UMUHIMU WA SWALA NA NAFASI YAKE KATIKA UISLAMU

A: HUKUMU YA SWALA KWA MUJIBU WA QUR-ANI NA SUNNAH

Ewe ndugu yangu mpenzi; hebu kwa msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu tuzianze nasaha zetu kwa kumuomba Mola wetu Mtukufu atuwafikshe na kutuongoza katika kuijua haki, kuikubali na ksha kuifuata-Aamiyn Baada ya dua hiyo, hebu sasa tutazame kwa pamoja natujiulize nini hukumu ya ibada ya swala ndipo tutafahamu ni ipi nafasi na hukumu ya mtu asiye swali .

Ndugu yangu mpenzi, elewa na ufahamu kwamba swali katika sheria ni FARDH yaani WAJIBU.

Haya ni kwa mujibu wa aya chungu mzima za Qur-ani Tukufu. Hebu tusitafakari kwa pamoja aya hizi zifuatazo

“…BASI SIMAMISHENI SWALA, KWANI HAKIKA SWALA. IMEKUWA KWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA WAKATI MAALUM” [4:103]

Ukizingatia aya hii utakuta inaeleza kwa ufumbulizo na uwazi kabisa kwamba swali ni FARDHI, tenasi fardhi tu bali ni fardhi iliyowekewa wakati maalum na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake waumini kauli ya Mola karim Aliposema:

“… HAKIKA SWALAKWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA WAKATI MAALUM “ ni ishara na dalili bayana kwamba swala ndio kielelezo kikubwa cha Imani ya mja. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa hana Imani, mtu asiyeswali.

Ikiwa mtu hana Imani , vipi unamtazamia kuwa na dini? Hii ndio maana Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie akasema:

Mkimuona mtu aizoya Msikiti basi mshudieni kuwa yuna Imani kauli hii ya Bwana Mtume inazidi kutuonyesha ukweli usio pingika kwamba swala ndio nembo na kielelezo kikubwa cha Imani ya mja. Hebu tuitafakari na aya hii:-

“HIFADHINI (angalieni sana) SWALA (zote kuziswali) NA (khasa) ILE SWALA YA KATI NA KATI “[2:238]

Tukilizingatia neno la mwanzo lilotumika katika aya (HIFADHINI) tukaliweka katika sarufi ya kiarabu (Arabic Grammar), tutaambiwa na watu wa fani ya lugha kuwa neno hili ni tendo la amri.

Kwa hivyo basi neno hili (HIFADHINI) inbamaanisha kuwa suala la kuhifadhi swala ni amri itokayo kwa Mwenyezi Mungu kuja kwa waja wake na wala sio ombi.

Sasa kama tunakubaliana na ukweli huu ulio dhahiri kuwa swala ni amri ya Mola amuamrisha mja wake, je! Huoni kwamba kuacha swala ni kupinga na kuivunja amri ya Muumba wako?

Avunjaye na kupinga amri ya Bwana wake hufanywaje na Bwana wake, hasa ukizingatia kwamba siku zote amri hutoka kwa Mkubwa aliye kuja juu kwa mdogo aliye chini kama ambavyo ombi hutoka kwa aliye chini kuja kwa aliye juu.

Hebu jaribu kuwa mkweli, mwanao au mkeo akivunja amri yako, unakuwaje na unchukua hatua gani? Ukiukir ukweli huu ndipo utaiona nafasi yako mbele ya Mola wako wewe usiyetaka kumsujudia Mola wako.

Naam, tumetangulia kusema huko nyuma kwamba swala ni FARDHI /WAJIBU, hebu sasa tulitazame neno WAJIBU limeaanishwa vipi na sheria ili uione nafasi yako wewe usiyeswali.

Wataalamu wa fani ya fiq-hi wamelianisha neno wajibukwa kusema (WAJIBU/FARDHI ni lile jambo ambalo Allah ameliwajibisha juu yetu, hulipwa mtu aliye baleghe (mtu mzima),mwenye akili timamu kwa kulitenda/kulitekeleza (hilo la wajibu)na huaadhibiwa kwa kuwacha kulitenda, kama vile swala, funga na kuwatii wazazi).

