudanganyeni) MAISHA YA DUNIA. WALA YULE GHARURI (mdanganyaji mkubwa; Iblisi) ASIKUGHURUNI JUU YA ALLAH. KWA YAKINI SHETANI NI ADUI YENU, BASI MFANYENI ADUI (yenu, kwa hivyo msimtii) KWA ANALIITA KUNDI LAKE LIWE KATIKA WATU WA MOTONI”. [35:5-6]

Allah anatutajia baadhi ya wasifu wa watu walioghurika kupitia kauli yake:

“SEMA: JE! TUKUJULISHENI WENYE KHASARA KATIKA VITENDO (vyao)? HAO AMBAO BIDII YAO (hapa duniani) IMEPOTEA BURE KATIKA MAISHA YA DUNIA, NAO WANAFIKIRI KWAMBA WANAFANYA AMALI NJEMA! HAO NI WALE WALIOZIKATAA (waliozikanusha) ISHARA ZA MOLA WAO NA (wakakataa) KUKUTANA NAE. KWA HIVYO VITENDO VYAO VIMERUKA PATUPU, WALA HATUTAWASIMAMISHIA MIZANI SIKU YA KIYAMA. HIVYO JAHANAMU NI MALIPO YAO KWA SABABU WALIKUFURU NA KUZIFANYIA MZAHA AYA ZANGU NA MITUME YANGU”. [18:103-106]

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anatubainishia ni nani mwenye akili na nani hamnazo, anasema:

“Mtu mwenye busara (akili) ni yule aliyeihifadhi nafsi yake na akafanya amali njema kwa ajili ya maisha baada ya kufa. Na mtu ajizi (mlemavu wa akili) ni yule aliyeifuatishia nafsi yake matamanio yake (hiyo nafsi) na akatamani kwa Allah matamanio (matarajio) matupu (yasiyo na amali njema)”. Tirmidhiy

Ewe ndugu yangu uliyemuamini Allah na Mtume wake, fahamu na uelewe kuwa kuna aina nyingi za ghururi.

Kama ambavyo zilivyo mbeya (sampuli) za wenye kughurika katika janibu (pande) zote mbili; janibu ya twaa na ile ya maasi.

Hebu nipe nafasi nikupigie mfano wa ghururi kwa janibu ya wana twaa (watu walio katika twaa ya Allah) ili tupate kwenda sambamba katika darsa yetu hii.

Sote tunatambua fika kwamba kutafuta elimu ni fardhi ya lazima kwa kila muislamu; mwanamume na mwanamke.

Mja akachagua kumtii Mola wake, akajiingiza katika harakati za kuitafuta elimu. Allah akambariki katika jitihada zake hizo akamruzuku elimu, lakini yeye baada ya kuipata hiyo elimu akawa anafanya ngojangoja kutenda amali kwa mujibu wa elimu aliyoipata.

Kisha akaghurika na kauli zilizopokewa katika kutaja ubora wa elimu na na fadhila za kuitafuta. Huku akighafilika na kauli zilizopokewa katika kutaja makamio makali kwa upande wa mtu asiyetenda kwa mujibu wa elimu yake.

Fahamu ewe ndugu yangu mwanachuoni, mwanafunzi, msikilizaji wa elimu na mpenzi wa elimu kwamba elimu uliyoruzukiwa na Mola wako inaweza kuwa ni hoja ama ya kukuokoa au kukuangamiza.

Elimu itakayokunufaisha na kukuokoa leo hapa duniani na kesho kule akhera ni ile iambatanayo na amali (matendo).

Ama elimu bila ya amali, haya ni maangamivu tu na si vinginevyo na ghururi tupu. Mfano mwingine, sote tunakongamana kwamba ni wajibu wa mwenye kujua kukifundisha alichokijua kwa wenzake wasiojua.

Huku akiamini kuwa elimu aliyonayo ni amana na ni neema ya Allah, kwa hivyo ataulizwa aliitumiaje: “KISHA KWA HAKIKA MTAULIZWA SIKU HIYO JUU YA NEEMA (mlizopewa mlizitumiaje)”. [102:8]

Mtu akijitua dhima hii kwa kuamua kufundisha, lakini akafundisha kwa malengo fulani. Akafundisha ili apate uongozi na vilivyo mikononi mwa watu na huku akidhania na kuitakidi kwamba yeye amesoma na anasomesha kwa ajili tu ya Allah.

