SIJIDA YA KUSAHAU (SIJIDATIS–SAH–U).
AINISHO/MAANA YA KUSAHAU:
Neno “Kusahau” lina maana mbili kama ifuatavyo:-
I . KUSAHAU KILUGHA:
Katika lugha ya kawaida kusahau kunamaanisha kupoteza kumbukumbu za kitu/jambo au kughafilika na jambo.
Bila ya kujali kuwa upotezaji huu wa kumbukumbu ni wa muda tu au ni wa milele.
II. KUSAHAU KISHERIA (KIFIQ-HI):
Muradi na mapendeleo ya neno “kusahau” katika somo letu hili ni yale makosa (kunguwao) anayoyafanya mwenye kuswali ndani ya swala yake.
Bila ya kuangalia amefanya makosa hayo kwa bahati mbaya (kwa kusahau) au kwa makusudi mazima.
FALSAFA/HEKIMA YA SIJIDA YA KUSAHAU:
Sheria ya Kiislamu imeyazingatia maumbile ya mwanadamu na kumuona kuwa ni kiumbe dhaifu anayesahau na kukumbuka kwa kuyazingatia maumbile haya ya mwanadamu ndipo sheria ikamuwekea kiumbe huyu “Sijida ya kusahau” katika swala yake ili:-
Amfukuzilie mbali shetani anayemtia katika wasiwasi huu wa kusahu.
Ayazibe makosa ambayo kwa namna moja au nyingine anaweza kuyatenda ndani ya swala yake.
III. HUKUMU YA SIJIDA YA KUSAHAU:
Sijida hii ya kusahau inaweza kuwa ama ni wajibu au ni suna.
Wakati gani sijida ya kusahau inakuwa ni WAJIBU?
Sijida ya kusahau inakuwa wajibu wakati ambapo mwenye kuswali anapokuwa maamuma nyuma ya Imamu wake.
Imamu wake huyu atakaposahau na kusahu kwake huku kukampelekea kusujudu kwa sababu ya kusahau huko.
Akasujudu sijida ya kusahau katika hali hii kutamuwajibikia maamuma aliye nyuma ya Imamu huyu kumfuata Imamu wake katika kusujudu huko hata kama yeye (maamuma) hakusahau.
Angalia maamuma huyu atapomkhalifu Imamu wake asimfuate katika huko kusujudu swala yake itabatilika na kutamuwajibikia kuirejea tena (kuiswali upya.
Wakati gani sijida ya kusahau inakuwa SUNA ?
Sijida ya kusahau itakuwa ni suna wakati ambapo mwenye kuswali atapoacha cho chote ambacho si katika jumla ya nguzo za swala kama kuacha kuleta Qunuut katika swala ya Sub-hi au swala ya Witri ya Ramadhani.
DALILI/USHAHIDI WA SIJIDA YA KUSAHAU:
Sijida ya kusahau imethibiti katika Suna ya Mtume. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah–Allah amuwiye radhi– amesema:
“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: Alituswalisha swala ya Adhuhuri au ya Alasiri, akatoa salamu. Dhul-yadaini akamwambia: Swala ewe Mtume wa Allah, je imepunguzwa (idadi ya rakaa zake)? Mtume akauliza: “Ni kweli ayasemayo (Dhul-yadaini)? (Maswahaba) wakasema: Naam, (Mtume) akaswali rakaa mbili nyingine, kisha akasujudu sijida mbili”. Bukhaariy
Tutazitaja dalili nyingine wakati tutakapotaja sababu za kusujudu sijida ya kusahau.
MGAWANYO WA MATENDO YANAYOWEZA KUACHWA NA MWENYE KUSWALI NDANI YA SWALA YAKE:
Matendo ya swala ambayo mwenye kuswali anaweza kuyaacha ndani ya swala yake ama kwa makusudi au kwa kusahau, yanagawika katika mafungu matatu. Ima mwenye kuswali atakuwa ameacha tendo linalloitwa:-
FARDHI na pia huitwa NGUZO, au
2. SUNAH na sunah ikusudiwayo hapa ni ile inayoitwa “Ba’adh”.
SUNAH isiyo “Ba’adh”, yaani suna iitwayo “Haiah”.
Hii ni kama vile Takbira za maguroguro (kuhama kutoka Qiyaamu kwenda rukuu, kutoka Itidali kwenda sijida na kadhalika) na kunyanyua/kuinua mikono wakati wa kuleta Takbira ya kuhirimia swala.
HUKUMU ZINAZOANDAMIA MATENDO HAYA:
FARDHI: Tendo la fardhi/nguzo lililoachwa kwa makusudi HUBATILISHA swala na lile lililoachwa kwa makusudi halikaliwi badali, yaani haliungwi na sijida ya kusahau.
2. SUNAH BA’ADH: Tendo la Sunah mithili ya Tashahudi ya mwanzo, mkao wake, Qunuut.
Mwenye kuswali akisahau kuleta cho chote miongoni mwa matendo haya, atapaswa kusujudu sijida ya kusahau.
SUNA HAIAH: Tendo linaloingia chini ya sunah hii ni mithili ya Tasbihi za rukuu, sijida na kadhalika.
Mwenye kuswali hawajibikiwi kusujudu kwa kusahau bila ya kuangalia kuwa aliacha makusudi au kwa kusahau.