Lengo na madhumuni ya nasaha hizi ni kujaribu kukumbusha utukufu, ubora na fadhila za mwezi huu mtukufu ambao ni msimu wa kheri nyingi.
Ni kutokana tu na kuujua mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa namna gani, ndio tunaweza kuupa hadhi na haki yake inayostahili.
Kuutukuza na kuupa mwezi huu haki yake kwa kujituma kwa makusudi na bidii zetu zote bila kuchoka kuyatenda yale yote tunayotakiwa kuyafanya ndani yake miongoni mwa mambo ya kheri na twaa.
Na athari ya mambo hayo kuonekana katika miezi kumi na moja ifuatayo baada ya Ramadhani kuonyesha shukrani zetu kwa Mola Muumba wetu kwa neema hii ya mwezi wa Ramadhani. Isitoshe ni ishara na dalili ya wazi ya kunadi sada (kutanakiwa).
Walengwa wa hadia hii ya Nasaha za Ramadhani ni wale watu wema waliojihakikishia mafanikio ya duniani na kahera kwa kutekeleza kwao maamrisho na makatazo ya Mola wao.
Wale watu ambao wamejipamba na sifa zote za utu na kuwa kigezo kwa kila mpenda haki. Wale walioandaliwa na Mola wao samahani (maghfirah) na ujira adhimu. Wale wanaotajwa na kauli hii ya Allah,
“BILA SHAKA WANAUME WENYE KUFUATA VIZURI NGUZO ZA UISLAMU, NA WANAWAKE WANAOZIFUATA VIZURI NGUZO ZA UISLAMU, NA WANAUME WANAOAMINI VIZURI NGUZO ZA IMANI, NA WANAWAKE WANAOAMINI VIZURI NGUZO ZA IMANI, NA WANAUME WASEMAO KWELI, NA WANAWAKE WASEMAO KWELI, NA WANAUME WANAOSUBIRI, NA WANAWAKE WANAOSUBIRI, NA WANAUME WANAONYENYEKEA NA WANAWAKE WANAONYENYEKEA, NA WANAUME WANAOTOA (zaka na) SADAKA, NA WANAWAKE WANAOTOA (zaka na) SADAKA, NA WANAUME WANAOFUNGA NA WANAWAKE WANAOFUNGA, NA WANAUME WANAOJIHIFADHI TUPU ZAO NA WANAWAKE WANAOJIHIFADHI, NA WANAUME WANAOMTAJA ALLAH KWA WINGI NA WANAWAKE WANAOMTAJA ALLAH (kwa wingi), ALLAH AMEWAANDALIA MSAMAHA NA UJIRA MKUBWA” (33: 35).
Tunarajia kwa fadhila zake Allah kuwa wewe msomaji wetu ni miongoni mwa watu hawa na kwa hivyo, utanufaika na kufaidika na nasaha hizi za Ramadhani.
Tunakutakia Ramadhani njema iliyosheheni rehma, maghfirah, radhi za Allah, taq-wa na kuachwa huru na moto.
“MOLA WETU! USIZIPOTOE NYOYO ZETU BAADA YA KUTUONGOZA, NA UTUPE REHEMA ITOKAYO KWAKO, HAKIKA WEWE NDIO MPAJI MKUU” (3:8).
SWAUMU (FUNGA) KATIKA UISLAMU
TUJIULIZE: KWA NINI TUNAFUNGA?
Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuumba mwanadamu katika sehemu kuu mbili, mwili (kiwiliwili) na roho. Akaziunganisha pamoja roho na mwili pamoja na tofauti ya maumbile na tabia zao na kuwa mwanadamu kamili. Akamweka kiumbe huyu mwanadamu katika daraja ya kati, baina ya wanyama na malaika. Juu yake kuna malaika watakasifu watoharifu ambao
“…..HAWAMUASI ALLAH KWA AMRI ZAKE, NA WANATENDA WANAYOAMRISHWA (yote)” (66:6).
Na chini yake kuna wanyama ambao hawakupewa akili wala amana, wao kuendeshwa na kusukumwa na matashi na matamanio yao.
Katikati ya makundi haya mawili ndio akamuweka mwanadamu aliyemkirimu kwa kumpa akili ambayo ndio neema pekee inayomtofautisha na hayawani wengine.
Akamletea na muongozo wa maisha na akampa uhuru na khiyari ya kuchagua – kuufuata muongozo huo au kutokuufuata,
“NA SEMA: HUU NI UKWELI ULIOTOKA KWA MOLA WENU, BASI ANAYETAKA NA AAMINI NA ANAYETAKA NA AKUFURU”…..(18:29).
Kisha akambainisha matokeo ya matumizi mazuri au mabaya ya uhuru na khiyari aliyompa
“……NA KAMA UKIKUFIKIENI MUONGOZO UTOKAO KWANGU, BASI WATAKOUFUATA MUONGOZO WANGU HUO HAITAKUWA KHOFU JUU YAO WALA HAWATAHUZUNIKA LAKINI WENYE KUKUFURU NA KUYAKADHIBISHA MANENO YANGU, HAO NDIYO WATAKAOKUWA WATU WA MOTONI, HUMO WATAKAA MILELE” (2: 38 – 39).
Sasa basi, mwanadamu atakapoitumia vema neema hii ya akili, muongozo na khiyari aliyopewa akayashinda matamanio yake maovu. Hupanda daraja mpaka kuwa juu ya malaika, mahala ambapo Mola wake alipomuweka:
“NA (wakumbushe watu khabari hii): TULIPOWAAMBIA MALAIKA MSUJUDIENI ADAM (yaani muadhimisheni kwa ile elimu yake aliyopewa) WAKAMSUJUDIA WOTE ISIPOKUWA IBILISI, AKAKATAA NA AKAJIVUNA……..” (2:34).
Hii ndio nafasi ya mwanadamu atakapoushinda unyama ambao ni sehemu ya maumbile yake, huwa mtukufu na karibu zaidi na Mola wake kuliko hata malaika.
Ama akiuachia unyama umshinde na kutawaliwa na matamanio maovu, huporomoka daraja na kuwa chini kabisa ya wanyama:
‘JE UMEMUONA YULE ALIYEFANYA MATAMANIO YAKE (kile anachokipenda) KUWA MUNGU WAKE? BASI JE ,UTAWEZA KUWA MLINZI WAKE (ukamuhifadhi nahayo, na hali ya kuwa hataki?) AU JE, UNAFIKIRI YA KWAMBA WENGI KATIKA WAO WANASIKIA AU WANAFAHAMU? HAWAKUWA WAO ILA NI KAMA WANYAMA, BALI WAO WAMEPOTEA ZAIDI NJIA” (25: 43-44)
Mwenyezi Mungu Mtukufu amemzawadia mwanadamu huyu mfumo sahihi wa maisha (Uislamu) uliogusa nyanja zake zote za maisha.
Akamuwajibishia ndani ya mfumo huo ibada za aina mbalimbali ambazo lengo jumla lake ni kuleta manufaa na kuondosha madhara. Ibada hizi kama atazitekeleza kama ipasavyo zitampa kinga kubwa dhidi ya unyama na matamanio maovu.
Amemfaradhishia swala mathalan ili imkinge na mambo maovu na machafu na kumuweka katika mazingira ya kumtii Mola wake kwa kuamrika katika maamrisho na kukatazika katika makatazo:
“SOMA ULIYOLETEWA WAHYI (uliyofunuliwa) KATIKA KITABU (hiki ulicholetewa) NA USIMAMISHE SWALA BILA SHAKA SWALA (ikiswaliwa vilivyo) HUMZUILIYA (huyu mwenye kuswali na) MAMBO MACHAFU NA MAOVU, NA KWA YAKINI KUMBUKO LA ALLAH (la kumzuilia mtu na mabaya). NA ALLAH ANAJUA MNAYOYATENDA”. (29:45)
Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kumtambua vema mwanadamu na udhaifu wa maumbile yake kutokana na kumuumba mwenyewe.
Ili asishindwe na unyama unaotokana na umbile lake na asiangushwe mweleka na matamanio maovu, akampa msaada.
Akamtayarishia ibada ya funga mwezi mmoja kila mwaka ili imtoe katika unyama na kumpeleka katika utu. Imtoe katika ulimwengu wa vitu na kumpeleka katika ulimwengu wa roho ambapo atayashinda matamanio maovu.
Imuonyeshe udhaifu wake mbele ya Mola Muumba wake na haja yake kwa Mola wake. Imuondoshee moyo wa ubinafsi na imjengee moyo wa huruma na upendo kwa kuhisi tabu ya njaa na kiu. Ikivunjilie mbali kiburi chake na kumvika taji la unyenyekevu.
Kauli jumla, muislamu ameamrishwa kufunga ili swaumu (funga) iwe ni chuo cha malezi ya nafsi. Ndani ya chuo hiki nafsi ya mja inajengewa mazingira ya kustahimili wakati wa shida (kukosa).
Nafsi inapewa chanjo/ kinga dhidi ya maasi na matamanio. Chuko hiki humtunukia mja shahada ya umiliki wa nafsi na utawala wa unyama na matamanio maovu. Utu na ukamilifu wa mwanadamu unatokana na uwezo wake katika kuimiliki na kuitawala nafsi yake ambayo:
“….KWA HAKIKA (kila) NAFSI NI YENYE KUAMRISHA SANA MAOVU ISIPOKUWA ILE AMBAYO MOLA WANGU AMEIREHEMU……..” (12:53).
Uwezo huu wa kuimiliki nafsi na kuikalia juu ndio unaompatia mja daraja na nafasi njema mbele ya jamii bali hata mbele ya Mola wake.
“NA AMA YULE ALIYEOGOPA KUSIMAMISHWA MBELE YA MOLA WAKE, AKAIKATAZA NAFSI YAKE NA MATAMANIO (maovu). BASI (huyo) PEPO NDIYO ITAKAYOKUWA MAKAZIYAKE”. (79: 40-41)
“BILA SHAKA AMEFAULU ALIYEITAKASA (nafsi yake). NA BILA SHAKA AMEJIHASIRI ALIYEIVIZA (nafsi yake)” (91: 8-9).