KAULI MBIU YA UISLAMU

Uislamu kama dini na mfumo sahihi na kamili wa maisha unalingana na kuhubiri juu ya kuwepo Mungu aliye Muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo humo.

Unawataka wanadamu wote waitakidi kuwa YEYE ni MUNGU MMOJA WA PEKEE ASIYE NA MSHIRIKA YEYE tu ndiye anayestahiki kukusudiwa na  viumbe wake wote kwa kumuabudu, kumuomba na kumtegemea.

YEYE hakuzaa wala hakuzaliwa wala YEYE hana anayefanana naye hata mmoja. Hii ndio kauli mbiu ya Uislamu, dini ya jamii ya wanadamu.

Na akili isiyo lemavu haiwezi kupinga au kukanusha kuwepo kwa Mola Muumba wa ulimwengu na walimwengu kwani kanuni huru za kiakili zinasema kuwa (kila natija/matokeo yana sababu yake).

Kwa kuichukua kanuni hii yenye mantiki kama mizani akili haitasita kukubali kuwa kila kiumbe kina Muumba.

 Kwa sababu kiumbe ni natija/matokeo yanayohitaji sababu na sababu hiyo ndiyo Muumba Mwenyewe.

Maadam akili imetumika kumjua Muumba Mkuu, basi uadilifu wa kiakili unamsukuma mwanadamu kumuamini.

Kauli mbiu ya Uislamu inawafikia walimwengu kupitia ujumbe wa Allah Mola Muumba unaofikishwa kwao kwa njia ya Mjumbe (Mtume).

                ALLAH (MOLA MUUMBA)


 

UJUMBE (Vitabu)

 
                          MJUMBE (Mtume)

 

                WALENGWA WA UJUMBE (Jamii ya wanadamu).

 

Huu ndio utaratibu kamili wa mawasiliano baiana ya Allah Mola Muumba na mwanadamu kiumbe muumbwa chini ya mfumo Islamu.

Uislamu ni AKIDA/ITIKADI na SHERIA

A. AKIDA:

Ni ile Imani ya kumuamini Allah kuwa ni Mungu Mmoja Muumba ulimwengu asiye na

Mshirika. Na kumuamini Muhammad kuwa ni Mtume wake kwa watu wote na kuwaamini

Mitume wake kwa watu wote waliomtangulia katika kufikisha ujumbe wa Mola wake kwa nyumati zilizoutanguila umati huu wake. Akida pia inahusisha  kuiamini:-

·                     Siku ya mwisho.

·                     Kusimamisha swala

·                     Kutoa zaka

·                     Kufunga Ramadhani

·                     Kuhiji Makah.

Mambo yote haya kwa ujumla wake ndio nguzo madhubuti na imara zinazolibeba jengo Uislamu.

Akida hii ya UISLAMU ni ndugu baba moja mama mmoja na akida za mbinguni zilizotangulia kabla yake.

Ambazo zote zina dhima ya kulingania kheri (wema) na kukemea mambo maovu na machafu. Uislamu umekuja kuikamilisha dhima hii.

Hii ndio AKIDA ya Uislamu kupitia kitabu cha Uislamu (Qur-ani Tukufu).

“MTUME AMEAMINI YALIYOTEREMSHWA KWAKE KUTOKA KWA MOLA WAKE NA WAISLAMU (Pia wameamini hayo). WOTE WAMEMUAMINI ALLAH, NA MALAIKA WAKE, NA VITABU VYAKE, NA MITUME YAKE (nao husema) HATUBAGUI BAINA YA YOYOTE KATIKA MITUME YAKE (wote tunawaamini)………..” (2:285)

Na Uislamu haumlazimishi mtu kuifuata Akida yake hii kwa nguvu bali aingie Uislamu baada ya kukinaishwa na hoja zake. Hivi ndivyo tunavyosema katika kitabu cha Uislamu:

 “WAITE (watu) KATIKA NJIA YA MOLA KWAKO KWA HEKIMA NA MAUIDHA (nasaha) MEMA NA UJADILIANE NAO KWA NAMNA ILIYO BORA………..” (16:125)

“HAKUNA KULAZIMISHWA (mtu kuingia) KATIKA DINI. UONGOFU UMEKWISHA PAMBANUKA NA UPOTOFU………..” (2:256)

Isitoshe Uislamu unawafundisha waislamu namna ya kujadiliana na watu wa dini nyingine.

“WALA MSIJADILIANE NA WATU WALIOPEWA KITABU (kabla yenu) ILA KWA YALE (majadiliano) YALIYO MAZURI……….” (29: 46)

           

 

B.  SHERIA

Sheria ya kiislamu ni mkusanyiko wa maneno ya Allah Mola Mwenyezi (sheria mama) na maneno ya Mtume wake kama sheria shereheshi/fafanuzi.

 Sheria hii imezienea nyanja zote za maisha ya mwanadamu kuanzia yale ya kibinafsi mpaka ya kijamii.

Inagusa matendeano ya kila siku baina ya watu, mahusiano ya watu wenyewe kwa wenyewe, watu wa viumbe wengine, watu na ulimwenguu wao na watu na Mola Muumba wao.

Kama inavyogusa mfumo wa familia, mirathi, ndoa, mazishi na kadhalika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *