IPE NYONGO DUNIA

Ewe ndugu yangu mpenzi–Allah akurehemu–ninakuusia pamoja na kuiusia nafsi yangu tuitafakari kwa pamoja kauli hii ya Mola Muumba wetu:

ENYI WATU! BILA SHAKA AHADI YA ALLAH NI HAKI. BASI YASIKUDANGANYENI MAISHA YA DUNIA, WALA YULE MDANGANYAJI MKUBWA (Iblisi) ASIKUDANGANYENI JUU YA ALLAH. KWA  YAKINI SHETANI NI ADUI YENU, BASI MFANYENI ADUI (yenu, kwa hivyo msimtii) KWANI ANALIITA KUNDI LAKE LIWE KATIKA WATU WA MOTONI. WALIOKUFURU ITAKUWA KWAO ADHABU KALI, NA WALE WALIOAMINI NA WAKATENDA MEMA WAO WATAPATA MSAMAHA NA UJIRA MKUBWA”.  (35:5-7)

Elewa na ufahamu ewe ndugu yangu kwamba miongoni mwa mambo yenye kumuhilikisha na kumuangamiza mwanadamu ni kuipenda mno dunia.

Mtu akaikusudia khasa aipate, akaipupia, akaipondokea kiasi akawa haoni wala hasikii ila dunia tu.

Akapenda na kukitafuta cheo ili aogopwe, atukuzwe na aheshimiwe, akaenda mbio huku na huko kutafuta mali.

Akajilimbikizia mali na kuihesabu bila ya kuitolea haki yake, akawa bakhili. Yote haya ni sifa mbaya ambazo hutakiwi kupambika nazo, ewe ndugu yangu muislamu.

Mambo haya hatima yake ni kukuangamiza na kukutupa katika adhabu kali ya milele ya moto wa Jahanamu:

“…MOTO AMBAO KUNI ZAKE NI WATU NA MAWE. WANAUSIMAMIA MALAIKA WAKALI, WENYE NGUVU HAWAMUASI ALLAH KWA AMRI ZAKE, NA WANATENDA WANAYOAMRISHWA (yote)”.  (66:6)

Fahamu ewe ndugu yangu katika Imani kwamba mtu mwenye kuipenda sana dunia, akaifanya kuwa ndio lengo lake kuu na ndio kila kitu.

Kwa mapenzi haya yaliyopindukia, huyu anajiingiza na kujitia mwenyewe katika khatari kubwa na makamio makali ya Allah. Huyu anaambiwa na Mola wake:

“WANAOTAKA MAISHA YA DUNIA NA MAPAMBO (starehe) YAKE, TUTAWAPA HUMU DUNIANI (ujira wa) VITENDO VYAO KAMILI; HUMU WAO HAWATAPUNJWA (lakini akhera hawatapata kitu). HAO NDIO AMBAO HAWATAKUWA NA KITU KATIKA AKHERA ILA MOTO, NA YATARUKA TUPU WALIYOYAFANYA KATIKA (dunia) HII, NA YATAKUWA BURE WALIYOKUWA WAKIYATENDA”. (11:15-16)

Na akasema tena Allah:

“ANAYETAKA (starehe za dunia hii)  IPITAYO UPESI (wala hana haja ya akhera), BASI TUTAMPA UPESI UPESI HUMO (lakini) TUNAYOYATAKA (tena) KWA YULE TUMTAKAYE, KISHA TUMEMFANYIA JAHANAMU ATAINGIA HUMO, HALI YA KUWA NI MWENYE KUDHARAULIWA NA KUFUKUZWA (huku na huku)”. (17:18)

Na akasema tena Allah akiwataka waja wake waipe nyongo dunia  na akiwakumbusha kuondoka na kumalizika kwake:

“NA WAPIGIE MFANO WA MAISHA YA DUNIA (maisha ya dunia) NI KAMA MAJI TUNAYOYATEREMSHA KUTOKA MAWINGUNI, KISHA HUCHANGANYIKA NAYO ( maji hayo) MIMEA YA ARDHI (ikaistawi), KISHA (baadaye) IKAWA (mimea hiyo) MAJANI MAKAVU YALIYO KATIKAKATIKA AMBAYO UPEPO HUYARUSHA HUKU NA HUKO. NA ALLAH ANA UWEZA JUU YA  KILA KITU”.  (18:45)

Nabii Isa Ibn Maryam–Amani ya Allah imshukie–anatuasa kwa kutuambia:

“Msiifanye dunia kuwa ndio mungu (wenu), nayo ikakufanyeni watumwa (wake)”.

Ewe ndugu yangu, Allah anazidi kutufahamisha juu ya dunia hii inayotughuri hata tukamsahau, tutafakari pamoja:

“JUENI YA KWAMBA MAISHA YA DUNIA NI MCHEZO NA UPUUZI NA PAMBO NA KUFAHARISHANA BAINA YENU (kwa nasaba), NA KUFAHARISHANA KWA MALI NA WATOTO. (Na hali ya kuwa vyote hivi hamdumu navyo. Mfano wake) NI KAMA MVUA AMBAYO HUWAFURAHISHA (wakulima) MAZAO YAKE, KISHA YANAKAUKA UKAYAONA YAMEPIGA UMANJANO (badala ya kupiga uchanikiwiti), KISHA YANAKUWA MABUA (hayana cho chote). NA AKHERA KUNA ADHABU KALI (kwa wabaya) NA (pia) MSAMAHA WA ALLAH NA RADHI (yake kwa wema). NA HAYAKUWA MAISHA YA DUNIA ILA NI STAREHE IDANGANYAYO (mara huondoka)”. (57:20)

Allah Mola Muumba wetu anazidi kutuasa na kutuonya juu ya dunia, ewe ndugu yangu tunasihike:

“AMA YULE ALIYEASI NA AKAPENDA ZAIDI (akayafadhilisha maisha) YA DUNIA. BASI KWA HAKIKA JAHANAMU NDIYO ITAKAYOKUWA MAKAZI YAKE”. (79:37-39)

Nae Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kutokana na mapenzi na huruma yake juu yetu, anatuambia:

“Kuipenda dunia ni kichwa (chanzo/asili) CHA KILA KHATIA (kosa/dhambi)”. Akazidi kutuambia: “Dunia ni nyumba ya asiye na nyumba (akhera) na ni mali ya asiye na mali na kwa ajili ya dunia hukusanya asiye na akili”.

Sasa ewe ndugu yangu mpenzi, baada ya kuzitafakari kwa  pamoja kauli hizo za Allah Bwana Mlezi wetu na hizi kauli za Mtume wetu ambaye Allah anatuambia:

“…YANAMUHUZUNISHA YANAYOKUTAABISHENI, ANAKUHANGAIKIENI (na) KWA WAUMINI NI MPOLE NA MWENYE HURUMA”. (9: 128)

Hebu sasa tuinamishe na kukuna vichwa vyetu tujiulize swali moja, je, unalijua swali lenyewe? Bila shaka hulijui, haya nitegee sikio swali linakuja hivi:

 JE, HII DUNIA YENYE KUAPIZWA NA KUSEMWA VIBAYA HIVI NI NINI/NI KITU GANI KHASA? Hilo ndilo swali tunalopaswa kujiuliza mimi na wewe ndugu yangu na hili lifuatalo ndilo ndilo jawabu sahihi ambalo linaweza kukupa alama mia kwa mia. 

Na tulipe masikio ya usikivu: Neno dunia ni fasiri ya kila kilichopo juu ya uso wa ardhi, yaani vyenye kutamaniwa na kuonwa tamu na namna kwa namna ya starehe zenye kupendwa na kupondokewa na kupupiwa na wanadamu.

Hiyo ndiyo dunia ielewe, msingi wa yote haya umekusanywa na kauli yake Allah:

“WATU WAMETIWA HUBA YA KUPENDA WANAWAKE NA WATOTO NA MIRUNDI YA DHAHABU NA FEDHA, NA FARASI WANAOTUNZWA VIZURI (leo ni magari, ndege n.k) NA WANYAMA NA MASHAMBA NA HAYO NI MATUMIZI YA MAISHA KATIKA DUNIA, NA KWA ALLAH NDIKO KWENYE MAREJEO MAZURI”.  (3:14)

Naam, khasa hii ndio dunia na hakuna awezaye kupinga kwani:

“…NANI MKWELI ZAIDI KATIKA MANENO KULIKO ALLAH?” (4:87) “…NA NANI MKWELI ZAIDI KWA USEMI KULIKO ALLAH?”  (4:122)

Mtu atapoyapenda hayo mapenzi ya kupindukia na lengo lake katika kuyapata hayo likawa ni utupu wa starehe na ladha.

Huyu kwa malengo yake haya atakuwa ni katika jumla ya wenye kuipenda dunia na wenye kuipondokea.

Mapenzi yake haya ya kuipenda dunia yakimshinda na kumkalia juu, hata yakamfanya akachupa mipaka.

Kiasi cha kumfanya kutokujali anaipataje dunia; je, anaipata kwa njia za halali zinazomridhi Mola wake au kwa njia za haramu zinazomuudhi Mola wake?

Akafikia hatua ya kujali kupata tu na sio anapataje, kuitafuta kwake dunia kukamfikisha kumsahau Mola wake na kujitumbukiza katika lindi la maasi. Huyu ndiye mpenzi wa dunia ambaye yamethibiti kwake makamio yaliyopokewa katika kuwataja wenye kuipenda na kuifanya dunia kuwa ndio lengo lao.

Ewe mpenzi ndugu yangu ninazidi kukuusia kuwa usia wa Mtume:

“Ipe nyongo dunia utapendwa na Allah na vipe nyongo vilivyomo mikononi mwa watu, utapendwa na watu”. Ibn Maajah

Kisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie–akatubainishia kuipa nyongo dunia ni vipi, akasema:

“Kuipa nyongo dunia si kuharamisha halali na wala si kufuja mali. Lakini kuipa nyongo dunia ni kutokuwa kilichomo mkononi mwako unakitegemea zaidi kuliko kilichomo mkononi mwa Allah. Na kuwa katika (kupata) thawabu za misiba (majanga) pindi utaposibiwa kwapendeza zaidi kwako kiasi cha (kutamani) lau ungebakishiwa misiba hiyo (ili uzidi kupata thawabu)”.Tirmidhy

Mtume wa Allah akazidi kusema:

“Kuipa nyongo dunia huupumzisha moyo na kiwiliwili na kuipondokea dunia hukithirisha mashaka/wasiwasi (mhangaiko wa moyo) na huzuni. Na kukaa bila ya kazi (jambo la kufanya) huufanya moyo kuwa mgumu (mkukutavu)”.

 

 

IPE NYONGO DUNIA

Ewe ndugu yangu mpenzi–Allah akurehemu–ninakuusia pamoja na kuiusia nafsi yangu tuitafakari kwa pamoja kauli hii ya Mola Muumba wetu:

ENYI WATU! BILA SHAKA AHADI YA ALLAH NI HAKI. BASI YASIKUDANGANYENI MAISHA YA DUNIA, WALA YULE MDANGANYAJI MKUBWA (Iblisi) ASIKUDANGANYENI JUU YA ALLAH. KWA  YAKINI SHETANI NI ADUI YENU, BASI MFANYENI ADUI (yenu, kwa hivyo msimtii) KWANI ANALIITA KUNDI LAKE LIWE KATIKA WATU WA MOTONI. WALIOKUFURU ITAKUWA KWAO ADHABU KALI, NA WALE WALIOAMINI NA WAKATENDA MEMA WAO WATAPATA MSAMAHA NA UJIRA MKUBWA”.  (35:5-7)

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *