KIYAMA: KILA MTU ATAKUWA NA LINALOMTOSHA SIKU HIYO

 

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tuendelee kuishi na kipengele kingine chini ya mada yetu mama kama ilivyo hapo juu. Allah Mtukufu anasema: “Siku tutakayo wakusanya wachaMngu kuwapeleka kwa Arahmani Mwingi wa rehema kuwa ni wageni wake. Na tukawachunga wakhalifu kuwapeleka Jahannamu hali ya kuwa wana kiu”. Maryam [19]:85-86

 

 

Na akasema tena Yeye aliye Mtukufu: “… Na tutawakusanya siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na viziwi. Na makaazi yao ni Jahannamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu”. Al-Irsaa [17]:97

 

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Watu watakusanywa (kabla ya Kiyama) wakiwa katika matabaka matatu; wenye matumaini na wenye khofu, na watu wawili wakimpanda ngamia mmoja, na (wengine) watatu ngamia mmoja na wanne ngamia mmoja na (mpaka) kumi ngamia mmoja. Na wengine walio bakia watakusanywa na moto ambao utapumzika nao pale watakapo pumzika na utalala nao pale watakapo lala na utaamka nao pale watakapo amkia na utashinda nao pale watakapo shindia”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

 

Na mepokewa kutoka kwa bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mtafufuliwa mkiwa uchi na mazunga (msio tahiriwa). Akasema bi. Aysha-Allah amuwiye radhi: Nikauliza: Ewe Mtume wa Allah! Wanaume na wanawake wataangaliana? Akasema: Hali itakuwa ngumu mno kiasi cha wao kutokuwa na nafasi ya hilo”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

 

Na katika upokezi wa Maimamu Nasaai, Ibnu Abi Haatimy & Tirmidhiy-Allah awarehemu-alijibu: “Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha”. SAHIH SUNAN TIRMIDHIY [2652]

 

  • Na tutawakusanya siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao.

 

Imepokewa kutoka kwa Qataadah, naye akipokea kutoka kwa Anas bin Maalik-Allah awawiye radhi-ya kwamba mtu mmoja aliuliza: Ewe Mtume wa Allah! Ni namna gani kafiri atakusanywa siku ya Kiyama akikokotwa juu ya uso wake? (Mtume) akajibu: “Hivi Yule aliye mtembeza kwa miguu miwili duniani hawezi kumtembeza hali ya kukokotwa juu ya uso wake siku ya Kiyama?” Akasema Qataadah: Kwa nini asiweze, naapa kwa utukufu wa Mola wetu Mlezi (anaweza). Na hiyo ndio kauli yake Yeye aliye Mtukufu: {“… Na tutawakusanya siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na viziwi. Na makaazi yao ni Jahannamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu}. Al-Irsaa [17]:97

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *