SABABU ZA SIJIDA YA KUSAHAU:
Mambo yafuatayo ndio yatakayo mpelekea mwenye kuswali kuleta sijida ya kusahau:
1. Mwenye kuswali kuacha mojawapo miongoni mwa suna za swala zinazoitwa “Ab-aadh”, mithili ya Tashahudi ya mwanzo na Qunuut (kwa ufafanuzi wa kina juu ya suna hizi, rejea SURA YA PILI, SOMO LA KWANZA, SWALA {x} Suna za swala).
Imepokewa kutoka kwa Abdullah Ibn Buhaynah-Allah amuwiye radhi–kwamba yeye amesema: Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-alituswalisha rakaa mbili za swala fulani.
Na katika upokezi mwingine: “Aliinuka kutoka katika rakaa mbili za swala ya Adhuhuri, kisha akasimama na wala hakukaa (Tashahudi ya mwanzo), watu (maamuma) nao wakainuka pamoja nae. Alipomaliza swala yake (kwa kuswali rakaa mbili za mwisho), (wakati) tukiingojea salamu yake, akakabiri (akasema Allahu Akbar) kabla ya kutoa salamu. Akasujudu sijida mbili na il-hali amekaa, kisha (ndio) akatoa salamu.” Bukhaariy & Muslim.
Imepokelewa kutoka kwa Al-Mughiyrah Ibn Shu’ubah–Allah amuwiye radhi–amesema: Amesema Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie:
“Atapoinuka mmoja wenu kutoka (katika) rakaa mbili (za mwanzo) na akawa hajatimia hali ya kusimama , basi na akae (kwa ajili ya Tashahudi ya mwanzo. Na atapotimia hali ya kusimama, basi na asikae (aendelee na swala yake) na atasujudu sijida mbili za kusahau”.Ibn Maajah, Abuu Daawoud & wengineo.
2. Mtu kuwa na shaka ya idadi ya rakaa alizoziswali. Katika hali hii, mwenye shaka anatakiwa aishike idadi ya chini na atimize rakaa zilizobakia.
Kisha atasujudu sijida ya kusahau kwa ajili ya kuunga imkani ya kwamba yeye amezidisha kitu katika swala yake.
Lau mtu atakuwa na shaka je, ameswali Adhuhuri rakaa tatu au nne? Shaka hii ikamtokea akiwa bado ndani ya swala, basi atachukulia kuwa ameswali rakaa tatu na aongeze rakaa moja nyingine ili zitimie rakaa nne zitakiwazo.
Halafu tena akimaliza asujudu sijida mbili za kusahau kutokana na imkani ya kuwa kaswali rakaa tano na hivyo kuwa amezidisha kitu katika swala yake.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Said–Allah amuwiye radhi–amesema: Amesema Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie:
“Atapotia shaka mmoja wenu ndani ya swala yake, na asijue ameswali rakaa ngapi, tatu au nne? Basi (cha kufanya) ni kuitupa shaka hiyo na ajengee alicho na yakini nacho. Kisha asujudu sijida mbili kabla ya kutoa salamu. Akiwa ameswali rakaa tano, (kusujudu huko) kutaifanya swala yake kuwa jozi (ya rakaa mbili za mwanzo na mbili za mwisho). Na akiwa ameswali kutimiza rakaa nne, zitakuwa (sijida mbili) hizo zimemdhalilisha na kumghadhibisha shetani”. Muslim.
Ama lau mtu alitia shaka nje ya swala (baada ya kutoka ndani ya swala) kwa yakini shaka yake hii haitaathiri usahihi na ukamilifu wa swala yake. Ila kama shaka hiyo itakuwa ni katika nia na Takbira ya kuhirimia swala, shaka hii itamlazimisha kuirudia (kuiswali tena) swala yake.
TANBIHI:
Kusahau kwa maamuma wakati wa kumfuata Imamu wake, kama vile kusahau Tashahudi ya mwanzo.
Kusahau kwake huku kutachukuliwa na Imamu wake na wala haitamlazimu kusujudu sijida mbili za kusahu baada ya salamu ya Imamu wake.
Dalili ya haya ni kauli yake Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie: “Imamu ni mdhamini (wa maamuma)”. Ibn Hibbaan
3. Kutenda kitendo kilichokatazwa kwa kusahau, ikiwa makusudi yake hubatilisha swala. Mithili ya mwenye kuswali kuzungumza maneno machache au kuongeza rakaa moja kwa kusahau.
Kisha akazinduka na kutambua kuwa yumo ndani ya swala, huyu katika mazingira haya ataleta sijida mbili za kusahau.
4. Kugurisha/kuhamisha kitu miongoni mwa matendo ya swala kukipeleka mahala si pake. Kikiwa kitu hicho ni nguzo/faradhi au ni suna ya “Ba’adh”.
Mfano wa haya ni mtu kusoma Suuratil–Faatihah (Al-hamdu) katika kikao (mkao) cha Tashahudi badala ya mahala pake ambapo ni katika Qiyaamu (kisimamo cha swala).
Au mtu kusoma Qunuut katika rukuu badala ya mahala pake ambapo ni katika Itidali ambayo huja baada ya kurukuu. Au mtu kuisoma sura ambayo ni suna, kuisoma baada ya Al-hamdu katika Itidali badala ya mahala pake ambapo ni katika Quyaamu.
Ni suna kwa mtu huyu kusujudu sijida mbili za kusahau mwishoni mwa swala yake kutokana na kuyafanya haya.
NAMNA YA KUSUJUDU SIJIDA ZA KUSAHAU NA MAHALA PA KUSUJUDU:
Kusujudu kwa kusahau ni sijida mbili kama sijida nyingine za swala. Mwenye kuswali atanuia kwa sijida mbili hizo kusujudu kwa kusahau.
Na mahala pa kusujudu ni mwishoni mwa swala yake kabla ya kutoa salamu. Angalia lau mwenye kuswali atatoa salamu kabla ya kusujudu kwa makusudi au kwa kusahau na muda (kitambo) ukarepa (ukarefuka), itafutu sijida hiyo.
Kama utakuwa haukupita muda mrefu, itamuelea kuidiriki sijida ya kusahau kwa kusujudu mara mbili kwa nia ile ile ya kusahau, kisha atoe salamu kwa mara nyingine tena.
TANBIHI:
1. Kama mwenye kuswali hakuleta sijida ya kusahau ambayo hukumu yake ni suna, swala yake haitabatilika. Hii ni kwa sababu sijida ya kusahau haikuwekwa kwa ajili ya kuacha tendo la wajibu.
2. Ama mwenye kuswali atapoacha mojawapo ya nguzo za swala kama rukuu au kusoma Al-hamdu. Basi hana budi kuileta nguzo hiyo aliyoiacha wala kusujudu kwa kusahau hakutakuwa kiungo cha nguzo hiyo. Bali sijida mbili za kusahau zitakuja baada ya kuileta hiyo nguzo aliyoisahau.