Hili ndilo ainisho (definition) sahali la WAJIBU, hebu sasa lichukuwe aanisho hili uliambatishe na swala, unafahamu nini?

Ikiwa wewe ni mkweli, uliokulazimu kwa amri ya Mola Muumba wako na kwamba ukiswali utakuwa umeikubali na kuipokea kuitekeleza amri ya Mola wako kwa maslahi na faida ya nafsi yako, hivyo utalipwa thawabu ambaazo ndizo “Dollar” za kuinunulia akhera.

Kinyume chake ni kwamba kama hukuswali utakuwa umeipuzana na kuivunja amri ya Molawako kwa maangamivu na khasara ya nafsi yako mwenyewe, kwa hivyo utaaadhibiwa kwanza hapa hapa duniani, kaburini na kesho akhera kama lilivyothibiti hilo katika hadithi ya Mtume –Rehema na Amani zimshukie. Tusome kwa mazingatio:

“… NA BILA SHAKA ADHABU YA AKHERA NI KALI ZAIDI NA IENDELEAYO SANA”[20:127]

“ANAYEFANYA MEMA ANAJIFANYIA (mwenye) NAFSI YAKE, NA MWENYE KUTENDA UBAYA NI JUU (ya nafsi) YAKE NAMOLA WAKO SI DHALIMU KWA WAJA WAKE.”[41:46]

 

B: NAFASI YA SWALA KATIKA UIISLAM

Katka kuonyesha umuhimu na nafasi ya swala,Bwana Mtume- Rehema na Amani zimshukie –ameijaalia swala kuwa inashika nafasi ya pili katika nguzo tano za uislam

“uislamu umejengwa juu ya nguzo tano: kushuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa ila Allah na Muhammad ni Mtume wa Allah, kusimamisha swala, kutoazakah, kufunga ramadhani na kuhiji Makkah-Mukaram” Bukhaariy.

Ukiitafakari hadithi hii utaona ya kwamba Mtume –Rehema na Amani zimshukie –anaumathihsha uislamu na mfano wa jengo kubwa, imara na madhubuti lililojengwa juu ya nguzo tano.

Hapana hata mmoja awezaye kupinga kwamba kuna jengo linaloweza kusimama bila ya nguzo. Kama tunakiri ukweli huu, basi ni dhahiri kwamba hapana uislam pasipo na nguzo tano hizi na pasipo na nguzo na uislam pana kufru tu si vinginevyo.

Eeh Mola wetu tukinge na ukafiri kwa kutujulia kuisimamisha swala maisha yetu yote Aamiyn. Inakupasa uelewe ewe nduguyangu mpenzi muislam kwamba swala ndio nguzo tukufu kabisa ya dini na nafasi na umuhimu wa swala katika uislamu ni kama vile ilivyo nafasi na umuhimu wa kichwa katika kiwiliwili.

Basi kama ambavyo asivyokuwa na uhai mtu asiye na kichwandivyo ambavyo hana uislamumtu asiye na swala. Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie anatuasa kwa kutuambia :

“Ye yote atakuyeicha swala kwa makusudi, bila ya shaka amekufuru” Twabraaniy.

Haya hebu jiulize ewe Ndugu yangu Muislamu na uihurumie nafsi yako, mtu aliyekufuru ana Uislamu ?!

Fahamu ewe Ndugu yangu unayemuasi Mola wako kwa kuacha kuswali kwamba sala ndio nguzo ya dini hii, dini haipo bila ya nguzo hii. Haya yanathibitishwa na kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –

“Swala ndio nguzo ya dini, atakayeisimamisha, hakika ameisimamisha dini na atakayeiacha, bila ya shaka huyo ameivunja dini”.

Kwa mantiki hii, mtu atakayeihifadhi nguzo hii kwa kuswali katika nyakati zake maalumu na akatimiza sharti na nguzo zote hali kujinyenyekeza kwa Mola wake na huku akiamini kuwa ni wajibu wake kuswali, huyo ndiye atakayefaulu duniani na akhera. Tunasoma ndani ya Qur-ani Tukufu :

“KWA YAKINI WAMEFAULU WAUMINI AMBAO WAO NI WANYENYEKEVU KATIKA SWALA ZAO” Al-Muuminun : 1-2.

Kinyume chake yule atakayeipuuzia swala, akaacha kuswali, huyo ndiye mtu muovu aliyepata khasara duniani na akhera kwa sababu ya kuikhalifu amri ya Mola Muumba wake.

Kwa mujibu wa kauli iliyotangulia ya Bwana Mtume, wewe usiotaka kuliweka paji lako la uso ardhini kumsujudia Mola wako umeichukua nyundo kubwa na nzito unaivunja na kuibomoa dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Dini ambayo amewatuma mitume wake wote, tangu Nabii Adam mpaka Mtume wa mwisho Muhammad – Rehema na Amani ziwashukie wote – kuja kuisimamisha katika katika ardhi hii. Je, mbomoa dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu si mgomvi wa Allah, na hivi mtu anaweza kugombana na Allah kisha akatazamia kupata salama ?! La hasha.

Ewe mpenzi ndugu yangu, elewa na ufahamu kwamba swala ndiyo ibada ya kwanza kabisa aliyoiwajibisha Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Amesema Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – :

“Cha mwanzo alichokifaradhisha Allah kwa umati wangu ni swala tano, na cha mwanzo kinachorufaishwa (kinachopanda mbinguni) katika amali (matendo) yao ni swala tano, na cha mwanzo watakachoulizwa katika amali zao ni swala tano ….”

Ndugu yangu mpenzi usiotaka kumsujudia Mola wako aliyekuumba, haikutoshi hadithi hii kuona ni jinsi gani ibada ya swala ilivyopewa umuhimu wa kwanza katika Uislamu ?!

Amali zako zote njema ni lazima zitanguliwe na swala tano ndipo zikubaliwe, kinyume na hivyo amali hizo hazina maana bali ni sawa sawa na mavumbi yapeperushwayo. Ushahidi wa haya ni kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –

“Cha mwanzo atakachokaguliwa/atakachohesabiwa mja siku ya kiyama ni swala, ikitengenea zimetengenea baki ya amali zake nyingine, ikifisidika (swala) zimefisidika (zimeharibika) baki ya amali zake nyingine”

Ndugu mpenzi muislamu, ukiyakiri maneno haya ya Bwana Mtume yatakufikisha katika ukweli na hakika kwamba swala ndio ibada mama.

Kadhalika ili kuonyesha utukufu wa ibada ya swala, utaikuta swala ndio ibada pekee aliyoitiwa Bwana Mtume na kukabidhiwa na Mola wake mbinguni. Ibada nyingine zote Bwana Mtume alikuwa akiletewa amri hapa hapa ardhini kupitia kwa malaika Jibril – Amani imshukie – Allah alimkuhutubu Mtume wake juu ya swala tano katika ule usiku wa Miraji pasina wasita wa Jibril.

 Amesema Anas – Allah amridhie – Imefaradhishwa swala kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie – usiku aliopelekwa mbinguni swala khamsini, kisha zikapunguzwa mpaka zikawa tano, kisha (Mtume) akaitwa ewe Muhammad ! Hakika maneno yangu hayabadilishwi na utapata wewe katika swala tano hizo ujira wa swala khamsini”

Ndugu yangu muislamu, hebu yatafakari kwa makini maneno ya Mtume wako, utauona utukufu wa ibada ya swala.

Ni kwa ajili hiyo ndio tunaona Allah anatuamrisha kuhifadhi na kudumisha swala na muislamu amewajibikiwa kuitekeleza swala muda wa kudumu roho yake katika kiwiliwili chake.

Akiwa mzima wa afya njema au mgonjwa asojiweza kitandani kwa sharti ya kuwa na fahamu za kujua alitendalo. Awapo vitani au katika hali ya amani, akiwa safarini au la, swala imemlazimu tu.

Mwanamume na mwanamke wote ni sawa katika amri hii ya swala, ila mwanamke hatoswali akiwa katika hali ya hedhi au nifasi. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuamrisha swala

“HIFADHINI (angalieni sana) SWALA (zote kuziswali) NA (khasa) ILE SWALA YA KATI NA KATI NA SIMAMENI KWA UNYENYEKEVU KATIKA KUMUABUDU ALLAH NA MKIWA KHOFU ( mmo vitani, basi swalini) HALI YA KUWA MNAKWENDA KWA MIGUU AU MMEPANDA (wanyama) NA MTAKAPOKUWA KATIKA AMANI BASI MKUMBUKENI ALLAH (swalini) KAMA ALIVYOKUFUNZENI YALE MLIYOKUWA HAMYAJUI” [2:238-239]

Ndugu yangu mpenzi, utabainikiwa kutokana na aya hii kwamba muislamu hana udhuru hata chembe unaomuhalalishia kuacha swala.

Hivyo basi muislamu atakayeitekeleza swala kama itakikanavyo, swala hiyo itakuwa ni hoja (wakili wa kumtetea) itakayomuokoa siku ya Kiyama, si hivyo tu bali itakuwa ni nuru itakayomuangazia na kumuongoza katika siku hiyo ngumu na nzito kama ambavyo itakovyokuwa ni sababu ya kufutiwa madhambi yake.

Imepokelewa kutoka kwa Sayyidna Uthman – Allah amuwie Radhi – amesema : nimemsikia Mtume – Rehema na Amani zimshukie – akisema :

“Hatawadhi mtu udhu wake vizuri kisha akaswali ila Allah humsamehe mtu huyo madhambi yaliyo baina ya swala hii na swala ijayo”.

Basi ni kheri na furaha iliyoje kwa yule aliyeitekeleza swala kwa ukamilifu, ukamilifu na unyenyekevu mpaka anamaliza muda wake wa kuishi hapa duniani (anakufa). Eh! Ole wake, tena ole wake na majuto yake yule aliyefanya kibri, akaacha kuitekeleza swala hata akaondoka duniani bila ya kumsujudia Mola wake. Hebu itegee sikio la usikivu kauli hii tukufu ya Allah asema nini juu ya watu hawa :

“(Na wawalete) HIYO SIKU KUTAKAYOKUWA NA MATESO MAKALI NA WATAITWA KUSUJUDU LAKINI HAWATAWEZA. MACHO YAO YATAINAMIA CHINI; UNYONGE UTAWAFUNIKA NA HAKIKA WALIKUWA WAKIITWA KUSUJUDU WALIPOKUWA SALAMA (na walikataa)” [68:42-43].

Watu wa peponi watawauliza watu wa motoni :

“NI KIPI KILICHOKUPELEKENI MOTONI ? WASEME : HATUKUWA MIONGONI MWA WALIOKUWA WAKISWALI. HATUKUWA TUKILISHA MASIKINI. NA TULIKUWA TUKIZAMA (katika maasia) PAMOJA NA WALIOKUWA WAKIZAMA” [74:42-45].

 Khasara na maangamivu yaliyoje, leo utawaona baadhi ya waislamu hawaswali na hoja yao kubwa shughuli nyingi hawana nafasi, wametingwa na kazi na wengine huthubutu hata kusema kwa kinywa kipana kabisa kwani ni lazima kuswali, kama ninafanya mema mengine haitoshi ?! Hebu itegee sikio kauli hii ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – :

“Yeyote yule atakayeihifadhi swala, iatkuwa (swala hiyo) ni nuru, hoja na uokovu kwa mtu huyo siku ya Kiyama, na yeyote yule asiyeihifadhi swala, haitokuwa (swala) ni nuru, hoja na uokovu kwa mtu huyo, bali atakuwa (motoni) siku ya Kiyama pamoja na akina Qaarun, Fir-aun, Haaman na Ubayyi bin Khalaf”.

Fahamu ewe ndugu yangu muislamu, swala ina nafasi na utukufu wa pekee katika Uislamu ndio maana tunamkuta Bwana Mtume mara nyingi anatuhimiza swala na swala ndio ulikuwa wasia wake wa mwisho wakati anaondoka duniani :

“Ninakuhimizeni na kukuusieni swala pamoja na wamilikiwa wa mikono yenu ya kuume”.

 

C. KHATARI YA KUACHA SWALA

Ndugu yangu Muislamu, bila shaka unatambua au umewahi kusikia kwamba Allah aliwaamrisha malaika pamoja na Ibliis wamsujudie baba yetu Nabii Adam – Amani imshukie – hali ya kumuamkia. Iblisi kwa ushupavu na kibri alichokuwa nacho alikataa kuitii na kuitekeleza amri ya Mola wake.

Ni kwa sababu hii tu Allah akamfukuza Iblis na kumtoa huko alikokuwa pamoja na Malaika na akamlaani mpaka siku ya kiyama, na kesho akhera ataingia motoni. Tusome kwa mazingatio :

“(na wakumbushe watu khabari hii) TULIPOWAAMBIA MALAIKA MSUJUDIENI ADAM ( yaani mwadhimisheni kwa ile elimu yake aliyopewa) WAKAMSUJUDIA WOTE ISIPOKUWA IBLIS, AKAKATAA NA AKAJIVUNA NA (toke hapo) ALIKUWA KATIKA MAKAFIRI (ila tu alichanganyika tu na malaika)” [2:34].

Basi wewe ndugu yangu mpenzi usiotaka kuswali, hujioni kuwa wewe ni mbaya zaidi kuliko Iblis ?!

Iblis alikataa kumsujudia Nabii Adam, wewe leo unakataa kumsujudia aliyemuumba Nabii Adam. Iblis alikataa kusujudu mara moja tu, wewe leo unakataa kusujudu mara thelathini na nne (34) kila siku, mara 238 kila wiki, mara 1020 kila mwezi, mara 12,104 kwa mwaka, mara ….. katika umri wako, jaza mwenyewe.

Iblis alikataa kusujudu sijida ya heshima kwa Nabii Adam, wewe unakataa kusujudu sijida ya ibada kwa Mola Muumba wako.

Hebu angalia tena adhabu aliyopewa Iblis kwa kuacha sijida moja tu alilaaniwa na kutolewa peponi na huku akisubiriwa kuliongoza kundi la watu wa motoni kuingia motoni.

Hii inamaanisha mwenye kuacha sijida 34 kila siku anastahiki kupata adhabu kali zaidi ya ile aliyopewa Iblis mlaaniwa, sikwambii asioswali juma moja au zaidi.

Ndugu yangu usioswali unatarajia nini ikiwa hali ni hiyo ?! Unaona uzito gani kumsujudia Mola wako ?! Aletwe Mtume mwingine ndio utasikia na kutii ?! Hebu ihurumie nafsi yako, huiwezi adhabu ya Mola wako.

Ndugu yangu umepewa neema ya akili, ishukuru neema hiyo kwa kuzingatia uambiwayo, umepewa masikio ili usikie, isikie haki na kuifuata, usijitie upofu na uziwi wa bure ukajuta na kuangamia. Zinduka, usiingie katika kauli ya Allah isemayo :

“NA BILA SHAKA TUMEWAUMBIA MOTO WA JAHANAMU WENGI KATIKA MAJINI NA WANADAMU (kwa sababu hii): NYOYO WANAZO LAKINI HAWAFAHAMU KWAZO, NA MACHI WANAYO LAKINI HAWAONI KWAYO, NA MASIKIO WANAYO LAKINI HAWASIKII KWAYO. HAO NI KAMA WANYAMA, BALI WAO NI WAPOTOFU ZAIDI. HAO NDIO WALIOGHAFILIKA” [7:179].

Tahadhari ewe ndugu yangu, usiwe na sifa hizi zilizotajwa, kwani hizi ni sifa za watu wabaya, watu wa motoni. Tumuombe Mola wetu Mtukufu asitujaalie kuwa miongoni mwa watu wa motoni, wasiotaka kumsujudia – Amin.

UMUHIMU WA SWALA NA NAFASI YAKE KATIKA UISLAMU

A: HUKUMU YA SWALA KWA MUJIBU WA QUR-ANI NA SUNNAH

Ewe ndugu yangu mpenzi; hebu kwa msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu tuzianze nasaha zetu kwa kumuomba Mola wetu Mtukufu atuwafikshe na kutuongoza katika kuijua haki, kuikubali na ksha kuifuata-Aamiyn Baada ya dua hiyo, hebu sasa tutazame kwa pamoja natujiulize nini hukumu ya ibada ya swala ndipo tutafahamu ni ipi nafasi na hukumu ya mtu asiye swali .

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published.