KITHIRISHA NA KULETA ISTIGHFAARI

Ndugu yangu mpenzi katika imani-Allah akuongoze-karibu tena katika jukwaa lako hili la wasia maridhawa kwa kila muislamu.

Ninakuusia bila ya kusahau kuiusia nafsi yangu kuleta istighfaari.

Elewa na ufahamu kwamba, katika jumla ya mambo muhimu yaliyokokotezwa kwa kila muislamu ni kukithirisha kuleta istighfaari.

Istighfaari ni agizo na amri ya Allah Mola Mkamilifu kwa waja wake viumbe dhaifu wakosaji. Hii ndio amri ya istighfaari ndani ya Qur-ani Tukufu, haya na tuamrike:

“…NA OMBENI MAGHFIRA (msamaha) KWA ALLAH; HAKIKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU”. [73:20]

Allah Mola Mwenyezi akamwambia Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie:

“…NA OMBA MAGHUFIRA KWA DHAMBI ZAKO NA (dhambi) ZA WAUMINI WANAUME NA WAUMINI WANAWAKE…” [47:19]

Allah Mola atoaye msamaha pindi mja anapokiri udhaifu wake na kurejea kwake, anasema katika kutaja wasifu wa waja wake wema wenye kuswali:

“NA WAKIOMBA MAGHUFIRA NYAKATI ZA KABLA YA ALFAJIRI”. [51:18] Nae Mfasiri Mkuu wa Qur-ani kwa kauli na amali (vitendo)-Rehama na Amani zimshukie-anasema kuhusiana na suala zima la istighfari. Haya na tumtegee sikio la usikivu wa kutii na kufuata:

 “Ye yote atakayelazimikiana na istighfari, Allah atampa faraja kwa kila huzuni. Na (atampa) njia ya kutokea katika kila dhiki na atamruzuku kwa namna asiyoitazamia”. Abuu Daawoud, Nasaai, Ibn Maajah &  Al-Haakim-Allah awarehemu.

Bwana Mtume anazidi kutuasa katika uwanja huu wa istighfaari, nasi tusichoke kumsikiliza kwa faida na maslahi yetu wenyewe:

“Furaha iliyoje kwa yule atakayekuta katika daftari lake la amali istighfaari nyingi”. Ibn Maajah, Twabaraaniy & Al-Baihaqiy-Allah awarehemu.

Ewe ndugu yangu-Allah atuwafikishe na istighfaari-ikutoshe katika kujua fadhila, manufaa na faida za istighfaari, kauli hii ya Allah Mtukufu:

“…WALA ALLAH HAKUWA WA KUWAADHIBU HALI YA KUWA WANAOMBA MSAMAHA (Istighfaari)”. [8:33]

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anatuambia:

“Kwa yakini shetani alisema: Naapa kwa utukufu wako, ewe Mola wangu! Nitaendelea kuwapoteza waja wako maadam roho zao zimo viwiliwilini mwao (wako hai). Mwenyezi Mungu akamwambia: Nami naapa kwa enzi na utukufu wangu sitaacha kuwaghufiria (madhambi yao) maadam wananiomba maghufira”. Ahmad & Al-Haakim-Allah awarehemu.

Ndugu yangu hebu na tuipe nafasi Qur-ani Tukufu iliyo muongozo na katiba yetu. Itusimulie juu ya ahadi hii aliyoichukua Iblisi baada ya kufukuzwa peponi na kubaidishwa (kutengwa) na rehema za Allah Mwingi wa rehema:

“AKASEMA: MOLA WANGU! KWA SABABU UMENIHUKUMU KUPOTEA, BASI NITAWAPAMBIA (viumbe wako upotofu) KATIKA ARDHI NA NITAWAPOTEZA WOTE. ISIPOKUWA WALE WAJA WAKO WALIOSAFIKA KWELI KWELI. (Allah) AKASEMA: HII NJIA YAO YA (kuja) KWANGU IMENYOOKA (wanaweza kunijia wakati watakao). HAKIKA WAJA WANGU, WEWE HUTAKUWA NA MAMLAKA JUU YAO, ISIPOKUWA WALE WENYE KUKUFUATA (kwa khiari zao) KATIKA HAO WAPOTOFU. NA BILA SHAKA JAHANAMU NDIPO MAHALA PAO WALIPOAHIDIWA WOTE”. [15:39-43]

Ewe ndugu yangu hiyo ndio ahadi iliyochukuliwa na adui yetu mkuu Iblisi mlaaniwa mbele ya Allah Mola wake na Mola wetu.

Hatutasalimika na shari ya muovu huyu ila kwa kujifunika mwavuli wa waja wa Allah waliosafika kweli kweli.

Kwani hawa Iblisi anakiri udhaifu wake mbele yao kwamba hana hila wala ujanja wa kuwapoteza.

Hao ndio waja wa Allah ambao Iblisi hana mamlaka juu yao.

Najua bila ya shaka kwamba sasa utakuwa unajiuliza ni kina nani hao waja wa Allah ambao Iblisi hana ubavu juu yao? Naam, usipate taabu Qur-ani Tukufu ilijua utauliza swali hilo, kwa hivyo ikakutayarishia jawabu tosha, haya na tuisikilize:

 NA WAJA WA RAHMAAN (Allah Mola Mwenye rehema, anaowapenda ni wenye sifa hizi):-

v     NI WALE WANAOKWENDA (na kurejea) ULIMWENGUNI KWA UNYENYEKEVU, NA WAJINGA WAKISEMA NAO (maneno mabaya) HUWAJIBU (maneno ya) SALAMA.

v     NA WALE WANAOPITISHA BAADHI YA SAA ZA USIKU KWA AJILI YA MOLA WAO KWA KUSUJUDU NA KUSIMAMA.

v     NA WALE WANAOSEMA: MOLA WETU! TUONDOLEE ADHABU YA JAHANAMU, BILA SHAKA ADHABU YAKE NI YENYE KUENDELEA. HAKIKA HIYO (Jahanamu) NI KITUO KIBAYA NA MAHALI (pabaya kabisa) PA KUKAA.

v     NA WALE AMBAO WANAPOTUMIA HAWATUMII KWA FUJO WALA HAWAFANYI UBAKHILI, BALI WANAKUWA KATIKATI BAINA YA HAYO.

v     NA WALE WASIOMUOMBA MUNGU MWINGINE PAMOJA NA ALLAH, WALA HAWAUI NAFSI ALIYOIHARIMISHA ALLAH ISIPOKUWA KWA HAKI. WALA HAWAZINI, NA ATAKAYEFANYA HAYO ATAPATA MADHARA (papa hapa ulimwenguni kabla ya Akhera).

v     NA WALE AMBAO HAWASHUHUDII SHAHADA ZA UWONGO, NA WANAPOPITA PENYE UPUUZI, HUPITA KWA HISHIMA (yao).

v     NA WALE AMBAO WANAPOKUMBUSHWA AYA ZA MOLA WAO HAWAZIANGUKII KWA UZIWI NA UPOFU,

v     NA WALE WANAOSEMA: MOLA WETU! TUPE KATIKA WAKE ZETU NA WATOTO WETU YABURUDISHAYO MACHO (yetu, nyoyo zetu) NA UTUJAALIE KUWA WAONGOZI KWA WAMCHAO (Allah)”. [25:63-68 & 73-74]

Haya mpenzi ndugu yangu-Allah akuhidi-tayari Qur-ani imetimiza jukumu lake kwako, tayari imekutajia sifa za waja wa Allah ambao Iblisi hajasiri kuwakaribia.

Sasa ni zamu yako, jipinde ujivishe sifa hizo ili uwe na kinga dhidi ya kirusi hatari Iblisi.

Naam, tulikuwa tukielezea fadhila, manufaa na faida za istighfaari, haya na tuendelee. Kauli hii ya Allah akitupa khabari za Mtume wake Nuhu-Amani imshukie-inayaeleza bayana hayo (fadhila, manufaa na faida za istighfaari), tuisikilize:

“NIKAWAAMBIA: OMBENI MAGHUFIRA KWA MOLA WENU. HAKIKA YEYE NI MWINGI WA MAGHUFIRA (msamaha). ATAKULETEENI MAWINGU YANYESHAYO MVUA NYINGI. NA ATAKUPENI MALI NA WATOTO, NA ATAKUPENI MABUSTANI NA ATAKUFANYIENI MITO”. [71:10-12]

Ewe ndugu yangu-Allah akurehemu-elewa na ufahamu kwamba toba na istighfaari ni katika jumla ya khazina za kheri.

Na ni miongoni mwa milango ya Quruba (sababu za kuwasogeza waja kwa Allah) na baraka na ni asili ya njia zote za kufikilia kheri za dunia na akhera.

Basi ni wajibu wetu kulazimikiana na toba na istighfaari nyakati za mchana na usiku.

Allah atuwafikishe kukithirisha kumtaka maghufira kwa madhambi tuyafanyayo usiku na mchana, kwa siri na kwa dhahiri, kwa makusudi na kwa bahati mbaya-Aaamiyn!

KITHIRISHA NA KULETA ISTIGHFAARI

Ndugu yangu mpenzi katika imani-Allah akuongoze-karibu tena katika jukwaa lako hili la wasia maridhawa kwa kila muislamu.

Ninakuusia bila ya kusahau kuiusia nafsi yangu kuleta istighfaari.

Elewa na ufahamu kwamba, katika jumla ya mambo muhimu yaliyokokotezwa kwa kila muislamu ni kukithirisha kuleta istighfaari.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *