BWANA MTUME AKUBALI USHAURI WA MASWAHABA

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ndiye aliyekuwa na imani thabiti kushinda watu wote kwamba ushindi na nusra ya Allah itakuwa upande wao.

Maswahaba wake wakapatwa na usingizi wakalala kutokana na uchovu wakati ambapo yeye Mtume alikesha akiswali na kumuomba Mola wake amtimizie ahadi yake ya kumnusuru.

Aliendelea kuwa katika hali hiyo mpaka kuchomoza kwa alfajiri, hapo ndipo akawaamsha maswahaba wake kujiandaa kwa ajili ya swala.

Akawaswalisha na baada ya swala akawahamasisha na kuwahimiza kupigana kwa ajili tu ya kutaraji radhi za Allah.

Baada ya khutba hiyo fupi ya uhamasisho, kisha haraka akatoka na baadhi ya maswahaba kuelekea kwenye eneo la maji ili kuwatangulia Mkurayshi.

Alipofika sehemu ya mwanzo ya Badri yenye maji, akaamrisha ipigwe kambi hapo kuzunguka maji. Miongoni mwa maswahaba alioambatana nao alikuwa ni Al-Hubaab Ibn Al-Mundhir; huyu alikuwa ni mtaalamu wa mambo ya maji, akasema:

“Ewe Mtume wa Allah, hivi haya ndio mashukio (kambi) aliyokuamrisha Allah kushukia. Au hii ni rai yako na mbinu ya vita tu?” Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamjibu:

“Hii ni rai tu na mbinu za vita (sio amri ya Allah)”. Hapo ndipo Al-Hubaab akasema:

“Ewe Mtume wa Allah, hapa si mahala panapofaa kupiga kambi (mashukio), waondoshe watu tuende mpaka karibu kabisa na sehemu ya maji iliyo karibu na watu (Makurayshi). Mimi ninaijua sehemu yenye maji mengi ya kutosha kabisa, tupige kambi hapo na tuvifukie visima vingine vyote visiweze kutoa maji. Hapa sisi tutajenga hodhi (birika kubwa la maji) na kulijaza maji tele, kwa mbinu hii sisi tutapata maji ya kunywa na wao watakosa”.

 Baada ya Al-Hubaab kumaliza kutoa ushauri wake huo, ndipo Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamuunga mkono kwa kusema:

“Hakika umetoa rai njema kabisa yenye kufaa”. Bwana Mtume akaamuru waondoke wote na kwenda kupiga kambi mahala aliposhauri Al-Hubaab, wakawa karibu kabisa na mahasimu wao. Hapana baina yao kizuizi cho chote zaidi ya mafungu ya mchanga.

Kazi yao ya kwanza waliyoifanya mara tu baada ya kupiga kambi ilikuwa ni kujenga hodhi la maji mahala ambapo aliposhauri Al-Hubaab. Kisha wakaviziba kwa mawe na mchanga visima vyote vilivyokuwa nyuma yao.

Ujenzi wa hodhi la maji ilikuwa ni rai ya Al-Hubaab iliyomfungulia mlango wa kutoa rai Sa’ad Ibn Muaadh.

Huyu alishauri Bwana Mtume ajengewe kibanda katika uwanja wa mapambano. Kutokea kibandani humo atakuwa akishuhudia maendeleo ya vita na kutoa maelekezo ya nini cha kufanya ili kufikia ushindi. Kadhalika kibanda hicho kitasaidia kumkinga kamanda mkuu (Bwana Mtume) dhidi ya mashambulizi ya adui.

Yatakayoelekezwa kwake kwa lengo la kummaliza ili kukata mzizi wa fitina kama walivyodai. Akasema Sa’ad:

“Ewe Nabii wa Allah, unaonaje tukikujengea kibanda ukawa ndani yake na tukakuwekea tayari vipando vyako. Kisha sisi tukawa mbele yako tukipambana na adui yetu, Allah akitupa ushindi dhidi ya adui yetu, hilo ndilo tulipendalo. Na kama mambo yatakuwa kinyume na matarajio yetu tukashindwa, wewe utaweza kupanda kipando chako na kwenda kujiunga na ndugu zetu tuliowaacha huko nyuma. Kwani waliobakia huko nyuma ni watu ambao sisi hatuwashindi kwa kukupenda; wao wanakupenda zaidi kuliko sisi. Lau wangelijua kuwa kutatokea vita, bila ya shaka wasingelibakia nyuma yako na Allah angekunusuru kwa kuwatumia wao”.

Sa’ad alipomaliza kutoa ushauri wake, Bwana Mtume akamsifia na kumuombea dua njema ikiwa ni ishara ya kuukubali na kuuridhia ushauri na rai yake hiyo.

Maswahaba wakautekeleza ushauri wake huo, wakajenga kibanda kwenye kilima kinacho chomozea uwanja wa mapambano na wakamuandalia kipando bora kabisa.

 

BWANA MTUME AWAPANGA MASWAHABA WAKE TAYARI KWA MAPAMBANO HUKU AKIWAHIMIZA KUWA NA SUBIRA NA IKHLAASWI.

 

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasimama na kuanza kupanga safu za vita na kuelekeza namna ya kujihami na kushambulia.

Akampa bendera yake ya vita Musw-ab Ibn Umeir, nae akaitwaa na kwenda kuiweka mahala alipomuamrisha kuiweka.

Kisha Mtume akasimama kuziangalia safu namna alivyozipanga, akaziamuru kuelekea upande wa magharibi ili jua liwe kwa nyuma yao.

Majeshi ya mushrikina yakawa yanalielekea jua. Kabla ya kuanza kwa mapambano, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliwakhutubia maswahaba wake akiwahimiza kupigana na kuwaraghibisha ujira adhimu.

Akamuhimidi Allah na kumsifia, kisha akasema:

“Ama baad, hakika mimi ninakuhimizeni kile kile alichokuhimizeni Allah na ninakukatazeni kile kile alichokukatazeni. Bila shaka Allah Mtukufu anaamrisha mema na anapenda ukweli na huwapa kheri watu wa kheri kwa mujibu wa daraja zao mbele yake.

Bila ya shaka nyinyi mmepambaukiwa kuwa katika daraja miongoni mwa daraja za haki ambapo Allah hakubali cho chote kwa ye yote ila tu kile kilichofanywa kwa kuikusudia dhati yake Allah pekee.

Na hakika kusubiri katika sehemu za vita na dhara ni miongoni mwa mambo ambayo Allah huleta faraja kwayo na kuwa ni sababu ya kupata uokovu akhera. Mnaye miongoni mwenu Mtume wa Allah akikutahadharisheni na kukuamrisheni.

Basi leo oneni haya kumuonyesha Allah jambo ambalo litamghadhibisha na kumfanya akuchukieni, kwani hakika Allah anasema:

“…BILA SHAKA KUKUCHUKIENI ALLAH NI KUKUBWA KULIKO KUJICHUKIA NYINYI NAFSI ZENU…” [40:10]

Jitahidini kumuonyesha Mola wenu katika meneo haya ya vita jambo litakalokuwajibishieni kile alichokuahidini miongoni mwa rehema na msamaha wake.

Hakika miadi yake ni ya haki, kauli yake ni kweli na adhabu yake ni kali kabisa isiyowezwa.

Na hakika si vinginevyo mimi na nyinyi ni milki yake Allah Mwenye uhai wa maisha, Msimamizi wa kila jambo.

Ni kwake yeye ndiko tulikotegemeza migongo yetu na kwake yeye tu tunajilinda na kutegemea na marejeo yetu sote ni kwake yeye. Allah anighufirie mimi na waislamu wote”.

 

BWANA MTUME AKUBALI USHAURI WA MASWAHABA

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ndiye aliyekuwa na imani thabiti kushinda watu wote kwamba ushindi na nusra ya Allah itakuwa upande wao.

Maswahaba wake wakapatwa na usingizi wakalala kutokana na uchovu wakati ambapo yeye Mtume alikesha akiswali na kumuomba Mola wake amtimizie ahadi yake ya kumnusuru.

Aliendelea kuwa katika hali hiyo mpaka kuchomoza kwa alfajiri, hapo ndipo akawaamsha maswahaba wake kujiandaa kwa ajili ya swala.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *