UZUSHI NA UONGO USIOJUZU HATA KWA MWANAMKE WA KAWAIDA TU SEUZE MKE WA MTUME WA ALLAH!

Uzushi na uongo huu haukupasa kujuzu hata kwa mwanamke duni tu hata awe mpumbavu kiasi gani kuudhihirisha uchafu wake wazi wazi kiasi hicho.

Na aje namna hivi katika weupe wa mchana akiambatana na hawara yake huku watu wote wakishuhudia, akayafichua maovu yake yaliyojificha!

Na akaitangazia kadamnasi aliyoyatenda, hata! Hili halikubaliwi na akili nyoofu; akili yenye mizani na chekeche lenye kuchuja lenye kufaa na lisilofaa.

Kwani maumbile ya mwanamke vyo vyote vile awavyo ni kupondokea kujionyesha mzuri mbele za watu, na kujitokeza mbele yao katika mandhari kamilifu kiasi awezavyo ili watu wasimpe mgongo.

Basi je, kwa maumbile haya ya mwanamke, inawezekana kweli kwa mama wa waumini; Aysha Bint Sidiq aliye mfano kwa wanawake waumini kuudhihirisha uchafu huo?!

Hivi ndio kusema halikumtosha kemeo la Allah katika kauli yake iliyoelekezwa moja kwa moja kwa wakeze Mtume:

“ENYI WAKE WA MTUME! ATAKAYEFANYA MAOVU DHAHIRI MIONGONI MWENU, ATAZIDISHIWA ADHABU MARA MBILI, NA HAYA NI SAHALI KWA ALLAH. NA MIONGONI MWENU ATAKAYEMTII ALLAH NA MTUME WAKE NA KUTENDA MEMA TUTAMPA MALIPO YAKE MARA MBILI NA KUMUANDALIA RIZIKI YENYE HISHIMA. ENYI WAKE WA MTUME, NYINYI SI KAMA YE YOTE TU KATIKA WANAWAKE WENGINE (nyinyi ni wakeze Mtume). KAMA MNATAKA (kufanya jambo la) KUMCHA ALLAH, BASI MSILEGEZE SAUTI (zenu mnaposema na wanaume) ILI ASITAMANI MTU MWENYE UGONJWA MOYONI MWAKE (kufanya mabaya nanyi) NA SEMENI MANENO MAZURI. NA KAENI MAJUMBANI MWENU, WALA MSIONYESHE MAPAMBO YENU KAMA WALIVYO KUWA WAKIONYESHA MAPAMBO YAO WANAWAKE WA ZAMA ZA UJAHILI. NA SIMAMISHENI SWALA NA TOENI ZAKAH NA MTIINI ALLAH NA MTUME WAKE. ALLAH ANATAKA KUKUONDOLEENI UCHAFU, ENYI WATU WA NYUMBA (ya Mtume) NA (anataka) KUKUTAKASENI KABISA KABISA. NA WATAJIENI (watu) YASOMWAYO MAJUMBANI MWENU KATIKA AYA ZA ALLAH NA (maneno ya) HIKIMA (ya Mtume). KWA HAKIKA ALLAH NI MJUZI WA MAMBO YA SIRI NA MJUZI WA MAMBO YA DHAHIRI”. [33:30-34]

Hivi baada ya kauli hii kali ya Allah, bado Bibi huyu mtukufu hakuwa na khofu ya kushukiwa na adhabu ya Allah kwa kutenda tendo chafu hilo?!

Hivi ni kweli kuwa hakuchelea kuipomosha daraja na cheo hiki kitukufu alichopewa na kukirimiwa na Allah, hata akajasiri kutenda uvundo huo?! Hivi tunaweza kuamini kuwa hakuogopa kuichafua twahara ya nyumba hii ambamo wahyi unashuka humo na kufunikwa na malaika?!

Ukweli unaoweza kusemwa juu ya hili ni kwamba huo ulikuwa ni uzushi duni na ni uongo usiokubaliwa na akili, dini wala busara ya kawaida tu. Wala haukubaliwi na mantiki ya kimazingira bali hata hali za jamii zijapotolewa dalili alfu juu yake.

 

II.  QUR-ANI TUKUFU YAUBOMOA UZUSHI HUU NA KUUFANYA KUWA NI MUHIMILI KATIKA KUWEKA SHERIA YA KULINDA HESHIMA/HADHI YA MTU.

Kwa ajili hii Qur-ani Tukufu haikutosheka tu na kuukadhibisha uzushi huo na kumkanushia tuhuma hizi nzito Bibi Aysha.

Bali uliyapatia dawa mazingira yake kwa pande zake zote; tiba ya hikima pevu ambayo italinda na kuhifadhi heshima za watu. Na kuzikatia njia ya kuongopa ndimi chafu zenye tabia hiyo chafu na kuilinda heshima na utukufu wa jamii ya Kiislamu.

Aya za Surat Nuur zimeanza kwa kuweka adhabu kemezi kwa jarima ya zinaa na kuamuru kuitekeleza kwa wazinifu bila ya huruma.