Hii pia si cho chote bali ni miongoni mwa aina za ghururi. Fahamu ewe ndugu yangu kwamba fahari, kiburi na majivuno ni sumu kali na ni adui mkubwa wa amali njema, kwani huzipomosha na kumrusha patupu mtendaji wa amali hizo zilizochanganyika na sifa mbaya hizo.

Au mtu akafanya ibada kwa ajili ya kuwaonyesha watu (ria) na kutafuta daraja/utukufu kwao. Huku yeye mwenyewe akijiona kuwa anafanya amali hizo kwa ajili ya Allah (Ikhlaaswi) na kwa ajili ya kujikurubisha kwake.

Huyu ni maghururi anaidangaya nafsi yake, kwani hana atakachokipata mbele ya Allah kwa amali yake hiyo. Ama daraja, utukufu na kuonwa na watu haya atayahodhi tu bila ya shaka kwa sababu ndio aliyoyakusudia.

Mtendaji twaa wa namna hii tunamnasihi amtegee sikio swahaba wa mtume; Abuu Dardaai-Allah amuwiye radhi-asemaye:

(Uzuri ulioje/wema ulioje wa usingizi na kula kwa watu wale wenye akili. Jinsi/namna wanavyoishinda kesha na funga ya watu wajinga. Amali ya uzani wa mdudu chungu ya mtu mwenye yakini na taqwa ni bora zaidi amali hiyo kuliko amali mfano wa majabali za watu walioghurika).

Hii ni baadhi tu ya mifano ya ghururi katika twaa, nakuomba ewe ndugu yangu usinitupe mkono katika darsa ijayo ili nikupigie mifano ya ghururi katka janibu ya maasi.

Ewe ndugu yangu Allah-akuongoze katika kuyafuata ayaridhiayo na kuyapenda.

Naam, sasa naomba uniazime fikra, moyo na usikivu wako nikupigie mifano ya ghururi kwa  janibu ya watu maasi.

Kukosea na kufanya madhambi iwe ni kwa bahati mbaya au kwa makusudi ni sehemu ya maumbile ya mwanadamu, hili halipingiki.

Sasa basi mtu anapoasi kisha akatubu na kumuomba maghfira Mola wake kwa ulimi tu, bila ya kujua sharti za toba na uhakika wake. Kisha kwa huku kutamka kwake: “ASTAGHFIRULLAH” kwa ulimi tu, akadhania na kuitakidi kabisa kwamba amekwishatubia na Allah amemghufiria. Huyu ni maghururi na hicho akifanyacho ni ghururi tu.

Hii nayo ni ghururi, mtu kukithirisha kufanya maasi na akaendelea na maovu hayo huku akizembea kutekeleza wajibu wake katika twaa.

Halafu akawa anajihalalishia uovu wake huo kwa hoja kwamba hiyo ndiyo ‘Qadari’ ya Allah kwake.

Na kwamba yeye hana khiyari ya kutenda ama kutokutenda, kwani yote ayatendayo au kuacha kuyatenda ameandikiwa na Allah Mola Muumba wake. Katika aina zote za ghururi hii ndio kubwa yao na mwenye kuifuata ghururi hii ni mzushi na si vinginevyo.

Kadhalika miongoni mwa ghururi kwa janibu hii ya watu maasi ni mtu kuwa na matumaini ya kupata maghfira huku akizembea kutekeleza maamrisho na kujiepusha ma maharimisho.

Baadhi ya watu maasi wasiofanya ibada hupata kusema: (Hakika Allah hana haja nasi wala amali zetu, madhambi yetu hayamdhuru wala twaa zetu hazimnufaishi).

Maneno yao haya ni haki iliyolengwa batili ambayo shetani ameitia moyoni mwa huyu maghururi.

Kisha akayapitisha ulimini kwake ili apate kumkata na kumtenga na maghfira na aache kuyahangaikia, jambo ambalo ni amri ya Mola wake. Hii nayo haipungui kwa cho chote katika mizani ya ghururi.

Ndugu yangu katika imani-Allah aithubutishe imani yako-nakusihi uendelee kunitegea sikio katika mifano hii hai ya ghururi ili uepuke kutumbukia humo kwa msaada wa Allah.

Utawaona baadhi ya watu wakibweteka kufanya amali njema zitakazowanufaisha mbele ya Allah, wakijinasibisha na kutegemea wema na uongofu wa baba zao.

Wanafanya hivyo bila ya kuwaiga katika mazuri yao hayo waliyoyafanya, hii ni ghururi mbaya na isitoshe ni upumbavu muovu.

Ingelikuwa wema na uongofu wa wazee unawafaa watoto wao  bila ya wao kushirikiana nao katika wema na uongofu huo.

Basi mwanawe Nabii Nuhu-Amani imshukie-angelinufaika na utume na amali za baba yake, lakini ilikuwaje, hii hapa Qur-ani Tukufu itegee sikio mwenyewe:

 “NA NUHU ALIMUOMBA MOLA WAKE (alipomuona mwanawe anaangamia) AKASEMA: EWE MOLA WANGU! MWANANGU NI KATIKA WATU WA NYUMBANI KWANGU (mbona anaangamia)? NA HAKIKA AHADI YAKO NI HAKI, NAWE NI MWENYE HAKI KULIKO MAHAKIMU (wote). AKASEMA (Allah): EWE NUHU! HUYU SI MIONGONI MWA WATU WAKO. YEYE NI (mwenye) MWENDO USIOKUWA MZURI. BASI USINIOMBE AMBAYO HUYAJUI. MIMI NAKUNASIHI USIWE MIONGONI MWA WAJINGA” [11:45-46]

Utaona kwa mujibu wa aya kwamba wema wa mzazi bila ya wewe mwenyewe kuwa mwema hautakunufaisha kwa cho chote mbele ya Allah ila kama utamfuata kwenye wema huo. Hivi ndivyo isemavyo Qur-ani:

“NA WALE WALIOAMINI NA WAKAFUATWA NA VIZAZI VYAO NA WATOTO WAO KATIKA IMANI. TUTAWAKUTANISHA NAO HAO JAMAA ZAO, WALA HATUTAWAPUNJA KITU KATIKA (thawabu za) VITENDO VYAO, KILA MTU ATALIPWA KWA KILE ALICHOKICHUMA”. [52:21]

Hii nayo haiachi kuwa ni aina ya ghururi, mtu kukutana na waja wema, akawatumikia kwa dhana njema kabisa.

Lakini akajiepusha na kujitenga na mwendo wao mwema na kulazimikiana kwao na twaa ya Allah. Kisha akataraji kwa kuwatumikia tu mabwana hawa bila ya kuwaiga katika mema yao ataipata tu pepo ya Allah kwa baraka zao. Hii ni ghururi na wazimu mtupu tu.

Aina za ghururi ni nyingi mno kuliko tulivyowafikiwa kuzitaja na wala mja hataokoka na ghururi hizi ila ni kwa kurejea kwa Allah na kutegemea fadhila na ukarimu wake.

Kurejea huko kuwe ni pamoja na kutinda na kupania katika kumtii na kujitahidi katika kumuabudu. Yote haya yaende sambamba na kujiepusha pamoja na kujitenga na maasi na kumshukuru kwa kukuwezesha kuwa katika twaa yake. Huku ukidumisha unyenyekevu, dua na istighfari mchana na usiku.

 

JIEPUSHE NA GHURURI ZA DUNIA

Ewe ndugu mpenzi katika imani-Allah akurehemu. Ninamuomba Allah atuwafikishe kufahamu kuwa miongoni mwa mambo yenye kuhilikisha ni “ghururi”.

Pengine utataka kuniuliza ghururi ni nini? Ikiwa hivyo ndivyo, basi ninakusihi uniazime sikio la usikivu. Ninasema, ghururi: ni kitendo cha mtu kuichanganya nafsi yake kwa kuionyesha mambo/vitu kinyume na uhalisia wake.

Kwa mantiki hii, tunaweza kusema kuwa ghururi ni madanganyo ya nafsi yanayotokana na uoni dhaifu (ujuzi duni) katika dhana nzima ya dini.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *