Mara tu baada ya Mtume kurudi kutoka Shamu aliiwasilisha mara moja faida kubwa iliyopatikana kutokana na biashara kwa Bi Khadijah.
Bi Khadijah aliifurahia sana faida hiyo ambayo hakuwahi kuipata kutoka kwa watu wengine aliowaajiri kabla ya Mtume Muhammad.
Kwa kigezo hiki Bi Khadijah akazidi kuthibitisha khabari zilizomfikia juu ya uaminifu na ukweli wa Nabii Muhammad, ukiachilia mbali yale aliyoelezwa na mtumishi wake Maysarah ambaye alikuwa msaidizi wa Mtume katika safari yao ya Shamu.
Sifa zote hizi njema zikamteka Bi Khadijah na kujikuta akimpenda Mtume na kutamani awe na mume mwenye sifa njema kama Nabii Muhammad.
Akamtuma mshenga kwa Mtume amuelezee nia yake ya kutaka kuolewa naye. Ni vema ikakumbukwa kwamba wakati huo Bi Khadijah alikuwa ana umri wa miaka arobaini na Bwana Mtume alikuwa amefikia umri wa miaka ishirini na tano.
Bwana Mtume kwa kuzingatia utukufu, heshima na tabia njema za Bi Khadijah bila ya kusita akakubali kumuoa bibi huyu.
Ndipo tena mipango na taratibu za harusi zikaanza na hatimaye wawili hawa wakawa ni mke na mume. Ndoa hii ilifungwa miezi miwili tangu Mtume kurejea kutoka Shamu.
Bibi huyu ameishi na Mtume kwa karibu robo karne yaani kipindi kisichopungua miaka ishirini tano. Kwa kipindi hiki chote Mtume hakumuolea Bibi huyu mke mwenza, naye ndiye mkewe wa kwanza.
Bi Khadijah alimzalia Bwana Mtume watoto sita, wawili wa kiume nao ni Kasim na Abdallah na wanne wa kike nao ni Zainabu, Rukia, Ummu Kulthum na Fatimah.
Ama Ibrahimu, huyu alizaliwa na Bi Mariah Mqibtwi wa Misri.
Ni vema tukakumbuka kuwa Bi Khadijah kabla ya kuolewa na Mtume alikuwa ameolewa na Bwana Abu Haalah ambaye alimfia. Hivi ndivyo Bwana Mtume alivomuoa Bi Khadijah – Allah amuwie Radhi mama yetu huyu-.