Khabari ya Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie kutoka Makkah kuelekea Madinah ziliugubika mji mzima wa Madinah.
Wenyeji wa mji huu Answaar wakawa waunguzwa na shauku ya kukutana na kumpokea mgeni huyu mtukufu, mwenye baraka anayehamia kwao.
Kila siku asubuhi walikuwa wakitoka kwenda kumngojea katika njia itokayo Makkah ili wamlaki kwa shangwe, hoihoi na furaha.
Waliendelea kumsubiri mpaka waliposhindwa kuvumilia ukali na joto la jua ndipo kurejea majumbani mwao.
Hio ndilo lililokuwa zoezi la kila siku mpaka siku ile Bwana Mtume alipofika Madinah kuanza ukurasa mpya wa da’wah akizungukwa na watu wenye nyoyo thabiti na imani isiyotetereka na walio tayari kumuhami hata kwa gharama ya uhai wao.
Kundi kubwa la wanasera na wataalamu wengi wa tarekh (historia) wanasema kwamba Mtume wa Allah Rehema na Amanzi zimshukie alifika mjini Madinah siku ya Jumatatu, mwezi kumi na mbili, mfunguo sita, katika mwaka wa kumi na tatu (13 wa utume).
Hii inawafikiana na tarehe 20 ya mwezi Septemba mwaka mia sita ishirini na mbili (622) Miladia.
Na kwamba kabla hajaingia Madinah alipiga kambi Qubah. Qubah ni kitongoji kilichopo umbali wa maili tatu (3) kusini mwa mji wa Madinah.
Hapo Qubah, Bwana Mtume alifikia nyumbani kwa Bwana Kulthum Ibn Al-hidmi, mkubwa wa kabila la Baniy Amri Ibn Auf.
Alikaa na kupumzika kwa wenyeji wake hawa kwa siku kadhaa.
Kazi ya mwanzo aliyoifanya Mtume wa Allah hapo Qubah, ilikuwa ni ujenzi wa msikiti na msikiti huu ukawa ndio msikiti wa kwanza kujengwa katika Uislamu. Huu ndio msikiti anaoutaja Allah na kuusifia ndani ya Qur-ani kwa kauli yake tukufu.
“………………MSIKITI ULIOJENGWA JUU YA MSINGI WA KUMCHA ALLAH TANGU SIKU YA KWANZA (ya kufika Mtume Madinah) UNASTAHIKI ZAIDI WEWE USIMAME HUMO. HUMO WAMO WATU WANAOPENDA KUJITAKASA NA ALLAH ANAWAPENDA WAJITAKASAO: (9: 108)
Hii ndio kauli ya Mufasirina walio wengi kwamba msikiti uliokusudiwa hapa ni Masjid Qubah. Bwana Mtume alishiriki katika ujenzi wa msikiti huu kwa mkono wake katika ubebaji wa mawe na miamba.
Alifanya kazi mpaka ikawa inaonekana athari ya uchovu. Maswahaba kutokana na kuijua daraja ya Mtume wa Allah walimsihi apumzike na awaachie wao kuifanya kazi hiyo peke yao, lakini Mtume hakupenda ila awe mmoja wao..
iii./KUSWALI MADINAH NA IJUMAA YA KWANZA BAADA YA HIJRAH.
MJI WA MADINAH WAZIZIMA KWA FURAHA YA KUJA KWA MTUME
Siku aliyowasili Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie Madinah, ilikuwa ni siku ya furaha kuu.
Mji huo haukuwahi kushuhudia katika historia yake siku ya furaha, shangwe, hoihoi, nderemo na vifijo kuliko siku hiyo ya watu walivaa nguzo zao nzuri nzuri kana kwamba wanaisherehekea siku kuu.
Wanawake nao hawakubakia nyuma, walisimama nje ya nyumba zao wakimpungia Mtume mkono wa karibu.
Watoto nao wakalipuka kwa furaha wakipiga makelele ya Amekuja Mtume wa Alah…………..! Mtume wa Allah……………!
Wajakazi na vigori wakawa wanaimba na kupiga madufu na wahabeshi wakicheza na mikuki yao, yote hayo yakiwa ni katika kumlaki na kumpokea Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie Imekuja riwaya katika sahihi Muslim na Bukhariy kutoka kwa Abuu Bakri amesema:
Tulipofika Madinah, watu walitoka majumbani na majiani (kutulaki), vijana na watumishi wakisema: Allaahu Akbari, amekuja Mtume wa Allah……..! Allaahu………! Akbar, Amekuja Muhammad! Allaahu Akbar, amekuja Muhammad………..Allaahu Akbar, amekuja Mtume wa Allah……..”
Kadhalika imepokelewa kutoka kwa Bi Aysha – Allah amuwiye radhi – amesema Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – alipowasili Madinah, wanawake, vijana wa kiume na wa kike wakaanza kuimba:
TALA-‘AL-BADRU ALAYNAA MIN THANIYYATILWADAA’I
WAJABA-SHHUKRU ALAYNAA MAA DA’AA LILLAHI DAA’I
AYYUHAL-MAB’UUTHU FIINA JI-TA BIL-AMRIL-MUTAA’I
Tafsiri:
Umetuchomozea mwezi sisi* kutoka njia ya upande wa Wadaa inapasa shukrani juu yetu* Muda wa kulingania kwa Allah mlinganiaji Ewe uliyetumwa wee katika sisi* Umeleta jambo kuliokuwa wajibu kulifuata.
Mchana ulipopanda (mchana wa saa sita), Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – alimpanda farasi wake, huku waislamu wakiwa wamemzunguka, wengine wakitembea kwa miguu na wengine wamepanda wanyama wakiwa na mapanga yao.
Kutokana na pupa yao katika kumuheshimu na kumtukuza Mtume wa Allah walisongamana kugomea hatamu za ngamia wa Mtume ili kutabaruku na Mtume.
Hiyoo Mtume anaelekea upande wa Madinah, kila alipoitia nyumba mojawapo miongoni mwa nyumba za Answaar walikuja mbele yake na kumwambia:
“Njoo ewe Mtume wa Allah kwenye nguvu, ulinzi na utajiri!” Nae Bwana Mtume akitabasamu kuonyesha shukrani na akiwaombea dua njema, halafu akasema huku akimuashiria ngamia wake: “Muacheni njia, kwani yeye ameamrishwa.
KHUTBA YA KWANZA YA MTUME – MADINAH
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie alipofika kwenye makazi ya ukoo wa Bariy Saalim Ibn Auf, ulimdiriki hapo swala ya Ijumaa.
Akaiswali swala hiyo katika uwanda wao pamoja na waislamu aliokuwa nao. Ijumaa hii ndio iliyofanya ukurasa wa swla za ijumaa katika Uislamu, yaani ndio iliyokuwa Ijumaa ya kwanza kuswaliwa.
Mtume alisimama, akamuhimidi Allah na Kumsifia kwa sifa zilizo laiki yake na khutbah yake ya mwanzo ikawa:
“Ama baad, enyi watu! Zitangulizenieni (wema) nafsi zenu. Jueni, wallah! Mmoja wenu atafikiwa ghafla na mauti na awaache mbuzi (mifugo) wake bila ya mchungaji.
Mola wake amwambie akiwa hana mkalimani wala bawabu wa kumzuia. Je, hakukujia mjumbe wangu na kukufikishia ujumbe wangu na nikakupa mali na kukufadhili kwa fadhila nyingi?
Basi leo umeitangulizia nini nafsi yako? Basi na aangalie kuliani na kushotoni asione chochote. Halafu aangalie mbele yake na hataona ila Jahanam.
Basi atakayeweza kuukinga uso wake kutokana na moto kwa kutoa japo nusu ya tende na afanye hivyo.
Na asiyepata (hata hicho kidogo cha kutoa) basi na atoe neno zuri, kwani hulipwa kwa neno hilo mfano wake mara kumi mpaka mia saba maradufu. Amani iwe juu yenu na juu ya Mtume wa Allah na Rehema na Baraka za Allah”
NGAMIA AENDA MPAKA ANAKITA MAGOTI MAHALA PA KUJENGWA MSIKITI WA MTUME.
Baada ya swala ile ya Ijumaa kumalizika, Mtume – Rehema na Amani zimshukie akampanda ngamia kuendelea na safari yake ya kuingia mjini Madinha.
Ngamia akendelea kwenda huku Bwana Mtume akiwa ameziachia hatamu zake, mpaka akakita magoti mahala pa kujengwa msikiti wa Mtume.
Mahala hapo palikuwa ni uwanja wa kuanikia tenda aliokuwa ukimilikiwa na vijana wawili mayatima wa ukoo wa Baniy Najjaar.
Uwanja huo ulikuwa ukielekeana na nyuma ya Abuu Ayyuub, Khaalid Ibn Zayd Al-answaariy . Mtume akashuka kutoka juu ya ngamia akaomba dua iliyomo ndani ya Qur-ani:
“ MOLA WANGU! NITEREMSHIE MTEREMSHO WENYE BARAKA MAANA WEWE NI MBORA WA WATEREMSHAJI” (23: 29)
Aliiomba dua hii mara nne. Hii ni dua ambayo Allah alimfundisha Mtume Nuhu – Amani imshukie aisome wakati wa kushuka kutoka ndani ya Safina. Kisha ikamjia ile hali inayomjia wakati wa kuja wahyi, walipomuondoka akasema:
“Hapa ndipo patakapokuwa makazi, Inshaallah, na akaamrisha ishushwe mizigo yake, kisha akauliza. Ni nyumba ipi ya jamaa zetu (wenzetu) iliyo karibu? Abuu Ayyuub akajibu: “Mimi ewe Nabii wa Allah, hii ndio nyumba yangu na huu hapa ndio mlango wangu” Mtume akamwambia: “Haya nenda ukatauandalie mahala pa kupumzika”
Akaenda kuandaa kisha akarudi na kusema
“ Ewe Mtume wa Allh, nimekwisha kukuandalia mahala pa kupumzikia, haya inukeni kwa baraka za Allah mkapumzike.”
MTUME AKAA KWA ABUU AYYUUB MPAKA ALIPOJENGA MSIKITI NA MASKANI YAKE.
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie akawa mgeni wa Bwana Abuu Ayyuub akaishi nae mpaka alipojenga msikiti na makazi yake.
Zawadi za aina kwa aina za vyakula na vinywaji zikawa zikimiminika mfululizo kwa Mtume wa Allah wakati alipokuwa nyumbani kwa Abuu Ayyuub.
Zawadi ya kwanza aliyoletewa akiwa nyumbani hapo ni sahani ya chakula iliyoletwa na Zayd Ibn Thaabit ikiwa na mkate uliochochevywa kwa maziwa na samli, akampa Mtume huku akimwambia: “ Hii ni zawadi kutoka kwa mama yangu”
Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie akapokea na kumuombe dua akisema: “Allah akubariki wewe na mama yako”
Akawaita maswahaba wake wakala ilikuwa hauingii usiku ila mlangoni pa Mtume kuna watu watatu kwa uchache waliobeba chakula.
Mtume alikaa nyumbani kwa Abuu Ayyuub kwa kipindi kisichopungua miezi saba na kisichozidi mwaka mmoja, mpaka alipoujenga msikiti na maskani yake.
Alikaa hapo pamoja na swahaba wake Usaamah Ibn Zayd, inasemekana kwamba Imam Aliy Ibn Abiy Twaalib pia alifikia hapo pamoja na Mtume ambaye alimkuta akiwa bado Qubah. Ama Bwana Abuu Bakri yeye alifikia nyumbani kwake Bwana Khubayb Ibn Isaaf.