WITO WA KUHUKUMIANA KWA KITABU CHA ALLAH

Muawiyah na Amrou bin Al-Aaswi wakauona uchovu na ukimwa wa vita ulio jitokeza katika jeshi lao, kufuatia hali hiyo Amrou akasema: Tuwalinganie kwenye kitabu cha Allah, pawepo na hakimu (muamuzi/msuluhishi) baina (upande) yetu na wao. Ndipo Muawiyah akaamuru kunyanyuliwa misahafu juu ya nyute za mikuki na mpiga mbiu aseme: Hiki ni kitabu cha Allah Mwenye izi na utukufu, kiwe hakimu baina yetu nanyi. Nani atakaye linda mipaka ya Shaamu baada ya (kuuliwa katika vita hivi) watu wa Shaamu? Nani atakaye linda mipaka ya Iraq baada ya (kumalizwa katika vita hivi) watu wa Iraq?

 

Wafuasi wa Imamu Aliy walipo iona misahafu iliyo nyanyuliwa juu, nao wakiwa wanakaribia kuibuka washindi, wakakhitalifiana. Kikawepo kikundi miongoni mwao kilicho sema: Tuuitike wito wa kuhukumiana kwa kitabu cha Allah Ataadhamiaye, na kiongozi wa kundi hilo alikuwa ni Ash’ath bin Qays Al-kindiy. Na kundi jingine likakataa ila kuendelea na vita mpaka upatikane ushindi, kwa kuwa wao walidhania ya kwamba unyanyuaji wa misahafu ni khadaa (tu ya vita). Na kiongozi wa kundi hili alikuwa ni Al-Ashtar na hiyo ndio ilikuwa rai ya Amirul-Muuminina; Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi. Lakini yeye akayafuata maoni ya wapinzani wake kwa sababu ya wingi wao. Akamtuma Al-Ash’ath; kiongozi wa kundi linalo taka kuhukumiana kwa kitabu cha Allah, aende kwa Muawiyah akamuulize anataka nini (kwa kunyanyua juu misahafu). Akamuendea na akamuuliza: Mmenyanyua juu misahafu kwa jambo gani? Akajibu: (Tumefanya hivyo), ili sisi na nyinyi tupate kurejea kwenye lile lililo amrishwa na Allah ndani ya kitabu chake. Nyinyi mumtume mtu mnaye mridhia na kumkubali nasi tumlete mtu tunaye mridhia na kumkubali. Na tutwae kwao ahadi ya kwamba watayafanyia kazi yale yaliyomo ndani ya kitabu cha Allah, hawatayakeuka hayo. Kisha sisi sote tuyafuate yale watakayo afikiana na kukongamana juu yake. Al-Ash’ath akarejea kwa Imamu Aliy, kumpasha khabari ile. Watu walipo yasikia maneno hayo yya mjumbe wa Amirul-Muuminina, wakasema: Tumeridhia na tumekubali. Watu wa Shaamu wakamteua Amrou bin Al-Aaswi na Abu Mousa Al-Ash’ariy akateuliwa na watu wa Iraq. [TAARIKHUT-TWABARIY 03/101, AL-BIDAAYAH WAN-NIHAAYAH 07/273, AL-MUNTADHWAM 05/121 & AL-KAAMIL 03/192]

Baada ya kuteuliwa mahakimu/waamuzi wa pande zote mbili, akaja Amrou ili upate kuandikwa mkataba na maagano baina ya pande hizo mbili, wakaandika:

KWA JINA LA ALLAH, MWINGI WA REHEMA, MWENYE KUREHEMU. Haya ndio maagano yaliyo fikiwa na Amiri (kiongozi) wa Waumini; Aliy”. Amrou akasema: Sisi hatumtambui kama kiongozi. Imamu Aliy akaamuru ifutwe ibara hiyo na akaagiza kuandikwe: “Haya ndio maagano yaliyo fikiwa baina ya Aliy bin Abi Twaalib na Muawiyah bin Abu Sufyaan. Aliy amefikia maagano haya kwa niaba ya watu wa Koufa na washirika wao na Muawiyah amefikia maagano haya kwa niaba ya watu wa Shaamu na washirika wao. Ya kwamba sisi tunaingia kwenye hukumu ya Allah na kitabu chake na wala tusikusanywe na chenginecho. Na kwamba kitabu cha Allah kitahukumu baina yetu tangu mwanzo wake mpaka mwisho wake. Tutakihuisha kile kilicho huishwa nacho na tutakiua kile kilicho uliwa nacho. Basi hukumu yoyote watakayo ipata waamuzi wawili hawa ndani ya kitabu cha Allah; nao ni Abu Mousa Abdullah bin Qays (kwa upande wa Aliy/Koufa) na Amrou bin Al-Aaswi (kwa upande wa Muawiyah/Shaamu), wataifanyia kazi. Na wasipo ipata hukumu ndani ya kitabu cha Allah, basi na ifuatwe Sunna adilifu, ikusanyayo, isiyo farikisha.

