Muislamu hadhulumu na wala hadhulumiwi.
Yeye hamdhulumu mtu kwa kigezo cho chote kile, hata kama anatofautiana nae katika imani. Wala hakubali kudhulumiwa na ye yote awaye.
Hii ni kwa sababu dhulma kwa aina zake zote imeharamishwa na kukaripiwa vikali kabisa ndani ya Qur-ani tukufu na suna ya mtume (hadithi) Tusome pamoja kwa mazingatio:-
“— MSIDHULUMU WALA MSIDHULUMIWE.” [ 2 : 279]
“— NA ATAKAYEDHULUMU MIONGONI MWENU TUTAMUONJESHA ADHABU KUBWA.” [25 : 19]
“— NA ALLAH HAWAPENDI MADHALIMU.” [3 : 57]
Na Allah amesema tena katika hadithi Qudsi.
“Enyi waja wangu, hakika mimi nimejiharamishia dhulma na nimeifanya (dhulma) kuwa ni yenye kuharamishwa baina yenu, basi msidhulumiane.” Muslim.
Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie anatahadharisha juu ya dhulma, anasema: Iogopeni/jiepusheni na dhulma, kwani hakika dhulma ni viza siku ya kiyama —“ Muslim
Eeh! Utukufu ulioje wa dini hii ya uislamu; dini ya haki, uadilifu na usawa.
Hakika hii nidini ambayo inayochukia dhulma na madhalimu na inaamrisha uadilifu, kufanya hisani na kuwapa jamaa na inakataza uchafu na uovu na dhulma.
Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie anatubanishia katika hadithi hii upeo wa dhulma na mwisho mbaya wa madhalimu.
Kweli huo ni mwisho mbaya kabisa kwani dhalimu atagubikwa na kiza totoro siku ya kiyama asiweze kuiona njia. Asijue aendeje na aende wapi:
— “NA KARIBUNI (hivi) WAFANYAO DHULUMA WATAJUA NI MGEUKO (mpinduko) WA NAMNA GANI WATAKAOGEUKA (watakaopinduka)” [26 : 227]
Akasema tena Bwana mtume Rehema na Amani zimshukie:
“Hakika Allah anampururia (anampa muda) dhalimu, akimtwaa hamponyoki, kasha akasoma:
“NA NAMNA HIVI NDIVYO INAVYOKUWA KUTESA KWA MOLA WAKO ANAPOWATESA (watu wa) MIJI WANAPOKUWA WAMEACHA MWENDO WALIOAMBIWA HAKIKA TESO LAKE (Allah) LINAUMIZA (na) KALI KABISA.” [11 : 102]. Bukhaariy na Muslim.
Hebu kabla ya kuziangalia na kuzichambua aina za dhuluma, tujiulize kwanza hii dhulma inayokemewa vikali na uislamu ni nini?
Tunaweza tukaiarifisha na kuianisha dhuluma kuwa ni (kuitumia/kuikalia haki ya mtu bila uhalali au (ni kuchupa/kuvuka mipaka ya Allah) Hii nidio maana ya dhulma tunayoikusudia hapa.
Na dhuluma mara nyingi hufanyiwa mnyonge/dhaifu asiyeweza kujinusuru nayo. Dhuluma hutokana na kiza kilichoko moyoni mwa mtu, ni kiza hiki ndicho kinachomzuia kuiona haki na kuheshimu haki ya mwenziwe.
Lau moyo wa dhalimu ungelikuwa na nuru basi angezingatia haki ya mwenziwe na kuiheshimu na asingelijasiri kumdhulumu.
Aina za dhuluma:
Kuna aina kuu tatu za dhuluma ambazo zinajumuisha:-
1. Dhuluma ya mja kwa Mola wake.
Aina hii ya dhuluma hupatikana kwa mja kumkufuru/kumkanusha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuhusiana na hili tunasoma:
“— NA WALIOKUFURU NDIO WALIOJIDHULUMUI (kweli kweli)” [2 : 254]
Kadhalika hupatikana kwa kumshriikisha Mwenyezi Mungu na kitu kingine katika ibada na hii ndiyo dhuluma kubwa isiyo na msamaha mbele ya Allah.
Tusome na tutafakari kama tuendelee kumshirikisha Allah au tuache na kutubu:
“— USIMSHIRIKISHE ALLAH, MAANA SHIRIKI NDIYO DHULUMA KUBWA.” [31 : 13]
“HAKIKA ALLAH HASAMEHI KUSHRIKISHWA NA HUSAMEHE YASIYOKUWA HAYA KWA AMTAKAYE. NA ANAYEMSHIRIKISHA ALLAH BILA SHAKA AMEBUNI DHAMBI KUBWA [4 : 48]
2. Dhuluma ya mja kwa mja mwenziwe au kwa viumbe vingine vya Mwenyezi Mungu.
Aina hii ya pili ya dhuluma hupatikana pale ambapo mtu atakapowafanyia maudhi wenziwe kwa kuwavunjia heshima.
Au kwa kuwadhuru katika miili au hisia zao, au kwa kutwaa mali zao akayatenda yote hayo pasina uhalali au haki.
Bwana mtume Rehema na Amani zimshukie anatutahadharisha na kutuonya juu ya dhuluma hii pale aliposema:
“Ye yote atakayeimega haki ya muislamu kwa kiapo chake (alichoapa ili imuhalalikie), basi (kwa kufanya hivyo) Allah amekwisha muwajibishia moto na kumuharamishia pepo.”
Mtu mmoja akauliza: Hata kama ikiwa ni kitu kidogo tu, ewe Mtume wa Allah? (Mtume) akajibu:
“Hata kama ni ujiti wa mpilipili tawa (aina ya mti unaotumika kama mswaki).” Kila musilamu kwa muislamu (mwenziwe) ni haramu: (kumwaga) damu yake, (kutwaa) mali yake na (kuvunja) heshima yake” Muslim
Maneno haya ya Bwana Mtume ni tafsiri sahihi ya kauli ya Allah ndani ya Qur-ani Tukufu,tusome:
“ENYI MLIOAMINI! MSILIANE MALI ZENU KWA (njia za) BATILI. ISIP0KUWA IWE BIASHARA KWA KURIDHIANA BAINA YENU (hiyo inajuzu) WALA MSIJIUE (wala msiue wenzenu). HAKIKA ALLAH NI MWENYE KUKUHURUMIENI NA ATAKAYEFANYA HAYA KWA UADUI NA DHULUMA, BASI HUYO TUTAMUINGIZA MOTONI NA HAYO NI RAHISI KWA ALLAH.” [4 : 29-30]
3. Dhuluma ya mja kwa nafsi yake.
Mja anapoiboronga na kuichafua kwa kutenda aina mbalimbali za maasi. Hili hufanyika pale ambapo mja anapojasiri kutenda aliyokatazwa na kuharamishiwa na Mola wake na kuacha kutenda aliyoamrishwa kuyatenda:
“— NAO HAWAKUTUDHULUMU SISI (walipokhalifu amri yetu) LAKINI WALIKUWA WAMEJIDHULUMU NAFSI ZAO (kwa huko kuacha kututii).” [2 : 57]
Kama ambavyo ni haramu kudhulumu, kadhalika ni haramu kuisaidia dhuluma na madhalimu japo kwa upande wa neno.
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie anatuambia:
“Madhalimu na wasaidizi wao (wote kwa pamoja wataingizwa) motoni.” Dailamiy
Ikiwa utakuwa umeisoma darasa hii kwa moyo uliosalimika na kwa insafu (uadilifu) hutoshindwa kuona ni jinsi gani uislamu kama dini na mfumo sahihi wa maisha ulivyolishughulikia suala la kulinda na kuhifadhi haki za jamii ya wanadamu.
Umetoa umuhimu wa pekee katika kulinda haki ya mtu ya kuishi, kumiliki na kuheshimu wa utu wake