Kabla hatujaanza kuzieleza suna za udhu, ni vema tukajikumbusha suna ni nini ?
Neno “Suna” lina maana mbili : maana ya kilugha na maana ya kisheria.
Suna katika lugha imefasiriwa kwa maana ya NJIA.
Maana ya suna kifiq-hi ni NJIA iliyopokewa kutoka kwa Mtume kwa maneno au vitendo.
Suna kifiq-hi zimegawanyika sehemu mbili :-
i) Suna Muakkadah (Suna kokotezwa)
ii) zisizo Muakkadah (Suna zisizokokotezwa)
Suna Muakkadah ni zile alizodumu nazo Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – kuzitenda na hakuziacha ila kwa udhuru mkubwa sana. Hukumu ya suna muakkadah ni kulipwa thawabu mtendaji na kulaumiwa na sheria mwenye kuacha kuitenda.
Ama suna zisizo muakkadah ni zile ambazo Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie- alizitenda baadhi ya wakati na kuziacha wakati mwingine. Hukumu ya suna hii ni kulipwa thawabu mtendaji na wala haadhibiwi mwenye kuacha kuzitenda.
Suna zisizo Muakkadah huitwa MANDUBU au MUSTAHABBU, haya ni majina mengine ya suna zisizo muakkadah.
Sasa tuanze kuziangalia suna muhimu za udhu, moja baada nyingine :
1. Kupiga Bismillah mwanzoni mwa kutawadha. Imepokelewa kutoka kwa Anas –Allah amuwie Radhi – amesema : Baadhi ya maswahaba –Allah awawie Radhi – walitaka kutawadha, lakini hawakuyapata maji. Mtume akawauliza :
“Je yuna yeyote miongoni mwenu maji ?”
Yakaletwa maji kidogo, (Mtume) akautia mkono wake ndani ya kile chombo chenye maji, kisha akasema :
“Tawadheni kwa BISMILLAH” {Yaani semeni hivyo mnapoanza kutawadha}Anasema Anas : Nikayaona maji yakibubujika kwa wingi kutoka vidoleni mwa Mtume, mpaka wakatawadha watu wote na walikuwa kiasi cha watu sabini. Nasaai.
2. Kukosha vitanga vya mikono kabla ya kuviingiza chomboni ikiwa anatawadha kwa kutumia chombo mfano wa kopo.
Haya ni kwa mujibu wa riwaya iliyopokelewa na Abdallah bin Zayd –Allah amuwie Radhi – aliulizwa kuhusiana na udhu wa Mtume –Rehema na Amani zimshukie – Akaagiza aletewe chombo cha maji ili awatawadhie udhu wa Mtume :
Akamwagia maji mkononi mwake, na akaviosha viganja/vitanga vyake mara tatu, kisha ndipo akaviingiza chomboni …. Bukhariy na Muslim.
3. Kupiga Mswaki : Hili linatokana na kauli ya Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – Lau si kuwaonea uzito umati wangu, ningeliwaamrisha kupiga mswaki pamoja na kila udhu” Bukhaariy na Muslim.
4 na 5. Kusukutua na kupandisha maji puani kwa kutumia mkono wa kulia na kisha kumeka kwa kutumia mkono wa kushoto.
Imepokelewa katika hadithi tuliyoitaja ya Abdillahi bin Zayd :
“ … akasukutua, akapandisha maji puani na kumeka kwa machoto matatu …” Yaani anasukutua na kumeka kwa choto moja, na hili alilikariri mara tatu.
6. Kuwatulia ndevu nyingi, yaani kuzichokoa ili maji yaweze kupenya ndani ya ngozi. Imepokelewa na Anas – Allah amuwie Radhi – Kwamba Mtume –Rehema na Amani zimshukie – alikuwa anapotawadha, huteka gao/choto la maji, akaliingiza chini ya taya lake na kuwatulia (akalimiminia) ndevu zake na kusema :
Hivi ndivyo alivyoniamrisha Mola wangu Mtukufu” Abuu Daawoud.
7. Kupakaza maji kichwa chote/kizima. Hili pia asili yake ni ile hadithi ya Abdalaah bin Zayd – Allah amuwie Radhi –
“… halafu akapakaza kichwa maji kwa mikono yake, akaipeleka mbele na kuirudisha nyuma (alikoanzia) : alianzia na sehemu ya mbele ya kichwa, kisha akaipeleka (mikono) mpaka kisogoni mwake, halafu akairudisha hadi akairejesha pale mahala alipoanzia“
8. Kuwatulia/kupachulia sehemu zilizo baina ya vidole vya mikono na miguu.
Kuwatulia vidole vya mikono hufanyika kwa kuipota/kuipacha mikono.
Ama vidole vya miguu huwatuliwa kwa kutumia kidole kidogo cha mkono wa kushoto; ukianzia na kidole kidogo cha mguu wa kulia na kumalizia na kidole kidogo cha mguu wa kushoto.
Dalili ya muongozo na maelekezo haya ni ile riwaya iliyopokelewa na kutoka kwa Laqiytwu ibn Swabrah –Allah amuwie Radhi – nikasema :
Ewe Mtume wa Allah, nielezee udhu akasema :
“ukamilishe na kuueneza udhu (kwa nguzo na suna zake) na watulia (sehemu zilizo) baina ya vidole, na balighisha katika kupandisha maji puani (yaingize ndani sana) isipokuwa utakapokuwa umefunga (usibalighishe)” Abu Dawud na Tirmidhiy
9. Kupakaza masikio maji, nje na ndani kwa maji mapya sio yale yaliyotumika katika kupakaza kichwa. Ushahidi wa haya ni ile hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Abbas –Allah awawie Radhi – Kwamba Mtume wa Allah –Rehema na Amani zimshukie – alipakaza maji kichwa chake na masikio yake ndani na nje yake” Tirmidhiy.
10. Kuosha na kupakaza maji viungo mara tatu tatu. Imepokelewa kwamba Uthmaan Ibn Affaan –Allah amuwie Radhi- amesema:
Je, nikuonyesheni udhu wa Mtume wa Allah –Rehema na Amani zimshukie – ? Kisha akatawadha mara tatu tatu. Muslim.
11. Kuanza kuosha mkono/mguu wa kulia kabla ya mkono/mguu wa kushoto. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah –Allah amuwie Radhi – kwamba Mtume wa Allah -Rehema na Amani zimshukie- amesema “Mnapotaka kutawadha basi anzieni na viungo vyenu vya kuliani” Ibn Majah.
12. Kusugua, huku ni kupitisha mkono juu ya kiungo wakati wa kukiosha. Imepokelewa na Abdallah bin Zayd -Allah amuwie radhi- kwamba Mtume wa Allah -Rehema na Amani zimshukie- alitawadha na akawa akisema hivi na huku akisugua. Ahmad.
13. Kufululiza, yaani kuviosha viungo kwa kufuatanisha kimoja baada ya kingine pasi na kutia mwanya kati yake, kiasi cha kutokauka kiungo cha mwanzo kabla ya kuoshwa kiungo cha pili. Kufanya hivi ni kumfuata Bwana Mtume, kwani hivi ndivyo alivotawadha.
14. Kurefusha kuosha mipaka/sehemu za uso, mikono na miguu. Amesema Mtume wa Allah -Rehema na Amani zimshukie-
“Hakika umati wangu wataitwa siku ya Kiyama (mbele ya hadhara ya Mwenyezi Mungu) hali ya kuwa wanang’ara nyuso, mikono na miguu yao kutokana na athari ya udhu. Basi awezaye miongoni mwenu kurefusha sehemu za uso, mikono na miguu yake na afanye hivyo” Bukhaairy na Muslim.
15. Kutofanya israfu katika utumiaji wa maji, ikawa mtu anayamwaga majo ovyo ovyo.
Ni muhimu tukakumbuka kwamba maji ni miongoni mwa neema kubwa kabisa alizoneemeshwa nazo binadamu, kwani maji ni uhai.
Kwa mantiki hii ni vema tukayatumia kwa uangalifu, ikiwa ni pamoja na kuvihifadhi vyanzo vya maji.
Tujiepushe na matumizi mabaya ya maji katika kila shughuli/kazi za maisha yetu ya kila siku, khasa khasa katika kutawadha na kukoga.
Imepokelewa na Ibn Umar -Allah awawie radhi- kwamba Mtume -Rehema na Amani zimshukie- alimpitia Sa’ad Ibn Abiy Waqqaas il-hali akitawadha (Mtume) akamwambia
“Ni ya nini israfu hii ewe Sa’ad ?” Sa’ad akauliza : Ewe Mtume wa Allah, hivi katika maji kuna israfu ? (Mtume) akamjibu : “Ndio, hata ukiwa kwenye mto upitao”
16. Kuelekea Qiblah wakati wa kutawadha kwani huo ndio upande mtukufu kuliko pande zote.
17 .Kutokuzungumza wakati wa kutawadha. Haya yote ni kumfuata Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie-
18. Kuomba/Kuleta dua hii baada ya kumaliza kutawadha, elekea Qiblah na sema :
(ASH-HADU AN LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU WAHDAHU LAA SHARIYKA LAHUU, WA ASH-HADU ANNA MUHAMMADAN ‘ABDUHUU WARASUULUH, ALLAHUMMAJ’ALNIY MINAT-TAWWABIYNA, WAJ-‘ALNIY MINAL-MUTATWAHHIRIYN, WAJ-‘ALNIY MIN ‘IBAADIKASWAALIHIYN, SUBHAANAKALLAHUMMA WABIHAMDIKA, ASH-HADU AN-LAA ILAAHA ILLA ANTA ASTAGHFIRUKA WA ATUUBU ILAYKA)
Dua hii ni kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie- aliposema :
“Atakayetawadha kwa ukamilifu, kisha akasema : -Ash-hadu …. (hadi mwisho) atafunguliwa milango yote minane ya pepo, aingie katika mlango autakao” Muslim.