Nabii Muhammad – Rehema na Amani zimshukie – alipotumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuja ulimwenguni kuuhusisha Uislamu ulioasisiwa na Mitume waliomtangulia, alimkuta mwanamke akiishi chini ya mazingira na kivuli cha ukandamizaji.
Katika ulimwengu ule, mwanamke hakuwa na haki yeyote ile katika jamii yake bali alionekana kama ni bidhaa inayoweza kuuzwa wakati wowote.
Mwanamke alichukuliwa kama ni chombo cha kumstarehesha na kukidhi matamanio ya kimwili ya mwanamume. Mwanamke alihesabika kuwa ni chombo cha uzalishaji na hakuwa na uchaguzi/uhuru wa kupanga na kuamua.
Haya kwa mukhtasari ndiyo mazingira ambayo Uislamu ulimkuta mwanamke akiishi chini ya anga lake. Mwenyezi Mungu kupitia mfumo sahihi wa maisha (Uislamu) ambao dhamana ya uongozi wake alimpa Nabii Muhammad – Rehema na Amani zimshukie – akamuondolea mwanamke unyonge, udhalili, dhulma, uonevu na unyanyasaji ule.
Uislamu ukamjengea mwanamke mazingira bora, kanuni na sheria ambazo zitamuhakikishia uhuru, usalama, amani, haki na usawa katika jamii yake.
Uislamu ukamtayarishia mwanamke anga zuri, chini ya anga hilo ataishi huku akijihisi kuwa ni binadamu kamili, mwenye haki sawa kama mwanamume na ukamdhaminia kupata haki zote kama binadamu bila ya kuhitajia upendeleo maalum kama tusikiavyo istilahi hii ikipigiwa kelele ulimwenguni kote bila ya utekelezaji wowote.
Uislamu ukamuondoshea mwanamke tuhuma ya kumpotosha Baba yetu Adam – amani iwashukie wote – peponi na kuwa yeye (mwanamke) ndiye asili na chanzo cha uovu wote huu utendekao ulimwenguni.
Uislamu ukabainisha kwamba ni shetani mlaaniwa ndiye aliyewapoteza Nabii Adam na mama yetu Hawaa, kama tunavyosoma katika kitabu cha Uislamu
“(Lakini) SHETANI (yule Iblis adui yao) ALIWATELEZESHA WOTE WAWILI (wakakhalifu amri ile, wakala katika mti huo waliokatazwa) NA AKAWATOA KATIKA ILE (hali) WALIYOKUWA NAYO …[2:36].
Uislamu unakiri na kutangaza wazi kuwa watu wote bila ya kujali rangi au hali zao kimaisha wameumbwa kutokana na nafsi moja tu. Tusome, tuzingatie na tukubali :
“ENYI WATU ! MCHENI MOLA WENU AMBAYE AMEKUUMBENI KATIKA NAFSI (asili) MOJA ….” [4:1]
Huu ni usawa wa binadamu katika mfumo adilifu wa maisha (Uislamu). Chini ya kivuli cha mfumo huu, mwanamke na mwanamume wanaogelea pamoja katika bahari moja ya usawa wa haki zote za msingi za binadamu bila ya kubaliwa. Isitoshe ule utukufu ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu aliompa mwanadamu katika kauli yake :
“NA HAKIKA TUMEWATUKUZA WANADAMU …” [17:70].
Huu ni utukufu aliozawadiwa mwanadamu yoyote bila ya kuangalia ni mwanamume au mwanamke, wote wanashirikiana kwa usawa katika utukufu huu.
Qur-ani Tukufu inapomzungumzia mtu au wanadamu, basi huwa inamkusudia mwanamume pamoja na mwanamke.
Ama inapotaka kumtaja mwanamume au mwanamke peke yake bila ya kumhusisha mwenzake basi hutumia istilahi “wanamume” au “wanawake”.
Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anazidi kuudhihirisha ulimwengu nafasi aliyonayo mwanamke katika mfumo huu sahihi wa maisha (Uislamu). Anatuonyesha uhusiano uliopo baina ya mwanamume na mwanamke katika kauli yake:
“Wanawake ni ndugu baba mmoja, mama mmoja na wanamume, wanayo haki kwa sheria (kufanyiwa na wanamume) kama ile haki iliyo juu yao kuwafanyia wanamume” Abu Dawoud.
Istilahi ya ndugu baba mmoja, mama mmoja aliyoitumia Bwana Mtume inatoa sura kamili ya usawa baina ya mwanamke na mwanamume.
Kwa jicho la mfumo kamili huu wa maisha (Uislamu) wanamume na wanawake kiasili ni sawa sawa bila tofauti yeyote mbele ya Mola wao.
Ila tofauti na ubora utajitokeza katika amali njema anazozifanya kila mmoja wao, ni dhahiri kuwa mzuri na mwingi wa amali njema hawezi kulingana sawa na mchache wa amali njema bila ya kuangalia ni mwanamume au mwanamke, hii ndio mojawapo wa misingi na kanuni za Uislamu.
Tusome kwa mazingatio na kutafakari :
“WAFANYAJI MEMA, WANAMUME AU WANAWAKE, HALI YA KUWA NI WAISLAMU, TUTAWAHUISHA MAISHA MEMA NA TUTAWAPA UJIRA WAO (Akhera) MKUBWA KABISA KWA SABABU YA YALE MEMA WALIYOKUWA WAKIYATENDA” [16:97].
Uislamu unazidi kumthibitishia na kumuhakikishia mwanamke nafasi ya usawa kwa kumpa fursa sawa ya kukubaliwa na kujibiwa dua sawa sawa/sambamba na mwanamume bila ya kupoteza amali zake njema. Hili linathibitishwa na Qur-ani Tukufu :
“MOLA WAO AKAWAKUBALIA (maombi yao kwa kusema) HAKIKA MIMI SITAPOTEZA JUHUDI (amali) YA MWANAMUME AU MWANAMKE (kwani nyinyi) NI NYINYI KWA NYINYI …” [3:195].
Muundo wa maelezo ya Qur-ani Tukufu NI NYINYI KWA NYINYI unatufahamisha kuwa kuna hali ya kutegemeana baina ya mwanamume na mwanamke na kwamba maisha ya kila mmoja wao hayakamiliki bila ya kushirikiana na mwenziwe.
Uislamu unauthamini mchango wa mwanamke katika jamii, ndio maana ukampa nafasi na haki sawa ya kushiriki katika vitakatifu vya kidini “Jihadi” sambamba na mwanamume.
Katika medani ya vita kuna watakaokufa mashahidi, kuna majeruhi, wapiganaji ni wanadamu wanahitaji huduma ya maji na chakula.
Nani atakayetoa huduma hizi ili kuipa ushindi dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ? Hapo ndipo unapoonekana umuhimu wa mchango wa mwanamke katika kuipigania dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Ni kutokana na sababu hii na nyinginezo ndio tunamkuta Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa haendi katika vita vyovyote ila ataambatana na wanawake. Bibi Umayyah bint Qays ni mwanamke anayetajwa sana katika vitabu vya historia ya Uislamu kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika vita vya Khaybar.
Kwa kuuona na kuuthamini mchango wa bibi huyu, baada ya kumalizika vita hivi Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alimtunukia kidani alichokivaa maisha yake. Alipokurubia kufa aliusia azikwe pamoja na kidani chake – Allah amuwie radhi -. Mwanamke huyu na wale wote watakaomuiga wanaingia katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu :
“LAKINI MTUME NA WALE WALIOAMINI PAMOJA WALIIPIGANIA (dini) KWA MALI ZAO NA NAFSI ZAO; NA HAO NDIO WATAKAOPATA KHERI; NA HAO NDIO WENYE KUFUZU (kufaulu) . ALLAH AMEWATENGENEZEA MABUSTANI YAPITAYO MITO MBELE YAKE, WAKAE HUMO. HUKO NDIKO KUFUZU KUKUBWA” [9:88-89]
Kadhalika Uislamu haukumuacha nyuma mwanamke katika uwanja wa elimu bali umemshirikisha kikamilifu sambamba na mwanamke. Hili linathibitishwa na kauli/agizo la Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – :
“Utafutaji/Kutafuta elimu ni fardhi ya lazima kabisa kwa kila muislamu mwanamume na muislamu mwanamke”. Utaona kupitia agizo/kauli hii ya Bwana Mtume, Uislamu umewajibisha mwanamke apate elimu.
Hivi baada ya haki hizi za msingi alizopewa mwanamke wa Uislamu, haki ambazo zinalindwa na kusimamiwa na sheria madhubuti, kuna mtu muadilifu atakayefunua kinywa kipana na kudai kuwa eti Uislamu unamdhulumu na kumkandamiza mwanamke ?!
Ndugu zanguni, ni lazima tukubali kuwa hapa kuna mambo mawili; Uislamu kama dini na mfumo sahihi wa maisha unaotawaliwa na sheria ya Allah na upande wa pili kuna wanaoitwa waislamu wanaitawaliwa na desturi/ada na mwenendo mbaya dhidi ya mwanamke. Kwa hivyo ni lazima tutofautishe baina ya vitu viwili hivi kama kweli tu waadilifu.
Kelele hizi na wimbo huu wa kunyanyaswa, kudhulumiwa na kunyimwa haki mwanamke zilizoenea leo ulimwenguni kote ni kelele zipigwazo na kambi za magharibi na mashariki.
Hawa hawana ushahidi wa kuyathibitisha madai yao haya bali kwa makusudi mazima wanataka kuipaka matope dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; hawa ndio Mwenyezi Mungu anataumbia :
“WANATAKA KUZIMA NURU YA ALLAH (Uislamu) KWA VINYWA VYAO; NA ALLAH ATAKAMILISHA NURU YAKE IJAPOKUWA WASHIRIKINA WATACHUKUWA” [61:8].
Tukifanya uchunguzi wa kiadilifu tutagundua kuwa ustaarabu wa kimagharibi ndio unaomnyima haki na kumdhulumu mwanamke.
Ikiwa mwanamke anapoolewa huko katika ulimwengu wa kwanza (Ulaya) kwa watu walioendelea kama wanavyodai ananyimwa hata haki ya kuitwa kwa jina la baba yake mzazi bali ananasibishwa na familia ya mume aliyemuoa.
Kwa mfano mwanamke anayeitwa Vicky James akiolewa na Michael Brown anaitwa Mrs Vicky Brown. Ikiwa mwanamke huyu hapati haki ya kuitwa kwa jina la baba yake aliyemzaa vipi unamtazamia kupata haki nyingine katika jamii hiyo ?!
Katika Uislamu, mambo ni kinyume kabisa na hivyo. Wakeze Mtume, ambaye kwa mujibu wa imani ya kiislamu ndiye kiumbe bora kuliko wote hawakupata kuitwa mathalan Bibi Muhammad bin Abdillahi, bali waliitwa kwa majina ya baba zao, kama Bibi Aysha binti AbuBakri, Hafsa binti Umar, Zaynab binti Jahshi na kadhalika.
Katika hali kama hii utawasikia na kuwaona watu wenye fikra lemavu waliorogwa na ukoloni mamboleo wakisema : Tunataka kuwa kama watu wa Magharibi. Huu ni udumavu wa fikra na mawazo. Hivi kumvua nguo mwanamke na kumuacha uchi mbele ya kadamnasi ya watu katika kile kinachoitwa mashindano ya urembo, ndiko kumpa haki na uhuru mwanamke ?
Huu ndio ustaarabu na maendeleo tunayotaka kuyaiga kutoka Magharibi ?! Je, kuja nyumbani kijana wa kiume na kumpiga busu mtoto wa kike mbele ya wazazi wake na kisha kumchukua kokote atakako na kumrudisha wakati autakao kwa madai ya uchumba na hili likapewa baraka zote za wazazi wa binti.
Kijana akishamtia binti mimba amkimbie na kumuacha aubebe mzigo huo peke yake na kwenda kwenda kumtafuta kimwana mwingine na kustarehe naye na kuendeleza uchafu wake. Je, huu ndio usawa, haki na uhuru anaopewa mwanamke na ulimwengu wa magharibi na sisi tukataga kuuiga kibubusabubusa ?
Haya si maendeleo bali maondoleo ya utu na maadili mema, na hizi ni tabia na silka za kinyama si za kibinadamu hata kidogo. Huu ndio ukweli, tukikubali au kukataa. Uislamu haukuja kumdhulumu, kumuonea na kumkandamiza mwanamke, bali umekuja kumkomboa kutoka katika jahilia na kumpa haki zote anazostahiki kuzipata kama binadamu.
Hebu tuhitimishe makala yetu haya kwa kuangalia mfano hai huu ambao unatoa sura/picha ya uhuru kamili ya kujieleza na kuchangia fikra aliopewa mwanamke chini ya mfumo sahihi wa maisha (Uislamu). Zama za ukhalifa(utawala) wa Sayyidna Umar – Allah amuwie radhi – wanawake walikuwa wakiwatoza wanamume mahari kubwa sana.
Hali iliyopelekea baadhi ya wanamume wenye kipato duni kushindwa kuoa. Sayyidna Umar kama kiongozi mkuu wa dola ile ya kiislamu aliliona tatizo hili na kujiona kuwa anawajibika kulitafutia ufumbuzi wa haraka.
Akaamua kuitisha mkutano wa hadhara na kupiga marufuku utozaji mkubwa wa mahari na badala yake akaweka kiwango maalum cha mahari. Hapo ndipo aliposimama mwanamke mmoja na kusema :
” Ewe Umar, ikiwa Mwenyezi Mungu mwenyewe ameturuhusu kuchukua mrundi wa mali (mali nyingi isiyo na idadi) vipi leo wewe unatuzuia na kutupiga marufuku kuchukua mali kidogo tu ?
Hebu jaribu kufikiri huyu ni kiongozi wa dola, anaambiwa maneno hayo mbele ya watu na anayemwambia ni mwanamke, unafikiri alichukua hatua gani ? Sayyidna Umar aliuheshimu uhuru wa kujieleza na haki ya kusikilizwa ya mwanamke huyu.
Akasalimu amri na kusema : Umar amekosea na mwanamke amepatia. Je, ni haki gani zaidi ya hizi tunataka apewe mwanamke ?!
Hebu mchukue mwanamke huyu na umlete katika jamii yetu ya leo. Je, atathubutu kufungua kinywa chake na kumwambia kiongozi/mtawala maneno hayo ya kumkosoa mbele ya hadhira tena bila ya kuanza kwa kumuita mtukufu/mheshimiwa raisi, akamuita kwa jina lake tu, na kiongozi huyo akakiri mbele ya watu kuwa kweli kakosea ?!
Hebu tuache chuki zetu na tujaribu kuwa waadilifu na wakweli ili tuweze kuiona haki kuwa ni haki na kuifuata na kuiona batili kuwa ni batili na tuiepuke.