Na kwamba adhabu hiyo itekelezwe mbele ya hadhara ili iwe ni maonyo kwao kwa sababu hiyo ni jarima iichafuayo jamii.

Na ni jarima yenye athari yenye kuendelea katika kuifisidi jamii na kuvunja heshima na hadhi yake. Hawajasiri kuitenda jarima hii ila wale ambao zimekhabithika nafsi zao na waliofilisika kiitikadi. Ama waumini, hawa kwa mujibu wa imani yao na ucha-Mungu wao ni watu walio mbali mno na jarima hii chafu:

“MZINIFU MWANAMKE NA MZINIFU MWANAMUME, MPIGENI KILA MMOJA KATIKA WAO MIJELEDI (bakora) MIA. WALA ISIWASHIKENI KWA AJILI YAO HURUMA KATIKA (kupitisha) HUKUMU HII YA ALLAH IKIWA NYINYI MNAMUAMINI ALLAH NA SIKU YA MWISHO. NA LISHUHUDIE ADHABU YAO (hii) KUNDI LA WAUMINI. MWANAMUME MZINIFU HAFUNGAMANI ILA NA MWANAMKE MZINIFU AU MWANAMKE MSHIRIKINA, NA MWANAMKE MZINIFU HAFUNGAMANI NAYE ILA MWANAMUME MZINIFU AU MSHRIKINA. NA HAYO YAMEHARIMISHWA KWA WAUMINI”. [24:2-3]

Kisha aya zikaendelea kuilinda jamii ya Kiislamu dhidi ya shari za watu hao mafasiki ambao husema katika heshima/hadhi za watu bila ya kuwa na ujuzi wa wayasemayo.

Na wavunjao heshima za majumba ya watu wasio na hatia, aya zikawalazimisha kusimamisha na kutoa ushahidi wa kutinda juu ya tuhuma zao hizo.

Walete hoja zisizokubali shaka kuthibitisha ukweli wa madai yao wanayo wazushia watu. Na wakishindwa kuleta ushahidi huo, basi wanastahiki kupata adhabu kemezi na kuvunjiwa heshima yao mpaka waache kuchezea heshima na hadhi za watu.

Hata wanandoa wenyewe pia sheria inawalazimisha kuleta ushahidi pale watakapo watuhumu wenziwao na uchafu huu muovu (zinaa). Wakishindwa kufanya hivyo, basi ni wajibu wao kuyakazia madai yao hayo kwa kuleta viapo vizito, washuhudie ndani yake kwamba wao ni wakweli katika madai yao hayo na wala hawasemi uongo:

“NA WALE WANAO WASINGIZIA WANAWAKE WATOHARIFU (kuwa wamezini), KISHA HAWALETI MASHAHIDI WANE, BASI WAPIGENI MIJELEDI (bakora) THAMANINI NA MSIWAKUBALIE USHAHIDI WAO TENA, NA HAO NDIO MAFASIKI. ISIPOKUWA WALE WENYE KUTUBU BAADA YA HAYO NA WAKATENGENEZA AMALI NZURI (hao Allah atawasamehe kwani) BILA SHAKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU. NA WALE WANAOWASINGIZIA WAKE ZAO (kuwa wamezini) NA HAWANA MASHAHIDI ILA NAFSI ZAO, BASI USHAHIDI WA MMOJA WAO UTAKUWA NI KUSHUHUDILIA MARA NNE KWA KIAPO CHA ALLAH: YA KWAMBA BILA SHAKA YEYE NI MMOJA WA WANAOSEMA KWELI. NA MARA YA TANO (aape) KWAMBA LAANA YA ALLAH IWE JUU YAKE IKIWA NI MIONGONI MWA WAONGO. NA (mke) ITAMUONDOKEA ADHABU KWA KUTOA SHAHADA MARA NNE KWA KIAPO CHA ALLAH: YA KWAMBA (huyu mume) NI MIONGONI MWA WAONGO. NA MARA YA TANO (aape) YA KWAMBA HASIRA YA ALLAH IWE JUU YAKE KAMA (mumewe) YU MIONGONI MWA WANAOSEMA KWELI (na yeye mke ndiye muongo)”. [24:4-9]

Baada ya hapo ndipo aya zilipoanza kulizungumzia tukio hili la uzushi, zikalielezea kwamba ni uzushi wa kundi ongo lililokusudia kwa uzushi huo  kueneza shari kwa waislamu. Na Allah akataka kheri kwao kwa tukio hilo na kwamba hapana budi Allah atawaadhibu waongo hawa kwa madhambi yao hayo:

“HAKIKA WALE WALIOLETA UWONGO HUO (wa kumsingizia Bibi Aysha-mkewe Mtume-kuwa amezini) NI KUNDI MIONGONI MWENU (ni jamaa zenu). MSIFIKIRI NI SHARI KWENU, BALI HAYO NI KHERI KWENU. KILA MTU KATIKA WAO ATAPATA ALIYOYACHUMA KATIKA MADHAMBI HAYO. NA YULE ALIYEJITWIKA SEHEMU YAKE KUBWA MIONGONI MWAO, ATAPATA ADHABU KUBWA (zaidi)”. [24:11]

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *