RISALA YA NABII MUHAMMAD ILIKUWA NI KWA WATU WOTE LAKINI MAKURAYSHI WALIWEKA KIZUIZI (PINGAMIZI)
Hapana shaka kwamba dhima kuu ya Mtume- Rehema na Amani zimshukie – ilikuwa ni kufikisha ujumbe wa Mola wake kwa watu.
Hili ndilo lililokuwa jukumu la kila Mtume aliyepelekwa na Allah kwa kaumu yake. Jukumu na dhima hii ya Mitume inabainishwa kupitia kauli hii ya Allah :
“(Hao ni) MITUME WALIOTOA KHABARI NZURI (kwa watu wema), WAKAWAONYA (wabaya), ILI WATU WASIWE NA HOJA JUU YA ALLAH BAADA YA (kuletwa hawa) MITUME … [4:165].
Allah analibainisha jukumu la Nabii Muhammad, anamwambia kupitia kauli yake hii :
“EWE MTUME! FIKISHA ULIYOTEREMSHIWA KUTOKA KWA MOLA WAKO, NA KAMA HUTAFANYA, BASI HUKUFIKISHA UJUMBE WAKE …” [5:67]. “HAKUNA JUU YA MTUME ILA KUFIKISHA TU …” [5:99]
Allah kwa kutambua uzito na ugumu wa jukumu hili analomtwisha mitume wake, jukumu ambalo litamjengea uadui na chuki kwa watu.
Uadui na chuki unaotokana na kuwataka watu wabadilike na kuuacha mfumo batili wa maisha waliojichaguliwa wao wenyewe na badala yake waufuate mfumo sahihi aliowachagulia Mola Muumba wao.
Allah anaahidi kumpa ulinzi mtume wake ili awe katika mazingira mazuri ya kuitekeleza kazi na jukumu lake hili, anamwambia :
“…NA ALLAH ATAKULINDA NA WATU. HAKIKA ALLAH ATAKULINDA HAWAONGOZI WATU WANAOKUFURU” [5:67].
Itatubainikia bayana kupitia kauli hiyo tukufu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyomo ndani ya Kitabu chake kitukufu kwamba jukumu la Mtume ni kufikisha ujumbe na sio kuwalazimisha watu kuamini ujumbe huo. Aya ifuatayo inaudhihirisha ukweli huu :
“HAKUNA KULAZIMISHWA (mtu kuingia) KATIKA DINI. UONGOFU UMEKWISHAPAMBANUKA NA UPOTOFU. BASI ANAYEMKATAA SHETANI NA AKAMUAMINI ALLAH, BILA SHAKA YEYE AMESHIKA KISHIKO CHENYE NGUVU, KISICHOKUWA NA KUVUNJIKA …” [2:256].
Ni hakika isiyo kificho kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alimtuma na Kumpeleka Mtume wake Muhammad – Rehema na Amani zimshukie – kwa watu wote.
Kwa mantiki hii ilikuwa ni wajibu wake kuhakikisha kuwa anaufikisha ujumbe wa Mola wake kwa watu wote, ijapokuwa mahala pa kuanzia (kitovu) ilikuwa ni kwa jamaa zake; makurayshi wenziwe
Ilikuwa ni jukumu lake kuufikisha ujumbe huo kwa jamaa zake na hatimaye kuueneza kwa mataifa yote kwa nguvu zake zote.
Bwana Mtume alikuwa akiukumbuka ukweli huu na kuutaja katika hadithi zake mbali mbali :
“Nimetumilizwa kwa watu (wote); wekundu na weusi …”. Akasema tena :
“Nimeletwa kwa watu wote, na (kwa kuletwa) kwangu wamehitimishwa mitume (hakuna tena Mtume baada yangu)” Akazidi kuthibitisha ukweli huu kwa kusema :
“Mimi ni Mtume wa niliyemdiriki nikiwa hai na (ni Mtume) wa atakayezaliwa baada yangu”.
Pia alikuwa akiueleza ukweli kupitia ulimi wa wahyi (ufunuo), akisema :
… NA QUR-ANI HII IMEFUNULIWA KWANGU ILI KWA HIYO NIKUONYENI NYINYI NA KILA IMFIKIAYO …”[6:19].
Qur-ani Tukufu na vitabu sahihi vya hadithi vimesheheni kauli zinazouthibitisha na kuukiri ukweli huu.
Tarekh (historia) ya Uislamu inatuambia kwamba Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – alikitumia kipindi kisichopungua miaka kumi na tatu (13) katika mji wa Makkah.
Kipindi chote hiki alikuwa akiifanya kazi moja tu, kazi ya kuufikisha ujumbe wa Allah kwa waja wake.
Aliifanya kazi hii kwa kuufuata utaratibu na muongozo wa Mola wake uliomtaka awalinganie watu kwa kutumia hekima na mawaidha mema :
“NA WAITE (watu) KATIKA NJIA YA MOLA WAKO KWA HIKIMA NA MAUIDHA MEMA NA UJADILIANE NAO KWA NAMNA ILIYO BORA (siyo kwa kuwatukana wao au kutukana dini yao) …” [16:125].
Hii ndio sera sahihi ya da’wah (propagation) katika Uislamu.
Pamoja na juhudi za makusudi alizozichukua Mtume katika kuufikisha ujumbe wa Allah kwa watu wa Makkah katika kipindi hiki kirefu ni idadi ndogo tu ya watu hawa iliyomuamini Mtume na kumfuata.
Idadi hiyo ilikuwa ni ndogo mno kwa kuzingatia jumla ya wakazi jumla ya wakazi wa Makkah na muda mrefu uliotumika.
Hili lilitokana na lilichangiwa na pingamizi kubwa lililowekwa na Makurayshi dhidi ya Uislamu. Makurayshi walitumia kila lililokuwa katika uwezo wao ikiwa ni pamoja na mabavu na vitisho ili kuhakikisha kuwa watu hawauamini Uislamu.
Tukio la kutuma ujumbe wenye zawadi kwenda kumshawishi mfalme Najaashi wa Uhabeshi {Ethiopia} awarejeshe Makkah waislamu waliokimbilia nchini mwake ni ushahidi tosha juu ya juhudi zao hizi ovu.
Ni uadilifu na busara ya Mfalme huyu ndio vilivyowaokoa waumini hawa na udhalimu na ukatili wa makurayshi.
Mwenyezi Mungu Mtukufu alipomuongozea Mtume wake watu wa Yathrib (Madinah), wakamuamini na kuwapa ahadi ya utii na kumnusuru mpaka aweze kufikisha ujumbe wa Mola wake kwa watu.
Ahadi hii ya utii na nusura iliyopambwa na imani isiyotetereka ilikuwa ni pigo kubwa lililoleta kizaizai kikubwa miongoni mwa Makurayshi.
Hofu hii ya Makurayshi ilitokana na ukweli kwamba Uislamu sasa utashika kasi na kuenea kwa kuwa tayari utakuwa umepata kituo ambacho wao watakuwa hawana udhibiti nacho kama ilivokuwa Makkah.
Makurayshi ili kukabiliana na kitisho walifanya juhudi za makusudi ili kuwashawishi watu wa Madina (Answaar) kuvunja na kutengua ahadi yao waliyoiweka kwa Mtume. Juhudi zao hizi zilipogonga mwamba ndipo walipobuni mbinu mpya.
Wakapanga mikakati madhubuti ya kuwazuia waislamu kuhamia Madinah kwenda kujiunga na ndugu zao wa Imani huko.
Kwani walitambua kwamba kuhama kwa waislamu kutoka Makkah kwenda Madinah, hakutamaanisha kingine zaidi ya kurudufika nguvu ya waislamu chini ya Mtume.
Jambo hili litaifanya kazi ya kupambana na waislamu kuwa ngumu na pengine kushindwa kabisa.
Hivyo wakaona njia pekee iliyo mikononi mwao ni kuwazuia hawa waislamu wa Makkah pamoja na Mtume kuhamia Madinah.
Kwa kiasi fulani njia hii ilifanikiwa kwa mda, kwani waliofanikiwa kuhama ni wale wenye nguvu tu, tena kwa kuondoka kwa uficho mkubwa chini ya pazia la kiza totoro cha usiku.
Ama wengi miongoni mwa wanaume wanyonge, wanawake na watoto waliendelea kuwa kifungoni Makkah, tena chini ya mateso makubwa.
Yote haya hayakutosha kuiondosha chuki ya Makurayshi dhidi ya Uislamu, wakaanza kupanga njama za kuukata mzizi wa fitina kama walivyouona kwa kumuua Bwana Mtume.
Ni ya nini mateso haya ?! Ni wa nini uadui huu ?!
Kwa nini makurayshi waliyafanya yote haya ?! Makurayshi waliufanya ukatili huu usiojali utu chini ya mwamvuli wa kile walichokiita
“kutetea na kulinda itikadi (dini) yao”.
Sasa je, ni kweli kuwa vita na dhuluma hii ililenga kuhifadhi dini yao kama walivodai ?
Madai yao haya kama yangelikuwa yana chembe ya ukweli ndani yake, basi Makurayshi wangelimpinga na kumzuia kila aliyejitoa katika dini yao au kuikhalifu.
Kwani historia inatuthibitishia kwamba Nabii Muhammad hakuwa ndiye mtu wa mwanzo kupingana na mfumo wa maisha wa Makurayshi.
Historia imewataja watu kama Zayd ibn Amri ibn Nufayl, Waraqah ibn Naufal, Abdullah ibn Jahshi, Uthmaan Bil-Huwayrith na Qussa ibn Saaidah kwa walijitoa katika kuufuata mfumo wa maisha (dini) wa kikurayshi na wakaamua kufuata mifumo mingine waliyoamini kuwa ni sahihi.
Kwa mfano huyu Bwana Zayd ibn Amri, yeye alikuwa akisimama pembezoni mwa Al-Kaabah ambapo mamwinyi wa Kikurayshi hubarizi, akawa anapaza sauti kuikosoa dini ya Makurayshi na kuwataka waifuate dini ya Nabii Ibrahim.
Qussa ibn Saaidah, huyu alikuwa akiitangaza wazi itikadi yake masokoni penye mkusanyiko wa watu wengi.
Si hayo tu, bali Makurayshi wengi walikuwa hawakushikamana ipasavyo na dini yao na wala hawakuitizama miungu yao kwa jicho la utakasifu na utukufu.
Kwa hivyo ni dhahiri kuwa Makurayshi hawakupupia kuilinda na kuitetea dini yao.
Kama hivi ndivyo, ni kwa nini basi Makurayshi walitumia mali, wakati na juhudi za makusudi kumpinga Mtume na kumzuia asihubiri Uislamu ?
Kwa nini Makurayshi hawakumuacha Mtume atoke Makkah na kwenda akutakako kuhubiri Uislamu kama walivyofanya waliomtangulia ?
Yote haya yalikuwa kwa sababu Makurayshi waliiona risala (daiwah) ya Nabii Muhammad – Rehema na Amani zimshukie – ni hatari dhahiri kwa maslahi na utawala wao, ambao ndio ulikuwa chemchem ya utukufu na utajiri wao.
Kwa mantiki hii kusimama na kuenea kwa Uislamu hakutamaanisha kingine zaidi ya kuanguka kwa maslahi yao ikawa ni lazima waupige vita Uislamu kwa gharama yeyote ile hata ikibidi kutoa maisha ya watu wasio na hatia.
Hii ndio sababu ya kweli ya upinzani na mapambano ya Makurayshi dhidi ya Mtume na Uislamu. Lakini Je, waliweza ?!