Wale mahakimu/waamuzi wawili wakatwaa kutoka kwa Imamu Aliy, Muawiyah na kutoka kwa majeshi ya pande zote mbili, ahadi na maagano. Ya kwamba wao (mahakimu) watapewa amani ya nafsi zao na watu wao (kwa maamuzi watakayo yafikia) na umma utawanusuru na kuwaunga mkono kwa hukumu watakayo ifikia. Na Abdullah bin Qays na Amrou bin Al-Aaswi wanayo ahadi ya Allah na maagano yake ya kuhukumu baina ya umma huu. Hukumu ambayo haitauingiza umma vitani wala kwenye kufarikiana. Na kwamba kumewaelea mahakimu wawili kuchelewesha hukumu mpaka mwezi wa Ramadhani na kwamba mahala pao pa kutolea hukumu, patakuwa ni mahala pa uadilifu kwa watu wa Koufa na watu wa Shaamu”.

Mkataba wa maagano yale ulishuhudiwa na kundi la jeshi la Sayyidna Aliy na kama hivyo kundi la jeshi la Muawiyah. Na mkataba ule uliandikwa siku ya Jumatatu, tarehe 17, mwezi wa Swafar, mwaka 37. Na wakawafikiana ya kwamba waamuzi wawili wale wakutane mahala paitwapo “Daumatul-Jandal” au mahala paitwapo “Adhruhi”, katika mwezi wa Ramadhani. Kisha watu wakamiminika kutoka mahala hapo palipo ingia ukorofi, ambapo yalikusanyika hapo makundi mawili ya waumini, yakipigana yenyewe kwa yenyewe. Lakini lile ambalo linalo lipunguza balaa hili ni kwamba makundi yote mawili yalikuwa yakimkusudia Allah kwa matendo yake. Kwa sababu wote walikuwa wanataka kuitekeleza hukumu yake Allah kwa mujibu wa Ijitihadi na rai zao. [TAARIKHUT-TWABARIY 03/103, AL-BIDAAYAH WAN-NIHAAYAH 07/277 na AL-MUNTADHWAM 05/122]

Amirul-Muuminina; Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-akaondoka Swaffein kurejea Koufa na ilhali jeshi lake likiwa katika mmeguko na ikhtilafu. Lilikuwepo kundi lililo ridhia kuhukumiana kwa kitabu cha Allah, likidhania ya kwamba hiyo ndio njia itakayo ondosha ikhtilafu na kuwakusanya pamoja Waislamu. Na kundi jingine lichukialo kuhukumiana huko, likisema vipi mtahukumiana na watu hao katika dini ya Allah. Na hawa wakajitenga na ndugu zao wakisema mmeipaka mafuta dini ya Allah (mmefanya khadaa). Na wale wakasema nyinyi mmefarikiana na Imamu wetu. Imamu Aliy alipo wasili Koufa, likajitenga naye kundi la wale walio ona ya kwamba tahakimu (kuhukumiana kwa kitabu cha Allah) ni upotevu. Kundi hili lililo jitenga likaenda mahala paitwapo “Haruuraa”, na kutokea hapo ndipo Khawaarij wakaitwa kwa jina la “Haruuriyyah”. Wakapiga kambi hapo wakiwa jumla ya watu elfu kumi na mbili na wakamtawaza Shabath bin Rib’ii kuwa amiri jeshi wao. Uimamu wa swala akapewa Abdullah bin Al-Kawaa Al-Yashkariy. Na suala la uongozi litakuwa ni shura baada ya fat-hi (ushindi) na baia iwe kwa ajili ya Allah Atukukiaye na kuamrisha mema na kukataza maovu.

Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-akamtuma kwao (hao walio jitenga) Abdullah bin Abbas na akamwambia: Usijibizane nao mpaka nije mimi. Lakini yeye hakuweza kujizuia kuongea nao, akawauliza: Ni lipi mnalo likanusha/kataa katika suala la waamuzi wawili hawa (walio teuliwa) na ilhali Allah ameamrisha wawepo baina ya wanandoa: “NA MKICHELEA KUTAKUWAPO MFARAKANO BAINA YA MKE NA MUME, BASI PELEKENI MUAMUZI KUTOKANA NA JAMAA ZA MUME, NA MUAMUZI KUTOKANA NA JAMAA ZA MKE. WAKITAKA MAPATANO ALLAH ATAWAWEZESHA…”. [04:35]

Basi (ikiwa tu kwa suala la wanandoa panahitajika muamuzi wanapo khitalifiana) ni vipi (asihitajike) kwa umma wa Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-(pale wanapo khitalifiana)? Wakamjibu: Jambo hili haliwi kwa rai na Qiyaasi, kwani suala hilo (la wanandoa) Allah ameyaacha maamuzi yake kwa waja. Na hili (la uongozi) amesha lipitisha kama alivyo ipitisha hukumu ya mzinifu na mwizi, kwa ajili hiyo basi waja hawana nafasi ya kuwa na maoni katika hilo. Ibn Abbas akawaambia, Allah Ataadhamiaye anasema: “…KAMA WANAVYO HUKUMU WAADILIFU WAWILI MIONGONI MWENU…” [05:95]

Wakamjibu wakasema: Na hilo jingine kadhaalika sio suala la wanandoa na kadhia ya kiwindwa (mnyama – kilicho tajwa na aya) ni mithili ya damu za Waislamu. Na wakaukosoa uadilifu wa Amrou bin Al-Aaswi, wakasema: Nyinyi mmewasimika watu katika amri ya Allah na ilhali Allah amekwisha ipitisha hukumu yake kwa Muawiyah na wafuasi wake. Ya kwamba ama wauliwe au warejee kwenye twaa ya Imamu na umoja wa umma. Na badala yake nyinyi mkafanya maagano/mapatano katika mikataba na ilhali Allah alikwisha yakata (yavunja hayo maagano) baina ya Waislamu na watu wanao wapiga vita, tangu ilipo shuka Surat Baraa.

Imamu Aliy akatoka kumuendea (Abdullah bin Abbas) na akashukia kwenye hema la Yazid bin Qays, baada ya kujua ya kwamba wao wataitupilia mbali rai yao. Akaswali hapo rakaa mbili na akamtawaza Aswbahaani kuwa kiongozi wa mahala hapo. Kisha akawatokea nao wakiwa katika baraza na Ibn Abbas, akawauliza: Kiongozi wenu ni nani? Wakajibu: (Ni) Ibn Al-Kawaa. Akawauliza tena: Ni wa nini/jambo gani uasi huu? Wakajibu: (Ni) kwa sababu ya uamuzi wenu (wa kuhukumiana kwa kitabu cha Allah, mlio utoa) siku ya vita vya Swaffein. Akawaambia: (Lakini mimi) niliwashurutizia waamuzi wa pande zote mbili; kuyahuisha yale yaliyo huishwa na Qur-ani na wayafishe yale yaliyo fishwa na Qur-ani, basi hakutupasii sisi kwenda kinyume na hukumu hiyo. Na wakikataa (kutwaa hukumu ya Qur-ani), sisi tutakuwa mbali na hukumu/uamuzi huo. Wakasema: Basi hebu tuambieni, wewe unaona ni uadilifu kuwapa watu jukumu la kutoa uamuzi katika kadhia ya damu? Akajibu: Hakika sisi hatujawafanya watu kuwa nndio mahakimu wa kutoa maamuzi, lakini sisi tumeifanya Qur-ani ndio iwe hakimu wetu. Na hii Qur-ani hakika si vinginevyo ni hati zilizo andikwa baina ya majalada mawili, yenyewe haineni ila watu ndio wanao izungumza. Wakauliza: Haya ni kwa nini mmeweka muda baina yenu? Akajibu: (Tumefanya hivyo) ili apate kujulikana mtu aliye jaahili na athibitike mtu mjuzi ajuaye. Na pengine Allah akaleta suluhu baina ya umma huu ndani ya kipindi hicho. Kwa kukutana nao na kuzungumza nao, wakaikubali rai yake. Ndipo akawaambia: Ingieni kwenye mji wenu, Allah akurehemuni. Wakaingia wote mpaka wa mwisho wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *