HAKI ZA WAZAZI

Hakuna mwanadamu mwenye akili timamu anayeweza kukanusha fadhila za wazazi kwa watoto wao.

Ni ukweli usiopingika kwamba wazazi wawili; baba na mama ndio sababu ya kuwepo mtoto katika ulimwengu huu.

Wazazi wana haki kubwa kwa watoto wao, kwani ni wao ndio waliowalea watoto wao wakati walipokuwa wadogo wasiojiweza kwa lo lote.

Wao ndio waliopata taabu na dhiki kwa ajili ya raha, buraha na furaha ya watoto wao, wakikesha kwa ajili ya usingizi wao.

Mama amembeba mwanawe tumboni mwake, akiishi kwa kutegemea chakula anachokila mama yake kwa kipindi cha miezi tisa kwa ghalibu. Hiki ni kipindi mpito cha dhiki na adha kubwa kwa mama:

“…MAMA YAKE AMEICHUKUA MIMBA YAKE KWA UDHAIFU JUU YA UDHAIFU…” [31:14]

Kisha baada ya kujifungua kwa uchungu mkubwa ambao pengine huyagharimu maisha yake.

Baada ya hapo ndipo hufuatia mzigo mzito wa ulezi na unyonyeshaji kwa muda usiopungua miaka miwili ya taabu, uchovu na shida.

Ni kutokana na kuutambua fika ugumu wa kipindi hiki ndio tukawa na msemo usemao: (Kuzaa si kazi, kazi kulea).

Baba nae kwa upande wake huhangaika huku na kule kwa ajili ya kuhakikisha kuwa unapata kila ukihitajiacho kwa ajili ya maisha yako.

Ikiwa ni pamoja na elimu, hukushughulikia kwa bidii zisizochoka mpaka unapokuwa mtu mzima unayeweza kujiendeshea mambo yako mwenyewe.

Na hapo ndipo wazazi wako huendelea kuwa washauri wema, wenye busara na wakutakiao mema katika maisha yako.

Ni kutokana na dhima hii kuu wanayoichukua wazazi kwa watoto wao. Ndio Allah Mola Mwenyezi akawaamrisha watoto kuwashukuru na kuwatendea wema wazazi wao:

“NA TUMEMUUSIA MWANADAMU (kuwafanyia ihsani) WAZAZI WAKE. MAMA YAKE AMEICHUKUA MIMBA YAKE KWA UDHAIFU JUU YA UDHAIFU NA (kumnyonyesha na kuja) KUMUACHISHA KUNYONYA KATIKA MIAKA MIWILI, YA KWAMBA UNISHUKURU MIMI NA WAZAZI WAKO, MAREJEO YENU NI KWANGU”. [31:14]

Na akasema tena:

“NA MOLA WAKO AMEHUKUMU KUWA MSIMUABUDU YE YOTE ILA YEYE TU. NA (ameagiza) KUWAFANYIA WEMA (mkubwa) WAZAZI. KAMA MMOJA WAO AKIFIKIA UZEE (naye yuko) PAMOJA NAWE, AU WOTE WAWILI, BASI USIWAAMBIE HATA AH! WALA USIWAKEMEE, NA USEME NAO KWA MSEMO WA HISHIMA (kabisa). NA UWAINAMISHIE BAWA LA UNYENYEKEVU KWA (njia ya kuwaonea) HURUMA (kwa kuwaona wamekuwa wazee). NA USEME: MOLA WANGU! WAREHEMU (wazee wangu) KAMA WALIVYONILEA KATIKA UTOTO”. [17:23-24]

Ni wajibu wako bali ni sehemu ya dini wewe kuwatendea wema wazazi wako, huku ukikiri kuwa ni haki yao.

Uwatendee wema kwa kauli na amali kwa kutumia mwili, mali na kila ukimilikicho huku ukiamini pasi na shaka kwamba wewe na kila ulichonacho ni mali ya wazazi wako.

Utekeleze amri yao muda wa kuwa si katika kumuasi Allah na katika lile ambalo ndani yake unaweza kufikwa na madhara:

“NA (wazazi wako) WAKIKUSHURUTISHA KUNISHIRIKISHA NA (yale) AMBAYO HUNA ILIMU NAYO, USIWATII; LAKINI KAA NAO KWA WEMA HAPA DUNIANI ( maadamu ni wazee wako, ila usiwafuate tu mwendo wao mbaya). SHIKA NJIA YA WALE WANAOELEKEA KWANGU, KISHA MAREJEO YENU NI KWANGU, HAPO NITAWAAMBIENI MLIYOKUWA MKIYATENDA”. [31:15]

Zungumza na wazazi wako kwa kauli laini, wakunjulie uso wako unapozungumza nao. Uwatumikie upeo wa uweza wako kama wanavyostahiki.

Usione kero na udhia wanapofikia hali ya utu uzima, hali ambayo ina mtihani mkuu unaohitajia subira kubwa.

Wauguze wanapougua na wala usione uzito kuwasafisha pale inapobidi. Kwani kumbuka na wewe umezaa na pengine utafikia hali hiyo ya utu uzima na kuhitajia msaada wa watoto wako kwa karibu.

Msaada uliojaa huruma na mapenzi kama wanavyohitajia wao kwako hivi sasa. Kwa hivyo watendee wema wazazi wako leo ili Allah awatume wanao kukutendea wema kesho.

Kumbuka ukiwatupa wazazi wako leo, nawe kesho utatupwa na wanao. Kwani kama utendavyo ndivyo utakavyotendewa pengine na kuzidi.

Elewa na ufahamu ewe ndugu yangu kwamba Allah ameipa haki ya wazazi daraja ya juu kabisa. Baada ya haki yake YEYE na Mtume wake, inayofuatia ni haki ya wazazi:

“MUABUDUNI ALLAH WALA MSIMSHIRIKISHE NA CHO CHOTE NA WAFANYIENI IHSANI WAZAZI WAWILI…” [4:36]

Na akasema tena:

“…YA KWAMBA UNISHUKURU MIMI NA WAZAZI WAKO…” [31:14]

Amesema Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi:

“Aya tatu zimeshuka zikikutana na mambo matatu, Allah halikubali moja bila ya (kupatikana) mwenziwe;

Ya kwanza ni kauli yake Allah: “ENYI MLIOAMINI! MTIINI ALLAH NA MTUME WAKE…” [4:59]

Basi atakayemtii Allah bila ya kumtii Mtume wake, twaa yake hiyo ya kumtii Allah haitokubaliwa ila amtii na Mtume.

Ya pili ni kauli yake Allah: “NA SIMAMISHENI SWALA NA TOENI ZAKA…” [2:110]

Basi atakayeswali bila ya kutoa zaka (na ilhali uwezo anao), swala yake hiyo haitakubaliwa.

Ya tatu ni kauli yake Allah: “…YA KWAMBA UNISHUKURU MIMI NA WAZAZI WAKO…” [31:14]

Basi atakayemshukuru Allah na akaacha kuwashukuru wazazi wake, shukurani zake hizo hazitakubaliwa”.

Hili ndilo lililomfikisha Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kusema:

“Radhi ya Allah imo ndani ya radhi ya wazazi na ghadhabu ya Allah imo ndani ya ghadhabu ya wazazi”.

Ikutoshe kuiona hadhi na daraja ya wazazi wako kwamba Mtume wa Allah ameutanguliza wema wa wazazi juu ya jihadi katika dini ya Allah.

Imekuja katika hadithi ya Ibn Masoud-Allah amuwiye radhi-amesema: Niliuliza ewe Mtume wa Allah ni amali gani ipendezayo zaidi kuliko zote mbele ya Allah? Akajibu: Kuswali swala kwa wakati wake (uliowekwa na sheria). Nikauliza (tena) kisha inafuatia amali ipi? Akajibu: Kuwatendea wema wazazi wawili. Nikauliza (tena) kisha ipi? Akasema: Kupigana jihadi katika dini ya Allah”. Bukhaariy & Muslim

Kauli hii ya Bwana Mtume katika hadithi yake hii inonyesha umuhimu wa haki ya wazazi.

Haki ambayo leo imetupwa na kuachwa kutekelezwa na watoto wengi ambao wamewakata pande wazazi wao sambamba na kuwaasi.

Leo sio ajabu tena kumuona mtoto akiwadharau na kuwafedhulikia wazazi wake.

Hawajali na pengine kufikia hata hatua ya kuwatukana huku akijisifu kuwa amewapa vidonge vyao. Leo haishangazi tena kumuona mtoto akimpiga mzazi wake.

Mwingine huthubutu hata kusema msinibabaishe eti kwa sababu tu ya kunizaa, kwani hata mimi ningetangulia ningeweza kukuzaeni, kwani kuzaa ni kazi! Ebo! Allah Mola Mwenyezi anakukataza kuwaambia wazazi wako hata neno (ah!) achilia mbali kuguna au kuwafokea, seuze kuwaambia maneno mabaya hayo!

“NA AMBAYE ANAWAAMBIA WAZAZI WAKE: KEFULE NYIE! OH! MNANITISHIA KUWA NITAFUFULIWA; NA HALI KARNE NYINGI (watu wengi) ZIMEKWISHA PITA KABLA YANGU (wala hazikufufuliwa)? NA HAO (wazee wake) WAWILI HUOMBA MSAADA WA ALLAH (na humwambia mtoto wao): OLE WAKO! AMINI (haya unayoambiwa), HAKIKA AHADI YA ALLAH NI KWELI. LAKINI YEYE HUSEMA: HAYAKUWA HAYA (mnayoyasema) ILA NI VISA VYA WATU WA KALE (tu si maneno ya kweli). HAO NDIO AMBAO IMELAZIMIKA HUKUMU JUU YAO (ya kutiwa motoni)…” [46:17-18]

Acha ujuvi, kumbuka kuwatendea wema wazazi wako ni kwa faida na maslahi yako mwenyewe. Na kuacha kufanya hivyo, haiwi ila ni kwa maangamivu ya nafsi yako.

Hebu tuitegee pamoja kauli hii ya Mtume wetu-Rehema na Amani zimshukie-sikio la usikivu na mazingatio:

“Atakayependa kurefushiwa umri wake na kuzidishiwa riziki yake, basi na awatende wema wazazi wake na awaunge ndugu zake”. Ahmad

 

HAKI ZA WAZAZI

Hakuna mwanadamu mwenye akili timamu anayeweza kukanusha fadhila za wazazi kwa watoto wao.

Ni ukweli usiopingika kwamba wazazi wawili; baba na mama ndio sababu ya kuwepo mtoto katika ulimwengu huu.

Wazazi wana haki kubwa kwa watoto wao, kwani ni wao ndio waliowalea watoto wao wakati walipokuwa wadogo wasiojiweza kwa lo lote.

Wao ndio waliopata taabu na dhiki kwa ajili ya raha, buraha na furaha ya watoto wao, wakikesha kwa ajili ya usingizi wao.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *