KERO ZA MAKURAISHI DHIDI YA MASWAHABA WA MTUME

Kero na maudhi ya Makurayshi hayakuishia kwa Bwana Mtume bali yaliwagusa na kuwakumba pia na maswahaba wake.

Makurayshi walipoona kwamba Nabii Muhammad, sasa amezungukwa na kundi kubwa la watu, amepata wafuasi wengi na tayari amekuwa ni mtu mwenye heshima anayetajika vema, wakabuni mbinu mbali mbali za mateso na adhabu dhidi ya wafuasi hawa.

Ili iwe ni onyo kwa wengine wanaotaka kumfuata, wasimfuate ili wasalimike na adhabu na mateso. Pia kuwafanya wale wote waliokwishamfuata Nabii Muhammad wabadilishe uamuzi wao na kurejea tena katika mila na dini ya wahenga wao.

Sehemu kubwa ya adhabu iliwakumba zaidi wanyonge miongoni mwa mafakiri na watumwa. Wakawa wakiwaadhibu kwa kuwafunga kamba za mikono na miguu na kisha kuwalaza kwenye mchanga uunguzao wa jangwani katika wakati wa jua la utosi na kuwawekea mawe mazito vifuani mwao huku wakiwapiga kwa mijeledi, sambamba na kuwachoma kwa moto.

Mateso na adhabu kali hizi kali ziliwafanya baadhi ya maswahaba kushindwa hata kukaa, wengine walipoteza fahamu na kuchanganyikiwa kabisa. Kuna wengine ambao walipoteza maisha yao adhabuni. Fani na aina hizi za mateso na maovu haya zilidhihirisha unyama na ukatili waliokuwa nao makurayshi dhidi ya Uislamu na wafuasi wake.

Miongoni mwa wahanga wa mateso haya, ambayo yalisababishwa na uamuzi wao wa kuachana na imani potofu ya ushirikina na kuifuata imani sahihi ya kiislamu chini ya uongozi wa Nabii Muhammad ni Muhabeshi Bilali bin Rabbaah. Bilali alikuwa ni mtumwa chini ya Umayyah bin Khalaf.

Bwana wake huyu alikuwa akimlaza chali katika mchanga wa jangwani wakati wa jua kali kabisa, kisha huamrisha awekewe jiwe zito kifuani mwake na kumwambia :

Wallah, utaendelea kuwa katika adhabu hii mpaka umkufuru Muhammad na umuabudu lata na uzzah!. Naye Bilali akisema huku akiwa adhabuni : “Ahad …. Ahad!” yaani Mungu mmoja … Mungu mmoja!

 Bwana Abu Bakri katika pitapita zake akamuona Bilali akiwa chini ya adhabu na mateso makali haya, akamwambia Umayyah :

Hivi humuogopi Mungu kwa kumuadhibu maskini huyu ? Umayyah akamjibu : Wewe ndiye uliyemponza kwa kumuharibu na kumtoa katika dini yetu.

Bwana Abu Bakri akamwambia : Mimi ninaye kijana barobaro na mwenye nguvu kuliko huyu, tena yu katika dini yako, nikupe kijana huyo awe badala ya Bilali ?

 Umayyah akasema : Nimekubali. Bwana Abu Bakri akampa Umayyah kijana wake naye akamtwaa Bilali na kumuacha huru. Hivi ndivyo Bilali alivyonusurika na mateso haya kwa sababu tu ya imani yake.

Ammaar bin Yaasir pia alikuwa ni miongoni mwa wahanga wa mateso haya makali. Ammaar alisilimu yeye na wazazi wake wakati Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipokuwa akiitumia nyumba ya Al-Arqam bin Abul-Arqam kama msikiti na kituo cha kukutana na wafuasi wake.

Yeye alikuwa ni mtu wa thelathini na kitu kusilimu. Familia hii ilikuwa ikadhibiwa na Bani Makhzum katika mchanga uunguzao wa jangwani.

Mtume alikuwa akiwapitia wakiwa ndani ya adhabu na kuwaambia :

“Subirini enyi familia ya Yaasir, bila ya shaka miadi yenu ni pepo“. Yaasir baba yake Ammaar – Allah awawie radhi wote – alikuwa akiwa matesoni.

Mkewe, mama yake Ammaar akamtolea maneno ya ukali Abu Jahal, maneno haya yalimkera na kumchoma Abu Jahal.

Akaamua kumchoma mkuki mbeleni na kumuua mbele ya mwanawe. Historia ya Uislamu haiandikiki bila ya kumtaja bibi huyu, kwani yeye ndiye mtu wa kwanza kuuawa shahidi katika Uislamu.

Baada ya kifo cha baba na mama yake, Ammaar alizidishiwa adhabu maradufu. Wakati walimuadhibu kwa kumlaza katika mchanga wa jangwani na kumuwekea jiwe kubwa kifuani, mara nyingine wakimuunguza kwa moto na huku wakimuambia :

Hatutakuachilia mpaka umtukane Muhammad na uwataje kwa wema lata na uzzah. Akafanya kama wanavotaka kutokana na adhabu kali ndipo walipomuachia.

Akamuendea Bwana Mtume il-hali akilia, Mtume akamuuliza “Kuna nini nyuma yako ?”. Akamjibu : ni shari ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ! mambo yalikuwa hivi na hivi. Mtume akamuuliza : “Unaonaje moyo wako, ukoje ?” Akajibu : ninauona umejaa imani.

Mtume akamwambia : “Ewe Ammaar, wakirudia (kukuadhibu) nawe rudia (kusema uliyoyasema)”. Hapo ndipo Mwenyezi Mungu alipoteremsha kauli yake :

 “ANAYEMKUFURU ALLAH BAADA YA UISLAMU WAKE (inamngojea adhabu kubwa) ISIPOKUWA YULE ALIYESHURUTISHWA, HALI YA KUWA MOYO WAKE UMETUA JUU YA UISLAMU (wake) …” [16:106].

Ammaar bin Yaasir alitoa mchango mkubwa katika vita vyote alivyopigana Bwana Mtume dhidi ya maadui wa Uislamu ambao walipania kuufuta kabisa Uislamu katika uso wa ardhi hii.

Tutakuwa tumefanya sivyo iwapo hatutomtaja Khabbaab bin Al-Aratt kama mhanga wa mateso na adhabu kali za makurayshi kwa waislamu hawa wanyonge.

Huyu alikuwa akivuliwa nguo na makafiri, kisha wakambandika mchanga wa moto mgongoni na wakati mwingine mawe ya moto ili kumshurutisha kumkufuru Allah.

Lakini Khabbaab – Allah amwie radhi – akathibiti na imani yake pamoja na mateso hayo makubwa. Orodha ya wahanga wa mateso kwa sababu tu ya imani yao haikamiliki bila ya kumtaja Swuhayb bin Sinaan – Allah amuwie radhi – huyu pia aliadhibiwa vikali kabisa, lakini mateso na adhabu aliyopewa havikuwa kitu mbele ya imani yake thabiti. Kamwe hakuyumbishwa na adhabu, bali ilimzidishia imani juu ya imani.

Aamir bin Fuhayrah, naye ni mmoja wa walioonja adhabu na mateso makali ya makurayshi kwa sababu ya imani yake ya Mungu Mmoja asiye na mshirika.

Aliokolewa katika adhabu hii na Bwana Abu bakri ambaye alimnunua na kisha kumwacha huru ikiwa ni alama ya mapenzi na udugu wa kiislamu.

Aamir aliuuawa baadaye katika vita vya Biir Maunah, alisema alipochomwa mkuki : naapa kwa Mola wa Al-Kaaba nimefuzu.

Tukiendelea kuwataja wahanga wa mateso, tunakutana na Abu Fukayhah aliyekuwa mtumwa wa Swafwaan bin Umayyah. Huyu alisilimu pamoja na Bilali.

Bwana wake aliposikia habari za kusilimu kwake, alimfunga kamba za miguu na akaamrisha akokotwe katika mchanga uunguzao wa jangwani.

Akapitishwa katika sanamu “Juali” mojawapo wa miungu ya Makurayshi, Umayyah akamuuliza : huyu ndiye mungu wako ? Akajibu :

Allah ndiye Mola wangu na Mola wa (sanamu) hili. Kusikia jibu hilo, Umayyah akamkaba koo Abu Fukayhah kwa nguvu kabisa.

Nduguye Umayyah aliyekuwa ameambatana nae akamwambia : Mzidishie adhabu mpaka Muhammad wake aje amuokoe na kumnasua katika adhabu kwa uchawi wake.

Waliendelea kumuadhibu mpaka wakadhania amekufa, baada ya muda akazindukana. Huyu pia alinunuliwa na Bwana Abu Bakri na kumuwacha huru – Allah awawie radhi wote -.

Wanawake wa kiislamu pia walikuwa miongoni mwa watu walioathirika. Tumeshamwona shahidi wa kwanza ndani ya Uislamu; Mama Sumayyah, mama wa Ammaar.

 Wengine ni Bibi Zunayrah aliyeonja adhabu kali ya Abu Jahl. Abu Jahl alimuadhibu mama huyu mpaka akapofuka. Alipopofuka, Abu Jahl akamwambia :

Miungu yetu lata na uzzah ndiye waliokupofua macho yako. Akamjibu : Hawatambui lata na uzzah ila anayewaabudu, hii ni amri ya mbinguni na Allah ni muweza juu ya kunirejeshea tena uoni wangu.

Akapambazukiwa kesho yake il-hali akiwa anaona tena, hapo ndipo makurayshi waliposema : Haya yanatokana na uchawi wa Muhammad.

 Bwana Abu Bakri akamnunua na kumuacha huru kwa ajili ya kutafuta radhi za Mola wake. Bi Nahdiyah, Ummu Unaysi pia ni miongoni mwa wahanga wa mateso kwa ajili ya Uislamu wao.

 Hawa tuliowataja ni baadhi tu ya wengi ambao hatuwezi kuwataja wote tukawamaliza. Wote hawa waliteswa na kuadhibiwa kwa sababu tu ya imani, wako miongoni mwao waliokufa wakati wakiteswa, na kuna waliopata athari za maisha. Tusome :

“NAO HAWAJAONA BAYA LOLOTE KWAO (waislamu) ILA KUMUAMINI ALLAH MWENYE KUSHINDA (na) KUSIFIWA AMBAYE NI MWENYE UFALME WA MBINGU NA ARDHI NA ALLAH NI MWENYE KUONA KILA KITU. HAKIKA WALE WALIOWAADHIBU WAISLAMU WANAUME NA WAISLAMU WANAWAKE, KISHA WASITUBIE BASI WATAPATA ADHABU YA JAHANAMU NA WATAPATA ADHABU YA KUUNGUA (barabara).” [85:8-10]

KERO ZA MAKURAISHI DHIDI YA MASWAHABA WA MTUME

Kero na maudhi ya Makurayshi hayakuishia kwa Bwana Mtume bali yaliwagusa na kuwakumba pia na maswahaba wake.

Makurayshi walipoona kwamba Nabii Muhammad, sasa amezungukwa na kundi kubwa la watu, amepata wafuasi wengi na tayari amekuwa ni mtu mwenye heshima anayetajika vema, wakabuni mbinu mbali mbali za mateso na adhabu dhidi ya wafuasi hawa.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *